Bid’a ni Nini?

Katika masuala ambayo Waislamu wameyageuza kuwa ni ya kiuhasama baina yao ni suala linaloitwa Bid’a (Uzushi). Kwa muda mrefu kumekuweko na mijadala mikubwa baina ya wanavyuoni sio katika suala la ufahamu wa neno Bid’a tu, bali hata katika maudhui yanayotajwa kuwa ni bid’a. Kwa mfano, suala maarufu katika mjadala huu ni Maulidi, dua ya pamoja baada ya swala za faradhi, Qunuti katika swala ya Alfajiri na mengineo mengi yaliyowekea mijadala. Kwenye makala hii sitaki kuingia masuala haya yanayozungumziwa katika bid’a bali nataka nifafanue ufahamu wa bidaa yenyewe nikiamini kuwa huenda ikawa ni ukumbusho kwa mwenye moyo na masikio ya kusikia.

Bid’a Maana ya Kilugha na ya Kisheria:

Tamko hili ni la kiarabu hivyo ni muhimu kuliangalia katika upande wa kilugha. Kwenye kamusi za lugha ya kiarabu tamko hili limefasiriwa kwa maana mamoja licha ya kutafautika tu kiibara lakini maelezo yote hayo yanalenga tafsiri moja. Napenda nitaje tafsiri ya Bid’a kimukhtasari nayo ni kama vile alivyofasiri Abu Hayyan katika Al-Baharil Muhiit:

البدعة: ما اخترع مما لم يكن موجوداً

Bid’a: ni kuja na jambo jipya ambalo halikuweko.

Maana haya ya kilugha yamepatikana katika Quran Tukufu tutaje tu aya mbili

بَدِيعُ ٱلسَّمَٰوَٰتِ وَٱلأَرْضِ وَإِذَا قَضَىٰ أَمْراً فَإِنَّمَا يَقُولُ لَهُ كُنْ فَيَكُونُ 

Sheikh Abdalla Al-Farisy, amelifasiri neno ‘badii’ (بَدِيعُ) muumbaji pasina na ruwaza yaani mfano. Hivyo akaifasiri aya hiyo hivi: Yeye (MwenyeziMungu) ni Muumbaji wa mbingu na ardhi pasina na ruwaza. Kwa maana kwamba MwenyeziMungu kabla ya kuumba Mbingu na Ardhi ni kuwa hazikuweko hiyo Yeye (SWT) ndiye aliyeziumba hakuna mwengine aliyeziumba kabla yake.

Katika sura ya Al-ahqaaf Aya 9 MwenyeziMungu SWT akasema:

(قُلْ مَا كُنتُ بِدْعًا مِنَ الرُسُلِ)

Sema: “Mimi sio kiroja (Mpya) katika Mitume. [الأحقاف: 9]

MwenyeziMungu katika Ayah hii anamwambia Mtume wake aseme kuwaambia Maqureishi kuwa yeye Mtume Muhammad sio mtume wa kwanza kutumilizwa kwa watu bali walitumilizwa wengi miongoni mwa manabii na mitume kabla yake.

Na imekuja katika Lisanil –Arabi ikieleza tamko la Mubtadii’ (المبتدع)

الّذي يأتي أمراً على شبهٍ لم يكن

Mtu anayekuja na jambo halikuweko nyuma yake na mfano yake.

Haya ndio maana ya kilugha nayo ni kama tulivyotaja hapo nyuma kwamba ni kuja ama kufanya jambo jipya ambalo halikuweko nyuma. Nukta muhimu ni kwamba hakuna tofauti baina ya wanavyuoni wa kilugha katika kulifasiri neno hili.

Tukija kwenye maana ya kisheria na hapa ndio ni muhimu sana kwani kuna tofauti ya Wanavyuoni katika kueleza Bid’a kisheria. Pamoja na kwamba kuna maelezo ambayo yanakurubia kukubalika na wengi ya wanavyuoni nayo ni kama alivyoeleza Imam Shaatiiby katika kitabu chake cha Al Muwafaqat fii Usul Shariah

طريقة في الدين مخترع تضاهي الشريعة

Njia katika Dini iliozushwa linaloshabihiana na sheria (Lakini ikawa inagongana nayo)

Sheikh Ataa Bin Khalil Abu Rashta akaileza Bid’a kwa kusema:

