Jumla

Afrika Kufaulu ni Mpaka Iwafurushe Wakoloni Wamagharibi pamoja na Mfumo wao Wakisekula Wakirasilimali

Kusambaza ni Kuunusuru Uislamu

Alhamisi, 19 Julai 2018 Kenya ilikuwa mwenyeji wa mkutano wa tatu wa wamiliki wa hisa wa Shirika la Uwekezaji katika Miundo Mbinu ya Afrika (Africa50). Shirika hili lilianzishwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) pamoja na mataifa ya Afrika. Kuanzishwa huku kulijadiliwa mwaka 2012 na viongozi wa Afrika kuhusiana na Mpango wa Maendeleo ya Miundo Mbinu ya Afrika (PIDA) ambao ulilenga kutoa suluhisho la kiubunifu juu ya miundo mbinu ya Afrika. Mei, 2013 Mawaziri wa Fedha wa Afrika waliidhinisha Africa50 na makao makuu yake kuzinduliwa Casablanca, Morocco mnamo Septemba 2014. Shirika hilo limejumuisha zaidi ya mataifa ishirini ndani na nje ya Afrika ikiwemo pamoja na Kenya, Nigeria, Misri, Morocco, Democratic Republic of Congo n.k.

Ilhali Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) ilianzishwa mwaka 1964 na inajumuisha: Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB), Shirika la Fedha za Maendeleo ya Afrika (ADF) na Shirika la Fedha la Nigeria (NTF). AfDB inadai ati lengo lake ni kupigana na umasikini na kuinua hali ya maisha barani kote kupitia kuwekeza katika miradi ya ummah na ya kibinafsi na kubuni mipango itakayopelekea kuchangia kuendelea kwa uchumi na jamii. AfDB inatoa michango ya kifedha kwa serikali na makampuni yanayowekeza katika eneo la nchi wanachama (RMC). Makao makuu yake ni Abidjan, Cote d’Ivoire.

Lakujiuliza ni; je tangu kubuniwa kwa AfDB mwaka 1964 na Africa50 mwaka 2014 mpaka hivi sasa hali ya nchi wanachama na bara la Afrika kwa ujumla ikoje? Jibu ni kwamba hali ni ya kutamausha na kutia majonzi. Kuanzia nchi wanachama hadi Barani kote raia jumla wamekata tamaa na maisha yao kutokana na kudidimia kwenye lindi la uchochole  hali iliyosababishwa na   sera mbaya za kiuchumi za mfumo wa kikoloni wa kirasilimali zinazobebwa na watawala wakisekula wakibebari. Kwani mashirika haya mawili na mengineyo ambayo hatuku yataja ikiwemo pamoja na Umoja wa Afrika (Africa Union) iliyobuniwa mwaka 1963 yote ni mashirika ya kiwakala yanayodhibitiwa na wakoloni nyuma ya pazia. Lakini mbele ya pazia yanajidhihirisha kuwa ni mashirika huru na yaliyo na ari na uchu wa kunyanyua hali na kutoa suluhisho kwa matatizo ya Afrika! La hasha yote yanaendeshwa na vibaraka ambao ni watumwa watiifu kwa wakoloni wa magharibi na ambao daima wako tayari kuwafanya mtaji na kuwatoa kafara wenzao wa Afrika ili kuwaridhisha mabwana zao wakoloni waliowapa madaraka hususan Uingereza, Marekani, Ufaransa, Ujerumani n.k.

Kwa kifupi hii ndiyo hali ilivyo:

Kwanza, mataifa wanachama ya Kiafrika yanayomiliki asilimia kubwa ya hisa (nguvu ya upigaji kura) ndani ya AfDB ni 1.Nigeria (Kibaraka wa Muingereza) –asilimia 8.638, 2.Misri (Kibaraka wa Muamerika) –asilimia 5.697 na 3.Afrika Kusini (Kibaraka wa Muingereza) – asilimia 5.122 kisha ndiyo mataifa mengine kutoka Afrika.

