Ameer Suali na Jawabu

Mkataba wa Maridhiano Kati ya Eritrea na Ethiopia Jijini Asmara

Kusambaza ni Kuunusuru Uislamu

بسم الله الرحمن الرحيم

 Jibu la Swali
(Imetafsiriwa)

Swali

Mkataba wa maridhiano kati ya Eritrea na Ethiopia ulitiwa saini jijini Asmara mnamo Julai 2018. Msemaji wa Wizara ya Kigeni ya Ethiopia, Meles, alithibitisha kuwa mkataba huu wa Asmara uliotiwa saini hivi majuzi na Eritrea ulikuwa kwa matakwa ya nchi zote mbili pasi na upatanishi kutoka kwa mtu wa tatu. Hili lina ukweli wa kiasi gani? Je, ulikuwa huru na ushawishi wa kimataifa na wa kieneo? Makubaliano ya Asmara yaliwakilisha makubaliano ya Algiers kama ziada kwake, sasa kwa nini kulikuweko na ngoja ngoja ya takriban miaka 18 kutekeleza makubaliano haya? Na Allah akulipe kheri.

Jibu

Taarifa ya msemaji rasmi wa Wizara ya Kigeni ya Ethiopia, Meles, iliyosema kuwa makubaliano ya Asmara yalikuwa kwa matakwa ya nchi mbili hizo ni ya urongo na ya kupotosha! Ukifuatilia na kutafakari juu ya yaliyotokea yaonyesha kuwa Amerika iko nyuma ya yale yaliyotokea na yanayotokea ili kupata maslahi yake na kuangazia ushawishi wake juu ya harakati za Ulaya na China barani Afrika. Huu hapa ndio ufafanuzi wake:

Kwanza: Maelezo ya makubaliano ya Asmara: makubaliano haya yalikamilishwa mnamo 9/7/2018. Ethiopia na Eritrea kisha zikatangaza mwisho wa hali ya kivita baina yao, baada ya mkutano ulioitwa “wa kihistoria” kati ya Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed na Raisi wa Eritrea Isaias Afwerki jijini Asmara. Waziri wa Habari wa Eritrea, Yamani Jabr Miskil, alitangaza katika mtandao wa Twitter: “taarifa ya Amani na urafiki wa pamoja ilitiwa saini baina ya pande mbili hizi, na hali ya kivita baina ya nchi mbili hizi imemalizika, na enzi mpya ya Amani na urafiki kuanza… nchi mbili hizi zitafanya kazi pamoja ili kuimarisha ushirika wa karibu katika nyanja za kisiasa, kiuchumi, kijamii, kitamaduni na usalama” (AFP, 9/7/2018). Ili kuelewa ni nani aliye nyuma ya Makubaliana hayo tutaja matukio ibuka kabla na baada yake:

1- Yaliyojiri kabla ya makubaliano:

