Jumla

Jinsi ya Kunufaika na Mwezi mtukufu wa Ramadhani

Kusambaza ni Kuunusuru Uislamu

بسم الله الرحمن الرحيم

Sifa njema zote zinamstahiki Mwenyezi Mungu (swt) aliyetuwezesha kuona tena  Mwezi mtukufu wa Ramadhan. Mola (Swt) ameuteua mwezi huu kwa tukio kubwa nalo ni kushukishwa ndani yake Quran kwenye usiku mmoja wa Lailatul Qadr ambao amali njema mja atakayoifanya ndani yake ni bora kuliko ya miezi elfu. Quran ni muongozo unaosilihi wanadamu wote. Asema Allah Taala:

شَهْرُ رَمَضَانَ الَّذِي أُنزِلَ فِيهِ الْقُرْآنُ هُدًى لِّلنَّاسِ وَبَيِّنَاتٍ مِّنَ الْهُدَىٰ وَالْفُرْقَانِ ۚ

TMQ 2:185

(Mwezi huo mlioambiwa mfunge) ni Mwezi wa Ramadhani ambao imeteremshwa katika (mwezi) hii Quran iwe ni uongozi kwa watu na hoja zilizo wazi wa uongozi na hoja zilizowazi na upambanuzi (wa baina ya haki na batili)

Ni muhimu kila moja wetu Ramadhani inapomuingilia ajipige msasa wa kutosha kwa kujiuliza maswali msingi. Kwa mfano, miongoni mwa maswali yafaa mtu ajiulize ni;  Je zile Ramadhani zilizopita zilimgeuza kimaadili. Je  kuna mema aliyoyazidisha ambayo miaka ya nyuma ilikuwa hayafanyi. Na je kuna mabaya yoyote aliyoyaacha aliyokuwa akiyafanya kwa miaka mingi? Pasina na kujiuliza maswali haya itakuwa hatuathiriki wala kunufaika na kuingia Ramadhani. Mola asitujaalie miongoni wa watu hao.

Hakika tukitafakari kwa kina tutakuta zama zinakwenda kwa kasi sana kiasi cha kuwa Ramadhani ya mwaka jana bado ipo kwenye kumbukumbu kwenye mabongo ya wengi wetu. Wengi wetu twaweza kumbuka futari tuliofuturu kwa mwezi mzima au baadhi ya siku!  Kwa hakika siku zinaenda!

Amepokea Imam Ahmad kutoka kwa Abu Huraira asema:

: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ : ( لا تَقُومُ السَّاعَةُ حَتَّى يَتَقَارَبَ الزَّمَانُ ، فَتَكُونَ السَّنَةُ كَالشَّهْرِ ، وَيَكُونَ الشَّهْرُ كَالْجُمُعَةِ ، وَتَكُونَ الْجُمُعَةُ كَالْيَوْمِ ، وَيَكُونَ الْيَوْمُ كَالسَّاعَةِ ، وَتَكُونَ السَّاعَةُ كَاحْتِرَاقِ السَّعَفَةِ ).

Alisema Mtume wa MwenyeziMungu Rehema na Amani zimshukie Qiyama hakitosimama mpaka zama zikurubiane, Mwaka uwe kama mwezi  na Mwezi uwe mfano kama wiki na wiki nayo iwe kama siku na siku iwe kama saa na  kutakuja zama ambao mwaka utakua kama mwezi na mwezi utakuwa kama wiki na wiki itakua kama siku nayo siku iwe kama saa moja nayo saa moja iwe kama kuchoma jani kavu

Imam Assuyuti katika kitabu chake Al-haawiy lilfataawa akasema: “Maana ya kukurubia zama inaamaanisha kupunguka kikweli yaani katika kukurubia kwa Qiyama moja katika alama zake ni kuwa  masaa ya mchana na usiku yatapungua”. Akaendelea kusema “huenda maana ya ku kurubiana zama inaamaanisha kwenda mbio kwa siku na kuondoshwa Baraka katika kila jambo likiwemo pia wakati”.

Kwenda kwa kasi muda kunamaanisha safari yetu kwenda kukutana na Mola wetu inaenda kwa kasi sana hivyo kwa hesabu rahisi kwa mtu aliefikisha umri wa miaka thelathini basi ni kumaanisha umri wake aliokadiriwa hapa duniani umeondoka miaka hiyo.

