Ameer Suali na Jawabu

Matukio ya Kisiasa Ndani ya Kurdistan na Iran

Kusambaza ni Kuunusuru Uislamu

بسم الله الرحمن الرحيم

Majibu ya Maswali
(Imetafsiriwa)

Swali:

Mnamo tarehe 06/01/2018, Iran ililituhumu jimbo la Kurdistan kuwepo nyuma ya maandamano ya nchini Iran, na mnamo 07/01/2018 jimbo la Kurdistan lilikanusha tuhma hizi. Kumegunduliwa ripoti za habari wakati wa maandamano makubwa yaliyo fanyika jimbo la Kurdistan, hususan katika mkoa wa Sulaymaniyah mnamo 19/12/2017, zinazo sema kwamba Iran ilicheza dori kubwa katika maandamano hayo. Je, yaweza kusemwa kwamba jimbo la Kurdistan lilikuwa na mkono wake ndani ya maandamano hayo ya Iran mnamo 28/12/2017 kama kesi ya kulipiza kisasi? Kwa maana nyengine:

1- Je, yaliyotokea nchini Iran na katika jimbo hilo ni kama hatua ya kukirudi kitendo? 2- Je, maeneo haya mawili yalichukua hatua za haraka kibinafsi au nguvu kutoka nje iliyasukuma? 3-Ikiwa ni hivyo, nguvu hii ni nani? Je, maandamano haya yanakusudia kubadilisha serikali katika jimbo hilo au Iran? Na Allah akulipe kheri.

Jibu:

Matukio mawili haya sio hatua ya kukirudi kitendo, na tuhma za Iran kwa Erbil ni aina mojawapo ya kuchanganyikiwa kisiasa kutokana na natija ya matukio ya ndani. Erbil kwa sasa hivi imeshughulishwa na mgogoro wake, ambao unakaribia kulivuruga eneo lake, na haina uwezo kulingana na dhurufu zake za sasa, kuingia katika barabara za Iran! Kuchanganyikiwa huku kisiasa kulikuwa wazi wakati Iran ilipo zituhumu nguvu kadhaa kwa uchochezi wa maandamano hayo; maafisa wa Iran wamezilaumu nguvu za kigeni. Balozi wa Iran wa Umoja wa Mataifa, Ghulam Ali Khoshro, alisema mnamo Ijumaa: “Kwamba Tehran ina ushahidi mzito kuwa “maandamano” haya yamepokea muongozo wazi wazi kutoka ng’ambo”… (BBC Arabic 07/01/2018). Hivyo basi, tuhma za Iran kwa Erbil zimo ndani ya kuchanganyikiwa huku: (Katibu wa Baraza la Ushauri la Iran, Mohsen Rezai, alisema mnamo 6/1/2018 kuwa maelezo zaidi ya mandhari ya matukio nchini Iran yalipangwa mjini Erbil, jimbo la Kurdistan la Iraq … (Russia Today 07/01/2018). Jimbo hilo limekanusha tuhma hizo kupitia Sven Dzii, msemaji wa jimbo hilo (Chanzo chake kimetangulia kutajwa). Hivyo basi, kadhia sio kukirudi kitendo, lakini kila mmoja ana malengo na masharti yake. Lakini, matukio hayo mawili yalianza kwa ghafla na kisha kuzungukwa na dhamira kutoka nje ili kufikia malengo yanayo husiana na jimbo hilo na Iran. Kuambatana na msururu wa matukio hayo, ufafanuzi wake ni kama ifuatavyo:

