Jumla

Demokrasia Nchini Kenya Ni Mvutano Kati ya Amerika na Uingereza ilhali Chaguzi Ni Njia Tu ya Kufikia Utawala na Kuthibitisha Uhalali Wake

Kusambaza ni Kuunusuru Uislamu

Kenya kama ilivyo nchi nyengine yoyote ya kidemokrasia ulimwenguni huchukua nidhamu yake ya utawala ya demokrasia kutoka kwa mfumo batili wa kirasilimali. Urasilimali ni mfumo ambao aqeedah yake ni ilmaniy -kutenganisha dini na serikali/maisha. Hivyo basi, huipa demokrasia kupitia wanademokrasia ukiritimba katika kudhibiti/kutunga sheria za mambo ya kimaisha kwa msingi wa akili zao finyu na kwa kipimo makhsusi cha vitendo kilicho jengwa juu ya manufaa/maslahi. Kwa hivyo, ili kuielewa hali iliyoko sasa nchini Kenya tunalazimika kuregelea historia yake, ambayo ni kuwa Kenya ni koloni ya Uingereza na mpaka leo iko chini ya mashiko yake kikamilifu. Kuthibitisha hili, tutaangazia siasa na uchumi wake ambazo ndizo nguzo kuu kulingana na mfumo wa kirasilimali ili kufafanua wamiliki wake halisi. Kenya inategemea kikamilifu makampuni ya Kiingereza kuimarisha uchumi wake, ambayo baadhi yake yakiwa ni Unilever, BAT, benki ya Standard Chartered, Safaricom, Base Titanium, Tullow, Bunson Travel Service, STA Travel Kenya, Scott Travel Group nk.   

Kisiasa; kihakika Kenya imeundwa ili kusalia kuwa koloni ya Uingereza mpaka leo, lakini; katika waraka ‘katiba’ ikatangazwa kuwa huru mnamo 1963 na kupewa mipaka yake na bendera yake ili kuwaziba macho watu kuwa iko huru. Baada ya Vita vya Pili vya Dunia Uingereza ilipata hasara nyingi na kutokana na hayo ikaunda mpango wa kupunguza matumizi yake ya kiuchumi kwa kutawala na kusimamia moja kwa moja koloni zake ili kuinua nchi yake. Katika mpango wake, iliamuliwa kuwa koloni zote za Uingereza zisimamiwe kupitia kwa vibaraka wao watiifu na Jomo Kenyatta alichaguliwa baada ya kuyeyushwa na maadili ya kimagharibi kwa muda mrefu. Kwanza alichaguliwa kama Waziri Mkuu kisha kuwa raisi wa kwanza wa Kenya. Jomo Kenyatta alichaguliwa si kwa sababu anatoka katika kabila kubwa la Wakikuyu nchini Kenya, lakini; kwa sababu ya kuwa tayari kwake kuitikia na kutenda kwa mujibu wa maagizo ya mabwana wa kikoloni wa Kiingereza na hili lilithibitishwa alipo anzisha mashambulizi makali dhidi ya Wakikuyu wenzake ambao hawaku jisalimisha chini ya utawala wake. Kwa kuwa waliuona utawala huo kuwa mabadiliko tu ya sura na rangi, lakini; sera za ubaguzi ziliendelea hususan katika kufikia afisi za juu, vyeo na ugavi wa ardhi zenye rutuba kufanywa kwa mataraji pekee, na wale walio kuwa karibu na Kenyatta, wandani wake wanaojumuisha Waingereza kwa gharama ya wenyeji maskota hadi wa leo!

Kama njia ya kuidhinisha kikamilifu utawala wa Kenyatta wenye kunyenyekea kwa Uingereza bwana mkoloni, ni wakati wa kifo chake mnamo 22 Agosti 1978 ambapo Uingereza ilimteua Bruce Roy Douglas McKenzie kuongoza matayarisho ya mazishi yake. Muundo wa mazishi ulipambwa katika hali iliyo shabihiana na mazishi ya mwenda zake Waziri Mkuu wa Uingereza Winston Churchill. Wawakilishi wakuu wa Kiingereza akiwemo mwana wa malkia Charles, mrithi wa ufalme wa Uingereza, alihudhuria mazishi yake.

Daniel Arap Moi akachaguliwa kama kibaraka mpya wa ukoloni wa Kiingereza kwa sharti kwamba aendeleza dori aliyo cheza Jomo Kenyatta. Moi aliitumikia Kenya bila ya wasiwasi wowote kwa sababu alifurahia usaidizi wa mabwana zake wa Kiingereza kwa muda wa miaka 24. Katika utawala wote wa Moi alishuhudia kuibuka kwa sura ya utawala wa Kiamerika ukipambana na utawala wa mabwana zake wa kikoloni wa Kiingereza barani Afrika, ikiwemo Kenya. 