البدعة هي مخالفة أمر الشارع الذي وردت له كيفية أداء… وهذا المعنى هو مدلول الحديث: «وَمَنْ عَمِلَ عَمَلًا لَيْسَ عَلَيْهِ أَمْرُنَا فَهُوَ رَدٌّ» [البخاري ومسلم]. فإذا فعل الرسول ﷺ فعلاً يبين فيه كيفية أداء أمر في الكتاب أو السنة ثم أديت أنت ذلك الأمر على خلاف فعل الرسول ﷺ، فتكون قد أتيت ببدعة وهي ضلالة وفيها إثم كبير

“Bid’a ni kuhalifu amri ya kisheria ambayo imeelezwa njia yake ya uitekelezaji na maana haya yapo kwenye ufahamu unaopatikana kwenye hadithi ya Bwana Mtume SAAW pale aliposema: Na yeyote afanyaye amali ambayo sio katika jambo letu basi ni lenye kurudishwa. Hivyo ikipatikana kuwa Mtume SAAW alifanya kitendo cha kisheria ambacho ndani yake kuna njia ya utekelezaji wa kitendo hicho iliotokamana na Quran na Sunna kisha mtu akakifanya kitendo hicho kinyume na jinsi alivyokifanya Mtume SAAW yaani akakifanya kwa njia inayogongana na ile ya Mtume SAAW basi hapo mtu huyo huambiwa amefanya bid’a na huandikiwa dhambi kwani amefanya upotevu.”

Kulingana na maelezo ya kuiarifisha Bid’a kisheria inamaaniisha kwamba mzushi ni Muislamu yeyote atakayetekeleza amri ya Kiislamu kwa njia inayokwenda kinyume na ile njia iliopatikana kisheria ya utekelezaji. Na hapa ndio inakuja ile hadithi ya bwana Mtume SAAW = Kila bid’a ni upotefu. Na hapa kuna nukta muhimu nayo ni kwamba hadithi inazungumza bidaa zote kwa maana ya kisheria wala sio maana ya kilugha.

Tukiangalia fahamu za wanavyuoni kuhusu Bid’a tutaona kuwa kuna ikhitilafu kubwa kati yao kwenye maana ya kisheria ya neno Bid’a kisheria wala sio katika upande wa maana ya kilugha. Na hapa naweka vipengele msingi vinavyotumika katika ikhtilafu juu ya suala hili:

Kauli ya Imam Shafii kuwa bidaa ni sampuli mbili: Amepokea Abu Nuai’m katika Hilyah kutoka kwa Imam Shafii Rehema za MwenyeziMungu ziwe juu yake.

البدعة بدعتان: بدعة محمودة، وبدعة مذمومة، فما وافق السنة فهو محمود، وما خالف السنة فهو مذموم

Bid’a ni aina mbili kuna nzuri iliosifiwa (Mahmudah) na bid’a mbaya iliokemewa (Madh-mumah). Bid’a itakayoafiki Sunnah itakuwa nzuri na itakayokhalifu Sunnah ndio yenye kukemewa. Kauli hii inatajwa kuwa Imam aliichukua kutokana na ufahamu wa athari ya Umar Bin Khattab RA

(نعمت البدعة هذه)

Bid’a nzuri hii ilioje (kitendo cha kuwakusanya Waislamu waswali taraweh kwa imam mmoja).

Na kuna wanavyuoni wengine wakubwa kama vile Imam Nawawiy wamekwenda kuigawanya Bid’a kwa vigawanyo takriban vitano.

Tofauti ya Kiufahamu wa hadithi ya Bwana Mtume SAAW:

كل بدعة ضلالة و كل ضلالة في النار

Kila Bid’a ni upotevu na kila upotevu ni motoni

Kuna baadhi ya wanavyuoni wanaona kuwa chochote kilichozushwa katika dini basi ni bid’a. Wanajenga msimamo wao huu kwa hoja ya kilugha kwani tamko la kullu (كل) ni lenye kukusanya kila jambo la kuzushwa ambalo mtume SAAW hakulifanya. Wengine miongoni mwa wanavyuoni ni wale waliosema kuwa sio kila jambo lililo zushwa ni bidaa bali ni mpaka liwe limekinzana na sheria na wala sio kwamba mujarad tu Mtume hakulifanya basi ni bid’a. Kwa wao wakasema kuwa bid’a ni aina mbili: nzuri (Hasana) na Mbovu (Sayiia). Rai yao hii wakaitilia mkazo kwa kusema tamko la Kullu hata kama hujumuisha lakini imekuja takhsisi katika baadhi ya dalili kwa mfano kauli yake SAAW