Kwanza: Matukio Jimboni Humo

1- Mashirika kadhaa ya habari yaliripoti kuzuka kwa maandamano mnamo 19/12/2017 eneo la Sulaymaniyah, miongoni mwa walimu na wafanyikazi ambao hawakuwa wamelipwa mishahara yao kwa muda wa miezi kadhaa, na kisha maandamano hayo yakajumuisha sehemu kubwa ya wakaazi wa mkoa wa Sulaymaniyah, na kisha kuenea sehemu nyenginezo za mkoa huo zikiwemo sehemu za mkoa wa Erbil. Kujihusisha kwa haraka kwa raia katika maandamano haya ni natija ya watu kutoridhika na hali ya kiuchumi ya jimbo hilo baada ya kushuka kwa kiwango cha rasilimali kuu za mafuta jimboni humo kutokana na Baghdad kuudhibiti mkoa wa Kirkuk pamoja na shinikizo nyenginezo zilizotiwa na Baghdad, hususan kufungiwa kwa ndege za kigeni kutua viwanja vya ndege mikoani Erbil na Sulaymaniyah, iliyoongezea matatizo ya usafiri kuelekea ng’ambo, huku ikiwalazimu wasafiri kusafiri kupitia uwanja wa ndege wa kimataifa wa Baghdad. Kilichotia msumari wa moto kwenye kidonda ni tuhma za ufisadi na ufujaji mali dhidi ya maafisa wa serikali wenye ushawishi mkubwa jimboni humo. Maandamano hayo yalisambaa kama moto nyikani, hususan katika maeneo ambayo ushawishi wa vyama vya Kikurdi dhidi ya Masoud Barzani na Chama chake cha Kidemokrasia cha Kurdistan ni mkubwa. Kuhama kwa familia za Kikurdi kutoka Kirkuk na kwengineko na kuja jimboni humo kumechochea kuzorota kwa hali mbaya za kimaisha huku kukiwa na hofu ya kuzuka kwa harakati pinzani ndani ya jimbo hili. Yote haya yanaashiria kuwa harakati hizi ni za kihamasa.

2- Maandamano haya yaliongozwa kimsingi dhidi ya serikali ya mkoa wa Erbil, inayo dhibitiwa na Chama cha Kidemokrasia cha Kurdistan, chama cha Barzani, aliye mafichoni baada ya kujiuzulu kwake kutokana na uraisi wa eneo hilo nyuma ya mpwa wake Nechirvan Barzani, na hili hufahamika kwa namna nyingi, zikiwemo:

A – Maandamano haya yalizuka kuanzia mkoani Sulaymaniyah, mkoa unaodhibitiwa na harakati na vyama vinavyo mpinga kibaraka wa Uingereza Masoud Barzani. Ngome ya vuguvugu la mabadiliko ni mkoa wa Sulaymaniyah, na tawi lenye nguvu la Talabani ndani ya Chama cha Umoja wa Kizalendo ni mkoa wa Sulaymaniyah vile vile. Vyama hivi vina uwezo wa kuchochea na kuandaa matukio ingawa havina uwezo wa kudhibiti matukio yote.

B – Taarifa ya Nechirvan, inafahamika kana kwamba maandamano hayo yanaongozwa dhidi ya serikali yake: “Raisi wa serikali ya jimbo la Kurdistan, Nechirvan Barzani, ameonya kuwepo kwa “njama kubwa” iliyo anzishwa dhidi ya jimbo hili na ni kubwa mno iliyopita taswira ya mtu yeyote”, na akagusia kuwepo kwa “vyama vinavyotaka kuleta fujo katika jimbo hilo na kuyapoteza mwelekeo maandamano hayo na kueneza ghasia”. Aliongeza kusema: “Kuna mikono fiche nyuma inayo jaribu kusababisha fujo katika Kurdistan na tutazima jaribio hilo,” akikusudia vyama hivi, ambapo hakuvitaja majina, “vinavyo unga mkono juhudi hizo za kuzua fujo, lakini halmashauri za kiusalama jimboni humu zitakabiliana vikali na hali hizi…” Alifafanua kuwa: “Tunakabiliwa na tishio hatari na njama kubwa zaidi ya taswira ya mtu yeyote, yaliyotokea katika mkoa wa Sulaymaniyah ni majaribio ya kuhujumu usalama na utulivu,” akitoa wito wa haja ya umoja na ushirikiano kwa wote kuweza kuyadhibiti haya. (Tovuti ya Kurdish Basnews, 21/12/2017)