 1. Waziri Msaidizi wa Amerika katika masuala ya Afrika, Donald Yamamoto aliwasili jijini Addis Ababa mnamo Alhamisi 26/4/2018, (… katika ziara rasmi ya siku tatu ambapo atakutana na Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed Ali na Waziri wa Kigeni. Ziara hii ni sehemu ya ziara iliyo anzishwa na Yamamoto mnamo 22 mwezi huu, iliyo jumuisha Eritrea na Djibouti, na kutamatisha na Ethiopia … 27/04/2018 www.aa.com.tr/ar).
 2. Abiy Ahmed alifanya ziara yake ya kwanza nchini Saudi Arabia mnamo 17/5/2018 kwa mwaliko rasmi wa Mfalme Salman Bin Abdul Aziz.
 3. Wa kwanza kumzuru Abiy Ahmed, alikuwa Mfalme Mtarajiwa, Bin Salman, mnamo 7/6/2018. Shirika la Habari la Ethiopia liliinukuu afisi ya Waziri Mkuu ikisema kuwa Abiy Ahmed “alisifu kuimarika kwa mahusiano na Saudi Arabia. Alisema shukrani kwa Muhammad Bin Salman, uhusiano kati ya nchi mbili hizi umeimarika na kuwa imara na karibu zaidi kuliko wakati wowote kabla, na kwamba Mfalme huyo Mtarajiwa wa Saudi ametoa ahadi ya kusaidia juhudi za Addis Ababa za kuongeza kasi maendeleo na kuwashajiisha wawekezaji wa Kisaudi kuwekeza nchini Ethiopia …”
 4. Wizara ya Kigeni ya Amerika ilisema katika taarifa iliyotolewa mnamo 21/6/2018, “Amerika imeshajiishwa na maendeleo ya hivi karibuni ambayo Ethiopia na Eritrea zimefanya katika kutatua hitilafu zao za muda mrefu … Isaias na Abiy wameonyesha uongozi jasiri kwa kuchukua hatua hizi za kuleta amani. Amerika inatarajia kurudi kamili kwa mahusiano ya kawaida na kupatikana kwa matarajio yetu ya pamoja katika nchi zote mbili ili kufurahia amani na maendeleo ya kudumu.” (Reuters, Juni 21, 2018)
 5. Katika mahojiano na ‘Addis Standard’, Balozi wa Amerika nchini Erthiopia, Michael Raynor, alisema, “Hakika, tumeziambia pande zote mbili, na hadharani, na tunaendelea kusema kuwa sisi tuko kucheza dori hiyo. Katika siku ya Makubaliano ya Algiers Amerika ilikuwa mdhamini rasmi; tulikuwa na dori ya kimuundo iliyo anzishwa katika wakati makubaliano hayo yalipo fanywa. Tumeshajiisha matokeo haya kwa muda kadhaa kwa serikali zote mbili na katika kufanya hivyo tumesema ‘Ikiwa kwa ushirikiano mutahisi kuna dori ya manufaa ambayo Amerika inaweza kucheza, tutafanya kila tuwezalo ili kusaidia hilo’… Nadhani tumeshacheza dori yenye manufaa. Kama nilivyosema, tumekuwepo na mikutano na nchi zote mbili kwa miezi kadhaa sasa ili kushajiisha matokeo haya.” (addisstandard.com 02/07/2018)

Yote haya yanaonyesha kuwa Makubaliano haya yametayarishwa na Amerika na wafuasi wake; watawala nchini Saudi Arabia, na hili ni kutokana na ufuatiliziaji matukio kabla ya mkutano huo.

2- Yaliyojiri baada ya Makubaliano:

 1. Amerika imetangaza usaidizi wake kwa makubaliano hayo ya amani baina ya Eritrea na Ethiopia baada ya miaka ya mzozo. Hii ilikuwa katika taarifa ya Waziri wa Kigeni wa Amerika, Mike Pompeo, mnamo Jumanne. Alisema, “Amerika inakaribisha kujitolea kwa ajili ya amani na usalama mnamo Julai 9 baina ya Dola ya Eritrea na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kifederali ya Ethiopia, yakitamatisha kikamilifu miaka 20 ya mzozo.”

Pompeo alisisitiza: “kurudisha mahusiano katika hali ya kawaida na kutabanni Tangazo la Pamoja la Amani na Urafiki kati ya Eritrea na Ethiopia itawapa watu wao fursa za kuangazia matarajio shirika ili kuleta mafungamano ya karibu ya kisiasa, kiuchumi, na kijamii … (en.haberler.com, 10/07/2018)

 1. Isaias Afwerki alizuru Saudi Arabia mnamo 23/07/2018 baada ya Makubaliano ya Asmara mnamo 09/07/2018. Yeye na Mfalme Salman walitathmini (“maendeleo katika uwanja wa kieneo …” Adel Al-Jubeir pia alizungumza na mwenzake wa Eritrea wakati wa mkutano wake naye “mahusiano ya pande mbili kati ya nchi mbili hizo na maudhui za maslahi ya pamoja” … (Middle East, 24/07/2018)
 2. Zaidi ya miezi miwili baada ya Tangazo la Asmara chini ya ufadhili wa Mfalme Salman, Raisi wa Eritrea Isaias Afwerki na Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed Ali walitia saini mnamo Jumapili 16/9/2018 Makubaliano ya Amani ya Jeddah kati ya nchi mbili hizo. Kutia saini huku ilikuwa mbele ya Mfalme Mtarajiwa wa Saudi Arabia (Sky News Arabiya, 16/09/2018)

Hivyo basi, kutokana na msururu wa matukio hayo ya juu, inajitokeza kuwa Amerika na vibaraka wake ndiyo waendeshaji wa matukio haya wakisubiri Makubaliano ya Asmara kupitia kuunda mazingira kwa ajili yake pamoja na usaidizi wake wazi kwao baada ya kutiwa kwake saini.