كل عين زانية

Kila jicho ni lenye kuzini

Wakasema hapa tamko kullu haijumuishi macho ya manabii na mitume kwani zipo aya na hadithi zinazoashiria kuhifadhika kwao na maasia ikiwemo zinaa. Wakaendelea kusema kuwa lau jambo litazushwa lakini likawa halikinzani na sheria basi hilo sio bid’a bali litaitwa Sunnah hasanah- Sunnah njema. Wanatilia nguvu msimamo huu kwa hadithi aliyoipokea Imam Muslim katika Sahih yake kuwa Bwana Mtume SAAW alisema:

مَنْ سَنَّ فِي الْإِسْلَامِ سُنَّةً حَسَنَةً، فَعُمِلَ بِهَا بَعْدَهُ، كُتِبَ لَهُ مِثْلُ أَجْرِ مَنْ عَمِلَ بِهَا

Wakasema tamko la sanna hapa humaanisha kuanzisha na wala sio kuhuisha kama wanavyosema wanavyuoni wengine. Hivyo kwa mujibu wa wanavyuoni wanaona kuwa sio kila bidaa ni uzushi wanaifahamu hadithi kama: ‘Mwenye kuanzisha katika Uislamu jambo jema baada yake watu wakafuata kufanya jambo hilo basi hulipwa malipo kama mfano wa malipo ya yule aliyefanya jambo hilo.

Ama waliosema kuwa tamko la Sanna hapa ni maana ya kuhuisha ataifasiri hadithi hii: Mwenye kuhuisha Sunnah yaani jambo jema watu baadaye wakafanya alilolihuisha basi ana malipo kama malipo ya yule atakayelifanya.

Hivyo ndivyo vipengele msingi vilivyosababisha kuwepo kwa mjadala wa Bid’a. Kuna mambo kadhaa hapa bado nahisi hayaja kuwa wazi kwa pande zote mbili juu ya suala la Bid’a. Nami napenda kusaidia kuyabainisha ili huenda suala hili likafahamika zaidi.

Kwanza: Kuna maamrisho ya kisheria ambayo yamedokezwa ndani yake njia ya kuyatekeleza kama vile Swala na nguzo zake zote ambapo mtu hulazimika kuswali kwa njia maalumu aliyoifanya Mtume SAAW. Hivyo lau mtu ataswali swala ya faradhi akasujudu mara tatu kimakusudi badali ya kusujudu mara mbili kama alivyokuwa akiswali Mtume SAAW basi ataitwa mzushi na kitendo chake hicho kitaitwa bid’a.

Pili: Yapo matendo ya kisheria ambayo ndani yake haikupatikani ujinsia wa kuyatekeleza bali kumepatikana tu masharti na nguzo ya utekelezaji ambayo ni lazima yatimizwe ndio yakamilike kisheria. Mfano ni suala la kuoa, tumehimizwa wanaume wa Kiislamu kuoa wanawake wenye dini. SAAW alisema

فَاظْفَرْ بِذَاتِ الدِّينِ تَرِبَتْ يَدَاكَ [البخاري]

Takeni kufaulu kwa kuchagua wanawake wenye Dini ndio mtapata kufaulu.

Pamoja na kwamba Mtume SAAW alihimiza watu kuoa wanawake wenye dini lakini hakuja na njia maalumu ya uchumbiaji wa mwanamke mwenye dini. Ndio, sheria hata kama imeeleza hukumu za kuchumbia lakini hakuna utaratibu uliobainishwa kisheria wa utekelezi wa uchumba yaani jinsi gani ya kuendeleza mchakato wa kuchumbia mwanamke mwenye dini. Je, kwa mfano kuchumbia mwanamke mwenye dini ni kusimama mbele yake huku ukimsomea ayatul kursiy kisha labda ukasonga hatua nyengine mbele na kusoma suratul Falaq na Nass kisha ukapiga hatua nyengine ukipiga Bismilahi na mwishowe kuinua mkono wako wa kulia na kuanza kuchumbia. Laa yote hayo hayakuja kama njia ya kumchumbia mwanamke mwenye dini. Kwa maana hii, mwanaume atakayeoa mwanamke asiye na dini haambiwi kuwa amefanya bid’a bali hapo itaangaliwa hukumu ya kisheria inayofungamana na kuoa mwanamke aso na dini. Ama mtu akioa pasina masharti ya ndoa basi kitendo chake hicho huitwa batili kwa mfano ndoa iso kuwa na walii kisheria haiambiwi ni bidaa bali husemwa sio sahihi.

