Jumla

IFUNGWEJE MISIKITI

Kusambaza ni Kuunusuru Uislamu

Ya niimal wakili, waniiman naswiri,

Kwa jinalo nasajili, hilino langu shairi,

Kwetu ni jambo thakili, ugani nalokariri,

Ifungweje misikiti, patukuzwapo Manani,

 

Nyoyoni inatudhili, kadhia hino si siri,

Wageni toka awali, ndio waliotudhuri,

Kanama wagonjwa wali, sasa ndwele inaduri,

Ifungweje misikiti, patukuzwapo Manani,

 

Msikiti kiswahili, kiarabu masjidi

Kimaani ni mahali, mtu anaposujudi

Kumsabihi Jalali, Mola aliye Wahidi,

Yawaje ni marufuku, kuswali misikitini,

 

Huyuno anaeswali, akenda kifudifudi,

Liguse bapale hili, tini pasi ukaidi,

Kuko ndiko kiasili, kwambwako ni kusujudi,

Iweje ni marufuku, kuswali misikitini?

 

 

Msikiti ni pahali, anapoabudiwa Mungu,

Kwa ibada mbali mbali, zilo na thawabu tungu,

Kuzuiliwa kuswali, ndanimwe huwa kutungu,

Ifungweje misikiti, patukuzwapo Manani,

 

Hii sasa idhilali, twafanyiwa na majungu,

Aletwamuru kuswali, Muumba nti na Mbingu,

Na ndiye aliyekuli, misikiti ni ya kwangu,

Ifungweje misikiti, patukuzwapo Manani,

 

Faradhi tumeatwili, ijumaa na jamaa,

Jamaa ni ya wawili, na watatu na kupaa,

Nini haswa mushikili, zifikie kuambaa,

Ifungweje misikiti, patukuzwapo Manani,

 

Ni kwakua gonjwa hili, korona limetuvaa,

Laonwa katili nduli, lichewalo kuzagaa,

Ifanywe kuwa muhali, mikusanyiko kufaa,

Ifungweje misikiti, patukuzwapo Manani,

 

Mbona watu si akali, hujazana masokoni?,

Kwani humuno mwahali, hatari hakuna sini?,

Yambwa kuwa na umbali, kati ya watu ni wani,

Ifungweje misikiti, patukuzwapo Manani,

 

Kuosha mikono pili, kwa maji pamwe sabuni,

Tatu kupawa ratili, barakoa za nyusoni,

Hadhari hini batili, kuweko misikitini?,

Ifungweje misikiti, patukuzwapo Manani,

 

Tauni ndio dalili, ya kufunga misikiti?

Ni wapi walikoswali, katika wao wakati?

Maswahaba kukabili, iloshuka nakamati,

Kwenye nyumba ya Aali, ama wanamokeleti?,

Ifungweje misikiti, patukuzwapo Manani,

 

Nawatupe tafswili, maulama ilo nyeti,

Pasipo na kubadili, muradi wa kalimati,

Lengo lisiwe kunali, masilahi yakinoti,

Ifungweje misikiti, patukuzwapo Manani,

 

Ramadhani yawasili, mwezi wetu wa swaumu,

Na gonjwa hili katili, korona latuhujumu,

Mola fanya tasihili, hali zazidi ugumu,

Ifungweje misikiti, patukuzwapo Manani,

 

Ni wewe kinga kamili, Ya Rabana Ya Karimu,

Shariazo ni jamili, na faafu kuhukumu,

Hawa wanotutawali, kwao ziwile ni sumu,

Ifungweje misikiti, patukuzwapo Manani,

 

Kwa ndia yake Rasuli, na turudishe Khilafa,

Ni ya umma sirikali, ipwekeshao Raufa,

Na ngao yao ya kweli, dhidi ya kila maafa,

Ifungweje misikiti, patukuzwapo Manani,

 

Wajibu hino amali, ya kum’bai Khalifa,

Tufanyeni kulihali, kabula ya kwetu kufa,

Nimalizile kauli, hapano natawakafa,

Ifungweje misikiti, patukuzwapo Manani,

 

MTUNZI – MOHAMMED BAKARI

ALMUFTI

MOMBASA – KISAUNI