Jumla

Mwanamke wa Kiislamu na Watoto Wake; Dhati Halisi ya Umma wa Kiislamu!

Kusambaza ni Kuunusuru Uislamu

Bila shaka yoyote watoto ni chimbuko la furaha na ridhaa kuu; huyafanya maisha kuwa matamu, na huleta matumaini. Baba huwaona watoto wake kuwa chimbuko la usaidizi wa siku za usoni, pamoja na kuwakilisha ongezeko la idadi na kudumu kuendelea kwa familia. Mama huwaona watoto kuwa chimbuko la matumaini, maliwazo na furaha maishani, na kama matarajio siku za usoni. Matarajio yote haya yanategemea malezi mazuri ya watoto hawa na kuwapa matayarisho muwafaka kwa maisha, ili wawe watu wakakamavu na wenye kuleta faida ndani ya mujtamaa, chimbuko la kheri kwa wazazi wao, jamii na mujtamaa kwa jumla. Ndipo watakapo kuwa kama vile Allah (swt) alivyo wafafanua:

((الْمَالُ وَالْبَنُونَ زِينَةُ الْحَيَاةِ الدُّنْيَا…))

(Mali na watoto ni mapambo ya maisha ya dunia . . .) (Al-Kahf:46)

Ikiwa elimu na malezi yao yatapuuzwa, watakuwa na utambulisho ‘shakhsiyya’ mbaya, mzigo kwa familia yao, jamii na mujtamaa kwa jumla. Hivyo basi mama ni sharti aelewe jukumu kubwa alilo nalo juu ya watoto wake.

Mwanamke wa Kiislamu kamwe hasahau kuwa jukumu la mama katika malezi ya watoto na kuunda utambulisho ‘shakhsiyya’ wao ni kubwa zaidi kuliko jukumu hilo kwa baba, hii ni kwa sababu kimaumbile watoto huwa karibu sana na mama yao na hutumia muda mwingi wakiwa pamoja naye; hivyo basi anajua yote kuhusu tabia zao, hisia zao ukuaji wa kifikra utotoni mwao na katika kipindi kigumu cha kubaleghe kwao.

Hivyo basi, mwanamke anayefahamu mafundisho ya Uislamu na jukumu lake binafsi la kuwa mwalimu maishani, hujua jukumu lake kamili la malezi ya watoto wake, kama lilivyo elezwa ndani ya Qur’an:

((يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا قُوا أَنْفُسَكُمْ وَأَهْلِيكُمْ نَارًا وَقُودُهَا النَّاسُ وَالْحِجَارَةُ…))

(Enyi mulio amini! Ziokoeni nafsi zenu na za jamaa zenu na Moto ambao kuni zake ni watu na mawe . . .) (At-Tahreem:6)

Imepokewa na Abdullah ibn ‘Umar (ra) Mtume (saw) pia amelieleza jukumu hili katika hadith hii:

عَنْ عَبْدِ اللَّهِ بْنِ عُمَرَ يَقُولُ: سَمِعْتُ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّه عَلَيْهِ وَسَلَّمَ يَقُولُ:  ((كُلُّكُمْ رَاعٍ وَكُلُّكُمْ مَسْؤول عَنْ رَعِيَّتِهِ، الإِمَامُ رَاعٍ وَمَسْؤولٌ عَنْ رَعِيَّتِهِ، وَالرَّجُلُ رَاعٍ فِي أَهْلِهِ وَهُوَ مَسْؤولٌ عَنْ رَعِيَّتِهِ، وَالْمَرْأَةُ رَاعِيَةٌ فِي بَيْتِ زَوْجِهَا وَمَسْؤولَةٌ عَنْ رَعِيَّتِهَا، وَالْخَادِمُ رَاعٍ فِي مَالِ سَيِّدِهِ ومَسْؤولٌ عَنْ رَعِيَّتِهِ…))

“Nyote ni wachungaji na nyote mutaulizwa juu ya mulivyo vichunga, kiongozi ni mchungaji na ataulizwa kuhusu raia wake, na mume ni mchungaji wa familia yake na ataulizwa kuwahusu, na mke ni mchungaji wa nyumba ya mumewe na ataulizwa kuihusu, na mtumishi ni mchungaji wa mali ya bwana wake na ataulizwa kuihusu…”

