Jumla

Tushirikiane Tuokoe Vijana Kutokana na Uovu wa Itikadi ya Kisekula na Mfumo wa Kirasilimali

Kusambaza ni Kuunusuru Uislamu

Hakika, ujana ni umri uliojaa nishati na ubunifu kiasi kwamba kila jamii iliyokuwa na vijana inatakiwa kujivunia nao kwani ndio kipaumbele katika kufaulisha kila nyanja ya maisha. Lakini, lakusikitisha vijana leo wanapata tabu na wanapatisha watu wengine tabu ikiwemo wazazi wao, ndugu zao, jirani zao na jamii kwa ujumla.

Kila pembe ya dunia ikiwemo Kenya tunasikia sauti za kudai mageuzi ili kuboresha hali za vijana. Mikakati, sera na sheria zikipitishwa ili kuwanusuru vijana kutokana na matatizo wanayopitia ikiwemo ukosefu wa ajira, matumizi ya mihadarati na pombe, mimba za “mapema”, idadi kubwa ya maambukizi ya ukimwi, ukosefu wa maadili na heshima kwa wazee n.k.

Michakato yote hii inayofanywa na serikali za kisekula duniani ipo tu katika jaribio la kupambana na athari ya tatizo wala kattu haifichui chanzo cha matatizo wanayopitia vijana. Kabla ya kuingia kwenye kutatua tatizo ingekuwa lazima kwanza kuangalia kiini chake. Tukiangalia kwa makini tutakuta kuwa chanzo ni kuwepo kwa itikadi ya kisekula (kutenganisha dini na maisha) na mfumo wa kirasilimali ambazo chimbuko lake ni akili ya mwanadamu. Kutenganisha Dini au muongozo wake katika maisha ya wanadamu ni kuwafanya wanadamu wasimuogope Mwenyezi Mungu na sheria zake bali wawe na kila aina ya uhuru wa kufanya wanayoyataka. Kwa maana hiyo, watu wakiwemo vijana ni masekula wanaoendesha mambo yao kwa mujibu wa matamanio (uhuru) yao. Fauka ya hayo, mfumo unaowatawala wa kirasilimali upo kulinda matamanio yao na unapima vitendo vyao kwa mujibu wa maslahi na manufaa pekee! Kwa mfano kamare, mihadarati, pombe n.k licha ya kuwa na madhara katika jamii lakini kwa warasilimali ni biashara yenye faida kubwa kiuchumi. Kwa maana haya hata zile kampeni za kupambana na madawa ya kulevya n.k hayo ni danganya toto tu. Hivyo matatizo wanayopitia vijana kattu hayatarajiwi kumalizika na badala yake kila kukicha yanazidi kutokana na wao kujifunga na itikadi ya kisekula na mfumo wa kirasilimali.

Kinyume chake ni kuwa suluhisho la matatizo ya wanadamu ambao miongoni mwao ni vijana lipo ndani ya Uislamu. Kwani ni Dini ambayo chimbuko lake ni kutoka kwa Mwenyezi Mungu (swt). Muumba wa mbingu na ardhi na vilivyomo ndani yake ikiwemo watu ambao miongoni mwao ni vijana. Hakika, Muumba ndiye anayestahili kupangilia viumbe namna gani viishi na sio kinyume chake. Kwa maana hiyo Uislamu ukamfunga mwanadamu na kumfanya kuwa mtumwa wa Muumba na jukumu lake ni kwenda mbio kutafuta radhi Zake kwa kujifunga na kipimo cha halali na haramu pasina kujali lawama ya anayelaumu. Uislamu umemsifu kijana kiasi kwamba akapewa nafasi miongoni mwa watu aina saba watakaopata kivuli Siku ya Kiyama. Amesimulia Abu Huraira (ra) kwamba Mtume (saw) alisema:

(سَبْعَةٌ يُظِلُّهُمُ اللَّهُ فِي ظِلِّهِ يَوْمَ لاَ ظِلَّ إِلاَّ ظِلُّهُ الإِمَامُ الْعَادِلُ، وَشَابٌّ نَشَأَ فِي عِبَادَةِ رَبِّهِ)

“Mwenyezi Mungu atawapa kivuli watu aina saba katika Siku ambayo hakutakuwa na kivuli isipokuwa Chake. Mtawala muadilifu, Kijana ambaye amelelewa kumuabudu Mola wake…” [Bukhari na Muslim]

Kupitia maelezo hayo ni wazi kwamba Uislamu umeweka suluhisho msingi nalo ni kwa watu jumla kujifunga na maamrisho na makatazo ya Mwenyezi Mungu (swt). Kwa sababu hakuna mamlaka ya kusimamia utekelezwaji wa Uislamu kiukamilifu ndio tunashuhudia matatizo ya kila aina na watu wakitenda kila aina ya uovu kiasi kwamba ufisadi umeenea bara na baharini. Serikali zote zilizopo duniani zipo kwa ajili ya kudhamini uhuru wa watu!

Hivyo basi ni jukumu letu tushirikiane katika kukemea ulinganizi unaolenga kufanya watu wawe na utambulisho (fikra, fahamu na tabia) wa kisekula. Na wakati huo huo tupaze sauti zetu dhidi sheria zinazopitishwa ili kupigia debe Uislamu Poa bali pia kupambana na Uislamu na Waislamu kwa kisingizio cha kupambana ugaidi, itikadi kali na misimamo mikali. Muhimu zaidi tushirikiane kufanya kazi ya kurudisha tena maisha ya Kiislamu kupitia kusimamisha serikali ya Kiislamu ya Khilafah kwa njia ya Utume. Hakika ni kupitia Khilafah kutekeleza kiukamilifu Shari’ah (Qur’an na Sunnah) ndio kutapelekea vijana na watu jumla duniani kupata utulivu, maendeleo, heshima, hadhi, cheo na ufanisi wa kweli katika maisha ya dunia na akhera. Khilafah itakuwa ndio mlinzi na ngao ya kweli kwa wanadamu wote. Shiriki Kampeni ya #OkoaVijana: www.facebook.com/HTKisauni

Ali Nassoro Ali

Mwanachama wa Afisi ya Habari ya Hizb ut Tahrir Kenya

Makala Na.54: Ijumaa, 16 Dhul-Qa’da 1440 | 2019/07/19