Ameer Suali na Jawabu

Hadith Juu ya Kugawanyika kwa Ummah

Kusambaza ni Kuunusuru Uislamu

Jibu la Swali

Kwa: Muhsin Al-I’thamat

Swali

Bismillah Ar-Rahman Ar-Raheem

Amiri wetu, Allah akuhifadhi, Assalam Alaikum wa Rahmatullah wa Barakatuhu. Nimetumia juhudi zangu nyingi kutafuta hadith juu ya kugawanyika kwa Umma katika riwaya yake ya pili inayo taja “yote yatakuwa Peponi isipokuwa kundi moja“; nimeisoma hadith hii iliyo sahihishwa na Al-Hakim kuwa daraja ya Ghareeb, na Al-Maqdasi asema kuihusu kwamba ni sahih zaidi kushinda riwaya ya “yote yatakuwa Motoni isipokuwa kundi moja” ambayo iko katika daraja ya Mash’hoor. Ikiwa una wasaa tafadhali niongoze, na Allah aibariki elimu yako na wakati wako. 

Amiri wetu, kuhusiana na maneno “imesahihishwa na Al-Hakim”, imejitokeza katika kitabu Kashf Al-Kahfa’ cha Al-Ailouni ukurasa wa 150 yanayo someka “Imesimuliwa na Ash-Sha’rani katika Al-Mizan kutoka katika hadith ya Ibn An-Najjar. Imesahihishwa na Al-Hakim kuwa Ghareeb katika maelezo, nayo ni:

ستفترق أمتي على نيِّف وسبعين فرقة، كلها في الجنة إلا واحدة

“Umma wangu utagawanyika zaidi ya makundi sabiini, yote yatakuwa Peponi isipo kuwa moja”.

Katika riwaya ya Ad-Dailamy: “الهالك منها واحدة” “Miongoni mwayo moja litaangamia.” Wanazuoni wamesema: Hao ni wapagani (Zanadiqa). Najua kuwa maneno haya ya ziada “Az-Zanadiqa” yameongezwa kwa juu (Mawdhu’), lakini kile ninachotaka kujua ni wapi Al-Hakim alisahihisha riwaya hii bila ya nyongeza hii ya ziada ya “Az-Zanadiqa”?

Jibu

Wa Alaikum Assalam Wa Rahmatullah Wa Barakatuh,

Kwanza: Ama kuhusu swali lako kuhusu kugawanyika kwa Umma, hadith zote zinazo simulia juu ya kadhia hii zinagawanyika vigawanyo vitatu:

1- Ile inayo taja kugawanyika kwa Umma makundi sabiini na tatu.

2- Ile inayo taja makundi sabiini na tatu pamoja na ziada ya maneno; “yote yatakuwa Motoni isipokuwa kundi moja”

3- Ile inayo taja makundi sabiini na tatu pamoja na ziada ya; “yote yatakuwa Peponi isipo kuwa kundi moja

Ama kuhusu kigawanyo cha kwanza, yaani, hadith isiyokuwa na ziada, ni Sahih, na wala sijaona yeyote aliye iorodhesha kama Dhaifu kwa kadri ya elimu yangu:

Katika Sunan ya Abu Daud kutoka kwa Abu Huraira asema: kwamba Mtume wa Allah (saw) amesema:

«افْتَرَقَتْ الْيَهُودُ عَلَى إِحْدَى أَوْ ثِنْتَيْنِ وَسَبْعِينَ فِرْقَةً وَتَفَرَّقَتْ النَّصَارَى عَلَى إِحْدَى أَوْ ثِنْتَيْنِ وَسَبْعِينَ فِرْقَةً وَتَفْتَرِقُ أُمَّتِي عَلَى ثَلَاثٍ وَسَبْعِينَ فِرْقَةً»

“Mayahudi wamegawanyika makundi sabiini na moja au sabiini na mbili na Manaswara wamegawanyika makundi sabiini na moja au sabiini na mbili. Umma wangu utagawanyika makundi sabiini na tatu.”

Katika Sunan ya Tirmithi kutoka kwa Abu Huraira asema kwamba Mtume wa Allah (saw):

«تَفَرَّقَتْ الْيَهُودُ عَلَى إِحْدَى وَسَبْعِينَ أَوْ اثْنَتَيْنِ وَسَبْعِينَ فِرْقَةً وَالنَّصَارَى مِثْلَ ذَلِكَ وَتَفْتَرِقُ أُمَّتِي عَلَى ثَلَاثٍ وَسَبْعِينَ فِرْقَةً»

“Mayahudi waligawanyika makundi sabiini na moja au sabiini na mbili na Manaswara vile vile. Umma wangu utagawanyika makundi sabiini na tatu.”