Mnamo miaka ya thamanini Amerika ikafaulu kushawishi na kukusanya pamoja waliokuwa vibaraka wa Uingereza kama Jaramogi Oginga Odinga na mwanawe Raila Odinga ambao walikuwa wakilingania ‘demokrasia na vyama vingi’ kuandaa mapinduzi ambayo hayakufaulu, lakini; yakatoa fursa zaidi kupanua athari ya Amerika nchini Kenya. Watu walipoteza maisha katika jaribio la mapinduzi na Raila Odinga akatiwa nguvuni, kutuhumiwa kwa kosa la uhaini na kuwekwa kizuizini pasi na kuhukumiwa kwa miaka sita. Raila aliachiliwa mnamo Februari 1988 na kukamatwa tena mnamo Septemba 1988 kwa kuwa kibaraka wa Amerika kwa ‘kuunga mkono vuguvugu la kutetea demokrasia na haki za kibinadamu’. Huku Raila akiwa gerezani Amerika ilifaulu pakubwa kuathiri na kumvuta mkikuyu mkubwa, mwenye usemi katika jamii na aliyekuwa kibaraka wa Uingereza, Kenneth Matiba. Kwa hivyo Raila alipoachiliwa kutoka gerezani mnamo 12 Juni 1989, alifungwa tena mnamo 5 Julai 1990 pamoja na Kenneth Matiba na aliyekuwa Meya wa Nairobi Charles Rubia kwa kulingania mfumo wa vyama vingi na watetezi wa haki za kibinadamu. Raila hatimaye aliachiliwa huru mnamo 21 Juni 1991, na mnamo Oktoba, alikimbilia hifadhi nchini Norway kwa usaidizi wa rafiki yake na kibaraka wa shirika la ujasusi la Kiamerika FBI hali zilipoonyesha kuwa serikali ya Kenya inapanga kumuua bila ya mafanikio.

Huku Raila akiwa ng’ambo, Amerika ikafaulu kuanzisha kuundwa kwa chama cha FORD chini ya uongozi wa Jaramogi Oginga na Kenneth Matiba, ambacho baadaye kilisambaratika kutokana na kuchakachuliwa na Moi na kuzaliwa FORD-Kenya kilicho ongozwa na Jaramogi Oginga Odinga, na FORD-Asili kilicho ongozwa na Kenneth Matiba. Kenneth Matiba akafaulu kushindana dhidi ya Daniel Arap Moi katika uchaguzi wa 1992 lakini; akanyimwa ushindi kwa sababu hakuwa katika kambi ya Uingereza. Badala yake, Moi akatangazwa mshindi!  

Mnamo 1994 baada ya babake Raila kufariki FORD-Kenya ikawa chini ya uongozi wa Kijana Wamalwa kikaragosi wa Uingereza. Raila akaamua kupambana na Wamalwa kung’ang’ania uongozi wa chama na uchaguzi kukumbwa na kashfa na Raila kukihama na kujiunga na NDP kilicho undwa na Stephen Wilfred Omondi Oludhe. Raila kama kibaraka wa Amerika kutoka katika jamii ya Waluo iliyo ya tatu kwa ukubwa nchini akajaribu kugombea uraisi kwa mara ya kwanza mnamo 1997 na kuibuka wa tatu, lakini; alihifadhi kiti chake kama mbunge wa Langata. Kutokana na ushauri na baraka kutoka kwa bwana wake Amerika, Raila akaamua kumuunga mkono Moi kikaragosi wa Uingereza na hasimu wake mkuu, na kuingia katika muungano wa kisiasa kati ya chama chake, NDP na KANU kuunda kile kilichoitwa ‘KANU Mpya’ iliyopelekea Raila kuteuliwa kuwa waziri wa kawi kuanzia mnamo Juni 2001 mpaka 2002. Lengo kuu la Amerika lilikuwa kupatiliza fursa iliyo iva kwa ‘miito ya mageuzi’ nchini Kenya ili Raila aweze kumrithi Moi. Hili lilithibitishwa kwa uchaguzi uliofuatiwa wa KANU baadaye mwaka huo; Raila akachaguliwa kuwa Katibu Mkuu wa chama (akamuondoa J.J. Kamotho). 

