Jumla

MSIMAMO WA KIISLAMU JUU YA RIPOTI YA BBI

Kusambaza ni Kuunusuru Uislamu

بسم الله الرحمن الرحيم

Mnamo Jumatano, 27 Novemba 2019, Wakenya walishuhudia uzinduzi rasmi wa ripoti ya BBI kutoka kwa Rais Uhuru Kenyatta ndani ya Bomas huko Nairobi. Tukio hilo lilikuwa ni kilele cha mkono wa kheri baina ya Rais Uhuru Kenyatta na Raila Odinga mnamo 9 Machi 2018 uliofanyika Harambee House. Kabla ya mkono wa kheri, Kenya ilikuwa ndani ya mzozo wa kiuchaguzi uliohusisha muungano wa upinzani NASA ukiongozwa na Raila Odinga na Chama cha Jubilee kikiongozwa na Uhuru Kenyatta. Licha ya kwamba uchaguzi wa urais uliofanyika mnamo 8 Agosti 2017 ulibatilishwa na kuagizwa ufanywe upya na Mahakama ya Upeo ya Kenya mnamo 1 Septemba 2017. NASA ilikataa kushiriki na kujiepusha na uchaguzi wa marudio uliofanyika mnamo 17 Oktoba 2017 ambapo Chama cha Jubilee kilishiriki na kutangazwa mshindi. Sababu kubwa ya NASA kujiepusha na uchaguzi huo ni kwamba matatizo yaliyotajwa kuwa ndio sababu ya kubatilishwa uchaguzi yalikuwa hayaja suluhishwa na yalijumuisha usimamizi mbaya wa uchaguzi ambao ulitakiwa kufanyiwa mabadiliko IEBC na kuuondoshwa kwa miswada ya mabadiliko ya uchaguzi iliyokuwa imewasilishwa bungeni na utawala wa Jubilee.

Kilichofuatia baada ya uchaguzi wa marudio mnamo Jumanne, 17 Oktoba 2017 ilikuwa ni machafuko ya kila wiki na ukosefu wa usalama yalizozidi kwa kuapishwa kwa Raila Odinga mnamo 30 Januari 2018, nchi ilikuwa inakaribia kutotawalika, na wasiwasi ulikuwa juu hususan mji mkuu Nairobi ilhali wawekezaji wakihofia maisha yao na uwekezaji wao! Hivyo basi, kama ilivyotokea mnamo 2007/08 wahusika wakuu walikutana Harambee House na kupeana mikono kutoka wakati huo wasiwasi ulipotea, wandani wa Raila wakateuliwa katika mashirika ya serikali miongoni mwa vyeo vingine! Zaidi ya hayo, mnamo Mei 2018 tumekazi ya BBI ikasajiliwa rasmi katika gazeti la serikali na kupewa kazi ya kutafuta maoni ya mwelekeo gani bora kuhusiana na kutatua matatizo yanayowakabili Wakenya na kuwasilisha ripoti kwa Rais Uhuru Kenyatta na Raila Odinga. Kwa kuongezea, amani na usalama ilirudi ilhali wawekezaji na uwekezaji wao wakahisi salama chini ya mchakato mpya wa kisiasa kiasi kwamba tukashuhudia ziara ya kipekee ya Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza, Theresa May mnamo Alhamisi, 30 Agosti 2018 ndani ya miaka 30 tangu ziara ya Margaret Thatcher nchini Kenya. Kwa mara nyingine Waziri Mkuu wa zamani aliwapongeza Raila na Uhuru kwa kutanguliza maslahi ya nchi kwanza na kudhamini usalama wake.

Hivi sasa nchi inakodolea mzunguko mpya wa mzozo huku wengine wakitaka ripoti ya BBI kupelekwa bungeni ili kuboreshwa zaidi na kutekelezwa. Upande wa pili, tunao wengine wanaotaka kura ya maoni, ili ripoti ipitishwe na kutekelezwa. Na katika mchakato huu ndipo Waislamu wamejipata njia panda ima kuikubali ripoti na kufuata njia ya bungeni au kura ya maoni pasi na kuzingatia ima wameisoma ripoti au la.

