Ujumbe wa Ameer

Risala Kutoka Kwa Amiri wa Hizb ut Tahrir Kwenda Kwa Wale Wanaoihami Dawah Hii

Kusambaza ni Kuunusuru Uislamu

بسم الله الرحمن الرحيم

(Imetafsiriwa)

Sifa njema zote ni kwa Allah na dua na salamu zimshukie Mtume wa Allah na jamaa zake na maswahaba zake na wale waliokuja baada yake,

Kwa wale wote walionitumia risala kupitia ukurasa wangu wa Facebook, wakishtumu maandishi hayo meusi kupitia mtandao…

Kwa wale wote walio niandikia, wakishtumu maandishi ya kikundi cha waasi ‘Nakithin’ (waliovunja kiapo) na wale waliotoka (chamani) na wale ambao kwa sasa wanachukuliwa hatua za kinidhamu…

Kwa wale wote walio niandikia; wakishtumu maandishi hayo maovu ya yule aliyetekwa na kiburi chake…

Kwa wale wote walionitumia jumbe zao, wakishangazwa ni vipi watu hawa na wafuasi wao wanajidhalilisha kiasi hicho…

Kwenu nyote, nawasalimu kwa maamkuzi ya Kiislamu:

Assalamu Alaikum Wa Rahmatullah Wa Barakatuh

Kaka na Dada Zangu Wapendwa,

Haishangazi kuwepo kwa aina hiyo ya watu na wafuasi wao, maadamu wema na ubaya ungalipo ulimwenguni… watu aina hiyo wamekuwepo tangu zamani na wangalipo mpaka leo na wanatarajiwa kuwepo siku za usoni vile vile. Baadhi ya wanachama wa Kamati ya Uongozi wa Hizb walikihama chama wakipinga muelekeo wa Amiri muasisi Abu Ibrahim (Allah amuwiye radhi). Na wakati wa enzi ya Amiri wa pili Abu Yusuf (Allah amuwiye radhi), baadhi ya wanachama wa afisi ya Amiri walivunja kiapo chao. Na leo, wanaume, walio na usemi na uzito kwa sababu ya Hizb, wamepotea njia, wamekiangusha chama, Hizb iliwapa hadhi lakini wakaamua kushikamana na dunia.

﴿وَلَكِنَّهُ أَخْلَدَ إِلَى الْأَرْضِ وَاتَّبَعَ هَوَاهُ

“…lakini (badala yake) alishikamana na dunia na akafuata matamanio yake.” [Al-A’raf: 7:176]

Kupotea njia kwao hakukuwa tu ni kupotea njia; bali walikhini amana na kuzua urongo. Baada ya kufanya dhambi hilo kubwa kwa kumkhini yatima mali yake, kiongozi wao asema: nimerudisha thamani ya nyumba hii – kana kwamba ni mkweli – lakini hamwambii mwenye nyumba, bali amwambia mtu aliyeadhibiwa na wala hayumo ndani ya Hizb! … kama ambaye kwamba mmiliki wa nyumba hiyo hajulikani na wala hakumkabili mara kadhaa juu ya kadhia hii! Je hili sio jambo la kushangaza mno?

Na mmoja wao akamuuliza kuwa kwani haitoshi kwa Amiri kukuomba radhi naye akamjibu kuwa haitoshi! Hivyo basi wanazidanganya nafsi zao kabla ya kumdanganya Allah; kana kwamba kuna ombi la kuomba radhi! Wanafuata barabara ya uvumi mchafu. Wamedumu katika kudanganya, kwa matarajio ya kupata watu vipofu, wasioona sasa wala mbeleni, ambao watawaamini. Mmoja wao alisema: Amiri alituma agizo kwa wanachama kuuandikia usimamizi wa mtandao wa Facebook ufunge ukurasa wa mtu huyo. Na mwengine wao akajibu kwa kutoa hakikisho kubwa kwamba hili lilifanyika na ukurasa huo kufungwa. Kana kwamba Amiri alitingishwa na ukurasa huo wa kutamausha au hata kushughulika kuufungua! Hivi ndivyo jinsi wanavyozua.

