Kupandisha Kiwango cha Chini cha Mshahara ni Suluhisho Hadaifu la Kuziba Viraka

Mfumuko wa bei umepanda kwa viwango visivyoingia akilini katika nchi kama Venezuela ni asilimia 284.4, Sudan ni asilimia 259.80, Lebanon ni asilimia 208.13, Syria ni asilimia 139.46, Zimbabwe ni asilimia 96.4, Uturuki ni asilimia 69.97, Suriname ni asilimia 61.5 na Argentina ni asilimia 55.1. (Trading Economics, Alhamisi, Mei 5, 2022). Nchi zilizotajwa ni baadhi tu ya mifano ili kutoa taswira ya kutamausha ya mataifa duniani kote. Hivyo basi, gharama ya maisha inaendelea kupanda kutokamana na uchocheaji wa kimakusudi wa mfumuko wa bei. Kwa hiyo, nchi nyingi zinakabiliwa na ukosefu wa usalama na ustawi duniani kote ikijumuisha Amerika, ambapo mfumuko wa bei umefika asilimia 8.5 kikiwa ni kiwango cha juu zaidi kwa kipindi cha miaka 40. (Bureau of Labor Statistics, 12/04/2022).

Kiuhakika, umechochewa kimakusudi na wale walioko uongozini katika tawala za kidemokrasia duniani kote wakiongozwa na Amerika na washirika wake. Kwa mfano, baada ya Vita vya Pili vya Dunia mnamo 1945, Amerika iliibuka ikiwa na nguvu zaidi na kinara wa ulimwengu ambaye alizipiku dola kuu za zamani kwa maana Uingereza, Ufaransa na Ujerumani. Dola kuu za zamani zilipata pigo kubwa la kiuchumi kutokana na vita na hivyo usemi wao wa kiulimwengu ukapungua. Amerika ilipatiliza fursa ya mamlaka makubwa yenye kutiwa shime na nguvu zake za kiuchumi ikabuni sera hadaifu ya kifedha ya kiulimwengu ya kubadilisha sarafu za mataifa mengine kwa kutumia dola ya Amerika na huku dola ya Amerika ikibadilishwa kwa kiwango maalumu cha dhahabu ya kiwango cha wakia (aunsi) au gramu 28.3495 kwa dola 35. Mnamo1958 sera hiyo ikaanza kufanyiwakazi rasmi chini ya mwito wa nidhamu ya Bretton Woods.

Amerika ilifurahia ziada katika mafanikio ya kibiashara ambayo yaliidhamini kuwa na kifua cha kifedha ambacho ili kipatiliza kuwakopesha washirika wake ‘dola kuu za zamani’ kutoka katika dhiki za kiuchumi. Fauka ya hayo, iliweza kumakinisha hifadhi zake za dhahabu na kudhibiti madeni yake. Hivyo basi, ilisonga mbele kama mdhamini wa amani duniani kote. Ikiwa imetanua kutokamana na hadhi yake mpya ya kiulimwengu isiyokuwa na mshindani, ilianza kupiga njama za kisiasa na kuzindua vita vya ng’ambo ili kuweza kuwapokonya washirika wake makoloni yao mtawalia.

Katika miaka ya sitini (1960) baadhi ya mataifa ambayo yalikuwa yamedhoofika kiuchumi kutokamana na Vita vya Pili vya Dunia yalianza kunyanyuka na kurudi tena katika ulingo wa kimataifa japo chini ya udhibiti makini wa Amerika. Kwa upande mwingine, Amerika ilikuwa inakumbwa na mapungufu ya kibiashara na ilikuwa inataabika kifedha kutokana na kuzidi kwa matumizi ya ummah na mzunguko wa fedha. Vita vya Vietnam viliuvunja mgongo wa Amerika na kuisababishia hifadhi zake za dhahabu kupungua kiasi kwamba haikuweza kuhimili hitajio la ubadilishanaji wa dola ya Amerika kwa dhahabu.

Mnamo 1971 Amerika rasmi ikatangaza kusitisha ubadilishanaji wa dola kwa dhahabu na kuandaa mazingira ambayo yalipelekea kusitishwa rasmi kwa nidhamu ya ubadilishanaji kwa kiwango maalumu mnamo mwaka 1973. Hata hivyo, ubadilishanaji wa sarafu za mataifa mengine ulifungwa kwa dola ya Amerika ambayo haikunasibishwa na chochote isipokuwa kuwa na matumaini kwa nguvu za Amerika! Na hilo likapelekea milango ya uchocheaji wa mfumuko wa bei kutangazwa wazi kuwe imefunguliwa tangu wakati huo hadi sasa. Huku thamani ya dola ya Amerika ikiendelea kupungua kwa viwango vya kushtusha, ndivyo zilivyo nchi nyingine ambazo zimezitia sarafu zao katika mnyororo wa dola ya Amerika.

