Ameer Suali na Jawabu

Kuacha Masafa katika Swala ni Uzushi (Bid’ah) Ambao Watawala Wanapata Dhambi lake

Kusambaza ni Kuunusuru Uislamu

بسم الله الرحمن الرحيم

 Jibu la Swali
Kuacha Masafa katika Swala ni Uzushi (Bid’ah) Ambao Watawala Wanapata Dhambi lake
(Imetafsiriwa)

Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, na swala na salamu zimshukie Mtume wa Mwenyezi Mungu na jamaa, maswahaba na wafuasi wake,

Kwa wale wote waliotuma wakiniuliza kuhusu nafasi ya mita mbili baina mwenye kuswali na yule aliye baada yake wakati wa swala za Ijumaa na swala za jamaa… na wanasema kuwa watawala katika baadhi ya nchi za Waislamu walifunga misikiti, na pindi walipoifungua, waliwalazimisha wanao swali kuwa mbali mbali kwa mita mbili. Mamlaka hizi zinahalalisha hili kwa kuwa mgonjwa amepewa udhuru na huswali kwa kukaa hivyo, kwa qiyas hiyo anaweza kuwa na umbali wa mita mbili kutoka kwa yule aliye baada yake, hata kama si mgonjwa, lakini anahofia ugonjwa, basi anapaswa kuweka masafa … na wanauliza: Je, inaruhusiwa kwa watawala kuwalazimisha waumini kuswali kwa kuacha nafasi kama ilivyo tajwa? Au uachaji nafasi huu ni uzushi (Bid’ah) ambao watawala wanapata dhambi lake? Wale wanaouliza wanasisitiza kupata jibu…

Katika kujibu maswali yao, Ninasema, na Mwenyezi Mungu Ndiye Mlinzi wa mafanikio:

Nyuma tumewahi kutoa zaidi ya jibu moja kuhusiana na uzushi (bid’ah), na ikiwa waulizaji watayatafakari, jibu litakuwa wazi kwao kuwa uwekaji masafa kama ulivyo tajwa ni uzushi ambao watawala wana madhambi kwa ajili yake endapo watawalazimisha watu kwa huu uwekaji masafa, na ufafanuzi wa hilo ni kama ufuatavyo:

Kwanza: Mnamo Rajab 28, 1434 H, sawia na 07/06/2013 M, ili elezwa:

(Uzushi ni ukiukaji wa jambo la Kisharia, ambalo njia ya utekelezaji wake imefafanuliwa na Shari’ah. Uzushi, kilugha kama iliyo elezwa katika Lisaan al-Arab ni

المبتدع الّذي يأتي أمراً على شبهٍ لم يكن…، وأبدعت الشّيء: اخترعته لا على مثالٍ

“Mzushi ni yule ambaye anakuja na jambo kwa umbo ambalo halikuwepo kabisa…, na ‘umezua kitu’: umekibuni pasi na kuwepo mfano wake.” Maana yake ya kiufahamu ni hiyo hiyo. Ikiwa kwa mfano Mtume (saw) alifanya kitu kwa njia maalum na Muislamu akakengeuka kutokana na njia hii, basi hii ni uzushi. Hivyo basi uzushi ni mkengeuko kutokana na njia iliyo wekwa na Shari’ah kutekeleza jambo fulani la Kisharia. Na hii ndio maana iliyo vuliwa ya Hadith: «وَمَنْ عَمِلَ عَمَلًا لَيْسَ عَلَيْهِ أَمْرُنَا فَهُوَ رَدٌّ» “Na yeyote anaye fanya amali ambayo hakuna amri yetu juu yake basi, basi itakataliwa.” [Bukhari na Muslim]

Kwa mfano, endapo mtu atatekeleza Sijda tatu katika swala zake kinyume na mbili, atakuwa amezua katika hilo na kukengeuka kutokana na njia ya Mtume (saw). Endapo mtu atarusha vijiwe vinane badala ya vijiwe saba katika Mina basi atakuwa amefanya uzushi kwa sababu kitendo hicho ni kinyume na kitendo cha Mtume (saw). Na endapo, kwa mfano, mtu ataongeza au kupunguza maneno katika Adhan, basi atakuwa pia ametumbukia katika uzushi kwani Mtume (saw) ameidhinisha maneno maalum ya Adhan.