Lakushangaza ni kuwa Amerika ilishindwa kwa ujanja na Uingereza mnamo 2002 wakati Moi alipo muidhinisha Uhuru Kenyatta mwana wa mtawala kibaraka wa kwanza wa Uingereza nchini Kenya; kuwa mgombea uraisi katika uchaguzi mkuu wa 2002. Hili lilimfanya Raila kuhama ‘KANU Mpya’ na kuasisi vuguvugu la Rainbow pamoja na wanachama wengine waasi wa KANU waliohisi chaguo la Moi kuwa baya. Kisha Raila akalibadilisha vuguvugu la Rainbow na kuunda chama cha LDP. Kisha LDP ikaungana na chama cha DP kilichoongozwa na Mwai Kibaki, NPK kilichoongozwa na Charity Ngilu na FORD-Kenya kilichoongozwa na Michael Kijana Wamalwa wakaunda muungano wa NARC ulio husisha vyama 15 vya kisiasa lakini hivi vinne vikawa ndio wahusika wakuu.    

Wakati huu Amerika ikapiga mahesabu yake kuwa kwa kuwa nchini Kenya ina Raila pekee kama kikaragosi wao muaminifu na waliosalia wote ni watiifu kwa Uingereza wanaomzunguka kibaraka wao. Walimshauri Raila kumuunga mkono Mwai Kibaki kikaragosi wa Uingereza, lakini; kwa masharti ya mkataba wa maelewano (MOU) kuwa NARC itakapo chukua uongozi, ataunda cheo cha Waziri Mkuu kwa Raila Odinga na kuteua nusu ya baraza lake la mawaziri kutoka upande wa LDP. NARC ikafika uongozini kwa ushindi mkubwa sana wa asilimia 61% dhidi ya KANU 31% hivyo basi Uhuru Kenyatta kukubali kushindwa na Mwai Kibaki kuapishwa afisini mnamo 30 Disemba 2002 kama raisi wa tatu wa Kenya. Mara moja Kibaki akakataa kuheshimu MOU na hili likamaanisha kuwa Uingereza iliishinda kwa ujanja Amerika kwa mara ya pili. Lakini; bado Raila akabakia katika serikali ya Kibaki, lakini; akipanga njama dhidi yake. Moja ya njama hizo ilikuwa ni kuanzisha kura ya maamuzi ya katiba iliyolenga kupunguza nguvu za raisi.  

Mnamo 2005, Raila akafanya kampeni dhidi ya Mwai Kibaki huku akiongoza wenzake kuasi serikali iliyo kuwa upande wa kuipigia kura ya ‘Ndio’ na Raila akilingania kura ya ‘La’. Mnamo 21 Novemba 2005, timu iliyoongozwa na Raila ikaishinda timu ya Kibaki kwa asilimia 57% na 43% mtawalia katika matokeo ya kura ya maamuzi. Hivyo basi, Amerika ikaishinda Uingereza katika kura hiyo ya maamuzi. Mwai Kibaki alisonga mbele na kumuadhibu Raila na ambaye ni tishio kwa serikali yake na maslahi ya bwana wake mkoloni. Akalifuta kazi baraza zima la mawaziri mnamo 23 Novemba 2005. Lilipoundwa upya wiki mbili baadaye, Raila na wanachama wote wa LDP waliachwa nje! Amerika ikamshauri Raila kupatiliza fursa ya kufaulu katika kampeni iliyo muwezesha kushinda kura ya maamuzi kusajili chama kipya cha upinzani, vuguvugu la chungwa ODM-Kenya; kwa kuwa chungwa ilikuwa ndiyo alama ya kura ya ‘La’ katika kura ya maamuzi ya katiba. Mnamo Agosti 2007 chama hicho kilichakachuliwa na watiifu wa Uingereza walio pelekea kukigawanya kuwa vyama viwili huku Raila akichukua ODM na Kalonzo Musyoka akichukua ODM-Kenya.

Mnamo 2007, Raila akafanya jaribio lake la pili la kugombea uchaguzi wa uraisi. Wakati huu Amerika ilikwenda katika uchaguzi mkuu huku vichwa vyao vikiwa juu kwa kuzingatia kuwa Raila alikuwa ni kiongozi wa upinzani na alikuwa ameshinda kura ya maamuzi hivi punde. Licha ya hayo, Raila alinyimwa ushindi katika uchaguzi mkuu wa 27 Disemba 2007 na Mwai Kibaki kutangazwa mshindi mnamo 30 Disemba 2007. Raila alipinga ushindi huu na kutoa wito kwa jamii ya kimataifa kuingilia kati; huku Kalonzo Musyoka kinara wa chama cha ODM-K akimkumbatia na kumuunga mkono Kibaki na moja kwa moja kuzawadiwa cheo cha Makamu wa Raisi.