Kwa maneno haya anajaribu kuvifahamisha vyama vya Kikurdi vinavyo pinga vikali kura ya maamuzi mkoani Sulaymaniyah, na vilivyo na mafungamano na Waamerika na wafuasi wao katika miji mikuu ya Baghdad na Tehran. Kutokana na vyama hivyo vilivyo chochea upinzani na maandamano dhidi ya serikali ya Barzani: vugu vugu la mabadiliko, lililozuka baada ya kugawanyika kutoka kwa Muungano wa Kitaifa msukumo wa pili wa kisiasa katika uchaguzi wa 2009 jimboni Kurdistan. Baada ya upinzani huo, vugu vugu hilo la mabadiliko, lililoongozwa na Gorran na kundi hilo la Kiislamu, lilijiondoa kutoka katika serikali ya Erbil, na kinara wa kundi hilo, Yassin Hassan, alisema katika mahojiano na Al Jazeera, “Baada ya kuwafyatulia risasi waandamanaji, kundi hilo la Kiislamu na vugu vugu la mabadiliko yaliamua kujiondoa kutoka kwa serikali hii kikamilifu, na hivyo tunataka kuvunjiliwa mbali kwa serikali hii mara moja na kuundwa kwa serikali ya uokovu wa kitaifa.” (Al Jazeera Net 21/12/2017)

Shirika la habari la BBC mnamo 26/12/2017 pia liliripotia msimamo wa mmoja wa viongozi wa vugu vugu hilo la mabadiliko, Yusuf Muhammad, na Raisi wa bunge la jimbo la Kurdistan nchini Iraq. Alijiuzulu ili kudhaifisha msimamo wa serikali ya Erbil mbele ya upinzani; Raisi huyo wa bunge la jimbo la Kurdistan nchini Iraq alitangaza kujiuzulu kwake kupinga dhidi ya kile alicho kiita kudhibitiwa mamlaka halali na kikundi au vikundi vya watu fulani pekee. Yusuf Muhammad alikikashifu vikali kikundi hicho cha watu juu ya kudhibiti siasa, uchumi, ardhi, mali na nyanja zote za maisha, pamoja na ubaguzi katika ugavi wake jimboni humo. Alisema kuwa kukataa kwa Amerika kura hiyo ya maamuzi, iliyo wakilishwa katika barua iliyo tumwa na Waziri wa Kigeni wa Amerika Rex Tillerson ni fursa ya dhahabu iliyopotezwa na serikali ya jimbo hilo… (BBC 26/12/2017) Hiki ni kiashiria cha utiifu wa bwana huyu na vugu vugu lake.

3- Hivyo basi, kuanza kwa maandamano kuanzia mkoa wa Sulaymaniyah, yaliyo ongozwa na vyama pinzani kwa Chama cha Kikurdi cha Kidemokrasia cha Barzani, kushiriki kwa viongozi wa wa vyama hivi katika maandamano haya, kukamatwa kwa baadhi ya viongozi hao na majeshi ya usalama, kujiondoa kwa vyama hivi kutoka katika serikali ya Erbil ili kuidhaifisha, kulingania kuvunjiliwa mbali kwake, kujiuzulu kwa kinara wa bunge miezi michache kabla tarehe iliyo pangwa ya uchaguzi, na tishio la Al-Abadi jijini Baghdad la kuingilia kati, yote yanaashiria kuwa mwanzo, ingawa ghafla, una mwelekeo wa pili wa malengo yatokayo nje yanayolizunguka vugu vugu hili la kimaumbile ili kufikia malengo yanayo husiana na jimbo hili.