Ama, kukengeuka kutokana na jambo la Shari’ah ambalo halina njia maalum ya kulitekeleza ataanguka ndani ya moja ya hukmu ya kisheria, ikimaanisha: ima itakuwa ni Haram, Makruh, nk, hii ni ikiwa hotuba yake ni ya ukalifishaji (Khitaab Taklif), au itakuwa ni Baatil, Faasid, nk ikiwa hotuba ni yake ni ya maelezo (Khitaab Wadh’i).

Kwa mfano, imepokewa na Muslim kutoka kwa Aisha (ra) katika kuisifia kwake swala ya Mtume (saw) kwamba amesema:

«...وَكَانَ إِذَا رَفَعَ رَأْسَهُ مِنَ الرُّكُوعِ لَمْ يَسْجُدْ، حَتَّى يَسْتَوِيَ قَائِمًا، وَكَانَ إِذَا رَفَعَ رَأْسَهُ مِنَ السَّجْدَةِ، لَمْ يَسْجُدْ حَتَّى يَسْتَوِيَ جَالِسًا…»

“…Na alikuwa anapo inua kichwa chake kutoka katika rukuu hasujudu, mpaka asimame wima, na alikuwa anapo inua kichwa chake kutoka katika sijda, hasujudu mpaka akae sawasawa.”

Kutokana na haya, katika riwaya hii Mtume (saw) anatuonyesha kwamba Muislamu pindi anapo inusha kichwa chake, asisujudu mpaka asimame wima, na anapo inuka kutoka kwa sijda yake, asirudi katika sijda mpaka akae sawasawa. Hii ndio njia iliyo agizwa na Mtume (saw) na endapo yeyote atakengeuka kutokana na njia hii iliyo pendekezwa, basi atakuwa ameingia ndani ya uzushi. Hivyo, endapo Muislamu aliye ndani ya swala atatekeleza sijda moja kwa moja baada ya Rukuu bila ya kusimama wima baina ya hizo mbili, basi atakuwa ameanguka ndani ya uzushi kwani ni kinyume na njia ambayo Mtume (saw) alituonyesha. Huu ni uzushi mbaya na yeyote anaye ufanya ameingia ndani ya dhambi kubwa.

Lakini, imepokewa na Muslim kwa riwaya ya ‘Ubaydah Bin Samit kwamba:

إِنِّي سَمِعْتُ رَسُولَ اللهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: «يَنْهَى عَنْ بَيْعِ الذَّهَبِ بِالذَّهَبِ، وَالْفِضَّةِ بِالْفِضَّةِ، وَالْبُرِّ بِالْبُرِّ، وَالشَّعِيرِ بِالشَّعِيرِ، وَالتَّمْرِ بِالتَّمْرِ، وَالْمِلْحِ بِالْمِلْحِ، إِلَّا سَوَاءً بِسَوَاءٍ، عَيْنًا بِعَيْنٍ، فَمَنْ زَادَ، أَوِ ازْدَادَ، فَقَدْ أَرْبَى

“Hakika mimi nilimsikia Mtume wa Mwenyezi (saw): Akikataza uuzaji wa dhahabu kwa dhahabu, fedha kwa fedha, ngano kwa ngano, mawele kwa mawele, tende kwa tende, chumvi kwa chumvi, isipokuwa kwa kiasi sawa kwa sawa, aina kwa aina, na yeyote atakaye zidisha, au akataka azidhishiwe, basi ameingia katika riba.” Endapo Muislamu atakiuka Hadith hii na kuuza dhahabu kwa dhahabu kwa nyongeza (riba), na sio uzani kwa uzani, basi haisemwi kuwa amefanya uzushi, bali itasemwa kuwa amefanya haram yaani riba.

Kwa kutamatisha: Ukengeukaji kutokana na njia iliyo fafanuliwa na Mtume (saw) ni uzushi. Na ukengeukaji kutokana na amri jumla ya Mtume (saw) pasi na kuwepo njia maalum iliyo agizwa ya utekelezaji wake inaangukia ndani ya mojawapo ya hukmu za kisheria (Ahkaam Shar’iyah): Haram na Makruh, Fasid na Baatil… Hili liko thabiti kwa mujibu wa dalili.) Mwisho wa nukuu.

Tulitoa maelezo ya kina zaidi kuhusu uzushi mnamo 08 Dhu al-Hijjah 1436 H sawia na 22/09/2015 M na pia tulitoa majibu mengine kabla na baada hapo ambayo yanayo tosheleza zaidi, kwa idhini ya Mwenyezi Mungu.