Kufuatia miezi miwili ya ghasia, iliyopelekea maelfu ya watu kuuwawa, kunajisiwa, kuwa wakimbizi na uharibifu mkubwa kuonekana katika mali na uchumi kwa jumla. Makubaliano kati ya Raila na Kibaki, yalitoa mwanya wa ugavi wa mamlaka na kuundwa kwa cheo cha Waziri Mkuu, yalitiwa saini mnamo Februari 2008. Ilisimamiwa na aliyekuwa Katibu Mkuu wa UM Kofi Annan ‘kikaragosi wa Amerika ‘; yaliungwa mkono na Jendayi Frazer – Waziri Msaidizi wa Kigeni wa Masuala ya Afrika kama mpatanishi pamoja na ziara ya Condoleeza Rice mnamo 17 Februari 2007. Raila Odinga aliapishwa kama Waziri Mkuu, pamoja na ugavi wa mamlaka katika baraza la mawaziri, mnamo 17 Aprili 2008. Hii ilikuwa mara ya kwanza kwa utawala wa Amerika kuhisi kupata kitu cha kihakika katika mamlaka chini Kenya. Huku Uingereza ikitumia fursa ya hali iliyoko kumuinua Uhuru Kenyatta kwa kumchagua kuwa Naibu Waziri Mkuu na mrithi wa Mwai Kibaki katika uchaguzi mkuu ujao wa 2013.

Kama sehemu ya kuandaa mazingira muwafaka baina ya Uingereza na Amerika kulingania katiba mpya kukaibuka kwa ‘kusemekana’ kuwa ghasia zilitokana na changamoto zinazo lighubika taifa tangu uhuru, hivyo basi mageuzi msingi na vifungu vilitungwa na kura ya maamuzi kupendekezwa. Lakushangaza ni kuwa mwanzoni Uhuru mtiifu mkuu wa Uingereza wakati huo hakuwa upande wa kura ya ‘Ndio’ na pia alihofia ikiwa atashirikiana na Raila muonekano wake wa kitaifa utafinikwa na ule wa Raila ambaye ni mshindani wake mkuu katika uchaguzi mkuu ujao. Raila alikuwa akiunga mkono katiba, itakayo anzisha serikali za kaunti zinazo shabihiana na muundo wa Kiamerika na mapendekezo mengineyo kutoka kwa bwana wake Amerika ambayo yalipitishwa kupitia ziara ya Joe Biden mnamo 7 – 9 Juni 2010.

Mnamo 2010, Uingereza alimshauri ‘Uhuru’ kushikamana na kambi ya ‘Ndio’ na wao ‘Uingereza’ kuunga mkono hasimu wake mkuu ambaye sasa amegeuka kuwa rafiki William Ruto katika kambi ya ‘La’. Hivyo basi, hatimaye wangeutumia msimamo wa Ruto ambaye angeibuka kama kiongozi shupavu wa kambi ya ‘La’ na kiongozi wa chama cha URP kwa manufaa ya Uhuru Kenyatta. Kambi ya ‘Ndio’ ilishinda kwa asilimia 68.6% huku kiongozi wa kambi ya ‘La’ William Samoe Ruto (wakati huo Waziri wa Elimu) akikubali kushindwa. Hii ilithibitisha kufaulu kwa karata ya Uingereza ambayo baadaye iliitumia Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) kuwaunganisha Uhuru Kenyatta pamoja na William Samoe Ruto wanaotoka katika maeneo yaliyo na wapiga kura wengi eneo la Kati na Bonde la Ufa la Kenya kwa mwito wa kilaghai wa ‘Amani na Maridhiano’. Hivyo basi, idadi ya wapiga kura maeneo hayo ikiongezewa kutoka kwa makabila mengine yanayo egemea kwao ilikuwa ni jambo la uhakika kwao kushinda uchaguzi mkuu wa 2013, ambao daima hutegemea hadithi ya ukabila.   