Mwelekeo huu wa pili ni natija ya shinikizo la makundi ya kieneo ya upinzani wa Kikurdi dhidi ya ushawishi wa Barzani, pamoja na shinikizo za Baghdad za kuing’oa serikali ya Barzani mkoa wa Erbil. Ikifuatiwa na yale yaliyosikika kutoka Uturuki, Iran na Baghdad ya haja ya kuwaadhibu waliohusika na tukio la kura ya maamuzi ya kuitenga Kurdistan, na vyama vyote hivi na serikali zote hizi ni tiifu kwa Amerika, ikiongezewa katika hili, kinacho shuhudiwa katika sera ya Trump jimboni humo, pamoja na mwito wa “Amerika Kwanza”, ni kuwa Amerika haija tosheka na sera yake inayo tekelezwa maeneo ambayo vibaraka wa Uingereza wanapatikana, bali ikiwa maslahi yao katika baadhi ya maeneo yatahitaji, itawaadhibu au kuwadhalilisha, kama ilivyotokea katika usanii wa kampeni dhidi ya ufisadi nchini Saudi Arabia, na kama inavyo jitokeza leo kwa viongozi wa chama cha Peoples’ Congress jijini Sanaa baada ya kuuwawa kwa Swaleh. Hivyo basi, Amerika inawasukuma vibaraka wake wa kieneo na wa jimboni humo kutia shinikizo zaidi kwa serikali ya Barzani kuing’oa na kumaliza utawala wa Uingereza juu ya serikali ya Erbil. Ikiwa haitaweza kufanya hili hivi karibuni, itaunda dhurufu kwa ajili ya hilo kupitia shinikizo za kufuatana.      

Hili ndilo aghalabu lililotokea na linalotokea jimbo la Kurdistan

Pili: matukio nchini Iran

1- Maandamano yaliyozuka mnamo 28/12/2017 yalianza kupinga hali ya kiuchumi na hali za kimaisha za watu, ukosefu mkubwa wa ajira, umasikini na kiwango kikubwa cha bei za bidhaa; inaripotiwa kuwa kiwango cha ukosefu wa ajira kiko juu mno. Waziri wa mambo ya ndani wa Iran, Abdul Ridha Rahmani Fadhli, alifichua katika mkutano wa waandishi habari mnamo 1/10/2017 kuwa “kiwango cha ukosefu wa ajira kwa sasa kinazidi asilimia 12% huku asilimia hii katika baadhi ya miji ya Iran ikifikia 60%, ikiwemo Ahwaz (eneo la Waarabu) na Kermanshah (eneo la Wakurdi) na Baluchistan. Kiwango hiki cha ukosefu wa ajira miongoni mwa watu wanaomiliki shahada ya sayansi na waliohitimu chuo kikuu kiko juu mno… ” (2/10/2017). Ripoti zinaonyesha kuwa asilimia 21% ya waliohitimu chuoni hawana ajira, na kwamba milioni 15 ya Wairani wanaishi chini ya msitari wa umasikini hii ikimaanisha kuwa natija ya kutekelezwa kwa nidhamu ya kirasilimali athari yake mbaya inajitokeza kwa raia jumla nchini humo kama ilivyo hali katika nchi zote zinazo tekeleza nidhamu hii ya kimagharibi, na kwa kuwa nidhamu ya kiuchumi ya kirasilimali inatekelezwa nchini Iran, ugavi wa rasilimali huko ni mbaya, kuna ulimbikizaji wa mali katika mikono ya matajiri wachache na kuwanyima wengi kutokana na kujinufaisha kwayo. Zaidi ya hayo, huko kuna kufeli katika kukabiliana na kadhia ya umasikini, mabenki huko yanaendeshwa kwa riba, na huko kuna utekelezwaji wa nidhamu ya kidhulma ya ushuru katika rasilimali iliyo fungamanishwa na sera na mapendekezo ya Mfuko wa Fedha wa Kimataifa (IMF).