Majanga yanawiana na mfumuko wa bei. Janga la kupangiliwa la Covid-19 na mzozo wa Urusi na Ukraine tayari inayatishia mataifa duniani kote kutokamana na kuporomoka kwa sarafu zao ambazo haziwezi kuhimili mihemko ya kuagizia bidhaa kutoka ng’ambo na kutimiza majukumu ya kifedha kama vile kulipa mikopo. Hivyo basi, ikizilamisha tawala za kidemokrasia ili kuwalaza watu kwa kutumia ‘kuzidisha kiwango cha chini cha mshahara.’ Wanadai kwamba kuzidishwa kwa kiwango cha chini cha mshahara utawakinga ‘wafanyikazi’ kutokana na moto wa mfumuko wa bei! Alas! Ni mbinu tu ya kijinga ili kuwahadaa watu ambao ni vipofu wa kimfumo! Kisha tawala hiyo hiyo inasonga mbele na kuzidisha ushuru kwa bidhaa! Mfano mzuri ni utawala wa Kenya ambao umependekeza utozaji ushuru kwa bidhaa msingi ambazo awali zilikuwa hazitozwi ushuru, kisha Jumapili, Mei 1, 2022 utawala huo huo ukatangaza kuzidisha asilimia 12 ya kiwango cha chini cha mshahara!

Kiuhakika, mbinu hizo za kisiasa ndio kitambulisho cha tawala zote za kidemokrasia za kirasilimali ulimwenguni. Hudai kuwa wanawajali raia, lakini kiuhalisia wapo kwa ajili ya kulinda kipote cha warasilimali masekula ambao wanamiliki utajiri wote kwa gharama ya wanadamu wote duniani. Hiyo ndio sababu kwa nini idadi kubwa ya uongozi wa miungano ya wafanyakazi ni watiifu kwa matajiri warasilimali! Miungano ya wafanyikazi inatumika kama vyombo vya kudhibiti hisia za wafanyakazi. Hivyo basi, kuzidishwa kwa kiwango cha chini cha mshahara ni sera ya kisiasa isiyokuwa na natija yoyote ya kiuhakika. Badala yake vitanzi vya kiuchumi vinaendelea kukaza duniani kote pasina kuzingatia ima mtu ni mfanyakazi au la. Warasilimali masekula wanaendelea kukiritimba utajiri na serikali ipo kuwalinda wao kwa gharama yoyote ile. Kwa hiyo, kuzidishwa kwa kiwango cha chini cha mshahara ni suluhisho hadaifu la kuziba viraka.

Katika Uislamu hakuna suala la ‘kiwango cha chini cha mshahara.’ Kwa maana nyingine haitarajiwi kuwepo na maandamano ya wafanyakazi kutokamana na mfumuko wa bei. Kwa sababu Uislamu sio mfumo uliotungwa na mwanadamu kama vile mfumo wa kirasilimali wa kisekula. Badala yake ni kuwa Uislamu ni mfumo unaochipuza kutoka kwa Muumba, Mwenyezi Mungu (swt). Uislamu kama mfumo una nidhamu ambazo zinatatua kila tatizo linalowakabili wanadamu. Miongoni mwa nidhamu hizo ni ile ya utawala wa Dola ya Kiislamu ya Khilafah, Nidhamu ya Kijamii, Nidhamu ya Kiuchumi, Nidhamu ya Elimu na Nidhamu ya Mahakama.

Kuhusiana na suala la kiwango cha chini cha mshahara. Uislamu unapeana kipaumbele mkataba baina ya muajiri na muajiriwa, kwa sababu unaruhusu mtu ima kuwa muajiri au muajiriwa (mfanyakazi). Mwenyezi Mungu (swt) alisema: “أَهُمۡ يَقۡسِمُونَ رَحۡمَتَ رَبِّكَ‌ۚ نَحۡنُ قَسَمۡنَا بَيۡنَہُم مَّعِيشَتَہُمۡ فِى ٱلۡحَيَوٰةِ ٱلدُّنۡيَا‌ۚ وَرَفَعۡنَا بَعۡضَہُمۡ فَوۡقَ بَعۡضٍ۬ دَرَجَـٰتٍ۬ لِّيَتَّخِذَ بَعۡضُہُم بَعۡضً۬ا سُخۡرِيًّ۬ا‌ۗ وَرَحۡمَتُ رَبِّكَ خَيۡرٌ۬ مِّمَّا يَجۡمَعُونَ“Sisi tumewagawanyia baina yao maisha yao katika uhai wa duniani, na tukawanyanyua baadhi yao juu ya wengine kwa daraja nyingi; kwa hivyo baadhi yao wanawafanya wengine wawatumikie… [43. Az-Zukhruf: 32] Kwa kuongezea, Bukhari amesimulia kutoka kwa Abu Hurairah (ra) kwamba Mtume (saw) alisema:

