Jumla

Jukumu Msingi la Mwanamke Katika Uislamu

Kusambaza ni Kuunusuru Uislamu

Mnamo Jumatano, 7 Agosti 2019 vyombo vya habari vya Kenya na Kimataifa viliripoti kuwa Baraza la Kitaifa la Kenya lilikumbwa na sintofahamu kwa muda mfupi baada ya Mwakilishi wa Wanawake kutoka Kaunti ya Kwale, Zuleikha Juma Hassan kuingia ndani ya bunge akiwa na mwanawe wa miezi mitano. Mbunge huyo alisema alichukua hatua hiyo ya kwenda na mwanawe Mwanabaraka bungeni ili aweze kufanya kazi siku hiyo ya Jumatano baada ya kupata shida ya kukosa mtu wa kukaa naye nyumbani, na lau asingekwenda kazini ingelimbidi yeye akae nyumbani na kukosa vikao vya bunge.

Zuleikha Juma Hassan ni muathiriwa wa mwito wa kisekula wa kihuria wa ukombozi wa wanawake (feminism) unaopigiwa debe duniani kote na Wamagharibi ili kuweza kuwafanya wanake kuwa watumwa wa kifikra kwa kisingizio cha uhuru.  Aliyekuwa akiongoza mwito huo ni Muamerika Betty Friedan, anayetambuliwa kama muasisi wa ukombozi wa mwanamke leo (modern-day feminism) kupitia kitabu chake, “Siri ya Uke” anadai kwamba  lau wanawake wa nyumbani wa Amerika  watachangamkia taaluma za kudumu, watakuwa na furaha na afya zaidi, ndoa bora na watoto wao watastawi. Msingi wa ujumbe unaolinganiwa na walinganizi wa haki za wanawake miako yote ni kwamba ajira ndio itakayowapa wanawake uwezo wa kujitimizia kibinafsi, thamani na mafanikio katika maisha. Lakini madai yake yalikuwa na yataendelea kuwa bandia!

Kilele cha fikra ya ukombozi wa wanawake kinaonekana wazi haswa katika ‘Usawa wa Kijinsia’ ambao unalenga kuzifanya sawa haki, majukumu na kazi za wanaume na wanawake katika maisha ya familia na mujtama; natija yake imekuwa moja miongoni mwa sababu za kuvunjika ndoa, umama na kiungo cha familia. Kwa kuwa ukombozi wa wanawake umewatoa wanawake majuumbani mwao kwa kisingizio cha kuweka kipaumbele tamaa ya mali na kufaulu kitaaluma kwa kutotilia maanani umama na mshikamano wa familia! Kwa hiyo, mujtama na familia zinataabika kutokana na kuvunjika kwa familia mara kwa mara ambapo kunakotokana na mabadiliko ya majukumu katika mujtama kiasi kwamba wanawake na wanaume wanashindania majukumu sawa au baya zaidi ni wanawake kushindana ili wawe ndio wachumaji wa familia huku wakitenda na kuwa na tabia kama wanaume, wanavaa kama wanaume na kujaribu kuwa na hisia chache kama wanaum n.k. Hivyo basi, si jambo la kushangaza kushuhudia vyombo vikuu vya habari vikipiga kelele wakati ukombozi wa wanawake unaposhambuliwa!

Kinyume na Uislamu, jukumu msingi la mwanamke ni mke, mama na muangalizi wa nyumba. Jukumu la umama limefafanuliwa na Mtume (saw) aliposema:

«الجنة تحت أقدام الأمهات»

“Pepo iko chini ya miguu ya kina mama.”

Pia imesimuliwa kwamba:

جاء رجل إلى رسول الله e فقال‏: يا رسول الله من أحق الناس بحسن صحابتي؟ قال: »أمك« قال: ثم من؟ قال: ‏»أمك« قال: ثم من؟ قال: »‏أمك« قال: ثم من؟ قال: »‏أبوك« ((متفق عليه)).