Pili: Kutokana na haya, endapo nchi katika nchi za Waislamu zitawalazimisha waumini kujitenga kwa mita moja au mbili baina yao, ima katika Ijumaa au katika jamaa kwa hofu ya maambukizi, hususan pasi na kudhihiri dalili za maambukizi, basi watatekeleza dhambi kubwa ambapo kujitenga huku ni uzushi, kwa sababu ni ukiukaji, kwani ni ukengeukaji wa wazi wa njia ya uwekaji safu na kukaribiana pamoja kama ilivyo bainishwa na Mtume wa Mwenyezi (saw) kupitia dalili ya Kisheria, ikiwemo:

– Al-Bukhari amepokea katika Sahih yake kutoka kwa Abu Sulayman Malik ibn al-Huwayrith aliye sema,”Nilikuja kwa Mtume (saw) tukiwa vijana wa umri sawa. Tukawa pamoja naye kwa masiku ishirini… Alikuwa mwenye huruma na mpole, na akasema,

«فَقَالَ ارْجِعُوا إِلَى أَهْلِيكُمْ فَعَلِّمُوهُمْ وَمُرُوهُمْ وَصَلُّوا كَمَا رَأَيْتُمُونِي أُصَلِّي وَإِذَا حَضَرَتِ الصَّلَاةُ فَلْيُؤَذِّنْ لَكُمْ أَحَدُكُمْ ثُمَّ لِيَؤُمَّكُمْ أَكْبَرُكُمْ»

“Rudini kwa watu wenu na muwaelimisha na muwaamrishe, na muswali kama mulivyoniona mimi nikiswali. Unapofika wakati wa swala, na aadhini mmoja wenu, kisha mkubwa kwenu awe imamu wenu.”

– Na al-Bukhari amepokea katika Sahih yake kutoka kwa Anas Bin Malik, aliye sema: Pindi Iqamah ilipo tangazwa, Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) aligeuza uso wake kwetu na kusema:

«أَقِيمُوا صُفُوفَكُمْ، وَتَرَاصُّوا، فَإِنِّي أَرَاكُمْ مِنْ وَرَاءِ ظَهْرِي» “Simamisheni safu zenu wima, na karibianeni, kwani hakika mimi huwaona nyuma ya mgongo wangu.”

– Muslim amepokea katika Sahih yake kutoka kwa al-Nu’man ibn Bashir (r.a), aliye sema Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) ametuelekeza kuziweka safu zetu wima kama mishale. Aliendelea kusisitiza hili mpaka alipo tambua kwamba tumeelimika kutoka kwake (kutambua umuhimu wake). Siku moja alikuja msikitini na kusimama. Alikuwa karibu kupiga takbira alipo gundua kifua cha mtu mmoja kiko nje ya safu, hivyo akasema,

«عِبَادَ اللهِ لَتُسَوُّنَّ صُفُوفَكُمْ، أَوْ لَيُخَالِفَنَّ اللهُ بَيْنَ وُجُوهِكُمْ» “Enyi waja wa Mwenyezi Mungu, hamutaacha kuweka safu zenu wima, au Mwenyezi Mungu atazifarakanisha nyuso zenu baina yenu.”

– Na Muslim pia amepokea katika Sahih yake kutoka kwa Jabir ibn Samrah, aliye sema: Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) amesema:

«أَلَا تَصُفُّونَ كَمَا تَصُفُّ الْمَلَائِكَةُ عِنْدَ رَبِّهَا؟» فَقُلْنَا يَا رَسُولَ اللهِ، وَكَيْفَ تَصُفُّ الْمَلَائِكَةُ عِنْدَ رَبِّهَا؟ قَالَ: «يُتِمُّونَ الصُّفُوفَ الْأُوَلَ وَيَتَرَاصُّونَ فِي الصَّفِّ»

“Je, hamtaki kuweka safu zenu kama wanavyo weka safu malaika mbele ya Mola wao? Tukasema: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu na vipi malaika huweka safu zao mbele ya Mola wao? Akasema (Mtume Mtukufu): Wanakamilisha safu ya kwanza na wanakaribiana katika safu hiyo.”

– Na Al-Hakim amepokea, na kusema kuwa ni hadith sahih kwa sharti la Muslim, kutoka kwa Abdullah bin Umar, Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) amesema:

«مَنْ وَصَلَ صَفّاً وَصَلَهُ اللَّهُ، وَمَنْ قَطَعَ صَفّاً قَطَعَهُ اللَّهُ» “Mwenye kuunga safu na Mwenyezi Mungu atamuunga, na mwenye kukata safu Mwenyezi Mungu atamkata.”