Katika Al-Bab kutoka kwa Saad na Abdullah bin Amr na Auf bin Malik kwamba Abu Isa asema: Hadith ya Abu Huraira ni daraja ya Hasan Sahih.

Katika Al-Mustadrak ya Al-Hakim kutoka kwa Abu Huraira kwamba amesema, Mtume wa Allah (saw) amesema:

«افترقت اليهود على إحدى أو اثنتين وسبعين فرقة، وافترقت النصارى على إحدى أو اثنتين وسبعين فرقة، وتفترق أمتي على ثلاث وسبعين فرقة»

“Mayahudi wamegawanyika makundi sabiini na moja au sabiini na mbili na Manaswara wamegawanyika makundi sabiini na moja au sabiini na mbili. Umma wangu utagawanyika makundi sabiini na tatu.”

Amesema kuwa Hadith hii ni Sahih kwa vigezo vya (Imam) Muslim, na wala hawakuivua, na ina mashahidi (yaani, imesimuliwa na Maswahaba wengine)… Adh-Dhahabi ameafikiana naye.

Ama kuhusu kigawanyo cha pili chenye ziada ya “yote yatakuwa Motoni isipokuwa kundi moja”, riwaya nyingi zathibitisha kuwa Hadith hii ni daraja ya Sahih na Hasan:

Tirmidhi asimulia katika Sunan yake: Mahmoud bin Ghailan ametwambia, Abu Daud Al-Hafri ametwambia kwamba Sufyan al-Thawri kutoka Abd Al-Rahman bin Ziyad Al-Afriqi kutoka kwa Abd Allah bin Yazeed kutoka kwa Abd Allah bin ‘Amr kwamba amesema: Mtume wa Allah (saw) amesema:

«… وَإِنَّ بَنِي إِسْرَائِيلَ تَفَرَّقَتْ عَلَى ثِنْتَيْنِ وَسَبْعِينَ مِلَّةً وَتَفْتَرِقُ أُمَّتِي عَلَى ثَلَاثٍ وَسَبْعِينَ مِلَّةً كُلُّهُمْ فِي النَّارِ إِلَّا مِلَّةً وَاحِدَةً قَالُوا وَمَنْ هِيَ يَا رَسُولَ اللَّهِ قَالَ مَا أَنَا عَلَيْهِ وَأَصْحَابِي»

“Na hakika wana wa Israel waligawanyika makundi sabiini na mbili na Umma wangu utagawanyika makundi sabiini na tatu; yote yatakuwa Motoni isipo kuwa kundi moja. Wakauliza: ‘na ni lipi hilo, ewe Mtume wa Allah?’ akasema: ‘lile linao fuata yale ninayo fuata mimi na Maswahaba zangu’ Abu Isa asema daraja ya Hadith hii ni Hasan na Ghareeb.

Ibn Majah amevua katika Sunan yake: Amr bin Othman bin Said bin Katheer bin Dinar Al-Homsi ametwambia, Abad bin Yusuf ametwambia, Safwan bin Amr ametwambia kutoka kwa Rashid bin Saad kutoka kwa Auf bin Malik kwamba amesema: Mtume wa Allah (saw) amesema:    

«افْتَرَقَتْ الْيَهُودُ عَلَى إِحْدَى وَسَبْعِينَ فِرْقَةً فَوَاحِدَةٌ فِي الْجَنَّةِ وَسَبْعُونَ فِي النَّارِ وَافْتَرَقَتْ النَّصَارَى عَلَى ثِنْتَيْنِ وَسَبْعِينَ فِرْقَةً فَإِحْدَى وَسَبْعُونَ فِي النَّارِ وَوَاحِدَةٌ فِي الْجَنَّةِ وَالَّذِي نَفْسُ مُحَمَّدٍ بِيَدِهِ لَتَفْتَرِقَنَّ أُمَّتِي عَلَى ثَلَاثٍ وَسَبْعِينَ فِرْقَةً وَاحِدَةٌ فِي الْجَنَّةِ وَثِنْتَانِ وَسَبْعُونَ فِي النَّارِ قِيلَ يَا رَسُولَ اللَّهِ مَنْ هُمْ قَالَ الْجَمَاعَةُ»

‘”Mayahudi waligawanyika makundi sabiini na moja; moja ndio litakuwa Peponi sabiini yatakuwa Motoni. Na Manaswara waligawanyika makundi sabiini na mbili; sabiini na moja yatakuwa Motoni na moja litakuwa Peponi. Naapa kwa Yule ambaye nafsi ya Muhammad imo mikononi mwake, Umma wangu utagawanyika makundi sabiini na tatu; moja litakuwa Peponi na sabiini na mbili yatakuwa Motoni’. Wakauliza: ‘ni kina nani hao, ewe Mtume wa Allah?’ Akasema: ‘Ni Jumuiko la Waislamu (Jama’ah)’“.

