Habari na Maoni

Mivutano ya Kisiasa: Sarakasi Nyengine ya Kisiasa ya Demokrasia

Kusambaza ni Kuunusuru Uislamu

بسم الله الرحمن الرحيم

Habari:

Uadui na vita kati ya mirengo mikuu ya kisiasa; muungano wa Jubilee ukiongozwa na raisi wa Kenya Uhuru Kenyatta, na muungano wa NASA wa Raila Odinga, vimetawala vichwa vya habari katika vyombo vya habari vya Kenya. Tangu kumalizika kwa uchaguzi wa mnamo 8 Agosti 2017 ambapo ushindi wa Kenyatta ulibatilishwa na Mahakama ya Juu mnamo 1 Septemba 2017, mivutano mizito ya kisiasa juu ya kufanyika kwa marudio ya kura za uraisi ndani ya siku sitini kama inavyo ashiriwa na katiba imeibuka. Muungano wa Jubilee umeelezea kuwepo kwake tayari kwa marudio ya uchaguzi huo chini ya usimamizi wa tume iliyopo sasa ya uchaguzi ya IEBC. Kwa upande mwengine, NASA imeapa kususia uchaguzi huo ikiwa baadhi ya maafisa wa IEBC hawataondolewa afisini. Unatoa hoja kuwa IEBC inaegemea upande wa idara ya Jubilee na kwa hivyo haina uwezo wa kusimamia uchaguzi huru na wa haki. Kuongezea, Nasa imefanya maandamano dhidi ya maafisa ‘wafisadi’ wa IEBC. Jubilee imeyataja matakwa ya NASA kama jaribio la kulazimisha kuwepo kwa ‘serikali ya nusu mkate’.

Maoni:

Wanasiasa wa kidemokrasia wanatambulika kuwa watekaji nyara wa matarajio ya umma ili kuupotosha umma kuamini kuwa mivutano ya kisiasa ni vita vya kuwapigania maisha yao. Huku wanasiasa wakizozana, mtu wa kawaida anaendelea kuteseka kutokana na gharama kubwa ya maisha, huduma duni za afya kutokana na wauguzi kugoma kwa sababu ya nyongeza ya mishahara. Ilhali wanasiasa wamejitosa katika misuguano ya kisiasa ambayo mwishowe itakuwa kwa manufaa yao. Ni kinaya kuwa uchaguzi wa Agosti ulikuwa ghali zaidi katika Afrika ukimgharimu mlipa ushuru shilingi bilioni 50 ($499 milioni). Hazina ya Kenya ililazimika kupunguza matumizi katika sekta muhimu na kuelekeza rasilimali za umma kufadhili uchaguzi huo. Kuhusu ni kwa nini tunashuhudia ukosefu wa kuaminiana miongoni mwa wanasiasa na kuteremka mpaka chini kwa umma, hii imetokana na mtazamo wa kirasilimali kuhusu maisha; kwa kufanya ‘maslahi’ kuwa ndio kipimo pekee cha vitendo vya mwanadamu. Uchunguzi wa kimakini katika mgogoro wa sasa wa kisiasa unafichua namna gani demokrasia imesababisha ukosefu wa kuaminiana miongoni mwa wanasiasa. Katika hali ya kutafuta maslahi yao ya kibinafsi, wanasiasa wameunda migogoro kwa lengo la kufikia suluhisho la kati na kati.

Kwa kuwatazama wafuasi wa kila muungano, yaani Jubilee na NASA yaweza kusemwa kwa kukatikiwa kuwa Kenya inaugua ukabila. Mgogoro uliopo sasa umefichua zaidi mfumo wa kisiasa wa Kenya, ambao ni muundo wa siasa za kikabila ambao wanasiasa huutumia kujipatia umaarufu. Ukabila nchini Kenya ulianza tangu enzi za ukoloni wa Kiingereza. Wakoloni wa Kiingereza walikuwa wakitumia mbinu ya utawala ya wagawanye uwatawale. Wakoloni zaidi pia walikuwa wakichochea kabila hili dhidi ya kabila jengine.

Ama kuhusu kufanyika kwa uchaguzi mpya, kilicho muhimu hapa sio kudadisi ima Raila Odinga yuko tayari kurudi katika uchaguzi au Uhuru Kenyatta ana fursa nyengine ya kuchaguliwa tena. Badala yake fahamu ya kuwa na chaguzi za kuendelea ndio kadhia inayostahili kuangaziwa. Chaguzi za kuendelea katika demokrasia ni miongoni mwa majaribio ya kutapatapa kuficha kufeli kwake. Demokrasia imefeli kisiasa ulimwenguni na imeundwa kuchunga maslahi ya kikundi cha wachache. Chini ya kisingizio cha demokrasia, dola kuu za kimagharibi zimeingilia kati mambo ya kindani ya ‘nchi changa za kidemokrasia’ kuvuruga uchumi wao na kuozesha maadili ya watu wake.

Inasikitisha kuona Waislamu na zile mujtama zilizo funguka kiakili wanahadaiwa na urongo wa demokrasia pamoja na wanasiasa wake walafi ambao daima wana kiu ya kujinufaisha kibinafsi kwa gharama ya mtu wa kawaida. Kufeli kwa demokrasia kunatakiwa kuwasaidie watu kupigia debe mfumo badala, adilifu na kamilifu wa Uislamu; unaojumuisha suluhisho litokalo kwa Mola la kisiasa, kijamii na kiuchumi kwa wanadamu wote.

Imeandikwa kwa Ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir na
Shabani Mwalimu
Mwakilishi kwa Vyombo vya Habari Hizb ut Tahrir in Kenya