– Ahmed amepokea kutoka Abdullah ibn Umar kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) amesema:

«أَقِيمُوا الصُّفُوفَ فَإِنَّمَا تَصُفُّونَ بِصُفُوفِ الْمَلَائِكَةِ وَحَاذُوا بَيْنَ الْمَنَاكِبِ وَسُدُّوا الْخَلَلَ وَلِينُوا فِي أَيْدِي إِخْوَانِكُمْ وَلَا تَذَرُوا فُرُجَاتٍ لِلشَّيْطَانِ وَمَنْ وَصَلَ صَفّاً وَصَلَهُ اللَّهُ تَبَارَكَ وَتَعَالَى وَمَنْ قَطَعَ صَفّاً قَطَعَهُ اللَّهُ»

“Simamisheni wima safu, kwani hakika mnasimama na safu za malaika, na linganisheni baina ya mabega yenu, na zibeni mianya, na lainikeni mikononi mwa ndugu zenu, wala msiwache nafasi za shetani. Na mwenye kuunga safu Mwenyezi Mungu Aliye Tukuka atamuunga, na mwenye kukata safu Mwenyezi Mungu atamkata.”

Huu ni ufafanuzi kamilifu kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi (saw) wa namna ya kuswali kwa jamaa, na Maswahaba, MwenyezI Mungu awe radhi nao, walishikamana na hili. Malik katika Al-Muwata na al-Baihaqi katika As-Sunan al-Kubra amesimulia “kwamba Umar ibn al-Khattab alikuwa akiamuru safu zinyoshwe, na pindi wanapokuja kwake na kumwambia kwamba safu zimenyoka angepiga takbir.”

Tatu: Haisemwi kuwa maradhi ya kuambukiza ni udhuru unao ruhusu kuweka masafa katika swala, haisemwi hivyo kwa sababu maradhi ya kuambukiza ni udhuru wa kutokwenda msikitini na sio udhuru wa kwenda na waumini kuwa mbali kwa mita moja au mbili baina yao!! Kwa sababu maradhi ya kuambukiza (tauni) yalitokea wakati wa zama za Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) na haikuripotiwa kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) kwamba mgonjwa wa tauni alikwenda kuswali na kuweka umbali wa mita mbili kutoka kwa ndugu yake, lakini amepewa udhuru na huswali nyumbani kwake …

Matibabu katika eneo ambamo maradhi yameenea, hukolezwa bila ya malipo na kwa bidii chini ya ufadhili kutoka kwa dola na hawachanganywi na watu walio wazima… kama ilivyo simuliwa na Muslim katika Sahih yake kwamba Usama bin Zaid ameripoti kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu alisema:

«الطَّاعُونُ آيَةُ الرِّجْزِ ابْتَلَى اللَّهُ عَزَّ وَجَلَّ بِهِ نَاساً مِنْ عِبَادِهِ، فَإِذَا سَمِعْتُمْ بِهِ فَلَا تَدْخُلُوا عَلَيْهِ وَإِذَا وَقَعَ بِأَرْضٍ وَأَنْتُمْ بِهَا فَلَا تَفِرُّوا مِنْهُ»

“Tauni ni alama ya janga ambalo Mwenyezi Mungu Mtukufu huwaonja watu miongoni mwa waja wake kwalo. Basi pindi mtakapoisikia, msiingie iliko, na inapotokea katika ardhi mliomo ndani yake, msitoroke kutoka humo.” Yaani, mgonjwa aliye na maradhi ya kuambukiza hajichanganyi na walio wazima na hupewa matibabu ya kutosha, kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Ama kwa aliye mzima, huenda msikitini na kuswali swala za Ijumaa na jamaa kama kawaida, pasi na kuweka masafa.

Nne: Vilevile, sio sahihi kusema kwamba uwekaji masafa katika swala wakati wa janga la maambukizi hupimwa kwa Qiyas ya ruhusa ya kuswali kwa kukaa wakati wa ugonjwa. Kwani hii sio Qiyas ya kisheria, kwa sababu mgonjwa huswali kwa kukaa kwa ruhusa kutoka kwa Mwenyezi Mungu (swt) yaani kwa udhuru ambao ni ugonjwa. Nyudhuru ni sababu (asbaab) na sio illa ya kisheria (‘Illah), hivyo Shari’ hakuzihalalisha bali aliufanya kila udhuru kuwa ni udhuru kwa hukmu, ambayo udhuru huo umekuja kwa ajili yake na sio nyenginezo, kwani hukadiriwa kuwa ni udhuru maalum wa hukmu hiyo ulio kuja kwa ajili yake, na sio udhuru jumla kwa kila hukmu; haileti ufahamu (mafhum) wa kuwa ndio sababu ya uwekaji illah (wajh al-illah).