Uislamu umeweka jukumu juu ya mabega ya kila mtu; hakuna yeyote aliye achwa pasi na majukumu. Wazazi – hususan mama – wamefanywa kuwa wasimamizi katika kuwapa watoto wao malezi imara na elimu sahihi ya Kiislamu, kwa msingi wa sifa alizotangaza Mtume (saw) kuwa ametumilizwa kwa ajili ya kuzikamilisha na kuzieneza miongoni mwa watu:

(( إنما بعثت لأتمم مكارم الأخلاق ))
“Hakika nimetumilizwa ili nikamilishe tabia njema.”

Hakuna kinacho ashiria zaidi ukubwa wa jukumu la wazazi kwa watoto wao na wajibu wao wa kuwapa malezi sahihi kuliko hukmu ya maulama kuwa kila familia itilie maanani maneno ya Mtume (saw):

((مُرُوا أَوْلادَكُمْ بِالصَّلاةِ وَهُمْ أَبْنَاءُ سَبْعِ سِنِينَ ، وَاضْرِبُوهُمْ عَلَيْهَا وَهُمْ أَبْنَاءُ عَشْرٍ))
“Waamrisheni watoto wenu kuswali wanafika umri wa miaka saba, na wapigeni juu ya hilo wanapofika umri wa miaka kumi.”

Wazazi wowote wanao fahamu hadith hii lakini wakawa hawawafundishi watoto wao kuswali wanapofikia umri wa miaka saba au kuwapiga ikiwa hawataswali wanapofikia umri wa miaka kumi, ni wazazi waliomo kwenye madhambi na waliofeli katika jukumu lao; wataulizwa mbele ya Allah (swt) kwa kufeli kwao huku.

Nyumba ya familia ni taswira ndogo ya mujtamaa ambamo akili za watoto, fikra zao, hisia zao na matamanio yao huundwa wakati ambapo wangali wachanga na wako tayari kupokea maneno sahihi ya uongofu. Hivyo basi dori muhimu ya wazazi katika kuunda akili za watoto wao wa kiume na wa kike na kuwaongoza katika haki na amali njema iko wazi.

Wanawake wa Kiislamu daima wamekuwa wakifahamu jukumu lao katika malezi ya watoto wao, wanarekodi nzuri sana katika upande wa kuzalisha na kuathiri wanaume watukufu, na kutia ndani ya nyoyo zao maadili mema. Hakuna ushahidi mkubwa wa hili kuliko ukweli kuwa wanawake werevu na mahiri wameweza kuzalisha watoto waheshimika zaidi kuliko wanaume werevu na mahiri, kiasi ya kuwa huwezi kupata yeyote miongoni mwa wanaume watukufu wa Umma wetu walioweza kutawala matukio ya kihistoria ambaye hakuupata utukufu wake kupitia mamake.

Al-Zubayr ibn al-‘Awwam (ra) anarudisha shukrani zake kwa mamake Safiyyah bint ‘Abd al-Muttalib (ra) kwa utukufu wake, ambaye alikuuza ndani yake sifa nzuri na maumbile ya kipekee.

‘Abdullah, al-Mundhir na ‘Urwah, watoto wa al-Zubayr (ra) ni matunda ya maadili yaliyo kuzwa ndani yao na mama yao, Asma’ bint Abi Bakr (ra), na kila mmoja wao aliweka alama katika historia na kupata daraja ya juu.

‘Ali ibn Abi Talib (ra) alipata hekima yake, tabia njema na shakhsiyya njema kutoka kwa mamake maarufu, Fatimah bint Asad.

‘Abdullah ibn Ja’far (ra), bwana wa ukarimu wa Waarabu na kiongozi wao muheshimiwa zaidi, alimpoteza babake akiwa na umri mdogo, lakini mamake Asma’ bint ‘Umays (ra) alimlea kwa uangalifu na kumpa maadili na utambulisho ‘shakhsiyya’ mwema iliyopelekea mpaka yeye mama kuwa miongoni mwa wanawake watukufu katika Uislamu.