»قَالَ اللَّهُ تَعَالَى ثَلاَثَةٌ أَنَا خَصْمُهُمْ يَوْمَ الْقِيَامَةِ رَجُلٌ أَعْطَى بِي ثُمَّ غَدَرَ، وَرَجُلٌ بَاعَ حُرًّا فَأَكَلَ ثَمَنَهُ، وَرَجُلٌ اسْتَأْجَرَ أَجِيرًا فَاسْتَوْفَى مِنْهُ وَلَمْ يُعْطِهِ أَجْرَهُ« ‏”‏‏.‏

“Mwenyezi Mungu alisema, ‘Nitakuwa ni adui kwa watu aina tatu Siku ya Kiama: 1- Mtu ambaye aliyefunga mkataba kwa kutumia Jina Langu, lakini akathibitisha hiana; 2- Mtu anayemuuza mtu huru na kisha kula pesa hizo; na 3- Mtu anayemuajiri mfanyakazi na kunufaika kutokana na kazi yake kiukamilifu lakini hamlipi malipo ya kazi aliyofanya.’”

Kwa kuzingatia hayo hapo juu ni wazi kwamba ajira ni kutoa manufaa kutoka kwa aliyeajiriwa na kumpa muajiri na kutoa mali kutoka kwa muajiri na kumpa muajiriwa. Hivyo basi, inaweza kuelezwa kuwa ni mkataba wa kutoa manufaa kwa malipo. Mkataba wa kuajiri mfanyakazi ima ni kwa msingi wa kupata manufaa yanayotokana na kazi iliyofanywa na mfanyakazi au manufaa kutoka kwa mfanyakazi mwenyewe moja kwa moja. Lau mkataba msingi wake ni kupatikana manufaa kutokana na kazi, basi suala lililofungiwa mkataba ni manufaa yanayotokana na kazi. Mfano wa mkataba aina hiyo ni kama kumuajiri mhunzi, seremala n.k. Hata hivyo, lau mkataba msingi wake ni kupatikana manufaa kutokana na mtu mwenyewe, basi suala lililofungiwa mkataba ni manufaa yanayotokana na mtu. Mfano wa mkataba aina hiyo ni kumuajiri mkulima, mfanyakazi kiwandani, mfanyakazi serikalini, msaidizi wa nyumbani n.k. [Nidhamu ya Kiuchumi (kitabu cha Hizb ut Tahrir kopi ya Kiengereza), uk. 84 – 86].

Natija ni kuwa kuajiri kunahusisha kupatikanwa kwa manufaa kutoka kwa kitu kilicho ajiriwa. Ama kuhusiana na mfanyakazi, kuajiri ni kutumia juhudi yake. Kwa hiyo ni dharura katika ajira, kufafanua aina ya kazi, muda wa kazi, mshahara na juhudi inayohitajika. Lazima kazi ifafanuliwe ili iweze kujulikana kwa sababu ajira isiyojulikana ni batili (Fasid). Pia ni jambo la dharura kuweka wazi muda wa kufanyakazi, kama vile itakuwa ni kila siku, mwezi au mwaka. Vilevile, mshahara wa mfanyakazi lazima ufafanuliwe tokea mwanzo. Ibn Mas’oud (ra) alisema kwamba Mtume (saw) alisema:

‫                »إذا أجره ‫فليعلمه ً‫أجيرا ‫أحدكم ‫استأجر«

“Lau mmoja wenu ataajiri mfanyakazi basi amwambie mshahara wake,” kama ilivyoripotiwa katika Kanz al-Ummal na al-Daraqutni. Zaidi ya hayo, Mwenyezi Mungu (swt) alisema: لَا يُكَلِّفُ ٱللَّهُ نَفۡسًا إِلَّا وُسۡعَهَا‌ۚ “Mwenyezi Mungu haikalifishi nafsi yoyote ila kwa kadiri ya iwezavyo.” [2. Al-Baqarah: 286] Bukhari na Muslim wamesimulia kutoka kwa Abu Hurairah kwamba Mtume (saw) alisema: «إِذَا أَمَرْتُكُمْ بِشَىْءٍ فَخُذُوا مِنْهُ مَا اسْتَطَعْتُمْ» “Lau nitawaamrisha mufanye jambo, basi lifanyeni kwa kadiri ya munavyoweza.” Nidhamu ya Kiuchumi (kitabu cha Hizb ut Tahrir kopi ya Kiengereza), uk. 87].