Sio vyema kwa Waislamu kuonekana wakighurika na maisha ya dunia kama walivyo wamagharibi ambao kwa itikadi yao mbovu ya kutenganisha MwenyeziMungu na Dini yake na maisha ya dunia kumewafanya watumie wakati wao  wakikimbizana na dunia kwa kwa lengo la kukimu mahitaji ya kimada.Kwa kukataa kwao Uislamu wapo katika hasara kubwa sana kwani wanaghurika na uhai wa dunia ambao ni siku chache mno japo wanajidanganya na kuitegemea dunia yenye kuondoka. Hao ndio siku ya qiyama watajua kwa yakini maisha ya duniani ni mafupi mno. MwenyeziMungu SWT anaeleza haya katika surat Muuminina aya 113 /114/115

قَالَ كَمْ لَبِثْتُمْ فِي ٱلأَرْضِ عَدَدَ سِنِينَ. قَالُواْ لَبِثْنَا يَوْماً أَوْ بَعْضَ يَوْمٍ فَسْئَلِ ٱلْعَآدِّينَ . قَالَ إِن لَّبِثْتُمْ إِلاَّ قَلِيلاً لَّوْ أَنَّكُمْ كُنتُمْ تَعْلَمُونَ

Atasema: “Mlikaa muda gani katika ardhi kwa hisabu ya myaka.?”. Watasema: “Tulikaa siku moja au sehemu ya siku.Basi waulize wafanyao hisabu. Atasema: “Nyinyi hamkukaa (huko ulimwenguni) ila kidogo tu; laiti mngalikuwa mumejua

Uislamu umetuhimiza sana kupatiliza kila dakika yako sio kwa manufaa yako hapa duniani tu bali kesho Akhera. Mtume SAW moja katika nasaha kwa swahaba wake alimwambia na patiliza wakati wako wa faragha kabla haujakupita.  Mtume SAAW katika hadithi yake moja alituasa kupatiliza mambo matano kabla kukumbwa na mengine matano moja wapo akasema

وفراغك قبل شغلك

‘Napatiliza wakati ulionao kabla ya shughuli’ zako yaani kabla hujazongwa na matatizo yatakayochukua muda wako mwingi katika kuyashughulikia”

Hivyo kwa wenye akili huwa kila siku utawakuta wakipatiliza wakati wao katika  kufanya mema yatakayomfaa mbele ya Mola wake.Kwa mtu aina hii utamuona kwamba  kuingiliwa na Ramadhani kwake huwa ni fursa ya dhahabu kwani hujitayarisha kabla ya kuingia kwake na huhuzunika kwa kutoka kwake. Huweka nia ya kufanya kila jema huku akitaka baada ya Ramadhani awe hali yake ya uchaji Mungu imekua kwa kiasi kikubwa.Mtu huyu utamkuta akizidisha mema kwa wingi pasina kuhisi uvivu akijua kuwa Ramadhani kuipata ni bahati. Miongoni mwa mema ni kama:-

Kwa kuwa serikali imefunga misikiti isije hatua ikatulegeza tukarudi nyuma katika kutekeleza ibada. Tunatakikana kupatiliza kila fursa kuendelea kufanya ibada na mema mbalimbali katika msimu huu mtukufu.

  • Kuswali swala za jamaa hata majumbani mwetu na kukithirisha nawafila ikiwemo taraweh
  • Kusoma Quran tukufu na kujipinda kutaka kujua hukumu zilizoko ndani yake na hili ni kupitia kuhudhuria darasa mbalimbali msikitini.
  • Kuamrisha mema na kukataza maovu na hapa napenda kuzindusha kwama hakuna mema leo yatakayoshinda kule amali ya kuregesha upya maisha ya Kiislamu kupitia kusimamisha Dola ya Khilafah kwa mfumo wa Mtume SAAW. Na wala hakuna maovu makubwa yanastahiki kukatazwa kama watu kuishi katika nidhamu za Kikafiri za Kirasilimali zinazofunga kwenye minyororo ya wanadamu wenziwao na kuwa watumwa wao badali ya kuwa watumwa wa Mola wa viumbe
  • Kutoa swadaka

Naam haya ni machache ambayo tunatakiwa kuyapatiliza ndani ya Mwezi mtukufu wa Ramadhani.Hivyo ni muhimu kupatiliza muda kabla hujatutoka. Twamoumba MwenyeziMungu Atujaalia Afya na Uzima tuweze kufanya yale anayoyaridhi MwenyeziMungu SWT.

 

Shabani Mwalimu,

Mwakilishi kwa Vyombo vya Habari,

Hizb ut-Tahrir Kenya.