Pili: Uhakika wa Utawala Nchini Ethiopia na Eritrea:

1- Utawala Nchini Ethiopia:

 1. Abyssinia ilikaliwa na uvamizi wa Italia mnamo 1935. Mfalme wake Haile Selassie alitoroka kupitia Kenya hadi Misri, ambazo wakati huo zilikuwa chini ya ukoloni wa Kiingereza. Kisha alikwenda Uingereza na kukaa huko mpaka Uingereza ilipomregesha tena 1941 baada ya kuifurusha Italia kutoka Abyssinia kupitia washirika wake wakati wa Vita vya Pili vya Dunia, Uingereza ilimrudisha tena Haile Selassie mamlakani kama mfalme, na kisha Abyssinia ikawa chini ya ushawishi wa Uingereza … Wakati huo, Uingereza pia iliikalia nchi jirani ya Eritrea, ambayo ilikuwa chini ya utawala wa Italia tangu karne ya kumi na tisa. Mnamo 1950, Eritrea iliunganishwa na Ethiopia chini ya utawala wa Haile Selassie. Ushawishi wa Uingereza uliendelea nchini Ethiopia, ikiwemo Eritrea hadi 1974.

Pindi mapinduzi yalipotokea dhidi ya Mfalme huyo kupitia wanamageuzi wa kijeshi. Miongoni mwao alikuwa afisa Mengistu Haile Mariam, aliyeweza kutawala kuanzia 1977 baada ya mzozo baina ya maafisa hawa na kubakia mamlakani hadi 1991.

Harakati nyingi za kimapinduzi za siku hizo zilibeba miito ya kimapinduzi kama Ukombozi, Ujamaa, na kadhalika. Hivyo basi ikawa ndiyo miito ya mapinduzi ya Mariam, ingawa Amerika ilikuwa nyuma yake kushambulia ushawishi wa kikoloni wa Uingereza … na kutokana na vitendo vyake ng’ambo vya kuipendelea Amerika, ni usaidizi wake kwa uasi wa Sudan Kusini ulioongozwa na John Garang, aliyekuwa mshirika wa Amerika. Usaidizi wa Ethiopia uliendelea kwa ajili ya harakati hii hadi kusini ilipotenganishwa kutoka Sudan kwa ushirikiano wa serikali ya Bashir nchini Sudan…

 1. Lakini Mengistu alijulikana kwa umwagaji damu wake, hivyo basi Amerika ilihofu kuwa watu wangeasi na Uingereza ingeregea. Hivyo ilimuondoa na kumleta Meles Zenawi ambaye anatoka katika chama cha ‘Tigray People’s Liberation Front’, cha kabila la Kikristo la Tigray, ambalo ni asilimia 5 ya wakaazi jumla wa Ethiopia na kimeungana na vyama vyengine vya kikabila, kikiwemo chama cha ‘Oromo Liberation Front’. Mojawapo ya kazi muhimu sana iliyofanywa na Zenawi kwa ajili ya Amerika ni kuingilia kwake kati nchini Somalia mnamo 2016, kwa kuagizwa na Amerika kupigana na harakati za Kiislamu na kupindua utawala wa Mahakama za Kiislamu nchini Somalia. Jeshi la Ethiopia lingalipo nchini Somalia ili kutafuta utulivu kwa ajili ya ushawishi wa Amerika.
 2. Baada ya kifo cha Zenawi mnamo 2012, alirithiwa na Haile Mariam Desalegn wa kabila hilo hilo. Lakini ghasia ziliibuka na kupelekea hali ya taharuki. Matukio ya Oktoba 2015 yakatokea, baada ya serikali kuamua kupanua mji mkuu wa Addis Ababa na kunyakua ardhi ya ukulima iliyopo karibu. Ardhi hizi ni milki ya kabila la Oromo, ambalo idadi yake ni asilimia 40 ya raia jumla, likifuatiwa na Amharic asilimia 20, serikali baada ya mwaka wa 2016 ikakimbilia kutangaza hali ya taharuki, na kuwakamata zaidi ya watu elfu 29 na kuwauwa zaidi ya watu 500 ndani ya miezi ya maandamano. Hofu ya Amerika ikaamshwa, ikamuamuru kujiuzulu kwa sababu ya kushindwa kutuliza hali hiyo, na kuhatarisha ustawi wa eneo zima la Pembe ya Afrika.
 3. Desalegn alijiuzulu mnamo 15/2/2018. Amerika ikamleta mtu kutawala Ethiopia kutoka katika kabila kubwa zaidi la waasi, lenye Waislamu wengi, la Oromo, Abiy Ahmed, mwana wa kabila hilo, mamake ni mkristo wa kabila la Amharic na vile vile mkewe, hii ni ili kuyatia mkononi makabila mawili makubwa zaidi ya Ethiopia. Alishikilia nyadhifa katika Taasisi ya Jeshi na kisha katika taasisi ya upelelezi, na kisha katika nyadhifa za kisiasa … Aliingia afisini kama waziri mkuu mnamo 2/4/2018. Abiy Ahmed alipangiwa kuuwawa mnamo 23/6/2018, (kulipo fanyika shambulizi la guruneti wakati wa mkutano wa hadhara katika mji mkuu wa Addis Ababa baada ya kuwahutubia maelfu ya watu. Alisema baada ya mlipuko huo, “jaribio lisilo fanikiwa kwa nguvu zisizotaka kuona umoja wa Ethiopia”. Ubalozi wa Amerika jijini Addis Ababa ulishutumu shambulizi hilo: “Ghasia hazina nafasi Ethiopia inapotafuta mageuzi ya maana ya kisiasa na kiuchumi.” (Al-Hurra, 23/6/2018).

