Jumla

Maumivu ya Uchumi Unaogemea Riba

Kusambaza ni Kuunusuru Uislamu

Ziara ya rais Uhuru Kenyatta huko Uchina tarehe 24 Aprili, 2019 imezua tumbo joto nchini Kenya hasa baada ya jaribio lake kuomba tena mkopo wa kitita cha bilioni Sh368 kwa utawala wa Uchina. Mkopo huu ni kufadhili upanuzi wa reli ya kisasa Standard Gauge Railway (SGR) kutoka Nairobi kupitia Naivasha hadi mjini Kisumu. Gazeti la The Standard Makala yake ya Alhamisi 25 Aprili, 2019 liliweka kwa ukurasa wake mbele: Shock report on debt even as Uhuru goes for more.’ (Ripoti ya kutamausha kuhusu deni na bado Uhuru aenda kuomba zaidi). Gazeti lilitaja ripoti iliyotolewa na Taasisi ya masuala ya Kiuchumi (IEA) iliyosema kuwa raia wa Kenya kwa kipindi cha miezi watahitajika kufanya kazi huku kiwango kikubwa cha mishahara yao kikilipia madeni. Hata hivyo utawala wa Uchina ulikataa kuikopesha mkopo huo.

SGR inayoanzia Mombasa hadi Nairobi ni mradi uliotajwa kugharimu kiasi kikubwa zaidi cha pesa (US$ 3.6) bilioni tokea Kenya ipate ‘uhuru’. Hoja kuu ya serikali katika kuupigia debe mradi huo ni kudai kwake kuwa utarahisisha usafirishaji wa makasha kutoka bandarini hadi Jijini Nairobi tena kwa haraka na rahisi. Ummah ukaelezwa kwamba kwa mwaka SGR itaweza kusafirisha tani milioni 22 za shehena za mizigo. Ingawaje hadi sasa kiasi cha mizigo inayosafirisha kupitia reli hii ya kisasa ni tani milioni 8 ambacho ndiyo kiwango sawa cha usafirishaji kwa reli ya zamani. Fauka ya haya wafanyibiashara wengi wamepata na wanaendelea kupata hasara kwani kupitia SGR hubidi wagharamikie urudishaji wa makasha yao baada ya kupakua mizigo kwenye bandari kavu ya Nairobi. Gharama hizi ilikuwa haziko kwenye usafirishaji wa barabara ama reli ya zamani. Sasa suali ni Je kweli SGR inalenga nafuu yoyote ya kiuchumi kwa Kenya?

Hatua ya kuomba mkopo mwengine kupanua SGR hadi magharibi mwa Kenya ni kuonesha kwamba mradi huu kama ilivyo miradi mengine katika mataifa yanayoitwa ya ulimwengu wa tatu imeanzishwa na kumalizika kwa madeni. Mwezi Mei 2014, serikali ilitia saini mkataba na benki ya Uchina Exim Bank kukopeshwa mkopo wa kitita cha 324 bilioni, uliofadhili ujenzi wa reli yenye kilomita 385 za reli ya kisasa kutoka Mombasa hadi Nairobi. Mkopo huu ambao unajumuisha kiwango cha Riba ya asilimia 3.6 ambayo ni juu zaidi ya kiwango cha kipimo cha utozaji riba kama ilivyoainishwa na London Inter Bank – bodi ya kimataifa inayohusika na kazi ya kuweka viwango vya riba kwenye mikopo ya mabenki, utalipwa kwa muda mwongo mmoja na nusu (miaka kumi na tano), kwa awamu ya kila miaka mitano. Kama alivyosema mmoja ya waasisi wa Dola ya Marekani Benjamin Fraklin wakopeshaji huwa na kumbumbu nzuri kuliko wanaokopeshwa, ni wazi kuwa Wakenya walalahoi wataendelea kuishi katika kulipa madeni.hali Kenya itaendelea

Uchina inaona mradi wa SGR kama moja wapo ya mipango yake ya muda mrefu utakaomwezesha kustawisha zaidi uchumi wake ukitilia maana kwamba mpango huo uko umetengewa Trilioni US$ 1.2. Mradi huu unaojulikana pia kama Mpango wa Mkanda na Barabara unadaiwa kuwa na malengo ya kuimarisha miundombinu ni kuiwezesha Uchina kudhibiti ulimwengu kwa kuufangamanisha na mikakati yake ya kidiplomasia, kifedha na biashara. Kwa kuwa Uchina sasa imeanza kuingia katika ushindani wa kiuchumi na mataifa ya Kimagharibi yenye uchumi mkubwa kama vile Marekani na Uingereza ni wazi kuwa mradi wake huo ni moja wapo ya jaribio lake la kujiinua zaidi kiuchumi kwa kutanua eneo lake la kibiashara. Hatua ya Uchina kukataa ombi la Kenya lililotokamana na wasiwasi wa ulipaji wa madeni wa serikali ya Kenya ambayo sasa inadaiwa na taifa hilo Bilioni Sh.634.Tayari kwa mwaka huu wa fedha 2018/2019 Kenya inahitajika kulipia mikopo pamoja na malimbikizi ya riba Bilioni Sh870 ilhali madeni jumla yamefikia Trilioni Sh.5.4.