Ahmad amevua kutoka katika Musnad yake: Abu Al-Mughira asema, Safwan ametwambia, asema, Azhar bin Abdullah Al-Hawzni aliniambia kwamba Abu Al-Mughira katika sehemu ya Al-Harazai kutoka kwa Abu Amir Abdullah bin Luhai aliyesema alikwenda Hajj pamoja na Muawiya bin Abu Sufyan, tulipo karibia Makkah, aliswali swala ya adhuhuri, na kutwambia kwamba Mtume wa Allah (saw) amesema:

«إِنَّ أَهْلَ الْكِتَابَيْنِ افْتَرَقُوا فِي دِينِهِمْ عَلَى ثِنْتَيْنِ وَسَبْعِينَ مِلَّةً وَإِنَّ هَذِهِ الْأُمَّةَ سَتَفْتَرِقُ عَلَى ثَلَاثٍ وَسَبْعِينَ مِلَّةً يَعْنِي الْأَهْوَاءَ كُلُّهَا فِي النَّارِ إِلَّا وَاحِدَةً وَهِيَ الْجَمَاعَةُ»

 “Hakika watu wa vitabu viwili waligawanyika katika dini yao makundi sabiini na mbili, na hakika Umma huu utagawanyika makundi sabiini na tatu: sabiini na mbili yote yatakuwa Motoni isipokuwa moja litakuwa Peponi, na hilo ni jumuiko la Waislamu (Jama’ah).”

At-Tabarani amevua katika As-Saghir: Isa Bin Muhammad As-Simsar Al-Wasiti alitwambia, Wahab bin Bakiya alitwambia, Abdullah bin Sufyan Al-Madani alitwambia, kutoka kwa Yahya bin Saeed Al-Ansari kutoka kwa Anas bin Malik aliyesema: Mtume wa Allah (saw) amesema:

«تفترق هذه الأمة على ثلاث وسبعين فرقة كلهم في النار إلا واحدة، قالوا: وما هي تلك الفرقة؟ قال: ما أنا عليه اليوم وأصحابي»

“‘Umma huu utagawanyika makundi sabiini na tatu yote yatakuwa Motoni isipokuwa moja, wakauliza: ‘Ni kundi lipi hilo? Akasema: ni lile linalo fuata yale ambayo mimi na Maswahaba zangu tunafuata leo.’”

Abdullah Bin Sufyan pekee ndiye aliyesimulia kutoka kwa Yahya.

Al-Bayhaqi amesimulia katika Dala’il An-Nubuwa: Abu al-Husain bin Al-Fadl Al-Qattan alitwambia, Abdullah bin Jaafar Al-Nahawi alitwambia, Ya’qub bin Sufyan alitwambia, Abu al-Yaman alitwambia, Safwan alitwambia, kutoka kwa Al-Azhar bin Abdullah, kutoka katika riwaya ya Abu Amir Abdullah bin Luhai kwamba amesema: Tulikwenda Hajj na Muawiya, tulipo karibia Makkah, aliswali swala ya adhuhuri, na akasema: Mtume wa Allah (saw) amesema:

«إن أهل الكتاب افترقوا في دينهم على اثنتين وسبعين ملة، وإن هذه الأمة ستفترق على ثلاث وسبعين ملة يعني الأهواء، كلها في النار إلا واحدة، وهي الجماعة»

“Hakika watu wa kitabu waligawanyika katika dini yao makundi sabiini na mbili, na hakika Umma huu utagawanyika makundi sabiini na tatu: yote yatakuwa Motoni isipokuwa moja, nalo ni jumuiko la Waislamu (Jama’ah).”