Hakujaondolewa lawama kuwa mabadiliko ya ndani ya kijeshi na usalama aliyofanya hayana uhusiano wowote na hili, kupitia kumsimamisha kazi kamanda wa jeshi vilevile kiongozi wa upelelezi jumla nchini mwake mnamo 8/6/2018, kwani taasisi hizi zinatuhumiwa kwa mauwaji ya mamia ya waandamanaji na kukamatwa kwa maelfu yao katika maandamano hayo tangu 2015.

Hivyo basi, Amerika inadhibiti hatamu za uongozi nchini Ethiopia, hususan baada ya Abiy Ahmed kuchukua afisi. Anatekeleza mipango na maelekezo ya Amerika ili kuondoa taharuki baina ya vibaraka wa Amerika katika eneo hilo ili liwe nguvu imara dhidi ya hatua zozote za Ulaya na upanuzi wowote wa kiuchumi wa China.

2- Ama kuhusu Utawala Nchini Eritrea:

Kama tulivyo sema tayari, baada ya mapinduzi kwa Haile Selassie na kumalizika kwa ushawishi wa Uingereza nchini Ethiopia, ikiwemo Eritrea, Mengistu Mariam alichukua udhibiti wa serikali na alikuwa mnyanyasaji na mmwagaji damu, hivyo Amerika ilihofia uasi wa watu na utumiaji wa hali hiyo kwa Uingereza ili kuregea kwake kwa sababu inajulikana kwa uvumilivu wake wa muda mrefu katika mambo haya, hivyo basi ikamuondoa Mengistu na kumleta Zenawi mnamo 1991. Wakati huo huo kulikuweko na harakati ya uhuru wa Eritrea, hivyo Amerika ilijibu matakwa yao ili kutuliza hali hiyo, na uhuru wa Eritrea ukatangazwa mnamo 1993 na Afwerki kuekwa madarakani. Lakini, katika tangazo hilo la uhuru, haikufafanua mipaka ya dola hiyo mpya. Afwerki alihofia kuwa Ethiopia huenda ikarudi na kuiunganisha kwake tena. Mnamo 12/5/1998, alitekeleza vitendo vya kijeshi ili kuweka wazi mipaka hiyo, kinyume na mpango wa Amerika, ambayo ilimteua kama kiongozi tu, aliendelea kukataa mpango wa majadiliano wa Amerika uliowasilishwa na Susan Rice mnamo 30/5/1998 na alikaribia kufaulu katika kuchora mpaka, lakini Amerika akaliona hili kama uasi dhidi yake na kuamua kumtia adabu, bali ilimfedhehesha kimakusudi na kumuamuru Zenawi kuanzisha vita katili mnamo 4/2/1999 kwa Eritrea na vita hivi vilikola kasi na kuwa na umwagikaji damu zaidi mnamo 12/5/2000 hadi ikaondoa mipaka yote iliyochorwa na kuingia kwa kina ndani ya Eritrea kwa njia ya kufedhehesha, kwa hivyo Afwerki akakubali makubaliano ya Algiers mnamo 18/6/2000, pamoja