Na kabla ya matukio ya hivi karibuni, ujumbe kutoka Mfuko wa Fedha wa Kimataifa (IMF) ulizuru Tehran mnamo 18/12/2017; daima hufanya mashauriano ya kila mwaka pamoja na serikali ya Iran. Kinara wa ujumbe huo, Catriona Purfield, aliwahutubia maafisa wa Iran: “Kutokana na hali hii isiyo tabirika na kuongezeka kwa hofu katika nidhamu ya kifedha ya Iran, serikali yapasa kuongeza kasi mageuzi katika mabenki na kuongeza mtaji wa mabenki na taasisi za utoaji mikopo. Aliongeza kusema kuwa: “Tathmini ya ubora wa rasilimali inapaswa kuanza kufanywa mara moja, mikopo ya wahusika inapaswa kutathminiwa, na mipango kuanzishwa kuzigeuza rasilimali za benki na kuwa pesa taslimu ili kutatua tatizo la mikopo iliyo telekezwa ulipaji wake… gharama za ugeuzaji huu wa rasilimali za benki zaweza kumudiwa kupitia utoaji bondi za mikopo za serikali,” aliongeza kusema (Ukurasa rasmi wa Al-Alam ya Iran 19/12/2017). Na utekelezwaji wa matakwa hayo ya serikali ulisababisha ongezeko la bei, ukosefu wa ajira na umasikini uliyo pelekea watu kuishi katika hali mbaya na maandamano dhidi ya serikali hii, na kupelekea watu kudhihirisha mateso yao kwa njia zote.

2- Maandamano haya yalianzia jijini Mashhad lililo Mashariki mwa Iran, mwito ukiwa “Tunapinga ongezeko la bei,” lakini baadaye kuenea hadi miji 80. Maelfu ya vijana na wafanyi kazi walishiriki na walighadhabishwa na maafisa wafisadi, ukosefu wa ajira na kupanuka kwa mwanya baina ya matajiri na masikini. “Maandamano haya yalitokana na mambo matatu: kwanza, ni sera ngumu za IMF katika kufanya marekebisho ya kiuchumi, na pili, udhaifu wa serikali na maafisa wake katika kutatua matatizo ya kiuchumi, na mwisho; kukwepa uwazi na kuhisabiwa katika maamuzi yanayofanywa na serikali,” Ahmad Tavakkoli, mwenyekiti wa shirika la uwazi na haki nchini Iran, alisema katika mahojiano na shirika la habari la Fars mnamo 30/12/2017 “Yote haya yanapaswa kuongezewa katika matumizi ya nje ya Iran kwa wanamgambo na wafuasi wao nchini Lebanon, Syria na Yemen.

Hii inalifanya tatizo la kiuchumi kuwa mzigo mkubwa kwa Wairani, mpaka kuwapelekea kuandamana na hata zaidi ya hili; kuituhumu serikali kwa usaliti wa maisha ya raia wake. “Wairani wengi wanaamini kuwa hakuna haja ya serikali yao kulisaidia kundi la Hamas eneo la Gaza, Hezbollah nchini Lebanon, serikali ya Assad nchini Syria, Mahouthi nchini Yemen, huu ni usaliti” (Arabic 21: 01/01/2018). Yote haya yanaonyesha kuwa kuanza kwa maandamano haya ilikuwa ghafla yakihusiana na mambo ya uchumi. Lakini serikali ilikabiliana nayo kwa kutumia nguvu na kupelekea vifo na majeruhi. Baadhi ya ripoti zinaonyesha kuwa idadi ya waliotiwa nguvuni tangu kuanza kwa maandamano hayo mnamo 28/12/2017 imeongezeka na kufikia zaidi ya 1,700. (BBC Arabic 07/01/2018).