Ni muhimu kutambua kwamba Uislamu unatilia mkazo mkataba na sio suala la kiwango cha chini cha mshahara. Kunapotokea mzozo aina yoyote baina ya waliofunga mkataba, basi Khalifah atatatua masuala yaliyochipuza kutokana na mkataba huo. Kukiwa na utepetevu aina yoyote upande wa Khalifah, basi mmoja kati ya waliofunga mkataba ataielekea Mahkamat ul-Madhalim (Mahakama ya Vitendo vya Kudhulumiwa) ili kupata utatuzi. Kwa hiyo, maandamano ya kiviwanda hayatokuwepo kwa sababu kutakuwepo na nyenzo za kutatua mapungufu yoyote baina ya waliofunga mkataba. Kwa kuwa kufanyakazi ni kitendo cha Ibadah (kuabudu) kwa hiyo hakuna chochote kitakachoruhusiwa kwa sharti kinakwenda kinyume na maamrisho ya Kiislamu.

Mkataba wa ajira katika Uislamu unapeana kipaumbele vigezo vinne: 1-aina ya kazi, 2-muda wa kazi, 3-juhudi inayotarajiwa na 4-kiwango cha mshahara. Ugumu wa maisha au mfumuko wa bei hauzingatiwi kuwa ni sehemu ya mkataba. Hata hivyo, mkataba unaweza kuvunjwa na muajiri lau hawezi kumudu baadhi ya nukta mfano mshahara. Mfanyakazi anaweza kuuvunja mkataba na kukaa mezani na muajiri wake na kufunga mkataba mpya au akaamua kutafuta ajira mahali pengine lau kwa mfano anahisi kuwa mshahara anaopata haukidhi mahitaji yake. Lakini ni haramu kuzusha fujo, kufanya ghasia, kumuibia muajiri eti wadai nyongeza katika kiwango cha chini cha mshahara.

Katika serikali ya Khilafah raia wote wataamiliwa kwa usawa mbele ya Shari’ah ya Kiislamu pasina na kuzingatia wanafanyakazi au la. Serikali ya Kiislamu itajituma kuwawezesha raia wake kukidhi haja zao msingi ambazo ni chakula, mavazi na makazi; na mahitaji ya kijamii ambayo ni matibabu, elimu na usalama. Raia wote watafurahia mahitaji msingi na kijamii pasina kuzingatia dini zao, hali zao (umasikini au utajiri) au kabila. Khalifah, mtawala na wanaotawaliwa wote wataamiliwa sawa mbele ya Shari’ah ya Kiislamu na HAKUNA ulinzi kwa kuwa yuko afisini kama invyosemekana katika mfumo wa kirasilimali ambapo watawala wako katika bonde lao na wanaotawaliwa wakiwa juu ya jingine!

Kuhusiana na suala la mfumuko wa bei, serikali ya Khilafah iliyosimamishwa kwa njia ya Utume itatumia dhahabu na fedha kama sarafu yake.  Hii itailinda kutokamana na uhaini wa kifedha unaendelezwa na tawala za kirasilimali za kisekula. Hivyo basi, kupelekea dola kuwa imara kindani na kutatua masuala ya mfumuko wa bei kwa mpigo. Kwa upande mwingine, itatekeleza sera ya kujitosheleza na kusafirisha nje ziada kwa kubadilishana kwa dhahabu na fedha kwa kila atakayekuwa tayari kufanyakazi na Khilafah miongoni mwa nchi ambazo haziko vitani nazo. Kwa kuongezea, raia hawatoporwa mali zao kupitia utozaji ushuru wenye kutiliwa shaka na ukandamizaji kama inavyoshuhudiwa ndani ya tawala hizi za kirasilimali za kisekula.

Kwa kutamatisha, kiwango cha chini cha mshahara na mfumuko wa bei zote zimebuniwa kimakusudi na kila moja hutumika kama njama ya kisiasa kutoka kwa wale walioko uongozini au wanaotaka kuingia uongozini. Viongozi masekula walio na uchu wa mamlaka wanaweza kuchochea mizozo ya kiviwanda ili kuweza kuwapindua walioko madarakani. Kwa upande mwingine, walioko mamlakani wanaweza kupatiliza fursa ya kuuza sura ili kujikurubisha kwa raia vipofu wa kisiasa, kijamii na kiuchumi kwa ajili ya kujinusuru na janga linalowakodolea macho kwa kujaribu kuzidisha kiwango cha chini cha mshahara kisha kukipora kupitia ushuru! Suluhisho la kimsingi pekee kwa matatizo yanayomkabili mwanadamu ni #TurudisheniKhilafah.

Ali Nassoro Ali

Mwanachama wa Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir

Comments are closed.