Jumla

Nani Mtetezi wa Raia Katika Dola Hizi za Kikoloni za Kisekula?

Kusambaza ni Kuunusuru Uislamu

Kenya imeshuhudia matukio kadhaa japo katika maeneo na taasisi tofauti lakini yote yanaashiria muktadha mmoja. Tukio la kwanza ni lile la kubomoa majengo katika upanuzi wa barabara ya Mombasa-Malindi na Mombasa-Mariakani ambao kwa mujibu wa KeNHA na NLC wenyewe hawatolipwa maanake wamejenga katika hifadhi ya barabara! [Standard Digital, 9 Machi 2018]. Tukio la pili likiwa lile la kubomoa ya vibanda vya wauzaji ‘muguka’ ndani ya Kaunti ya Mombasa kwa kisingizio kwamba bidhaa hiyo ina madhara na inasababisha watumiaji kukosa hamu ya tendo la ngono na hata kuweza kupata maradhi ya kansa! [The Star, 6 Agosti 2018] Tukio la tatu ni lile la Bunge la Kitaifa siku ya Alhamisi 9 Agosti 2018 kuiangusha ripoti ya kuhusiana na sukari bandia huku baadhi ya Wabunge wakidai kuwa eti ilikuwa ina walenga maafisa wa kuu wa serikali bila kuzingatia itifaki ya kuwang’oa mamlakani! [Daily Nation, 10 Agosti 2018] Tukio la nne ni la kubomoa majengo yaliyojengwa pambizoni mwa mito ambalo limeanza hivi majuzi likiongozwa na Raisi kupitia kamati maalumu inayojumuisha asasi za serikali Nairobi! Huku Raisi akisema kuwa zoezi hilo linalenga kupambana na ufisadi katika umiliki wa ardhi kuambatana na vita vya ufisadi vinavyoendelea. [Capital News, 9 Agosti 2018]

Matukio haya kwa raia mwenye akili isiyokuwa makini atayashangilia na kuyaona kuwa ni uwajibikaji wa Serikali katika kuwasimamia raia mambo yao. Lakini ukweli ni kwamba matukio yote haya yanadhihirisha kufeli kwa serikali hizi za kikoloni za kisekula zinazoendeshwa kwa manufaa/maslahi na wala sio kwa msukumo wa kujali na kuwathamini raia wake. Kama inavyoshuhudiwa ifuatavyo:

Tukio la kwanza: Serikali ilikuwa wapi wakati raia wakitumia mali yao waliyoichuma kwa dhiki kisha kujenga/kuwekeza katika mijengo hiyo?! Hii ni wazi kuwa serikali hii inajali maslahi na iko tayari kuwatoa kafara raia wake ili kufikia masharti yoyote yanayofungamana na mikopo eti ya maendeleo na ndiyo maana hivi sasa kwa kuwa wamekodolea macho kitita cha mkopo baada ya kutia saini na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kudhamini mwanzo wa ujenzi wa upanuzi huo kutoka Mombasa hadi Kanamai. Maslahi yao ni kupokea na kuifuja mikopo hiyo na kuutia uchumi wa Kenya kitanzi kutokana na riba isiyoisha!

Tukio la pili: Kumetumika kipimo gani kutofautisha madhara ya miraa, pombe, bangi, madawa ya kulevya (heroine n.k), shisha na muguka? Kwani hizo nyingine hazidhuru lakini muguka pekee ndiyo inayodhuru? Ukweli ni kwamba tangu kuanza kwa biashara ya muguka wafanyi biashara wengi wa miraa wamekuwa wakilalalama kutokana na kudorora kwa mauzo tukizingatia kuwa muguka inauzwa rahisi ukilinganisha na miraa ambayo iko juu. Ukweli ni kwamba serikali ya kaunti haina budi kudandia hisia za raia hususan wakati huu ambapo serikali ya kaunti iko katika hatamu yake ya mwisho na baadhi ya viongozi wakuu wakikodolea macho siasa za 2022 ili waambiwe ni wachapaji kazi n.k napia kuwatumia raia kama ngazi katika meza ya mazungumzo ya kugawa ngawira za siasa za 2022. Ingelikuwa kweli wanawajali raia wangelipiga marufuku vileo vyote maanake asili vina dhuru afya ya mwanadamu. Lakini hii ni mbinu ya kuwanyooshea mkono wenye biashara ya miraa na huku wakiwa nyooshea mikono raia na katikati wakiwakandamiza wauza muguka!