Kwa kuwa tabaka la uongozi ndani ya mataifa ya kibepari halijali maslahi ya raia wake uongozi wa Kenya utaendelea kukopa ukijua wazi hasara itaishia kwa mlalahoi anayekamuliwa kila siku kwa kutozwa ushuru huku wakidai ni kuendeleza miradi! Kenya sasa inakabiliwa na hali inayojulikana ya kiuchumi kama ‘Public debt overhang’ nayo ni kudorora kwa hali ya uchumi kutokamana na madeni mengi.  Na hii ndiyo hali inayokabili Kenya na cha kusikitisha zaidi inachukua mikopo ili kulipia mikopo mingine! Hii ni dhihirisho kuwa uchumi wa mataifa ya kibepari yote ni madeni matupu.

Licha ya ukweli huu, inaonekana serikali haioni haya kupitia wizara yake ya fedha kwa kusema kwamba uchumi umekua kwa asilimia 6.3! Na vipi ione haya wakati mfumo wa kibepari wenyewe ambao serikali inaukumbatia hutumia vipimo vya kimakosa kuwa ukuaji wa uchumi au kuongezeka kwa pato jumla la kitaifa hawaangalii usambazaji wa bidhaa na huduma kwa mwananchi wa kawaida bali ni kukamuliwa na kubanwa zaidi ili awazalishie mapato mabwenyenye.

Ni aibu kwa serikali yoyote duniani inayodai kuwa na mamlaka ya kujitawala kuiona haijimudu kugharamia miradi yake yenyewe ila kwa mikopo ya kutoka nje licha ya kuwa na utajiri tele. Hali hii ya kukopa inayoshuhudiwa nchini Kenya bali na mataifa mengi leo haitokamani na uhaba wa rasilimali bali ni kutokana na ukosefu wa sera za kikweli za kunufaika na utajiri huo. Licha ya hayo, uongozi wa Afrika uliopo hauko huru kikweli katika kuamua jinsi ya kunufaisha raia wao kwa rasilimali hizo. Zaidi wanachokifanya ni kupora rasilimali kwa kushirikiana na mabepari wa Kimagharibi katika kufyonza utajiri huo kisha kuchukua mikopo kufadhili uongozi wao. Mikopo ambayo ukweli wake ni zana hatari zinazo tumiwa na mabepari kuendeleza ukoloni na utumwa wa kiuchumi kote duniani. Wakoloni wa kimagharibi walijiekea mipango ya kunyanyasa uchumi wa mataifa mengine kama vile taasisi za Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF).Taasisi pamoja na ule mkakati wao wanaouita Structural Adjustment uliokuweko kuanzia miaka ya themanini  ndiyo hasa hutumiwa na mabepari kukuza uchumi huku wakiendeleza umasikini kwa mataifa madogo kwa madai ya kuzikopesha kisha kuyawekea masharti magumu. Masharti hayo ni kuzitaka nchi ndogo kupeleka uchumi wao kulingana na sera mbovu za kimagharibi za kiuchumi kama ubinafsishaji wa mali na miradi, kudhibiti bei  na kuweka kila vigezo vitakavyosaidia mashirika yao kirahisi kuingia na kufanya watakayo.

Kuondokana na jinamizi hili la madeni na kukopa kwa hitajika mabadiliko ya kimfumo wa kiuchumi ambao hauchukui riba kama msingi wa kiuchumi nao ni mfumo wa Kiuchumi wa Kiislamu.  Nidhamu ya kiuchumi ya Kiislamu imejikita katika kuzitumia vyema rasilimali za nchi kwa malengo ya kunufaisha raia wake. Aidha, kunahitajika kuwa na uongozi usioegemea maamuzi ya taasisi au serikali nyengine nayo sio mwengine ila ni Khilafah ambayo haitopelekea sera zake ziwe za kisiasa au kiuchumi na nyenginezo kwa kusukuma na mataifa ya nje. Kwa hayo ni uongozi wa Khilafah pekee ndiyo  utakaokomboa dunia kutoka katika utumwa wa kiuchumi wa kibepari na sera zake mbovu za ukoloni mambo leo na kuwalinda wanadamu wote kutokana na utumwa wa mabepari walio na tamaa ya fisi.

Shabani Mwalimu

Mwakilishi kwa Vyombo vya Habari wa Hizb ut Tahrir Kenya