3- Inajulikana kuwa maandamano yoyote ya kiuchumi ikiwa yatacheleweshwa kutatuliwa kwake, kwa utatuzi sahihi, hususan ikiwa yatakabiliwa kwa kutumia nguvu, yatafuatiwa na maandamano ya kisiasa, na hayo ndiyo yaliyotokea. Miito ya kisiasa iliongezwa juu ya miito ya kiuchumi dhidi ya serikali na wale wanaoidumisha, na kukashifu uingiliaji kati wa serikali katika vita vya eneo hilo na kutumia mabilioni ya dola juu yake. Maandamano haya yalianza kutawaliwa na miondoko ya kisiasa inayopinga serikali na kushambulia nembo za serikali hii na viongozi wake. Kisha matukio haya yakatumiwa na Ulaya na Amerika; vyombo vya habari vya Ulaya vilionekana kuyashabikia maandamano haya, hususan Uingereza kama shirika la habari la BBC na runinga yake. Kwa upande wake, Raisi wa Ufaransa Macron alisema katika kujibu swali la gazeti la Al-Hayat kuhusu matukio nchini Iran, lililo chapishwa na gazeti hilo mnamo 4/1/2018: “Maandamano hayo yanamulika uwazi katika mujtamaa wa raia wa Iran. Hili lilinifanya kuwasiliana na Raisi Rouhani ili kumkumbusha haja ya kuepukana na ghasia na kuruhusu uhuru wa kujieleza kwa raia. Tutasubiri na kuona ule uwazi unaohitajika kwa Iran kwa jinsi itakavyo kabiliana na waandamanaji hao ili tuweze kuhukumu baadhi ya mambo huku tukifanya maandalizi ya ziara iliyo pangwa ya Waziri wa Kigeni wa Ufaransa, Le Drian nchini Iran na kisha ziara yangu nchini humo.” Na akatoa wito wa kuendelezwa kwa mazungumzo ya kudumu pamoja na Tehran. Lakini uingiliaji kati wa Ulaya kupatiliza matukio haya hauna thamani kwa kuwa sio thabiti.

4- Uingiliaji kati ulio na thamani ni wa Amerika. Raisi wa Amerika Trump alituma ujumbe katika ukurasa wake wa mtandao wa Twitter na kusema mnamo 1/1/2018 “Raia wa Iran hatimaye wanapinga dhidi ya ukatili wa serikali fisadi ya Iran. Pesa zote ambazo Raisi Obama aliwapa kwa ubwege zilielekezwa katika ugaidi na “mifukoni” mwao. Raia wana uhaba wa chakula, mfumko wa bei na ukosefu wa haki za kibinadamu, Amerika inatazama.” Waziri wa Habari katika ikulu ya White House alisema: “Idara ya Trump inajali mno. Maelfu ya waandamanaji hawa wametiwa gerezani na serikali,” akaongeza: “Kamwe hatutanyamaza kimya huku udikteta wa Iran ukigandamiza haki msingi za raia wake na tutawahisabu viongozi wa Iran kwa ukiukaji wowote.” (Gazeti la kielektroniki la Iraq 10/1/2018). Wengi wa maafisa wa Amerika, wakiongozwa na Raisi Donald Trump, wamewaunga mkono waandamanaji wa Iran dhidi ya serikali kuanzia siku ya kwanza. Mwakilishi wa kudumu wa Amerika katika Umoja wa Mataifa, Nikki Haley, aliliambia Baraza la Usalama la Umoja huo mnamo Ijumaa kuwa Amerika inawaunga mkono waandamanaji wa Iran, alisema, “Watu wa Iran wanalilia uhuru wao, ufanisi kwa familia zao na hadhi kwa taifa lao,”. Wito wa Washington kwa Baraza la Usalama ni dalili wazi kuwa Amerika ndiyo inayo endesha mawimbi ya maandamano, na kasi ya wito huo iliwashangaza wanachama wa Baraza hilo la Usalama. “Wanachama wa Baraza hili la Usalama walishangazwa na wito wa Haley wa kuitisha mkutano wa haraka wa Baraza la Usalama kujadili maandamano nchini Iran, lililazimika kutia shinikizo kwa upinzani nchini Urusi kuhudhuria mkutano huu,” Mwandishi wa BBC Barbara Pelt. Mjumbe huyo wa Amerika katika Baraza la Usalama alisema kuwa Washington inasimama “pasi na kuyumba pamoja na wale walioko nchini Iran wanaotafuta uhuru wao na ufanisi kwa familia zao na hadhi kwa taifa lao” (BBC Arabic 06/01/2018)