Mnamo 2013, Raila alikuwa na uhakika wa kumrithi Kibaki kwa matarajio kuwa Uhuru Kenyatta na William Ruto hawatakuwa kizingiti kwake kwa cheo uraisi, lakini; kwa mara nyengine tena, Uingereza ikaishinda kwa ujanja Amerika katika siasa za urithi za Kenya koloni yake. kwa kutumia hadithi ya Mahakama ya ICC kuyaunganisha maeneo mawili haya ya Kati na Bonde la Ufa nyuma ya watu hawa wawili. Walipigia debe hadithi ya kirongo ya udharura wa amani iliyo maanisha bila ya viongozi wawili hawa kufikia ngazi ya utawala hakutakuwa na amani wala maridhiano nchini Kenya ikizingatiwa matukio ya baada ya uchaguzi wa 2007 ambayo wengi wa waathiriwa ni jamii kutoka maeneo/makabila haya. Amerika ilipogundua hili ikashindwa kwa ujanja Raila akaanzisha kampeni ya kuunda muungano wa vyama unaojulikana kama CORD. CORD ilihusisha chama cha Raila cha ODM, chama cha Wiper cha Kalonzo Musyoka (kilicho kuwa ODM-K) na chama cha Moses Wetangula cha Ford Kenya (FK) kuwania uraisi na Raila akawa mgombea na Kalonzo Musyoka kama mgombea mwenza wake. CORD ilikuwa ikikabiliana na muungano wa Jubilee (Uhuru Kenyatta – TNA), William Ruto (URP), Charity Ngilu (NARC) na Najib Balala -Republican Congress (RC)). Jaribio la tatu la Raila kugombea uraisi lilikuwa mnamo 4 Machi 2013, lakini; Uhuru Kenyatta akatangazwa mshindi mnamo 9 Machi 2013. hivyo basi, Raila akenda kotini, iliyokuwa chini ya mashiko ya Uingereza, ikahalalisha ushindi wa Uhuru Kenyatta.    

Mnamo 2017, Amerika bila ya kuwa na mtu mwengine badala katika upande wa utiifu wakaamua kwa mara ya nne mfululizo kumuunga mkono Raila kwa uchaguzi wa uraisi. Ambapo walimunnga mkono Raila kuunda muungano wa NASA. NASA ilijumuisha ODM ya Raila, chama cha Wiper cha Kalonzo Musyoka, chama cha FORD-Kenya cha Moses Wetangula, chama cha ANC cha Musalia Mudavadi, chama cha NARC cha Charity Ngilu, chama cha PPK cha Moses Akaranga, chama cha CCU cha Wavinya Ndeti, na chama cha Muungano (MP). Mgombea uraisi wa NASA akawa Raila na Kalonzo mgombea mwenza wake wakikabiliana na chama cha Jubilee kikiongozwa na Uhuru Kenyatta kama mgombea wake wa uraisi na William Ruto mgombea mwenza wake.

Baada ya uchaguzi wa mnamo 8 Agosti 2017, kwa mara nyengine tena Uhuru Kenyatta akatangazwa mshindi mnamo 11 Agosti 2017. Raila kwa mara nyengine akapinga matokeo katika Mahakama ya Upeo ya Kenya na mara hii ushindi wa Uhuru Kenyatta ukabatilishwa mnamo 1 Septemba 2017. Hii ilimpatia Raila fursa ya kugombea kwa mara ya tano kushiriki marudio ya uchaguzi mnamo 26 Oktoba, 2017. Badala yake akajiondoa akitaja kuwa sababu zilizo pelekea kubatilishwa kwa uchaguzi bado hazijatatuliwa. Kwa hivyo Raila akaitisha mkutano bustani ya Uhuru Park Nairobi mnamo 25 Oktoba 2017 na kusema NASA imebadilishwa na kuwa ‘Vuguvugu la Kitaifa la Uasi’ kwa lengo la kushinikiza mageuzi nchini Kenya

Huo hapo juu ni ufafanuzi wa kina, lakini; tunaufupisha kuwa ni ‘mvutano kati ya Marekani na Uingereza kupitia vikaragosi wao nchini Kenya’. Mwishowe raia wakiwemo ‘wasomi na wasiokuwa wasomi’ ni sehemu tu ya kitendawili cha kisiasa. Ni hadaa tu ya ‘wahusika wakuu au mibabe ya kikabila’ wanao pigania maslahi yao, lakini; damu na jasho lao ndizo hutumika kama ngazi za kuwapandisha ‘Vibaraka’ mamlakani na hususan kushiriki kwao katika chaguzi ni kuhalalisha na kuidhinisha serikali ambazo ziko pale kuhudumia wamagharibi na sio wao. Kila damu inapomwagwa zaidi ndipo nafasi kubwa ya mazungumzo inapatikana mbele ya ‘meza ya mamlaka’ katika kila upande wa kisiasa.Muda uliobakia wa Marekani ni sasa kwa sababu hatima yao bila Raila ni giza kwao.

Enyi Waislamu na Wanadamu ulimwenguni kote epukeni demokrasia, inaleta maangamivu kwa kila inapopitia na kwa kila anayeikumbatia.

Ali Nassoro

Mwanachama wa Hizb ut Tahrir Kenya