na masharti yote yanayo hitajika na huku kadhia ya mipaka ikisalia bila ya kutatuliwa! Tulitoa maoni ya kisiasa wakati huo mnamo 20/3/1421H-22/6/2000 ndani yake tulisema: (… Mnamo Jumapili, 18/6/2000, Mawaziri wa Kigeni wa Eritrea na Ethiopia walitia saini Makubaliano ya Kusitisha Vita baina ya nchi zao; jijini Algiers mbele ya mtawala wake katika wadhifa wake kama mwenyekiti wa awamu ya sasa ya Shirika la Muungano wa Afrika (OAU), mbele ya wajumbe kutoka Amerika, Muungano wa Ulaya na Umoja wa Mataifa. Mkataba huo unafafanua mambo 15, kubwa yao ni: kuondoa mpaka wa kawaida baina ya nchi mbili hizo kupitia wajuzi wa kimataifa kutoka Umoja wa Mataifa. Kuvipeleka tena vikosi vya Ethiopia vilivyo kita kambi mjini Badme na maeneo ya mpakani wiki mbili baada ya kuwasili kwa majeshi ya kimataifa na kuondolewa kwa Eritrea katika eneo la kilomita 25 mpakani mwake na Ethiopia kama eneo la usalama, chini ya udhibiti wa majeshi ya kimataifa hadi mpaka utakapo chorwa na mzozo kutatuliwa …” Akitoa maoni juu ya kutiwa saini huku, Clinton alisema: “Haya ni maendeleo makubwa na ni mwisho wa mzozo mbaya katika Pembe ya Afrika”, alisema: “Ethiopia na Eritrea ni marafiki wa Amerika ikiwa wako tayari kuchukua hatua nyengine, sisi na washirika wetu kutoka katika kundi la kimataifa tutasonga mbele nazo.” Anthony Lake, mjumbe wa raisi alisema: “Huu ni wakati muhimu na unaomaliza mzozo wa miaka miwili.”

Ingawa mkataba huo ulitaja uchoraji mpaka, bado ungali haujatekelezwa! Ethiopia kamwe haikutilia maana uchoraji mipaka hii; iliikadiria Eritrea kuwa sehemu ya eneo lake na mojawapo ya maeneo yake. Wafalme wa Abyssinia na baada yao Mengistu Mariam alitaka kuziunganisha nchi mbili hizi kwa njia na mbinu kadha wa kadha kutokana na tamaa yao ya haja ya bandari nchini Eritrea.

Hii ndiyo sababu Afwerki alijaribu kuchora mpaka kijeshi na angefaulu lau si kwa shambulizi la Ethiopia mnamo 12/5/2000, kwa agizo kutoka Amerika kama adhabu kwa Afwerki, kama tulivyo taja juu. Afwerki alilazimishwa kukubali yote yale Ethiopia iliyoyataka na kutangaza waziwazi kukubali makubaliano hayo, ambayo yalifanywa chini ya pazia ya Shirika la Muungano wa Afrika (OAU), ambayo yalitiwa saini nchini Algeria mnamo 18/6/2000.

