Jumla

Ramadhani ni Mwezi wa Nussrah na Ushindi

Kusambaza ni Kuunusuru Uislamu

بسم الله الرحمن الرحيم

Saumu ndani ya mwezi mtukufu wa Ramadhani ilifaradhishwa mwaka wa 2 Hijria katika zama ambazo Waislamu walikuwa chini ya Dola yao ya Kiislamu ikiongozwa na Mtume (saw). Ilikuwa enzi ambayo tokea kwa Mtume (saw) na Makhalifa wengi waliochukua uongozi baada ya kufa kwake, wote walikuwa wakitawala kwa mujibu wa Shari’ah (Qur’an na Sunnah). Utajiri na rasilimali zetu zilisambazwa kwa haki kwa kila raia pasina kufungwa kwa matajiri pekee, ili masikini waweze kuondolewa dhiki zao. Vilio vya waliokuwa wanakandamizwa vilijibiwa kwa haraka na makamanda na wanajeshi wanaokwenda mbio kutafuta shahada kupitia Jihadi. Wazee, wanawake na watoto ima Waislamu au wasiokuwa Waislamu hadhi na heshima zao zilipewa kipaombele na kuhifadhiwa kwa hali yoyote. Hakika ni kupitia kutawaliwa na Uislamu kwa mujibu wa Shari’ah ndipo ilipofikia Ramadhani kuwa ndiyo mwezi wa Nussrah na Ushindi kwa makarne. Ndani ya Ramadhani, Uislamu na Waislamu walipata nussrah na ushindi katika Badr, kuikomboa Makkah, kuwashinda Wafursi katika Al-Buwayb, kukomboa Amooriyah na kuwashinda Matartar katika Ain-Jaloot na matukio makubwa zaidi! Enzi hizo bendera za Liwah na Rayah zilikuwa zikipepea na kuonyesha ishara ya kuweko na mlinzi na ngao inayo dhamini haki na rehema kwa wanadamu wote duniani!

Leo, Ramadhani inatujilia tukiwa katika zama ambapo utawala wa Uislamu kwa mujibu wa Shari’ah (Khilafah) HAUPO! Hakika tumo katika kiza kinene, maangamivu, machungu na fedheha. Licha ya kuwa tuna majeshi makubwa ndani ya Biladi za Waislamu kila kukicha ushindi ni kwa maadui zetu ambao wamenyanyua bendera zao za Ukafiri zilizojaa damu za watoto wetu, wanawake wetu na wazee wetu! Na licha ya kuwa na ardhi kubwa zilizojaa rasilimali tele, bado tunazama katika umasikini huku migongo yetu ikidhikika kutokana kuchakura majaani na kufurushwa na kuoteshwa vidole huku na kule. Hakika Ukafiri na Makafiri wakiongozwa na Marekani na washirika wake wanaendeleza mashambulizi ya kifikra na kijeshi dhidi ya Uislamu na Waislamu katika kila pembe ya dunia hivi sasa. Wanaendeleza uporaji wa mali zetu na uvamizi wa ardhi zetu na kuyakejeli matukufu yetu pasina kujali wala kuogopa!

Enyi Waislamu; mumeridhia kutawaliwa na Ukafiri  na Makafiri; wakituongoza kwa mujibu wa mfumo wao batili wa wa kisekula wa kirasilimali pamoja na nidhamu zake ambazo zinaendeleza ukoloni katika nchi zetu? Nidhamu chafu ikiwemo ya demokrasia inayompa mwanadamu mamlaka ya kujitungia muongozo/sheria kinyume na za Mwenyezi Mungu (swt)? Nidhamu ya kijamii inayonuka na inayopigia debe ufuska na usherati katika mujtama? Nidhamu ya Kiuchumi ovu iliyomakinishwa juu ya msingi wa utozaji riba na ushuru? Mutamjibu nini Mwenyezi Mungu (swt) mutakapokufa katika hali hii ambapo Ukafiri na Makafiri wapo juu yetu? Ilhali Ashatuambia: (إِنَّ ٱلدِّينَ عِندَ ٱللَّهِ ٱلۡإِسۡلَـٰمُ‌ۗ)Bila ya shaka Dini mbele ya Mwenyezi Mungu ni Uislamu.” [Aal-e-Imran: 19] na (وَرَضِيتُ لَكُمُ ٱلۡإِسۡلَـٰمَ دِينً۬ا‌ۚ)nimekupendeleeni Uislamu uwe ndiyo Dini.” [Al-Maidah: 3].