Ama kisingizio wanacho kitumia katika ukiukaji wao na uzushi wao ni “kuuhisabu uongozi”. Kana kwamba hili haliko wala halijaonekana wala kusikika! Mpangilio wa “kuuhisabu uongozi” umefafanuliwa kwa kina katika faili ya idara; miongoni mwa hao waliochangia kutunga faili hiyo ndio wanaoikiuka. Lakini kuna mwili mwengine mbali na nukta ya kuhisabu, nao ni Diwani ya Madhalim (Bodi ya kushughulikia malalamishi), inasimamiwa na watu mukhlisina na wacha Mungu, wasioogopa lawama ya yeyote isipokuwa Allah (swt), ingawa hatumtakasi yeyote kwa Allah. Kuhisabu na malalamishi ni mambo yaliyo thabiti, hakuna yeyote atakaye yakataa isipokuwa muovu, na hakuna yeyote atakaye ukataa uaminifu wao isipokuwa mashetani wa kibinadamu na wa kijini… hili wamekosa kuwa makini nalo wala kusitisha wayafanyayo. Mtu huyu kisha akatoa vitisho: kuwa sasa anayaelekeza maneno kwa Amiri kupitia mtandaoni (vitisho hafifu), lakini baadaye atazungumza maneno yenye cheche kali. Hii ndio jinsi ya vitisho vyao. Amekosa kutambua kuwa watu waliokuwa na nguvu, idadi kubwa na umoja kumshinda yeye hawakuweza kuiathiri Hizb wala mwanachama yeyote huru na mwema ndani yake … sembuse wao…

Kaka na Dada Zangu Wapendwa,

Kama nilivyo tangulia kutaja, si ajabu kuwepo kwa watu kama hawa. Wakati wowote kunapo kuwa na ulinganizi wa haki, huwepo watu kama hawa. Huzungumza urongo, uzushi na kudai kuwa wanasimama msimamo wa sawa, lakini ni madai yasiokuwa na msingi. Wanapo waona walinganizi wa haki wamesimama imara na kushikamana nayo, nyoyo zao hujaa chuki. Na wanapoona walinganizi hawa wakiungwa mkono na kukubaliwa na Ummah, nyoyo zao hujaa njama na vitimvi. Lakini wanapoona ukatili wa madhalimu dhidi ya walinganizi wa haki, hufurahi na kuzidisha uzushi juu yao, wakidhani kuwa watawaathiri na kuwaweka mbali na haki wanayo shikamana nayo.

﴿إِنْ تَمْسَسْكُمْ حَسَنَةٌ تَسُؤْهُمْ وَإِنْ تُصِبْكُمْ سَيِّئَةٌ يَفْرَحُوا بِهَا وَإِنْ تَصْبِرُوا وَتَتَّقُوا لَا يَضُرُّكُمْ كَيْدُهُمْ شَيْئًا إِنَّ اللَّهَ بِمَا يَعْمَلُونَ مُحِيطٌ

… “Yanapokufikeni mazuri huwachukiza na yanapo kusibuni mabaya hufurahi kwayo; lakini mukisubiri na kumcha Allah, njama zao hazitawadhuruni chochote. Hakika Allah ni mtambuzi wa wayafanyayo” [Al-i-Imran: 120].

Kaka na Dada Zangu Wapendwa,

Kurasa hizi ovu hazitakoma maadamu wema na uovu ungalipo duniani kama nilivyo tangulia kutaja juu. Watu waovu wanataka kutushughulisha na sumu yao na uzushi wao. Ikiwa tutashughulishwa nao, watakuwa wamefaulu, na ikiwa tutazikataa kurasa zao, mithili ya kutupa mbegu iliyooza, kutowatilia maanani, tutakuwa tumepangua vitendo vyao na watakufa na chuki zao. Hapa, sitaki kuwazuia kushiriki na kupata ufahamu juu ya kurasa hizi ovu, hivyo basi siwaamrishi wala siwakatazi. Lakini, ninacho waamrisha kwa mkazo ni kuwa musinitumie kurasa yoyote katika hizo. Nataka kujishughulisha katika kheri na njia iliyo nyoka, ili msafara huu unaobeba kurunzi ya nuru ambao wasafiri wake wataabiri chombo cha Khilafah Rashidah kwa idhini ya Allah katika muda uliopangwa na kukadiriwa na Allah. Na kwa kila jambo lina muda wake maalumu… Namuomba Allah (swt) hili liwe karibu.

