Jumla

Mtume (saw) Ni Kiigizo Chema

Kusambaza ni Kuunusuru Uislamu

Ummah mtukufu wa Waislamu kufaulu kwake duniani na akhera kunategemea kujifunga kikamilifu katika Uislamu (Qur’an na Sunnah) kama mfumo kamili wa maisha na kujiepusha na mfumo batili wa kisekula wa kirasilimali unaongozwa na Shetani na wafuasi wake katika masekula warasilimali:

يَـٰٓأَيُّهَا ٱلَّذِينَ ءَامَنُواْ ٱدۡخُلُواْ فِى ٱلسِّلۡمِ ڪَآفَّةً۬ وَلَا تَتَّبِعُواْ خُطُوَٲتِ ٱلشَّيۡطَـٰنِ‌ۚ إِنَّهُ

“Enyi mlio amini! Ingieni katika Uislamu kwa ukamilifu, wala msifuate nyayo za Shetani” [Al-Baqara: 208]

Hakika haiwezikani kujifunga kikamilifu na mfumo wa Uislamu mpaka Waislamu wamfuate/wamuige Mtume (saw):

لَّقَدۡ كَانَ لَكُمۡ فِى رَسُولِ ٱللَّهِ أُسۡوَةٌ حَسَنَةٌ۬

“Hakika nyinyi mnacho kiigizo chema kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu.” [Al-Ahzab: 21]

“Hakika, tabia ya Mtume wa Mwenyezi Mungu ilikuwa ni Qur’an.” [Muslim]

Na kumuiga Mtume (saw) hakukamiliki mpaka Waislamu wajifunge na aliyokuja nayo Mtume (saw):

هُوَ ٱلَّذِىٓ أَرۡسَلَ رَسُولَهُ ۥ بِٱلۡهُدَىٰ وَدِينِ ٱلۡحَقِّ لِيُظۡهِرَهُ ۥ عَلَى ٱلدِّينِ كُلِّهِۦ‌

“Yeye ndiye aliye mtuma Mtume wake kwa uwongofu na Dini ya Haki, ili aitukuze juu ya dini zote.” [Al-Fath: 28]

Bila kutimiza hatua hizo kamwe Ummah huu mtukufu wa Waislamu hauwezi kujifahari kuwa una mapenzi ya kweli kwa Mtume (saw). Mapenzi ya kweli kwa Mtume (saw) lazima yafungamanishwe na haki ya uwongofu aliyokuja nayo na itenganishwe na batili inayotokana na Shetani na wafuasi wake hususan wamagharibi wakoloni waliobeba mfumo wa kisekula wa kirasilimali. Mapenzi ya kweli kwa Mtume (saw) yamekitwa katika kujifunga na hukumu za kisharia ambazo hivi sasa hazitekelezwi kwa ukamilifu wake na badala yake zinatekelezwa baadhi tu tena kibinafsi bila msukumo wowote wa dola. Kwa upande mwingine Waislamu wanatawaliwa na kukandamizwa na vibaraka wa dola za kisekula za kirasilimali zinazopigia debe batili kupitia kuharamisha yaliyo halalishwa na kuhalalisha yaliyo haramishwa na Mwenyezi Mungu!

Kumuiga Mtume (saw) kiukweli ndiyo njia pekee itakayowapa Waislamu ujasiri na hamu ya kufahamu kuwa uhai wao hapa duniani ni kwa ajili ya Uislamu utawale na uwe juu ya dini nyingine zote! Na ili kufikia hatua hiyo ni lazima Waislamu wajifunge kikamilifu katika Uislamu na wafanye bidii usiku na mchana kuhakikisha kuwa Uislamu unarudi tena katika maisha yao jumla kupitia kurudisha tena Serikali ya Kiislamu ya Khilafah kwa Njia ya Utume. Na ili kufikia kilele hicho lazima Waislamu wajitoe muhanga na wawekeze juhudi ya hali na mali zao ili kuhakikisha kuwa Mwenyezi Mungu anawaridhia na kuwapa ushindi dhidi ya ufisadi unaoendelea hivi sasa duniani. Kinyume chake ni kuwa Waislamu na Uislamu utaendelea kupigwa vita na kuoteshwa vidole na kuitwa majina eti “Misimamo Mikali, Magaidi au Ugaidi n.k” kwa kuwa tumejiweka mbali na Uislamu kwa kutomuiga Mtume (saw) kama kiigizo chema.

Ali Nassoro Ali

Mwanachama wa Afisi ya Habari ya Hizb ut Tahrir Kenya