Alikuja mtu kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) akamuuliza, ‘ni nani miongoni mwa watu anayestahiki usuhuba mzuri kwangu?’ Mtume (saw) akasema: “mamako”, akauliza tena, ‘kisha nani?’ Mtume (saw) akajibu: “mamako”, akauliza tena, ‘kisha nani?’ Mtume (saw) akajibu: “mamako”, akauliza tena, ‘kisha nani?’ Mtume (saw) akajibu: “babako” (Bukhari na Muslim)

Hakika, Uislamu umeelezea jukumu la kweli la wanawake na kuwaheshimu wanawake katika tukio moja ambapo mwanamke alimuuliza Mtume (saw) kuhusu taarifa zinazohusiana na wanawake na Yeye (saw) alisema:

«أفما ترضى إحداكن أنها إذا كانت حاملا من زوجها وهو عنها راض أن لها مثل أجر الصائم القائم في سبيل الله، فإذا أصابها الطلق لم يعلم أهل السماء وأهل الأرض ما أخفي لها من قرة أعين، فإذا وضعت لم يخرج منها جرعة من لبنها، ولم يمص مصة، إلا كان لها بكل جرعة وبكل مصة حسنة، فإن أسهرها ليلة كان لها مثل أجر سبعين رقبة تعتقهن في سبيل الله»

“Je haridhiki mmoja wenu kwamba anapokuwa na uja uzito wa mumewe na huku yuko radhi na yeye ana ujira mfano wa aliyefunga na aliyesimama katika njia ya Mwenyezi Mungu, anapopatwa na uchungu wa uzazi watu wa mbinguni na ardhini hawajui kilichofichika tumboni mwake kinachomfurahisha yeye machoni. Na anapojifungua hakuna tone la maziwa linatoka na hakuna tone la maziwa mtoto analo nyonya isipokuwa atapa ujira wa jema moja. Na mtoto anapomkesheza usiku atapata ujira mfano wa aliye waacha watumwa sabini huru kwa ajili ya Mwenyezi Mungu.” [Tabarani]

Kwa kuongezea, Sheikh Abdullah Azzam (Rahimahullah) alisema kwamba:

“Kina mama hucheza dori kubwa katika kuunda kizazi. Kila mama anavyokuwa mzuri katika kulea watoto wake, ndivyo umma unavyofaulu kuundwa na unavyofaulu kuzalisha mashujaa. Ni nadra kuona mwanamume imara isipokuwa nyuma yake kuna mwanamke imara aliyeacha tabia zake ndani ya utambulisho (shakhsiya) wake kwa njia ya maziwa ambayo alinyonyeshwa na joto la kukumbatiwa kila alipohitaji hifadhi.”

Kwa kutamatisha wanawake katika Uislamu wanalindwa dhidi ya mkanganyiko na tabu zinazoshuhudiwa leo ndani ya mujtama za kisekula za kihuria kutokana na miito ya ukombozi wa wanawake ambayo imepelekea mashindano ya kimali/kimada baina ya wanaume na wanawake. Kwa kuwa mwanamume ni wajib kwake kuwa mchumaji na ikiwa hana uwezo basi jamaa zake wamsaidie na lau kama nao hawana uwezo basi dola ya Kiislamu ya Khilafah itamsaidia yeye kuweza kukidhi mahitaji ya familia yake kutoka katika Bait ul-Mal (hazina). Kwa sababu hiyo wanawake hawatofanywa watumwa kwa kutumia miito ya faida ya kiuchumi kwa pazia ya ukombozi wa wanawake! Hivyo basi kila mwanamke na mwanamume lazima ajiunge katika juhudi za kufanya kazi ya kurudisha maisha ya Kiislamu kupitia kusimamisha Khilafah. Kwa kuwa Khilafah itadhamini hadhi na heshima ya wanawake kwa kuwawezesha kutekeleza jukumu lao msingi la umama kwa kukata mahusiano na dola za kikoloni ambazo zinapigia debe ukombozi wa wanawake ili kuwakandamiza wanawake kwa kuwalazimisha kuacha majumba yao na watoto wao na badala yake kwenda na kukaa afisini na kuwa kama mashine za utengenezaji pesa!

Ali Nassoro Ali

Mwanachama wa Afisi ya Habari ya Hizb ut Tahrir Kenya

Makala Na.57: Ijumaa, 08 Dhul-Hijja 1440 | 2019/08/09