Jumla

Safari ya Ndege ya Kihistoria kwa Kenya ni ya Kuliunganisha Shamba la Kikoloni kwa Bwana Mkoloni

Kusambaza ni Kuunusuru Uislamu

Kenya mnamo Jumapili 28 Oktoba 2018 saa 11:20am iliingia katika mchakato wa kutimiza ndoto yake ya safari za ndege za moja kwa moja kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) Nairobi hadi Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa John Fitzgerald Kennedy (JFK) Mjini New York. Safari ya saa 15 ilikamilika Jumatatu saa 2:15pm kwa ndege kutua uwanja wa JFK ikiwa ndani yake imebeba maafisa wa kuu wa serikali wakiongozwa na Waziri wa Masuala ya Kigeni Monica Juma na mwenziwe Waziri wa Uchukuzi Macharia pamoja na Balozi wa Amerika nchini Kenya Bob Godec wakiwa ni miongoni mwa abiria.

Kenya imekuwa taifa la tano kutoka Jangwa la Sahara Afrika kutua Uwanja wa Kimataifa wa JFK baada ya Afrika Kusini, Nigeria, Ghana na Ethiopia. Ndoto hii imeweza kutimia baada ya Kenya kuidhinishwa na Marekani kama ilivyodhihirishwa na kauli ya Mamlaka ya Uwanja wa Ndege Kenya (KAA) “Kutokana na tangazo kati ya Mhehishimiwa Rais Uhuru Kenyatta na Rais Donald Trump, Uwanja wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) umefaulu kupata Hadhi ya Kuwa Nukta ya Mwisho ya Kuondokea.” (Soko Directory, 29/08/2018) Hii ni baada ya Rais Uhuru Kenyatta kuwa na mkutano na Trump mnamo Jumatatu 27 Agosti 2018 katika White House ambao ulikuwa wa kibiashara, uwekezaji na usalama kama ilivyodhihirishwa na Trump aliyesema kuwa “Tunafanya biashara nyingi. Tunafanya ulinzi na usalama mwingi.” (Standard Digital, 29/08/2018)

Uhalisia nyuma ya ndege hizi za moja kwa moja kuelekea Marekani ni kama ifuatavyo:

Kwanza: Marekani imeanzisha Vita vya Kiuchumi vya Karne ya 21 dhidi ya China na Umoja wa Ulaya (EU), Marekani inatumia vivutio vyote katika uwezo wake kuhakikisha inazivuta karibu nchi ambazo inazitizama kama zenye umuhimu na ambazo zinaweza kutumika katika mchakato wake mpya wa kiuchumi ulimwenguni hususan Afrika ambako China hivi sasa inapiga hatua kiuchumi na wanachama wa EU ambayo walikuwa ni wakoloni wa moja kwa moja wa bara hilo! Hivyo basi, Amerika inakwenda mbio ndani ya Afrika kuhakikisha inalidhibiti shamba la kikoloni na kuwekeza zaidi juhudi zake katika kukazanisha vitanzi katika shingo za China na EU!

Pili:  Ili kufikia malengo yake maovu ndani ya Afrika, Utawala wa Marekani chini ya Trump umeamua kuigawanya Afrika katika mitazamo miwili Pembe ya Afrika ikiongozwa na Misri na Jangwa la Sahara likiongozwa na Nigeria na Afrika Mashariki ikiongozwa na Kenya ndani ya Jangwa la Sahara. Hivyo basi, Marekani ikamualika Rais wa Misri Abdel Fatah el-Sisi mnamo Aprili 2017, Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari Aprili 2018 na Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta Agosti 2018. Mataifa haya matatu yanacheza dori muhimu katika maeneo yao husika kwa njia ya usalama unaongozwa na mipango ya Kiamerika ikiwa ni pamoja na miradi ya kupambana na ugaidi na kiuchumi Nigeria ndiyo yenye uchumi mkubwa na watu wengi barani Afrika, ikifuatiwa na Misri ikiwa ni ya tatu kwa uchumi mkubwa na watu wengi barani Afrika na kisha Kenya ndiyo ya kwanza yenye uchumi mkubwa na ya pili yenye watu wengi ndani ya Afrika Mashariki. Hiyo inamaanisha kuwa nchi hizi tatu na marais wake wana usemi katika masuala ya Afrika licha ya kuwa ni mataifa vibaraka wanaogemea Marekani na Uingereza na ambao sera zao za kigeni zimekitwa juu ya maslahi duni yanayotegemea ruwaza ya mabwana zao!