Baada ya kutathmini kwa kina matukio hayo hapo juu haina shaka kwamba ripoti ya BBI ni nakala iliyotungwa na wanadamu ambayo asili yake ni akili iliyo na kikomo na sio wahyi. Kwa kuongezea, ni nakala iliyopindishwa ili kuwahadaa na kuwatuliza watu walale hususan kipindi hichi ambapo Wakenya wanataabika kwa kuishi katika hali za kukatisha tamaa! Kenya ni dola ya kisekula ambayo itikadi (aqeedah) yake ni usekula (kutenganisha dini na maisha na dola) na mfumo wake wa kirasilimali unachipuza kutokana na kipaumbele cha uhuru wa kumiliki (uchumi) kwa hiyo unapima vitendo vya mwanadamu kwa msingi wa maslahi na manufaa. Kwa kuongezea, Kenya hadi sasa ni shamba la kikoloni ambalo viongozi (mameneja wa shamba) wake wameuza nafsi zao kwa mabwana zao Wamagharibi wakoloni na hivyo kipaumbele chao ni kuwa watumwa kwao na hivyo sera na sheria wanazozitunga ni kwa ajili ya kuwamakinisha wao na maslahi yao kwa gharama za raia wa kawaida!

 

Kama Waislamu sisi ni watumwa wa Mwenyezi Mungu (SWT) na kufaulu kwetu ni kumridhisha Mwenyezi Mungu (SWT) pekee kupitia kujisalimisha kwetu katika maamrisho na makatazo Yake (SWT) kwa msingi wa kipimo cha halali na haramu. Itikadi yetu ni: “لا إله إلا الله محمد رسول الله” “Hapana mungu isipokuwa Mwenyezi Mungu.

Muhammad ni mjumbe wa Mwenyezi Mungu” Kwa msingi wa itikadi yetu ni lazima tujifunge na Qur’an na Sunnah pekee. Mwenyezi Mungu (swt) asema:“يَـٰٓأَيُّہَا ٱلَّذِينَ ءَامَنُوٓاْ أَطِيعُواْ ٱللَّهَ وَأَطِيعُواْ ٱلرَّسُولَ” “Enyio mlio amini! Mtiini Mwenyezi Mungu, na mtiini Mtume” [An-Nisa: 59], “إِنِ ٱلۡحُكۡمُ إِلَّا لِلَّهِ‌ۚ” “Hapana hukumu ila ya Mwenyezi Mung tu” [Yusuf: 40], “وَمَنۡ أَحۡسَنُ مِنَ ٱللَّهِ حُكۡمً۬ا” “Na nani aliye mwema zaidi katika kuhukumu kuliko Mwenyezi Mungu” [Al-Maidah; 50] na “فَإِن تَنَـٰزَعۡتُمۡ فِى شَىۡءٍ۬ فَرُدُّوهُ إِلَى ٱللَّهِ وَٱلرَّسُولِ” “Na mkizozana katika jambo basi lirudisheni kwa Mwenyezi Mungu na Mtume” [An-Nisa: 59]. Kwa hiyo ripoti ya BBI ni natija ya mzozo wa kisiasa uliosababishwa na uchaguzi unaokwenda kinyume na Uislamu. Kenya kama ulivyo utawala wowote wa kisekula, inajivunia kuwa ni dola ya kidemokrasia kwa maana kwamba raia wanatunga, wanarekebisha na kufutilia mbali sheria ili kusimamia maisha yao kwa maana nyingine ni kuwa ubwana ni wa watu na watu ndio chimbuko la mamlaka kwa maana nyingine wanaweza kumchagua mwanamke au mwanamume kama mtawala/kiongozi wao na wanaweza kumuondosha wakati wowote wanapohisi kuwa hawakidhii maslahi au manufaa yao! Hii ni KINYUME na Uislamu ambapo ubwana ni wa Mwenyezi Mungu (swt) pekee kupitia Shari’ah Yake (Qur’an na Sunnah) na mamlaka ni ya watu (Ummah) lakini punde wanapomchagua Khalifah/mtawala/mwanamume hawezi kuondoshwa mpaka pale atakapotenda/kudhihirisha Ukafiri wazi.