Pia, historia imenakili majina ya wanaume wawili watukufu kutoka kabila la Banu Umayyah, wa kwanza alijulikana kwa shakhsiyya yake imara, uwezo, werevu, hekima na azma, na wa pili alichukua njia ya uadilifu, kheri, ucha Mungu na wema.

Wa kwanza ni ‘Abd al-Malik ibn Marwan (ra), ambaye mamake alikuwa ni ‘A’ishah bint al-Mughirah ibn Abi’l-‘As ibn Umayyah, ambaye alikuwa maarufu kwa shakhsiyya yake imara, azma na werevu wake. Wa pili ni ‘Umar ibn ‘Abd al-‘Aziz (ra), wa tano miongoni mwa Makhalifah waongofu, ambaye mamake alikuwa Umm ‘Asim bint ‘Asim ibn ‘Umar ibn al-Khattab (ra), aliyekuwa na shakhsiyya tukufu zaidi miongoni mwa wanawake wa zama zake. Mamake alikuwa mja mwema aliye muabudu Allah (swt) ambaye ‘Asim aliona ndani yake uaminifu na ukweli, na kufuata kwake njia ya sawa wazi wazi, pindi alipokataa kuongeza maji kwenye maziwa kama alivyo agizwa na mamake, kwa sababu alijua kuwa Allah (swt) anamuona.

Tunapogeukia Andalusia (Spain), tunamkuta kiongozi mahiri, mwenye maono ‘Abd al-Rahman al-Nasir ambaye, licha ya kuanza maisha akiwa yatima, aliweza kupanua mipaka ya dola ya Khilafah na kufika mpaka Magharibi, ambapo iliwafanya viongozi na wafalme wa bara Ulaya kujisalimisha kwa dola hiyo na dola ambayo taasisi zake za kielimu ziliweza kuzalisha wasomi na wanafalsafa kutoka katika mataifa yote yaliyokuja kutafuta elimu. Dola hii ilitoa mchango mkubwa kwa hadhara ya Kiislamu ulimwenguni. Ikiwa tutafanya utafiti juu ya siri ya utukufu wa mwanamume huyu, tutakuta kuwa unatokana na utukufu wa mamake aliye fahamu jinsi ya kukuza maadili makuu ya kuwa mtu mwenye maono.

Katika zama ya utawala wa ‘Abasiyya walikuweko wanawake wawili watukufu waliopanda mbegu za maono, utukufu na nguvu kwa watoto wao. Wa kwanza alikuwa mamake Ja’far ibn Yahya (ra), aliyekuwa Waziri wa Khalifah Harun al-Rashid. Wa pili alikuwa mamake Imam Shafi’: ambaye hakuwahi kumuona babake aliyefariki akiwa mchanga; mamake ndiye aliyemlea kwa uangalifu na kumsomesha.

Kuna mifano mingi ya aina hii ya wanawake katika historia yetu, wanawake walioweza kukuza katika watoto wao, shakhsiyya heshimika na mbegu za utukufu, na ambao walisimama kidete nyuma yao kwa kila walichopata katika utawala na cheo.

Vile vile hili liwe kwa wanawake na mama wa Kiislamu leo, hawana budi kusimama kidete kutekeleza majukumu yao na kuchukuwa mfano kutoka kwa watangulizi wao katika kuunda Umma wa Kiislamu ulio imara kwa kupitia kuwalea watoto wao wa kiume na wa kike kwa thaqafa imara ya Kiislamu. Hawana budi kutia motisha ndani ya nyoyo za watoto wao wa kushikamana imara na dini yao na da’wah ya Kiislamu hususan da’wah ya kurudisha Uislamu kama mfumo kamili wa maisha kupitia kusimamisha dola ya Kiislamu ya Khilafah, dola ambayo ndiyo iliyo zalisha mama na watoto waliotangulia kutajwa juu kama watu waliokuwa na shakhsiya heshimika za kipekee katika historia yote ya Uislamu.

Masoud Salim Mazrui

Mwanachama wa Hizb ut Tahrir Kenya

 

Kutoka Jarida la UQAB Toleo 13