Tukio la tatu: Wabunge hudai wamechaguliwa na kupewa mamlaka kwenda Bungeni ili kutunga sheria zinazowapa raia kipao mbele katika kuboresha maisha yao. Lakini kwa kuwa Bunge linatokana na nidhamu ya kidemokrasia na msingi wake ni sawa na wa nyumba ya buibui hivyo daima hauna umadhubuti kuweza kuhimili mawimbi ya hongo na rushwa! Na kudhihirisha wazi kuwa kiasili Wabunge wako kwa maslahi ya matumbo yao na raia ni sehemu ya ngazi kufikia maslahi hayo. Kelele tunazozisikia zinasababishwa na kuchelea kupigwa na chini baadhi yao katika siasa za 2022 ambapo wapinzani wao wanaweza kuzitumia dhidi yao. Kwa hiyo wanarushiana maneno ya lawama kila mmoja akimlaumu mwenzie kwa kuiangusha ripoti hiyo ili ajisafishe mbele ya raia!

Tukio la nne: Serikali hii ilikuwa wapi watu wakijenga/wakiwekeza katika maeneo hayo?! Inamaanisha kuwa ndani ya serikali kunao mpango maalumu wa kuwatia hasara au kuwatisha baadhi ya matajiri ili waweze kuwaondosha katika mpango wa siasa za 2022. Badala yake wafuate mchoro uliowekwa na wakoloni kupitia makubaliano kati ya vibaraka wao ya hivi majuzi ya 9 Machi 2018! Kama kweli serikali ilijali raia wake kupitia makubaliano ya hivi majuzi basi ingelianza na utekelezwaji wa ripoti ya TJRC ambayo ingeashiria kweli kuna muamko mpya nchini!

Matukio yote yanaashiria kuwa raia hawana mtetezi isipokuwa miaka nenda miaka rudi wanachagua vinyozi na kuwapa madaraka ya kuwanyoa zaidi! Lakusikitisha ni kuwaona raia jumla wakiwalaumu watu fulani au kabila fulani kwamba wao ndio chanzo cha hali duni ya taifa hili. Na kudai kwamba suluhisho lipo kwa kuwabadilisha na kuweka wengine au kutoka kabila jengine. Ilhali tatizo msingi ni mfumo wa kirasilimali wa kisekula unaotawala nchini Kenya. Kupitia mfumo huu na nidhamu zake kandamizaji na fisidifu kamwe hakuna anaye nusurika nao.

Suluhisho lipo ndani ya Uislamu kama mfumo safi utokao kwa Muumba wa mbingu na ardhi. Kupitia mfumo wa Uislamu serikali ya Kiislamu ya Khilafah huchipuza chini ya kiongozi mchaMungu na hukitwa juu ya Muongozo wa Qur’an na Sunnah (kipimo ni halali na haramu na sio hasara/faida/manufaa/maslahi). Hivyo basi mtetezi wa raia ni kiongozi wa kiulimwengu Khalifah anayewapa nusra Waislamu na wasiokuwa Waislamu popote walipo ili waweze kutokana na dhulma na maonevu dhidi yao kutoka kwa serikali za kisekula za kirasilimali. Hatua ya haraka kuichukua hivi sasa kwa Waislamu ni kuukumbatia mwito wa kufanya kazi kuregesha tena maisha ya Uislamu ili hadhi na cheo viweze kupatikana juu ya mgongo huu wa ardhi na akhera kwa kujifunga na maamrisho ya Allah (swt). Ama kwa wasiokuwa Waislamu wajitahidi kuupa nafasi Uislamu na kuusoma barabara kama mfumo badala ulio na uwezo wa kuutia urasilimali katika kaburi la sahau na sehemu yake kusimama Uislamu na kuwasimamia mambo yao kwa uadilifu ambao haujawahi kushuhudiwa katika karne hii ya urasilimali na hapo awali ujamaa.

Imeandikwa kwa Ajili ya Radio Rahma

Ali Nassoro Ali

Mwanachama wa Afisi ya Habari ya Hizb ut Tahrir Kenya

Makala Na.7 Ijumaa, 6 Dhul-Hijja 1439H | 2018/08/17