Tatu: Kukhalifu amri yoyote ya kisheria ambayo sheria haikuweka njia ya jinsi gani ya kuitekeleza huingizwa katika moja wapo ya zile hukumu tano za kisheria zinazojulikana kwa wana usuli kama Hukumu za Taklif nayo ni ima itakuwa ni kufanya haramu au jambo la makuruhu wala haisemwi kuwa ni bidaa.

Nne: Matendo yaliyofanywa na maswahaba ambayo Mtume SAAW hakuyafanya yeye lakini akayakiri hayaitwi kisheria kuwa ni bid’a. Mathalan kitendo cha swahaba Bilal (RA) cha kuswali rakaa mbili za kila anapomaliza kutawadha. Kitendo cha mmoja wa Ma-answar aliyekuwa akiwaswalishwa watu katika wa Msikiti wa Qubaa cha kusoma suratul Ikhlas katika kila rakaa kisha ndipo kusoma sura nyengine. Ndio kitendo hiki Mtume SAAW hakukifanya lakini alipoletewa mashtaka na maamuma wa msikiti huo akamwita Imam na kumuuliza kwa nini anafanya hivyo basi yule imam akajibu naipenda suratul Ikhlas basi Mtume SAAW akamwambia kama

((حبُّك إياها أدخلك الجنةَ))

Kuipenda kwako kutakuingiza peponi.

Kitendo hiki hakiitwi bid’a kwani Mtume kukiri kwake hilo ni kuonesha fadhila za suratul Ikhlas.

Mwenye kuzusha katika jambo letu hili (Dini) ambalo halitokamani na hilo (Dini yetu) basi ni lenya kukataliwa.

Kwa haya ni muhimu kuelewa kwamba hata wanavyuoni walioigawa bid’a kama Imam Shafii, Imam Nawawi na wengineo sio upande wa kisheria bali ni upande wa kilugha. Na hili linajengeka kihoja kutokamana na utaratibu wa kilugha kwenye hadithi hasa tukizingatia ibara ya

كل بدعة

Mtume SAAW katika hadithi hii hakuleta jina la Bid’a kwa sifa ya kiume ‘Mudhakkar’ yaani hakusema كل بدع  badali yake alitumia jina hilo kwa sifa ya kike. Hapa kuna uzindushi muhimu wa kilugha ambapo nahisi lau kungekuwa ni jitihada za kuelewa lugha ya Kiarabu labda suala la Bid’a lisingejengewa mijadala. Katika kanuni za lugha ya kiarabu jina lenye sifa ya kiume lina nguvu zaidi kuliko jina la sifa ya kike na ndio asili. Na hii ndio maana dhamiri ya kiume kilugha hujumuisha wanaume na wanawake ilhali dhamiri ya kike haiwezi kujumuisha jinsia zote bali ni kwa wanawake tu. Kuletwa jina la kike بدعة ni kumaanisha sio jina tu hivihivi bali linabeba sifa nyengine ya ziada nayo ni uzushi unaokwenda kinyume na sheria. Hivyo Bid’a inabakia kuwa ni jambo lililozushwa likawa na sifa ya kugongana na sheria.

Ama hoja ya Hadithi tuliotaja inayotumiwa kama ushahidi wa kuigawanya bid’a sioni kuwa ni hoja yenye nguvu. Ama hadithi isemayo:

مَنْ سَنَّ فِي الْإِسْلَامِ سُنَّةً حَسَنَةً، فَعُمِلَ بِهَا بَعْدَهُ

Hii hadithi ni sahihi ameipokea Imam Muslim kutoka kwa Jarir bin Abdillah lakini kulingana na maudhui ya hadithi hii utakuta neno sanna linabeba maana ya kuanza jambo ambalo tayari lajulikana katika dini wala sio kuja na jambo jipya. Na haya yako wazi ukifuatilia hadithi kwa ukamilifu wake:

