Uncategorized

Ndio;King Kaka Matatizo yaliyoko yamekita zaidi ndani ya Mfumo uliooza wa Kirasilimali

Kusambaza ni Kuunusuru Uislamu

Mwanamuziki wa mitindo ya Rappa Kennedy Tarriq Ombimba almaarufu King Kaka ameibua hisia kali miongoni mwa wanasiasa hasa baada ya kutoa wimbo wake akiwashtumu wanasiasa na wakenya kuwa wao ndio chanzo cha matatizo yanayokumba Kenya. Wimbo huo kwa jina “wajinga Nyinyi” ametaja tatizo la uhaba wa ajira na ufisadi kama matatizo sugu yanayokabili nchi. King Kaka ametaja baadhi ya wanasiasa waliohusishwa na kashfa mbambali za ufisadi. Wimbo wake huo umezua tafrani kwa wanasiasa ambao tayari baadhi yake wameonesha nia ya kumshtaki mahakamani huku raia wengi wakionekana kumuunga mkono msanii huyo.

Sio mara ya kwanza King Kaka kuibua mchecheto kwa wanasiasa hasa ikikumbukwa mwaka 2017, alitoa kibao chake kwa jina la “Mwizi Mkubwa” ndani yake akikashifu vitendo vya wanasiasa vya kuwahonga wafuasi wao ili wapate kuhudhuria kwenye mikutano na maandamano yao ya kisiasa. Kaka anaungana na msanii mwenzake Kama vile Eric Wainana kwenye wimbo wake (Kenya nchi ya Kitu kidogo) akielezea jinamizi la ufisadi nchini Kenya.

Hata kama wasanii wengi kwenye nyimbo zao zinazoangazia matatizo hulenga tu kujiongezea zaidi umaarufu wala sio mageuzi kwani hawana nia wala njia ya kuyatatua, sio siri kuwa matatizo aliyoyataja King Kaka ni ukweli mtupu. Kama waswahili walivyosema ukweli mchungu, mashairi yake “wajinga nyinyi” yalionekanwa kama mwiba kwa wanasiasa ambao licha ya maovu wanayoyafanya wao hutaka waonekanwe weupe kama pamba.

Katika kulaumu kwake wanasiasa kwamba wao pekee ndio wanaochangia matatizo kumeonyesha pia kumeonesha mtizamo finyo wa msanii huyo ambao kihakika ndio mtazamo wa wengi juu ya uhalisia wa mambo kwani hatakama kweli kwa njia moja wao huchangia matatizo hayo lakini masuala ni mapana zaidi. Kiasili matatizo yaliyoangaziwa ni natija ya mfumo muovu wa kibepari uliojenga mazingira ya watu kuwa na uchu na pupa wa kujikusanyia utajiri kwa njia yoyote chafu kama vile uizi, udanganyifu na ubadhirifu. Hivyo mali ya umma katika serikali za mabepari huishia kuibwa na walioko serikalini kwani hutumia vyeo vyao kufanikisha uovu huo. Na hilo sio siri Kwa mantiki hii ndio thuluthi ya bajeti ya Kenya huishia matumboni mwa ‘vigogo’ serikalini. Na havikuwa vita dhidi ya ufisadi ndani ya serikali za Kibepari ila usanii tu na jaribio la kuhadaa raia wawe na Imani kwamba serikali kweli inapambana na ufisadi. Na hata ikitokea kushikwa kwa watuhumiwa wa ufisadi huwa ni usanii wa kisiasa unaoishia tu mahakamani hatimaye kutopatikana na hatia!

Ama kwa nini wanasiasa wengi leo ndio wafisadi hili ni kwamba mfumo wa kisiasa wa Kidemokrasia umechanganya pesa na siasa kwa pamoja. Hatua hii hufanya mwanasiasa ajitafutie umaarufu kupitia pesa, kutafuta madaraka kwa kutumia pesa na kutumia pesa ili kusukuma ajenda ya kisiasa. Kidemokrasia siasa sio kusimamia maslahi ya umma bali ni ajira ya kuzalisha mapato.

Ukosefu wa kazi kwa vijana sio tatizo linalokumba Kenya tu bali ulimwengu kwa ujumla na hilo pia limesababishwa na mfumo wa Kirasilimali. Tatizo  hili hubuniwa kimakusudi na warasilimali kama moja wapo ya njia zao za kuendeleza unyanyasaji wa watu kiuchumi. Makampuni ya kirasilimali hudai kwamba kuajiri watu wengi ni kumaanisha kutumia pesa nyingi katika kuwalipa mishahara ambao kwa hesabu hio ni hasara na wao hawajui ila faida! Fauka ya haya hata wanapodai kufungua maeneo maalumu ya kiviwanda (Special Economic Zones) huu ni kutaka kukamua watu kwa kazi ngumu kwa mshahara duni. Na huu ndio mtindo wa makampuni ya kimataifa ambayo chini ya vazi la uekezaji huingia katika mataifa mengi hasa ya ulimwengu wa tatu.

Huu ndio uhalisia wa Ubepari na serikali zake ambao kiukweli kushuhudiwa ndani yake matatizo ni dalili ya kufeli kwake katika kusimamia maisha ya watu. Ispokuwa licha ya kufeli huko, warasilimali wakimagharibi hujenga ufahamu kwa watu kuwa matatizo wanayokumbana nayo hayatokamani na mfumo wao bali tabaka la kisiasa ndio linalokosea mfumo hivyo mara nyingi hushajiisha mabadiliko ya sura za wanasiasa ili watu wazidi kuamini kuwa mabadiliko ni kubadilisha sura za wanasiasa na wala sio kubadilisha mfumo wenyewe.

Kwa haya basi, watu walio na nia ya kweli ya kutaka kujiondoa kwenye matatizo haya kimsingi utawakuta hawashughuliki na kutia viraka mfumo ambao tayari ushaoza ama kuhadaika na michakato bandia ya mageuzi yawe ya kikatiba au kugeuza sura za watawala kwani yote hayo ni kuendeleza tu matatizo. Mabadiliko yanayohitajika kweli sio kwa Kenya tu bali dunia nzima kwa ujumla ni kuuleta mfumo wa Uislamu uliojengwa juu ya wahyi (Muongozo utokao kwa MwenyeziMungu swt). Uislamu una utaratibu wa kisiasa ambao humaanisha usimamizi wa kikweli mambo ya watu kwa mujibu wa sheria za Kweli za MwenyeziMungu. Kwa msingi huu kiongozi wa Kiislamu atakayevishwa majukumu ya kuongoza utamkuta akiogopa kudhulumu sio wanadamu tu bali hata wanyama huku akijua yote hayo ataulizwa siku ya Qiyama. Huyuhapa Umar RA akisema ‘Lau mbuzi anajikwaa njiani basi nitaogopo jinsi Mola wangu ataniuliza kwanini sikutengeza barabara?! Naam, hivi ndivyo Uislamu ukiwa ndani utawala wa Khilafah jinsi utakavyo kuwa na pupa ya kuondosha matatizo kwa umma kivitendo wala sio maneno tu.

Shabani Mwalimu

Mwakilishi kwa Vyombo vya Habari Hizb ut-Tahrir Kenya