5- Hili linaibua swali: Je, usaidizi wa Amerika kwa maandamano haya nchini Iran unamaanisha kwamba wanafanya katika kuipindua serikali ya Iran? Au ina lengo jengine inalotafuta kupitia kudandia mawimbi ya maandamano nchini Iran? Kujibu hili, tunasema yafuatayo:

Ama kusema kuwa usaidizi wa Amerika kwa hatua hizo ni kwa lengo la kubadilisha serikali sio sahihi kwa sababu wamesema hivyo wenyewe; Naibu Waziri wa Kigeni kwa Iraq na Iran, Andrew Beck, alisema katika gazeti la Al-Hayat lililo chapishwa mnamo 4/1/2018: “Tunazungumzia tu kuhusu kulindwa kwa waandamanaji na mwishowe tunataka kuona mabadiliko katika miondoko ya serikali hii kwa njia zaidi ya moja, lakini haswa kwa waandamanaji” na kusisitiza kuwa “idara hiyo inataka mabadiliko katika miondoko ya serikali hii na wala haitaki kuibadilisha serikali hio nchini Iran…” [imetafsiriwa kutoka kiarabu]. Amerika na dori yake katika serikali hio inajulikana; tulitaja hili nyuma katika “Jibu la Swali” mnamo 21/08/2013: (Dori ya Amerika katika mapinduzi ya Iran lilikuwa wazi kuanzia mwanzo… na matendo yote ya kisiasa ya eneo hili yanayo tekelezwa na Iran yote yanaafikiana na miradi ya Amerika …), na pia tulisema katika jibu jengine “Jibu la Swali” mnamo 23/02/2017 (Hivyo basi, dori ya Iran eneo hili ni sera ya Amerika iliyofanyiwa utafiti kwa umakinifu, na kwamba dori hii hupanuka na kunyauka kulingana na matakwa ya sera ya Amerika na kulingana na dhurufu), na kwa hivyo, kutangazwa kwa usaidizi wa Amerika kwa maandamano haya sio kwa lengo la kubadilisha nidhamu ya utawala iliyoko kwa sasa.

6- Hivyo basi ni kwa nini Amerika imelidandia na kulitumia wimbi hili? Hili ni muhimu kwa sababu mbili:

Kwanza, ni kuhamisha purukushani kutoka kwa kadhia ya Palestina na taarifa ya Trump kuhusu Al-Quds “Jerusalem” na kulishughulisha eneo hili kwa kadhia ya Iran. Hilo, ni ili igeuke kuwa adui nambari moja katika eneo hilo, na kisha watu wote kuiangazia Iran na si kwengineko, na kufifisha kuangaziwa kwa umbile la Kiyahudi, mvamizi wa Palestina.

Pili, ni kutafuta uhalalishaji wa kubakia hai kwa vibaraka wa Amerika eneo hili chini ya kisingizio cha kusimama dhidi ya Iran na kuilinda Amerika kutokana na hatari ya Iran. Taarifa ya Trump kuhusu Al-Quds (Jerusalem) na kuwa huu ndio mji mkuu wa umbile la Kiyahudi (ambao ni uadui mkubwa zaidi kwa Waumini) kama tulivyo sema katika toleo letu la 7/12/2017 ni kofi migongoni mwa vibaraka wa Amerika “Al-Quds (Jerusalem) imo ndani ya nyoyo na akili za Waislamu, na kunyamaza kimya kwa vibaraka hao juu ya taarifa ya Trump na kuendelea kwao kuwa vibaraka na kuiridhisha Amerika ni kashfa kubwa kwao … taarifa ya Trump dhidi ya Iran ilikuwa ni kamba waliyoning’inia kwayo kuhalalisha kuendelea kwao kuwa vibaraka wa Amerika licha ya taarifa ya Trump kuhusu Jerusalem … kwa kusema kuwa Trump anasimama usoni mwa Iran, adui mkuu, ni udhuru mbaya kushinda uhalifu. 