  جَاءَ نَاسٌ مِنَ الْأَعْرَابِ إِلَى رَسُولِ اللهِ ﷺ عَلَيْهِمِ الصُّوفُ فَرَأَى سُوءَ حَالِهِمْ قَدْ أَصَابَتْهُمْ حَاجَةٌ، فَحَثَّ النَّاسَ عَلَى الصَّدَقَةِ، فَأَبْطَئُوا عَنْهُ حَتَّى رُئِيَ ذَلِكَ فِي وَجْهِهِ. قَالَ: ثُمَّ إِنَّ رَجُلًا مِنَ الْأَنْصَارِ جَاءَ بِصُرَّةٍ مِنْ وَرِقٍ، ثُمَّ جَاءَ آخَرُ، ثُمَّ تَتَابَعُوا حَتَّى عُرِفَ السُّرُورُ فِي وَجْهِهِ، فَقَالَ رَسُولُ اللهِ ﷺ: «مَنْ سَنَّ فِي الْإِسْلَامِ سُنَّةً حَسَنَةً، فَعُمِلَ بِهَا بَعْدَهُ، كُتِبَ لَهُ مِثْلُ أَجْرِ مَنْ عَمِلَ بِهَا، وَلَا يَنْقُصُ مِنْ أُجُورِهِمْ شَيْءٌ، وَمَنْ سَنَّ فِي الْإِسْلَامِ سُنَّةً سَيِّئَةً، فَعُمِلَ بِهَا بَعْدَهُ، كُتِبَ عَلَيْهِ مِثْلُ وِزْرِ مَنْ عَمِلَ بِهَا، وَلَا يَنْقُصُ مِنْ أَوْزَارِهِمْ شَيْءٌ».

Watu kutoka ubeduini walikuja kwa Mtume SAAW wana nguo za sufi Mtume SAAW akaiona ile hali yao ni watu wenye kuhitaji msaada. Akawahimiza maswahaba zake kuwapa swadaqa. Wakawa wanasitasita kutoa hadi Mtume SAAW akakasirika usoni mwake. Akasema Jarir: Kisha jamaa mmoja wa Kianswari akaja na kitambaa cha pesa kisha akaja mwengine na chengine kisha watu nao wakafuata hivyo hadi Mtume SAAW uso wake ukawa umejeaa bashasha. Akasema Mtume SAAW kwamba mwenye kuanza jambo la kheri katika Uislamu na watu wakamuiga basi huandikiwa ujira wa kila aliyemfuata kufanya amali hiyo njema na wala ujira wao nao haupungui chochote. Na atakayeanza kufanya jambo ovu na kufuatwa na watu nyuma yake basi ana mzigo wa dhambi la kila atakayefanya na wala pia hakupungui chochote katika madhambi yao. Kwa hivyo lililo wazi hapa ni suala la utoaji wa sadaka nalo sio jambo jipya katika kuhimizwa kwake na Uislamu.

Ama hoja ya kuwa kuna takhsisi kuhusishwa katika tamko la Kullu hivyo ni ushahidi wa kwamba sio kila bidaa imekashifiwa, pia hoja hii ingesimama kuwa na nguvu lau hiyo takhsisi ya bidaa kungekuwa na dalili ya kisheria ya kukhusisha yaani kupatikane dalili iliohusisha bidaa fulani kwamba sio upotefu.

Ni muhimu kuelewa kuwa kitendo chochote ambacho hakikhalifiani na Uislamu huingia katika mlango wa Mubah hivyo na mlango huu umeelezwa kindani na wana usuli.

Kwa kifupi twasema kuwa ili jambo kisheria liitwe ni Bid’a lazima liwe limekusanya sharti tatu nazo-

  • Liwe limezushwa yaani ni jipya
  • Liwe limezushwa katika sheria za Dini
  • Liwe katika kuzushwa kwake limepingana na sheria za Dini

Masharti yanatokamana na ile hadithi ya bwana Mtume SAAW

من أحدث في أمرنا هذا ما ليس منه فهو رد

Atakayezusha katika jambo letu hili (Dini) lisilitokamana nalo basi sio lenya kukubalika

Mwisho twasema kwamba kulingana na hadithi Sahih za Bwana Mtume SAAW Bid’a ni moja wapo ya maasia makubwa sana kwa Uislamu. Hata hivyo, ni muhimu kufahamu kuwa kuyaita bid’a masuala yanayo patikana ndani yake ikhitilafu ni kosa kubwa kwani mas-ala hayo ni ya kijitihadi hivyo yanatoa nafasi ya watu kuwa na rai tofauti. Kinachohitajika ni kuheshima rai yoyote ile ya Kiislamu almurad imevuliwa kutokamana na machimbuko ya kisheria katika Uislamu wala sio mengineyo.

Shabani Mwalimu

Mwakilishi kwa Vyombo vya Habari wa Hizb ut Tahrir Kenya

Comments are closed.