Pia tulisema katika maoni hayo ya kisiasa kuwa: “Ethiopia na Eritrea ni nchi zinazofuata Amerika katika sera yao na watawala wao ni vibaraka wake. Ilimwezesha Meles Zenawi kuongoza chama cha ‘Tigray People’s Liberation Front’ (TPLF) na kuchukua uongozi jijini Addis Ababa pindi ilipotaka kumbadilisha kibaraka wake, Mengistu Mariam, mnamo 1991. Ndiyo iliyomruhusu Isaias Afwerki kuongoza chama cha ‘Eritrean People’s Liberation Front’ (EPLF) kwa ajili ya uhuru kutoka Ethiopia mnamo 1993. Kwa hivyo mzozo kati ya Ethiopia na Eritrea ni mzozo baina ya vibaraka au (marafiki) kama Clinton na ikulu ya White House au wajuzi wa sera ya Kimagharibi wavyopenda kuwaita. Amerika imejaribu kutatua tofauti zao kupitia majadiliano, na kutoa juhudi za mmoja wa wajuzi wake wakuu, Anthony Lake, aliyechukua zaidi ya mwaka mmoja bila ya kuweza kutatua mzozo huo; kwa sababu Afwerki hakufurahia mapendekezo ya Amerika, na kuyaona kama mapendeleo kwa Ethiopia … Pindi Afwerki alipofeli katika njia hii, Amerika iliamua kumtia adabu na hata kumfedhehesha kimakusudi kwa nguvu za kijeshi, ambayo ndiyo njia yake ya kukabiliana na vibaraka wake wanapofikiria uasi dhidi yake. Ni Amerika, iliyompelekea Zenawi kuanzisha vita vya mwisho dhidi ya Eritrea na ni balozi wa UN, Holbrooke, aliyempa idhini ya kuvianzisha. Mnamo Jumatano, 10/5/1998, kabla ya kuondoka Asmara na baada ya mkutano wake na raisi wa Eritrea, alisema, “Tunakaribia kutatua uadui na kuzuka kwa raundi mpya ya mapigano, ambayo, lau yatatokea, moja kwa moja yatakuwa ni vita vikubwa zaidi barani Afrika”. Hizi ni taarifa za uchochezi ambazo Holbrooke alizitoa kabla ya kuondoka Asmara, ambazo alimuonya kila mmoja aliyesikia wakati huo juu ya hatari kubwa. Holbrooke sasa amekuwa ni alama ya tishio kwa nchi anazozizuru ulimwenguni. Anafuata nyayo za muonyaji aliyemtangulia, Kissinger, katika kuchochea vita na kuleta majanga na kuona umwagaji damu za watu, rahisi kwa ajili ya kuhifadhi maslahi ya Amerika … Alhamisi, 22/4/2000) Mwisho.

Kutokana na hayo maelezo ya juu ni wazi kuwa dukuduku la Eritrea kwa mapendekezo ya Amerika halimaanishi kuwa si mfuasi wa Amerika. Bali, lamaanisha kuwa inataka kuirai Amerika kuisaidia kuchora mpaka baina yake na Ethiopia mwanzo na mwisho ili Eritrea isibakie katika hali ya “karibu na uhuru”. Kwa sababu kukosa kuchorwa mipaka hiyo na Ethiopia kumewafanya Waeritrea kubakia na wasiwasi kuhusu nia za Ethiopia.

Hivyo basi ni wazi kuwa Afwerki na Abiy Ahmed wote ni vibaraka wa Amerika. Si rahisi kwao kutamatisha makubaliano ya Asmara pamoja na vipengee walivyovitaja bila ya utambuzi, mipango ya Amerika na amri ya utekelezwaji wake.

Tatu: Kwa nini Amerika imesubiri miaka 18 baina ya makubaliano ya Algiers mnamo 2000 na makubaliano ya Asmara ya 2018? Hii ni kwa sababu ya maslahi yake:

Baada ya makubaliano ya Algiers, yaliyo dhaminiwa na Amerika, na kadhia muhimu zaidi ikiwa uchoraji mipaka, Ethiopia ilitaka kurefusha hili, lakini Eritrea ikasisitiza juu yake, ilhali Amerika haikujali au kutia shinikizo kutatua tatizo hili, kwa sababu maslahi yake yalikuwa yamelindwa, ima kadhia hiyo ikitatuliwa au la. Hii ni kwa sababu wote hao ni vibaraka wake na uadui baina yao hauathiri maslahi yake, huu ndio uliokuwa mtazamo wao wakati huo. Lakini, mambo yamebadilika katika miaka ya hivi karibuni yaliyoifanya Amerika kuzingatia tena sera yake juu ya Afrika, hususan Pembe ya Afrika:

1- Uhasama wa mara kwa mara wa utawala nchini Ethiopia na hili kimaumbile hudhoofisha serikali na kuifanya iyumbe na kuingilia kwa urahisi … Hivyo huenda ikalengwa na dola za kikoloni, hususan Uingereza katika upande wa ushawishi wa kisiasa, na China katika upande wa ushawishi wa kiuchumi, haya yaliifanya Amerika kurudi na kuwatulizia makini, iliyopelekea maridhiano kati ya Ethiopia na Eritrea na vipengee vyake vingi vinavyo itumikia Amerika.