Hivyo basi, Qiyas haiwezi kufanywa kwake, kwa sababu sababu yake ni maalum (khaas) kwa lile lililosababisha kuwepo kwake, na haipanuki kwa nyenginezo, hivyo haikisiwi dhidi yake. Hii ni kinyume na ‘illah, kwa sababu sio maalum (khaas) kwa hukmu ambayo ilipitishwa kwa ajili yake bali inapanuka hadi kwa nyenginezo, na Qiyas yaweza kufanywa juu yazo.

Tano: Pia, ruhusa ya kisheria ni katika hukmu za maelezo (Hukm Wadh’i), ambazo ni hotuba (Khitaab) ya Mtunzi wa Sheria inayo husiana na matendo ya waja katika maelezo, na kwa kuwa yenyewe ni hotuba ya Mtunzi wa Sheria, ni lazima kuwepo na dalili ya Kisheria inayoiashiria. Kwa mfano, kuhusu swala ya mgonjwa aliye kaa, Al-Bukhari amepokea katika Sahih yake kutoka kwa ‘Imran bin Husain akisema nilikuwa na baasili, hivyo nikamuuliza Mtume (saw) kuhusu swala. Akasema,

«صَلِّ قَائِماً فَإِنْ لَمْ تَسْتَطِعْ فَقَاعِداً، فَإِنْ لَمْ تَسْتَطِعْ فَعَلَى جَنْبٍ»

“Swali kwa kusimama ikiwa huwezi basi kwa kukaa, na ikiwa huwezi basi kwa ubavu.” Hii ni ruhusa, ambayo ni udhuru halali, na yote yaliyo elezwa katika dalili ya kisheria kuwa ni udhuru wa hukmu fulani, hukadiriwa ni udhuru, na wowote ambao hauna dalili yake huwa hauthaminiwi, na kamwe haukadiriwi kuwa ni udhuru wa kisheria … na kwa kuwa hakuna dalili kwamba mgonjwa anaweza kuswali kwa umbali wa mita moja au mbili na mwingine aliye karibu yake, basi taarifa hii haina thamani kisheria, na sio sahihi … Vipi basi ikiwa si mgonjwa, bali tu anahofia maradhi?

Sita: Mukhtasari wa yaliyo juu ni kama ufuatavyo:

1- Kubadilisha njia ambayo Mtume (saw) ameiweka kwa swala hukadiriwa kuwa ni uzushi. Bali, hukmu ya Kisheria katika hali hii ni kuwa mtu aliye mzima aende akaswali kama kawaida katika safu zilizo nyoka kwa kukaribiana pamoja, na bila ya kuacha nafasi, na mgonjwa aliye na maradhi ya kuambukiza asende na asiambukize wengine.

2- Endapo dola itafunga misikiti, na kisha kuwazuia watu walio wazima kutokana na kwenda misikitini kwa swala za Ijumaa na jamaa, basi itakuwa katika madhambi makubwa ya kukatiza swala za Ijumaa na jamaa, kwani misikiti ni lazima ibakie wazi kwa ajili ya swala kama ilivyo ashiriwa na Mtume (saw).

3- Vilevile, endapo dola itawakataza waumini kuswali kwa mujibu wa njia iliyo wekwa na Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) bali kuwalazimisha kuweka nafasi ya mita moja au mbili baina ya muumini mmoja na yule aliye karibu yake kwa hofu ya maambukizi, hususan pasi na kuonyesha ishara za maradhi, basi hili ni dhambi kubwa.

Hii ndio hukmu ya Sheria ambayo naipa uzito katika jambo hili, na Mwenyezi Mungu Ndiye Mjuzi zaidi na ni Mwingi wa hekima … Na namuomba Yeye, Subhanahu, awaongoze Waislamu katika njia sahihi ya kumuabudu Yeye, Subhanahu, kama alivyo amrisha, na wamelazimika kujifunga na njia ya Mtume Wake (saw), na kusimamisha Shari’ah halisi isiyo na mkengeuko wowote kupitia kusimamisha Khilafah Rashida … ambayo ndani yake kuna kheri na ushindi, kwa idhini ya Mwenyezi Mungu, Ambaye hashindwi na chochote mbinguni wala ardhini, Yeye Ndiye Mwenye nguvu, Mwenye hekima.

Wassalamu Alaikum wa RahmatuAllahu wa Barakatuhu.

17th Shawaal 1441 H

08/06/2020 M