Tatu: Kwa upande wa Kenya, ni taifa kibaraka mtiifu ndani ya Afrika Mashariki ambaye jeshi lake hivi sasa limo ndani ya vita vya kiwakala vinavyodhaminiwa na wamagharibi vikiongozwa na Marekani nyuma ya pazia katika kupambana na eti Ugaidi (Al Shabaab). Zaidi ya hayo ni kuwa mnamo 9 Machi 2018 kulitokea mapatano kati ya kibaraka mtiifu wa Marekani Raila Odinga na Uhuru Kenyatta kibaraka kipenzi wa Uingereza ambao ilipelekea kusitishwa kwa uadui na mihemko ya kisiasa eti  kuwafurahisha wawekezaji wa kigeni. Kenya ni taifa lililo na wasomi wachanga wengi na ndiyo mfano wa kuigwa wa ukuwaji wa demokrasia ndani ya Afrika Mashariki. Safari hizi za ndege ni zawadi kwa utawala wa Jubilee kutoka kwa utawala wa Trump kwa kazi nzuri ya kukubaliana kati ya vibaraka wakuu wa mabwana wa kimagharibi. Hivyo basi, utawala wa Uhuru ulihalalishwa kitaifa, kieneo na kimataifa na Marekani kama dola yenye nguvu duniani na Raila naye kuzawadiwa cheo cha ubalozi wa AU kusimamia maendeleo ya miundo mbinu! Hii ni zawadi ya pili kwa Uhuru kutoka Marekani ya kwanza ikiwa ni kuchaguliwa kwa Uhuru Kenyatta kuwa balozi wa Umoja wa Mataifa (UN) kama Mtetezi wa Kiulimwengu wa Ajenda ya Vijana mnamo Jumatatu 24 Septemba 2018! Ikimaanisha kuwa Amerika itapatiliza matukio haya mapya ili kuhakikisha kuwa inajiboresha kiuchumi duniani na hususan Afrika.

Kwa kutamatisha, safari hizi za ndege kama za reli wakati wa enzi ya Ukoloni wa Uingereza ambapo barabara za reli hazikuwekwa katika maeneo ambayo kiasili yalikuwa yanatarajiwa kuwa na uchumi mkubwa kutokana na watu wengi; bali yalitegemea urahisi na ufupi wa njia. Kwa mfano, lengo la barabara ya reli ya Kenya-Uganda iliyojengwa 1901, ili ya kuunganisha Uganda na pwani kwa gharama ya chini vilivyo. Kenya ilikuwa ni eneo la usafirishaji tu; kiasi kwamba barabara ya reli hiyo ilipitia katika maeneo yasiyokuwa na watu wengi ikielekea Ziwa Victoria, ikiifungua Afrika Mashariki. Ilhali Ghana, lengo lilikuwa ni kuunganisha migodi inayomilikiwa na watu wa Ulaya na kufikia hatua za kijeshi kuteka maeneo ya Afrika Magharibi (International Growth Centre, 15/10/2014). Hivi majuzi Barabara Kuu ya Thika na Reli ya Standard Gauge ambazo zimemeza mabilioni ya fedha ikiwa hazina lolote lakuonyesha katika kuinua maisha ya watu kwa njia ya moja kwa moja katika kukidhi mahitaji yao msingi. Lakini badala yake imepelekea raia wengi kutupwa ndani ya umasikini zaidi kutokana na mipango ya utozwaji ushuru isiyoingia akilini ikilenga kulipia madeni ambayo yamelimbikizana kutokana na mikopo ya kudhamini ujenzi wa miradi hiyo ambayo haikuwa muhimu!

Kwa hiyo mbwembwe zinazoshuhudiwa kutokana na sherehe za uzinduzi wa ndege za moja kwa moja ni mbinu tu ya serikali ya Kenya kujipatia pumzi na kujionyesha kuwa ni dola inayoegemea ukuwaji wa uchumi.  Lakini ukweli ni kwamba ni dola inayokuza umasikini na kuwasukuma watu katika maisha ya dhiki ambayo hayajawahi kushuhudiwa katika historia ya Kenya! Kwa upande mwingine, uhuru wa jamii ya Kenya utapigiwa debe zaidi kutokana na ongezeko la idadi ya watalii kutoka Marekani wakija na thaqafa yao mbovu. Ama kuhusu biashara tayari hakuna usawa kati ya mataifa hayo mawili tukizingatia kuwa Kenya ni soko la kutumia bidhaa na Marekani ni mzizi wa kiwanda kinachozalisha bidhaa na kuzijaza nchini Kenya kupitia msingi wa kirongo wa AGOA!

Mapinduzi ya kweli ya Kenya na Afrika jumla yamo katika kuukumbatia mradi wa dhahabu wa Khilafah. Khilafah iliyosimamishwa kwa njia ya Utume itahakikisha kuwa Afrika ina washirika na marafiki wa kweli. Ushirika na urafiki uliokitwa juu ya uchajiMungu kwa muongozo wa mfumo safi wa Uislamu chini ya Khalifa muadilifu anaye tawala kwa Qur’an na Sunnah. Khilafah itakuwa rafiki na mama wa kweli kwa Afrika kwa kuisadia Afrika katika kuikomboa kutoka kwa utumwa wa ukoloni hadi kwa Muumba wa mwanadamu. Khilafah itailinda Afrika si tu kwa kuwafurusha wakoloni bali pia kwa kuung’oa mfumo wao batili wa kisekula wa kirasilimali. Amani, usalama, maendeleo na ustawi wa kweli kwa Afrika utakuwa ni sehemu ya vipaombele vya Khilafah katika msingi wake wa ulinganiaji Uislamu ulimwenguni. Ili kufikia hapo Kenya na Afrika jumla inatakiwa kukata mahusiano na mataifa ya kisekula ya kikoloni yakiongozwa na Marekani ambaye ndiye mwagaji damu wa kiulimwengu kuanzia Yemen, Somalia, Iraq, Syria, Libya, Palestina hadi Afghanistan n.k.

Ali Nassoro Ali

Mwanachama wa Afisi ya Habari ya Hizb ut Tahrir Kenya