Enyi Waislamu tukumbukeni kuwa ili kulinda damu zetu, mali zetu, matukufu yetu na hadhi zetu lazima tujifunge kikamilifu na Uislamu: (يَـٰٓأَيُّهَا ٱلَّذِينَ ءَامَنُواْ ٱدۡخُلُواْ فِى ٱلسِّلۡمِ ڪَآفَّةً۬)Enyi mlio amini! Ingieni katika Uislamu kwa ukamilifu.” [Al-Baqarah: 208]. Hakika kujifunga na Uislamu ndiko kutakako ilainisha mioyo ya Waislamu na hususan vijana wanajeshi Waislamu walioko ndani ya Biladi zetu za Waislamu na kuwasababisha kukata minyororo ya utumwa kwa kuwatumikia watawala vibaraka wa wakoloni ambao kibla chao ni London, Washington, Paris n.k. Kisha kuwang’oa mamlakani kwa kumuitikia Mwenyezi Mungu (swt): (يَـٰٓأَيُّہَا ٱلَّذِينَ ءَامَنُواْ ٱسۡتَجِيبُواْ لِلَّهِ وَلِلرَّسُولِ إِذَا دَعَاكُمۡ لِمَا يُحۡيِيڪُمۡ‌ۖ)Enyi mlio amini! Muitikieni Mwenyezi Mungu na Mtume anapo kuitieni jambo la kukupeni uzima wa milele.” [A;-Anfal; 24]. Hakika kuitikia kwao iwe ni kwa kutoa nusra (nguvu za kijeshi) kwa chama cha Kiislamu kisichopaka mtu mafuta wala kujali lawama kutoka kwa anaye laumu miongoni mwa watu wanaopiga hesabu kwa misingi ya manufaa/faida/hasara. Nacho ni chama cha Hizb ut Tahrir mlinzi na ngao ya Ummah mtukufu wa Waislamu na wanadamu kwa ujumla. Kwa kutoa nusra ndiko kutahakikisha kuwa Uislamu unarudishwa katika maisha kupitia kusimamisha tena Serikali ya Kiislamu ya Khilafah kwa njia ya Utume.

Enyi Wanadamu kusimama kwa Khilafah si ushindi tu kwa Uislamu na Waislamu bali ni ushindi kwa wanadamu wote duniani! Hakika wanadamu wote wanateseka duniani chini ya mfumo muovu wa kisekula wa kirasilimali unao wapa kipaombele na kuwalinda wachache miongoni mwa matajiri ili kuendeleza kuwafanya watumwa wanadamu ili wawaabudu wao! Ramadhani ni mwezi wa ushindi kwa wanadamu; kwani Khilafah itasimama ili kuwahurumia na kuwatumikia wanadamu wote kwa mujibu wa Shari’ah na sio kwa ajili ya kuwatesa na kuwakandamiza wanadamu kama inavyo shuhudiwa katika serikali za kirasilimali za kidemokrasia ulimwenguni kote! Hakika Khilafah itaitabikisha Qur’an kwa ukamilifu wake ili kupatikane utulivu, maendeleo na ufanisi wa kikweli kwa wanadamu wote.

(شَہۡرُ رَمَضَانَ ٱلَّذِىٓ أُنزِلَ فِيهِ ٱلۡقُرۡءَانُ هُدً۬ى لِّلنَّاسِ وَبَيِّنَـٰتٍ۬ مِّنَ ٱلۡهُدَىٰ وَٱلۡفُرۡقَانِ‌ۚ)

“Ramadhani ni mwezi ambao Qur’an imeteremshwa kuwa ni uongofu (muongozo) kwa watu, hoja zilizo wazi za uongofu na upambanuzi”

[Al-Baqarah: 185]

 

Ali Nassoro Ali

Mwanachama wa Afisi ya Habari ya Hizb ut Tahrir Kenya