Kwa mujibu wa hayo hapo juu ni wazi kwamba ripoti ya BBI haiwahusu Waislamu. Kwa kuwa msingi wake ni mfumo wa kisekula wa kirasilimali ambao kutokana nao zimechipuza nidhamu zake zenye sumu kama vile demokrasia, mujtama wa kihuria, nidhamu ya kiuchumi ya ukandamizaji, sera ya kigeni kwa msingi wa ukoloni n.k. Kwa upande mwingine, Waislamu lazima warudie Uislamu wao kimfumo kwa kuwa una suluhisho ya matatizo yote yanayowakumba wanadamu duniani kote na yaliyo sababishwa na mfumo batili wa usekula wa urasilimali na nidhamu zake. Kuurudia kwao lazima kuanzie pale ambapo Mtume (saw) alipokuwa mtume mnamo 610 M na maisha yake na maswahaba zake (ra) yalikuwa mabaya na yaliyojaa changamoto kama tunayokumbana nayo sasa nchini Kenya na duniani kote. Lakini kila kitu kikabadilika mnamo 622 M pale ambapo Mtume (saw) na maswahaba zake (ra) walipohama Makkah kwenda Madinah na aliwasili kama mtawala na kuasisi Dola ya Kiislamu ya kwanza duniani, alipofariki (saw) mnamo 632 M, Abu Bakr (ra) akachukua utawala kama Khalifah/mtawala wa kwanza mpaka Khalifah wa mwisho (102) Abdulmaji II mnamo 1924 M. Katika kipindi chote hicho cha takribani karne kumi na tatu chini ya utawala wa Dola ya Kiislamu ikitawala kwa Shari’ah, Waislamu na wasiokuwa Waislamu na wanadumu jumla walishuhudia utulivu, amani na ustawi ambao haujawahi kushuhudiwa katika mgongo wa ardhi.

Tangu kuvunjwa kwa Khilafah mnamo 3 Machi 1924 M, Waislamu wamekuwa mayatima ambao damu zao zinamwagwa pasina huruma na mali zao kuporwa kilafi na maadui wa Uislamu na Waislamu ambao leo wanaongozwa na Amerika na washirika wake duniani. Khilafah ya Waislamu ambayo ilikuwa dola moja chini ya mtawala mmoja anayetawala kwa Shari’ah iligawanywa na kuwa vijidola 50+ vilivyokadhibiwa watawala wajinga (ruwaibidha) waliouza nafsi zao kwa mabwana zao Wamagharibi wakoloni kwa usaliti wao wa kuivunja Khilafah. Kwa hiyo suala msingi kwa Waislamu leo la kuwashughulisha, ni kufanyakazi ya kurudisha maisha ya Kiislamu kupitia kusimamisha Dola ya Kiislamu ya Khilafah kwa njia ya Utume. Ni kupitia Khilafah pekee ndipo Waislamu na wanadamu jumla watapata utulivu, amani na ustawi mambo ambayo yanaahidiwa na ripoti ovu ya kisanii ya BBI ambayo nia yake ni kudumisha mfumo batili wa kisekula wa kirasilimali na nidhamu zake zinazonuka ambazo ndio chanzo cha wanadamu kutaabika nchini Kenya na duniani.

Hivyo basi, Waislamu lazima wajiepushe na mijadala isiyokuwa na natija kuhusiana na ripoti ya BBI na badala yake wajiunge na ndugu zao wa Hizb ut Tahrir kufanya kazi pasina kuchoka katika ulinganizi wa Khilafah na wakati huo huo kufanya mijadala yenye natija inayolenga kupambana mzizi unaosababisha tabu kwa wanadamu unaojumuisha namna ya kuondosha mfumo wa kisekula wa kirasilimali na nidhamu zake fisadi na kuweka Uislamu na nidhamu zake tukufu zinazochipuza kutoka kwa Muumba (swt). Hakika, ulinganizi wa Khilafah ndio ulinganizi pekee wenye kuleta mageuzi ya kikweli na kimsingi ambayo kila mtu kutoka Mashariki kwenda Magharibi anayalilia. “وَيَوۡمَٮِٕذٍ۬ يَفۡرَحُ ٱلۡمُؤۡمِنُونَ” “Na siku hiyo Waumini watafurahi” [Ar-Rum: 4].

 

Ali Nassoro Ali