قَاتَلَهُمُ اللَّهُ أَنَّى يُؤْفَكُونَ﴿

“Allah awaangamizilie mbali! Vipi wanapotoka na haki?” [Al-Munafiqun: 4]

7- Huu pengine ndio ufafanuzi sahihi wa yale yaliyokuwa yakiendelea nchini Iran kuhusiana na maandamano yake  na taarifa za kutoka ughaibuni, hususan za Amerika.

Kwa kutamatisha, kuhadaiwa na nchi za kikoloni za kikafiri kwa mustakbali wa biladi za Waislamu imewezekana pekee kwa sababu ya watawala waovu (Ruwaibidha) wanaozitawala na kwamba wao ni watiifu kwa maadui wa Uislamu na Waislamu, na kuwafuata. Mtume wa Allah (saw) amelionya hili katika yale anayosimulia Ahmad katika Musnad yake kutoka kwa Abu Hurayrah kwamba amesema: Mtume wa Allah (saw) amesema:

«إِنَّهَا سَتَأْتِي عَلَى النَّاسِ سِنُونَ خَدَّاعَةٌ يُصَدَّقُ فِيهَا الْكَاذِبُ وَيُكَذَّبُ فِيهَا الصَّادِقُ وَيُؤْتَمَنُ فِيهَا الْخَائِنُ وَيُخَوَّنُ فِيهَا الْأَمِينُ وَيَنْطِقُ فِيهَا الرُّوَيْبِضَةُ قِيلَ وَمَا الرُّوَيْبِضَةُ قَالَ السَّفِيهُ يَتَكَلَّمُ فِي أَمْرِ الْعَامَّةِ»

“Kwa hakika watu watajiliwa na miaka ya uhadaifu; mrongo atasadikishwa na mkweli atakadhibishwa; khaini ataaminiwa na mwaminifu atafanywa kuwa khaini; na Ruwaibidha ndio watakaotamka (maamuzi). Ikaulizwa: Ruwaibidha ni kina nani? Akasema: Watu masafihi wanaozungumzia juu ya mambo jumla ya Umma.”

Imesimuliwa na Al-Hakim katika Al-Mustadrak na kuiorodhesha kama Hadith Sahih. Matatizo ya Umma huu ni watawala wake, lakini ni Umma bora ulioletwa kwa wanadamu; hautabakia kimya kwa muda mrefu juu ya utawala dhalimu wa Ruwaibidha hawa. Mtume wa Allah (saw) ametupa bishara njema ya kurudi kwa Khilafah Rashida baada ya utawala huu dhalimu kama ilivyotajwa katika Musnad ya Imam Ahmad na At-Tayalisi kutoka kwa Hudhayfah ibn Al-Yaman:

«… ثُمَّ تَكُونُ مُلْكًا جَبْرِيَّةً، فَتَكُونُ مَا شَاءَ اللَّهُ أَنْ تَكُونَ، ثُمَّ يَرْفَعُهَا إِذَا شَاءَ أَنْ يَرْفَعَهَا، ثُمَّ تَكُونُ خِلَافَةٌ عَلَى مِنْهَاجِ نُبُوَّةٍ»

“Kisha kutakuwepo na utawala wa utenzaji nguvu, utakuwepo kwa muda apendao Allah uwepo, kisha atauondoa atakapo penda kuuondoa, kisha itakuwepo Khilafah katika njia Utume” kisha akanyamaza.

وَيَقُولُونَ مَتَى هُوَ قُلْ عَسَى أَنْ يَكُونَ قَرِيبًا﴿

“…na wanasema, “Lini litakuwa hilo?” Sema, “Asaa likawa hivi karibuni” [Al-Isra’: 51]

24 Rabii’ Al-Akhir 1439 H

11/01/2018 M