2- Imeripotiwa kuwa Ethiopia ina hifadhi kubwa ya mafuta katika maeneo yake mengi na kazi ya uchimbaji wake tayari imeanza katika maeneo mengi (Ethiopiana.net 1/4/2013)… “Uchimbaji visima vya mafuta katika eneo hilo unatarajiwa kufikia mapipa bilioni 40 na kufika sokoni mnamo 2018 (Mogadishu Center 25/12/2016), na hivyo mafuta ni jambo jipya linaloisukuma sera ya Amerika kutulizia makini Pembe ya Afrika, hususan huku kampuni za China zikiongoza dori ya kiuchumi na utafutaji wa kiuchumi na uchimbaji wa mafuta ya Ethiopia.

Hili sio siri kwa Amerika na inaweza kuziona mandhari nzito zenye kukua za uvamizi wa kiuchumi wa China barani Afrika, hususan nchini Ethiopia, kwa sababu China inawekeza pakubwa katika soko la Ethiopia, China inafanya kazi kuimarisha uwekezaji wake barani Afrika, hususan Ethiopia, ambayo katika miaka ya hivi karibuni imekuwa eneo la kiviwanda la China. Katika upande wake utawala wa Ethiopia unafanya kazi kusahilisha uwekezaji wa kigeni na kuthibitisha kuwa ndiye mnufaikaji wa mwanzo na wa mwisho wa uwepo wa China katika eneo lake … (France 24, 5/6/2018), kwa hivyo hii ndiyo sababu ya kuharakisha kwa Amerika Ethiopia ili kufunga ushawishi wa kiuchumi wa China.

3- Majaribio mapana kupitia ushawishi wa Uingereza ili kupenya, Pembe ya Afrika yanaonekana. Maendeleo ya ghafla ya mahusiano kati ya Imarati na Ethiopia yanaonekana, baada ya mahusiano haya kupuuzwa, kwamba ni 2010 tu ndio Imarati ilifungua ubalozi wake jijini Addis Ababa! Ushirikiano kati yao umekuwa kwa kasi baada ya hapo. Makubaliano yametiwa saini katika nyanja tofauti tofauti, kama vile makubaliano ya ushirikiano wa kiufundi kwa usaidizi wa forodha, ufunguzi wa afisi ya uwakilishi wa Taasisi ya Biashara na Viwanda ya Dubai jijini Addis Ababa mnamo 2013, mamlaka ya ndege mnamo 2014, elimu ya juu, vijana na michezo mnamo 2015, Kamati ya Pamoja kati ya Imarati na Ethiopia ilibuniwa na kufanya mikutano yake katika ngazi ya mawaziri wa kigeni … Wakati wa ziara rasmi ya aliyekuwa Waziri Mkuu wa Ethiopia Hailemariam Desalegn, mnamo 2016 nchini Imarati, mahusiano ya pande mbili kati ya nchi mbili hizi yalishuhudia ukuaji wenye thamani katika nyanja zote, kutokana na msururu wa majadiliano yaliyo fanywa na Desalegn pamoja na uongozi wa kisiasa nchini Imarati.

Kama sehemu ya ziara rasmi jijini Abu Dhabi. Wakati huo aliyekuwa Waziri wa Afisi ya Mawasiliano ya Serikali, Getachew Reda alisema: “Ziara ya Desalegn ilijadili kadhia kadhaa za pande zote mbili zinazohusu ushirikiano kati ya nchi mbili hizi kwa njia inayotumikia maslahi ya pamoja, hususan katika nyanja za kiuchumi na uwekezaji na kadhia za kieneo na kimataifa,”. Waziri wa Ushirikiano wa Kimataifa wa Imarati, Reem Al-Hashemi alisema wakati wa kipindi kilicho andaliwa na Ubalozi wa Imarati jijini Addis Ababa kuwa Ethiopia ni mmoja wa washirika wa kimikakati wa Imarati barani Afrika, na kwamba nchi mbili hizo zinashirikiana pamoja (Al Ain Al Ikhbariya, 7/3/2018).