Pili, mataifa wanachama ya nje ya Afrika yanayomiliki asilimia kubwa ya hisa (nguvu ya upigaji kura) ndani ya AfDB ni 1.Amerika –asilimia 6.147, 2.Japan (Kibaraka wa Amerika)-asilimia 5.562 na 3.Ujerumani –asilimia 4.213, 4.Canada-asilimia 3.911 na 5.Ufaransa –asilimia 3.806 kisha ndiyo mataifa mengine kutoka nje ya Afrika.

Tatu, Kati ya nchi 4 wanachama wa AfDB na ambao pia ni wanachama wa Africa50 kutoka Afrika na ambao ni katika mataifa kumi (10) wanaomiliki uchumi mkubwa (GDP) Afrika ni 1.Nigeria –bilioni $ 375.771, 3.Misri –bilioni $235.369, 6.Morocco –bilioni $109.139 na 9.Kenya –bilioni $74.938.

Licha ya mataifa hayo kuwa na rasilimali za kutosha lakini la kushangaza ni  kuwa raia wa mataifa hayo wamezama ndani ya umasikini. Kwa mfano, inaripotiwa kwa sasa kuwa  Nigeria imeipita India na hivi sasa hiyo ndiyo inayoongoza kuwa na watu wengi masikini duniani! Hali hiyo ni sawia na mataifa yote ya barani Afrika ima ni katika wanachama wa AfDB, Africa50 au la!

Licha ya mataifa haya ya Afrika kuwa yameruzukiwa na rasilimali nyingi bado yanaghubikwa na na umasikini wa kupindukia. Tatizo ni kuwa uongozi wa mataifa haya upo mikononi mwa vibaraka wa wakoloni ambao wanatekeleza itikadi ya usekula na mfumo wa kirasilimali ambao ndio vyanzo vya utumwa na kudidimia kwa bara hili ima katika vita au umasikini wa kupindukia mfano Sudan Kusini, Congo n.k. Kubakia kwao mamlakani ndio kuendelea kwa sera potofu za kiuchumi zinazotilia maanani ukuwaji wa uchumi hewa kupitia uzalishaji wa taifa (GDP) lakini hawajali kuhusu usambazaji wa utajiri kwa raia jumla bali wanawatwii na kuwanyenyekea warasilimali wenye kumiliki mitaji kwa sura ya ‘wawekezaji’.

Suluhisho msingi ni kwa Bara la Afrika jumla kuukumbatia mwito wa mabadiliko ya kimsingi nao ni mwito wa kuikumbatia itikadi ya Uislamu na mfumo wake. Uislamu unatoka kwa Muumba wa wanadamu kinyume na itikadi ya kisekula inayotoka kwa akili finyu za wanadamu wachache wenye nguvu na waliojitwika mamlaka ya kupangilia maisha jumla. Mwito huu ni wa kulingania kurudi tena kwa Khilafa kwa njia ya Utume. Kupitia kurudi kwa Khilafa ndipo Afrika itaweza kuwafurusha wakoloni wamagharibi pamoja na mfumo wao wakisekula wakirasilimali. Hapo ndipo itaweza kuwa huru kivitendo na hatimaye kuweza kujitawala na kusimamia rasilimali zake kwa manufaa ya raia wake pasi na msukumo kutoka kwa wakoloni ambao hivi leo wanazipora mali za Afrika kwa mkono wa kulia na kisha kuwakopesha mikopo yenye madeni yasiyoweza kulipika kwa mkono wa kushoto ili Afrika ibakie kuwa watumwa kwa wamagharibi na hivi sasa China nayo imeanza kutekeleza sera hiyo hiyo kama wanavyofanya wakoloni wamagharibi.

Imeandikwa kwa Ajili ya Tovuti ya Radio Rahma

Ali Nassoro Ali

Mwanachama Katika Afisi ya Habari ya Hizb ut Tahrir Kenya

Makala Na.3 Tarehe: Ijumaa, 7 Dhul-Qaada 1439 | 2018/07/20

  1. https://www.afdb.org/en/documents/document/afdb-statement-of-voting-powers-as-of-31-may-2018-102674/
  2. https://answersafrica.com/largest-economies-africa.html
  3. http://databank.worldbank.org/data/download/GDP.csv
  4. https://www.theguardian.com/global-development/2018/jul/16/oil-rich-nigeria-outstrips-india-most-people-in-poverty