﴿إِنَّ اللَّهَ بَالِغُ أَمْرِهِ قَدْ جَعَلَ اللَّهُ لِكُلِّ شَيْءٍ قَدْرًا

“Hakika, Allah atatimiza jambo lake. Hakika Allah amejaalia kwa kila kitu qadari” [At-Talaq: 3]

Kutamatisha, nyinyi, kaka na dada zangu, ni kizuizi chenye kuhami dhidi ya maandishi haya maovu na uzushi usio na msingi. Nimeambiwa kwamba nyinyi ni wanaume wa wanaume, ambao huzidi kupata nguvu kutokana na wapinzani wenu, na hamuathiriwi na fitna na migogoro, bali haya huzidisha ari na kujitolea kwenu … Nyinyi ni wanaume wa wanaume ambao mithili yao ni kama wale ambao Allah (swt) amewasifu:

﴿الَّذِينَ قَالَ لَهُمُ النَّاسُ إِنَّ النَّاسَ قَدْ جَمَعُوا لَكُمْ فَاخْشَوْهُمْ فَزَادَهُمْ إِيمَانًا وَقَالُوا حَسْبُنَا اللَّهُ وَنِعْمَ الْوَكِيلُ* فَانْقَلَبُوا بِنِعْمَةٍ مِنَ اللَّهِ وَفَضْلٍ لَمْ يَمْسَسْهُمْ سُوءٌ وَاتَّبَعُوا رِضْوَانَ اللَّهِ وَاللَّهُ ذُو فَضْلٍ عَظِيمٍ

Wale ambao wanafiki waliwaambia, ‘Hakika watu wamekusanyika dhidi yenu, hivyo basi waogopeni.’ Badala yake hili likawazidishia Imani na wakasema, ‘Allah anatutosheleza, na ndiye wakili bora* Hivyo basi wakarudi na neema kutoka kwa Allah na fadhila, huku wakiwa hawakuguswa na uovu wowote. Na wakatafuta radhi za Allah, na Allah ni mwingi wa fadhila” [Al-i-Imran: 173-174]

Kumalizia, ningependa kusisitiza yale niliyosema juu: Musinitumie chochote kutoka katika kurasa hizo ovu na wala musihofu kutokana na wazushi hao, wala kutokana na kuendelea kwao na hilo, kwa sababu Allah, Mwingi wa Nguvu (Al-Qawi) na Mwingi wa Uwezo (Al-Aziz), huwahami waja wake waaminifu kwake

﴿إِنَّ اللَّهَ يُدَافِعُ عَنِ الَّذِينَ آمَنُوا إِنَّ اللَّهَ لَا يُحِبُّ كُلَّ خَوَّانٍ كَفُورٍ

“Hakika Allah huwahami wale walio amini. Hakika Allah hampendi kila mwenye kukhini mwenye kufuru [Al-Hajj: 38].

Namuomba Allah (swt) atufinike hapa duniani na kivuli cha Khilafah, ili tupate kuwa mashahidi na wanajeshi wake, na ili tubakie ndani ya kivuli chake (swt) kesho Akhera, siku ambayo hakutakuwa na kivuli isipokuwa chake Yeye, katika kiti cha enzi karibu na Bwana, Mwenye Uwezo Kamili, na kufaulu katika maisha yote mawili; hakika huko ndiko kufaulu kukubwa.

Wa Assalamu Alaikum wa Rahmatullah wa Barakatuh

 

Ndugu Yenu,

Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah

 

Usiku wa kuamkia Ijumaa, 18 Rabi Al-Akhir 1439 H                 

5/1/2018 M