Uingereza kupitia Imarati imejaribu kuiunganisha Ethiopia na mtandao na sera yake, ikitaraji kuishawishi Ethiopia na Eritrea. Hivyo basi, ziara hizi zilikuwa na malengo haya, “mnamo 15/6/2018 Sheikh Mohammad bin Zayed Al Nahyan alifanya mkutano rasmi na Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed jijini Addis Ababa, ambao ulilenga kuimarisha mahusiano na urafiki, ushirikiano na ushirika wa kimikakati baina ya nchi mbili hizo. Mnamo Jumanne 3/7/2018 Mfalme Mtarajiwa wa Abu Dhabi alimpokea Raisi wa Eritrea Isaias Afwerki na kuonyesha matarajio yake kuwa ziara hii ingechangia kuimarisha mahusiano shirika kati ya nchi mbili hizo, Imarati na Eritrea katika hatua ifuatayo, na kuletea kheri nchi mbili hizo rafiki na watu wake … (http://www.alkhaleej.ae 22/07/2018) Maendeleo haya na yanayojiri yameifanya Amerika kutulizia makini sana Afrika na hususan Pembe ya Afrika na kuwa mchangamfu kwake. Hivyo basi mnamo Septemba 2017, Amerika ilimteua Donald Yukio Yamamoto kama Waziri Msaidi wa Maswala ya Afrika, cheo chenye ushawishi zaidi katika uundaji sera za Amerika kwa bara la Afrika. Chaguo la Yamamoto kwa cheo hiki sio kwa kubahatisha. Yeye ni mmoja wa mabalozi wa Amerika aliye na ujuzi zaidi katika kadhia ya Afrika, hususan eneo la Pembe ya Afrika, ashawahi kuiwakilisha nchi yake kama balozi katika nchi za eneo hilo … Ametoa mchango mkubwa katika maandalizi ya Makubaliano ya Asmara kati ya Ethiopia na Eritrea ili kuondoa taharuki kati yazo na kuwa na uhusiano mzuri. Hivyo basi, makubaliano ya Asmara yalitiwa saini ili kuthibitisha na kama nyongeza ya mkataba wa Algeria ili kutatua kadhia baina ya Ethiopia na Eritrea, bali baina ya vibaraka wake eneo hilo. Ukhafifishaji uhasama pia unatarajiwa baina ya Ethiopia na Misri kuhusiana na bwawa. Abiy Ahmed alizuru Misri na kukutana na Sisi mnamo 10/7/2018 baada ya kutia saini Makubaliano ya Asmara kwa siku moja na akatia saini pamoja na Sisi Makubaliano ya kutabanni mtazamo mmoja baina ya nchi mbili hizo kwa kuheshimu haki ya kila mmoja ili kufikia maendeleo bila ya kukiuka maslahi ya mwengine … Na bila shaka yote haya ni kwa idhini ya Amerika. Pia kuhusiana na Sudan, mnamo Aprili, Amerika ilituma ujumbe wa kiufundi na kidiplomasia kama mradi wa upatanishi ili kuileta mitazamo ya nchi tatu hizi pamoja ili kuimarisha vibaraka wake dhidi ya uvamizi wa kiuchumi wa China na upenyaji wa kisiasa wa Uingereza.

Nne: Mwisho, inatia uchungu kuwa nchi za kikafiri za kikoloni, zikiongozwa na Amerika, zinadhibiti nchi za eneo hilo … Baadhi huenda hawajui kuwa Waislamu nchini Ethiopia na Eritrea wanawakilisha nusu ya wakaazi wake, bali kuna wale wanaokadiria idadi yao kuwa zaidi ya milioni 50. Baadhi yao pia huenda hawajui kuwa meli ya kwanza ya Waislamu waliogura kutoka Makka hadi Abysynnia ilitia nanga katika mji wa bandari ya Musawwa nchini Eritrea … Lakini, nchi mbili hizi zina maslahi kwa Amerika, China na Ulaya na hakuna maslahi yoyote yanapewa kwazo na Waislamu… kwa vyovyote vile. Yote haya si mageni au ya kushangaza, maadamu Waislamu watabakia bila ya dola kuchunga mambo yao, watakuwa “kama mayatima chakula rahisi cha mazimwi, hali yao haitaimarika isipokuwa kupitia Khilafah inayowaunganisha kwa Kitabu cha Allah (swt) na Sunnah za Mtume Wake (saw)

 (وَيَوْمَئِذٍ يَفْرَحُ الْمُؤْمِنُونَ * بِنَصْرِ اللَّهِ يَنْصُرُ مَنْ يَشَاءُ وَهُوَ الْعَزِيزُ الرَّحِيمُ)

“…Na siku hiyo waumini watafurahi. Kwa Nusra ya Mwenyezi Mungu humnusuru amtakaye. Naye ndiye Mwenye nguvu Mwenye kurehemu” [Ar-Rum: 4-5]

6 Safar Al-Khair 1440 H

15/10/2018 M