Jumla

Kamati ya Mpango wa Ujenzi wa Madaraja (BBI) na Mpango wa Punguza Mizigo (Marekebisho ya Katiba): Thibitisho la Kufeli kwa Nidhamu ya Kubahatisha ya Kidemokrasia

Kusambaza ni Kuunusuru Uislamu

Mnamo Ijumaa, 9 Machi 2018 mahasimu wa kisiasa Rais Uhuru Kenyatta na Raila Odinga walikutana faragha kisha wakatoa taarifa ya pamoja kwa vyombo vya habari. Taarifa iliyoashiria eti “Mwanzo Mpya” na iliyofuatiwa na kuundwa kwa BBI kwa lengo la kuunganisha taifa lote kupitia mchakato wa kura ya maoni kubadilisha muundo wa serikali ili kupunguza mizozo ya kisiasa kila wakati wa uchaguzi. BBI inatarajiwa kutoa ripoti yake rasmi Oktoba 2019. Fauka ya hayo, mnamo Alhamisi, 18 Julai 2019 Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ilitoa taarifa kwa vyombo vya habari kwamba ilipokea Kielelezo cha Mswada wa Marekebisho ya Katiba mnamo Alhamisi, 28 Februari kutoka kwa wanaounga mkono Mpango wa Punguza Mizigo (Marekebisho ya Katiba) wa 2019 uliodhaminiwa na Chama cha Muungano wa Tatu Kenya kinachoongozwa na Ekuru Aukot. Na kwamba baada ya IEBC kufanya uhakiki walitaarifu Ummah na washikadau wote kwamba Mpango huo ulitimiza masharti yote kwa mujibu wa sheria na hivyo mswada unasonga hatua za mbele ikiwemo kutumwa katika Kaunti 47 ili ukipitishwa na Kaunti 24 au zaidi basi unakwenda Bunge la Kitaifa na Seneti nao wakipitisha Rais ataweka saini na kuwa sheria au Bunge la Kitaifa na Seneti wasipopitisha basi itakwenda kwa wananchi ili iweze kupigiwa kura ya maoni!

Kamati ya BBI inadai kuwa imebuniwa kuweza kuwaunganisha Wakenya kupitia kubadilisha muundo wa serikali na upande wa pili Mpango wa Punguza Mizigo unadai kwamba umekuja kuwapunguzia mizigo Wakenya kupitia kudumisha muundo wa serikali na kupunguza nafasi za vyeo katika serikali! Hakika ni jambo la kusikitisha mno na la aibu kuona kwamba vinara wanaopigia debe Kamati ya BBI na Mpango wa Punguza Mizigo ni wale wale waliohusika katika mchakato wa kuleta Katiba ya 2010! Kwani Ekuru Aukot alikuwa katika Kamati ya Wajuzi waliokusanya mapendekezo ya Katiba ya 2010 na upande wa pili Raila na Uhuru walikuwa kambi ya walioshajiisha watu wapitishe Katiba ya 2010!

Ni jambo la kusikitisha na aibu kwa kuwa hawa wanaodaiwa kuwa ni viongozi wanawazungusha watu mduara pasina kuwaambia ukweli kwamba kiasili mabadiliko ya katiba ni mabadiliko ya maslahi ya watu wachache walioko au wanaoingia mamlakani na sio kwa raia jumla. Pili ni kwamba sio suluhisho la kudumu kwa matatizo yanayolikumba taifa sababu nidhamu yenyewe kiasili haitoki kwa Mwenyezi Mungu (swt) bali imetokamana na itikadi ya kisekula (kutenganisha dini na maisha/serikali). Nidhamu hii kiasili ipo kuweza kuhifadhi uhuru wa wanadamu ukijumuisha: uhuru wa kuabudu, uhuru wa kumiliki, uhuru wa maoni na uhuru wa kibinfasi. Kwa maana nyingine ni nidhamu ya kubahatisha sawa na mtu aliye kizani (matatizo) kila kukicha anatafuta mwangaza (suluhisho)!

Hakika wanadamu wanahitaji muongozo usiokuwa na shaka na unaotoka kwa Mwenyezi Mungu (swt). Muongozo huo ni Shari’ah (Qur’an na Sunnah) na kwamba kufaulu au kufeli kwa watu kunategemea wao kujifunga na Shari’ah. Hivyo basi, ili Wakenya na wanadamu jumla duniani wapate utulivu na ufanisi wa kweli wanahitajika kurudia muongozo wa Muumba (swt) kwa kujiunga na kufanya kazi ya ulinganizi wa kurudisha tena maisha ya Kiislamu kupitia kusimamisha serikali ya Kiislamu ya Khilafah kwa njia ya Utume ndani ya moja katika nchi za Waislamu mfano Pakistan, Bangladesh, Misri n.k.

Nidhamu ya utawala ndani ya Khilafah sio ya kubahatisha kama inavyoshuhudiwa leo katika nidhamu feki ya kidemokrasia! Kwa sababu muundo wa serikali yake, mapato na matumizi yake yamefungika na Shari’ah tokea Khalifah wa kwanza Abu Bakr (ra) alipochukua hatamu mwaka 632 mpaka Khalifah wa mwisho wa mia na moja Abdulmajid II mwaka 1924.

Ali Nassoro Ali

Mwanachama wa Afisi ya Habari ya Hizb ut Tahrir Kenya

Makala Na.55: Ijumaa, 25 Dhul-Qa’da 1440 | 2019/07/26