Al-Hakim amesimulia katika Al-Mustadrak katika Sahih mbili: Abu Al-Abbas, Muhammad bin Ya’qub alitwambia, Muhammad bin Ishaq As-Saghani, kutoka kwa Abu Al-Yaman, Al-Hakim bin Nafi’ al-Bahrani, kutoka kwa Safwan bin Amr, kutoka kwa Al-Azhar bin Abd-Allah, kutoka kwa Abi Amir Abdullah bin Luhai, kwamba amesema, tulikwenda Hajj pamoja na Muawiyah bin Abi Sufyan, akasimama akaswali swala ya adhuhuri mjini Makkah, akasema: Mtume (saw) amesema:

«…إِنَّ أَهْلَ الْكِتَابِ تَفَرَّقُوا فِي دِينِهِمْ عَلَى اثْنَتَيْنِ وَسَبْعِينَ مِلَّةً، وَتَفْتَرِقُ هَذِهِ الْأُمَّةُ عَلَى ثَلَاثٍ وَسَبْعِينَ كُلُّهَا فِي النَّارِ إِلَّا وَاحِدَةً وَهِيَ الْجَمَاعَةُ»

“Hakika watu wa kitabu waligawanyika katika dini yao makundi sabiini na mbili, na hakika Umma huu utagawanyika makundi sabiini na tatu: yote yatakuwa Motoni isipokuwa moja, nalo ni jumuiko la Waislamu (Jama’ah).”

Al-Hakim asema riwaya hizi (silsila ya upokezi) ni dalili za kujibu mjadala huu juu ya usahihi wa Hadith hii, Az-Zahabi aliafikiana naye.

Abu Daud amesimulia katika Sunan yake: Ahmad bin Hanbal na Muhammad ibn Yahya walitwambia, Abu Al-Mughirah alitwambia, Safwan alitwambia, na Amr bin Othman alitwambia, Baqiya alitwambia, asema, Safwan aliniambia kitu mithili yake, asema Azhar bin Abdullah Al-Harazi alinambia kutoka kwa Ubai Amir Al-Hawzni, kutoka kwa Muawiya ibn Abi Sufyan, aliye tuhutubia na kusema:

«أَلَا إِنَّ مَنْ قَبْلَكُمْ مِنْ أَهْلِ الْكِتَابِ افْتَرَقُوا عَلَى ثِنْتَيْنِ وَسَبْعِينَ مِلَّةً، وَإِنَّ هَذِهِ الْمِلَّةَ سَتَفْتَرِقُ عَلَى ثَلَاثٍ وَسَبْعِينَ: ثِنْتَانِ وَسَبْعُونَ فِي النَّارِ، وَوَاحِدَةٌ فِي الْجَنَّةِ، وَهِيَ الْجَمَاعَةُ»

‘”Hakika jueni kuwa watu wa kitabu kabla yenu waligawanyika makundi sabiini na mbili; hakika dini hii itagawanyika makundi sabiini na tatu; sabiini na mbili yatakuwa Motoni na moja litakuwa Peponi’. Na hilo ni jumuiko la Waislamu (Jama’ah)’“. [Al-Albani ameiorodhesha kuwa daraja ya Hassan]

Al-Aqeeli katika “Ad-Dhu’afa Al-Kabeer” Muhammad bin Marwan Al-Qurashi amesema: Muhammad bin Ubada Al-Wasiti amesema: Musa bin Ismail Al-Jabali amesema: Mu’adh bin Yasin Az-Zayat amesema: Al-Abrad bin Abi Al-Ashras, amesema kutoka kwa Yahya, kutoka kwa Anas bin Malik (ra), amesema: Mtume (saw) asema:

«تَفَرَّقُ أُمَّتِي عَلَى سَبْعِينَ أَوْ إِحْدَى وَسَبْعِينَ فِرْقَةً، كُلُّهُمْ فِي الْجَنَّةِ إِلَّا فِرْقَةً وَاحِدَةً، قَالُوا: يَا رَسُولَ اللَّهِ، مَنْ هُمْ؟ قَالَ: الزَّنَادِقَةُ وَهُمُ الْقَدَرِيَّةُ»

“‘Umma wangu umegawanyika makundi sabiini au sabiini na moja; yote yatakuwa Motoni isipokuwa moja’ wakauliza: ‘Ewe Mtume wa Allah, ni kina nani hao? Akasema: ‘Az-Zanadiqa nao ni Al-Qadariyah.'”

Al-Aqeeli asema Mu’adh bin Yasin Az-Zayat kutoka kwa Al-Abrad bin Al-Ashras ni mtu asiye julikana na maneno yake hayaku hifadhiwa.  

Al-Aqeeli pia amesimulia katika “Ad-Dhu’afa’ Al-Kabeer” Al-Hasan bin Ali bin Khalid Al-Laithi asema: Na’im bin Hammad asema: Yahya bin Yaman asema, kutoka kwa Yasin Az-Zayat, kutoka kwa Sa’d bin Saeed, kakake Yahya bin Saeed Al-Ansari kutoka kwa Anas kwamba amesema, Mtume wa Allah amesema:

«تَفْتَرِقُ أُمَّتِي عَلَى بِضْعٍ وَسَبْعِينَ فِرْقَةً، كُلُّهَا فِي الْجَنَّةِ إِلَّا فِرْقَةً وَاحِدَةً، وَهِيَ الزَّنَادِقَةُ»

“Umma wangu utagawanyika makundi sabiini na mbili, yote yatakuwa Peponi isipo kuwa kundi moja, nalo ni Az-Zanadiqa.”

Al-Aqeeli asema: Hadith hii haiwezi kutumiwa kama maregeleo kutokana na usahihi wake, na pengine Yassin aliipokea kutoka kwa babake au kutoka kwa Al-Abrad. Hadith hii haina chimbuko kutoka kwa Hadith ya Yahya bin Saeed au kutoka kwa Hadith ya Sa’d. Katika Al-Maudow’at ya Al-Jawzi (1/267) – kitabu cha As-Sunnah Wa Tham Al-Bida’ – sehemu ya kugawanyika kwa Umma huu:

Abd Al-Wahhab bin Al-Mubaarak asema kwamba Ibn Bakran asema kwamba Ibn Al-Atiqi asema kwamba Muhammad ibn Marwan Al-Qurashi asema: Muhammad bin Ubadah Al-Wasiti alitwambia: Musa Bin Ismail alitwambia, Mu’adh bin Yasin Az-Zayyat alitwambia, Al-Abrad bin Al-Ashras kutoka kwa Yahya bin Saeed kutoka kwa Anas bin Malik asema: Mtume wa Allah (saw):

«تَفْتَرِقُ أُمَّتِي عَلَى سَبْعِينَ أَوْ إِحْدَى وَسَبْعِينَ فِرْقَةً كُلُّهُمْ فِي الْجَنَّةِ إِلا فِرْقَةً وَاحِدَةً قَالُوا: يَا رَسُولَ اللَّهِ مَنْ هُمْ؟ قَالَ: الزَّنَادِقَةُ وَهُمُ الْقَدَرِيَّةُ»

“‘Umma wangu utagawanyika makundi sabiini au sabiini na moja, yote yatakuwa Peponi isipokuwa moja’, Wakauliza: ‘Ewe Mtume wa Allah, ni kina nani hao?’ Akasema: Az-Zanadiqa nao ni Al-Qadariya.'”

Imesimuliwa na Ahmad bin Uday Al-Hafidh kutoka kwa Hadith ya Musa bin Ismael kutoka kwa Yassin na Al-Abrad.

Silsila ya pili: Abd Al-Wahhab amesema kwamba Ibn Bakran amesema kwamba Al-Atiqi alitwambia, Yusuf bin Ad-Dakshi amesema, Al-Aqili amesema, Al-Hassan bin Ali bin Khalid Al-Laithi amesema, Na’im bin Hammad alitwambia Yahya bin Yaman alitwambia, kutoka kwa Yasin Az-Zayat kutoka kwa Sa’d bin Saeed kaka ya Yahya bin Saeed Al-Ansari kutoka kwa Anas, amesema: Mtume wa Allah (saw) amesema:

«تَفْتَرِقُ أُمَّتِي عَلَى بِضْعٍ وَسَبْعِينَ فِرْقَةً كُلُّهَا فِي الْجَنَّةِ إِلا فِرْقَةً وَاحِدَةً وَهِيَ الزَّنَادِقَةُ»

“‘Umma wangu utagawanyika makundi sabiini na mbili; yote yatakuwa Peponi, isipokuwa moja, nalo ni Az-Zanadiqa.'”

Silsila ya tatu: Al-Jariri asema: Al-‘Ushari alitwambia, Ad-Darqutni alitwambia, Abu Bakr Muhammad bin Uthman As-Saydalani amesema, Ahmad bin Daud As-Sajistani amesema, Uthman bin Affan Al-Qurashi amesema: Abu Ismail Al-Ayli amesema: Hafs bin Umar kutoka kwa Mis’ar kutoka kwa Sa’d bin Saeed amesema: Nilimsikia Anas bin Malik akisema: Mtume wa Allah (saw) amesema:

«تَفْتَرِقُ أُمَّتِي عَلَى بِضْعٍ وَسَبْعِينَ فِرْقَةً كُلُّهَا فِي الْجَنَّةِ إِلا الزَّنَادِقَةِ»

“‘Umma wangu utagawanyika makundi sabiini na mbili; yote yatakuwa Peponi, isipo Az-Zanadiqa.'”

Anas amesema, tunaamini hao ni Al-Qadariyah.

Hadith hizi haziwezi kuwa zatoka kwa Mtume wa Allah (saw); kuna udhaifu katika riwaya zake katika sehemu moja au zaidi, kama ifuatavyo:

Ibn Al-Jawzi katika Al-Mawdhu’at amezitaja hizo riwaya tatu za juu na kisha kusema:

 “Wajuzi katika fanni wamesema: Al-Abrad (ambaye ni mmoja wa watu waliotajwa katika silsila ya kwanza) alikuwa ni mtu mrongo na mzushi; Yasin amesimulia kutoka kwake, na riwaya hiyo ikabadilishwa na akaichanganya na kuibiwa na Uthman bin Affan (ambaye ni mmoja wa wasimulizi katika silsila ya tatu juu)” 

Kuhusu Al-Abrad, Muhammad bin Ishaq bin Khuzaymah amesema kwamba yeye ni mtu mrongo na mzushi.

Ama kuhusu Yasin (mmoja wa wasimulizi katika silsila ya pili), Yahya amesema kumhusu: “Maneno yake hayana uzito.” An-Nasa’I amesema: “Hadith hiyo inawachwa (Matrook)

Kuhusu Uthman, wanazuoni wa riwaya wamesema; Hadith ambayo ni daraja ya Matrook haijuzu kuandikwa isipokuwa kwa lengo la kujifunza (mfano wake).

Ama kuhusu Hafs bin Umar (msimulizi katika silsila ya tatu), Abu Hatim Ar-Razi amesema kumhusu, “Alikuwa mtu mrongo”, na Al-Aqili amesema kuwa huzua wanacho sema wanazuoni.

Katika Lisan Al-Mizan ya Ibn Hajr Al-Asqalani 362 – Abrad bin Ashras – kutoka kwa Yahya bin Saeed Al-Ansari… Ibn Khuzayma amesema: “Yeye ni mtu mrongo na mzushi.”

Hivyo basi ziada ya “yote yatakuwa Peponi isipo kuwa moja” si sahihi.

Pili: Ama kuhusu yale uliotaja katika swali lako; (Al-Hakim amepasisha kuwa Ghareeb katika maelezo), ambayo ni:

ستفترق أمتي على نيف وسبعين فرقة كلها في الجنة إلا واحدة

“‘Umma wangu utagawanyika zaidi ya makundi sabiini; yote yatakuwa Peponi, isipokuwa moja.'”

Sikupata usahihishaji huu kwa Al-Hatim, kwa kadiri ya elimu yangu; lakini, hata kama uliyo yataja yanapatikana kwengine ambayo mimi sina ufahamu nayo, au sikupata kuyaona, hayata kuwa na nguvu mbele ya wasahihishaji waliosema kuwa ziada hii (katika Hadith) ni dhaifu.  

Tatu: Kwa kutamatisha, Hadith ya kugawanyika kwa Umma kuwa makundi sabiini na tatu pasina na ziada hizi ni sahihi… na kwamba ziada ya kwanza:

 

كلها في النار إلا واحدة

“Yote yatakuwa Motoni isipokuwa moja” imeorodheshwa kuwa Hasan na wengi. Ama ziada ya pili:

كلها في الجنة إلا واحدة

“Yote yatakuwa Peponi isipokuwa moja”, imeorodheshwa kuwa dhaifu na wengi, na wale waliosema kuwa ni Sahih au Hasan ni wachache. Hivyo basi rai yangu (Tarjeeh) ni kuwa ziada inayo stahili kuzingatiwa ni:

كلها في النار إلا واحدة

“Yote yatakuwa Motoni isipokuwa moja”, ziada nyengine ni:

كلها في الجنة إلا واحدة

“…Yote yatakuwa Peponi isipokuwa moja”, hazipasi kuchukuliwa katika riwaya zote zilizo tajwa juu. Hii ndio mimi ninayo ona kuwa kauli yenye nguvu na Allah ajua zaidi.

Ndugu yenu,
Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah

24 Rabi’ Al-Akhir 1439 H
11/1/2018 M