Ameer Suali na Jawabu

Uhakika wa Maandamano Nchini Sudan

Kusambaza ni Kuunusuru Uislamu

بسم الله الرحمن الرحيم

 Jibu la Swali
(Imetafsiriwa)

Swali

Maandamano yaliyozuka kwa zaidi ya miezi miwili yangali yanaendelea mpaka leo. Je, yamechochewa na hali mbaya za kiuchumu? Au sababu ya maandamano hayo nchini Sudan ni taharuki katika mahusiano kati ya Khartoum na Washington baada ya ziara ya Naibu Waziri wa Kigeni wa Amerika, John Sullivan, jijini Khartoum mnamo Novemba 2017? Fununu ni kuwa miongoni mwa kadhia zilizoibuliwa katika mazungumzo yake na upande wa Sudan ni kadhia ya kutomteua Al-Bashir katika uchaguzi wa 2020, na kwamba Al-Bashir alikuwa na wasiwasi sana na kusafiri hadi Urusi ili kuichokoza Amerika, na huko alikubali kujenga kambi za kijeshi za Urusi. Je, hii ya maanisha kuwa Amerika imeamua kumbadilisha Al-Bashir na kuinyonga hali ya kiuchumi ya Sudan, na kuzuia vibaraka wake, hususan Saudi Arabia, kutokana na kuisaidia Sudan? Pia utafanua vipi usaidizi wa Al-Sadiq Al-Mahdi kwa maandamano hayo; je, ya maanisha kuwa Muingereza ana mkono ndani yake? Niwie radhi kwa swali hili refu. Jazak Allah Khair.

Jibu

Ili kupata jibu la wazi, mambo yafuatayo ni lazima yaregelewe upya:

1- Ndio, mnamo 16/11/2017, Naibu Waziri wa Kigeni wa Amerika, John Sullivan, alizuru Sudan na kukutana pamoja na Mawaziri wa Kigeni na Fedha, Mwenyekiti wa Wakuu wa Majeshi, wawakilishi wa Wizara ya Ndani na Usalama wa Kitaifa na Huduma za Kijasusi, ikiongezewa na Muhusika wa Mambo ya Ubalozi wa Sudan nchini Amerika. Pia alikutana na idadi kadhaa ya viongozi wa kidini katika kikao cha faragha, na kisha kutoa hotuba katika Ukumbi wa Shahid wa Chuo Kikuu cha Qur’an Al-Kareem, akizungumzia kuhusu sera ya Amerika juu ya Sudan. [Afisa huyo wa Amerika alitaka katika mkutano wake huu, kwa mujibu wa fununu zilizoripotiwa katika mtandao wa Sudan wa Times, kuwa serikali iregelee, irekebishe au kufuta idadi kadhaa ya sheria, kubwa yazo ikiwa ni ile inayozungumzia kuhusu kumuua mtu anayeritadi (kutoka katika dini yake (Uislamu) na kutoa wito wa “kuondolewa kwa kifungu cha mavazi katika sheria ya utangamano wa umma, ambayo inawaadhibu wanawake kwa kuwachapa mijeledi endapo watavaa nguo za utovu wa adabu, kwa mujibu wa mtazamo wa maafisa wa polisi watekelezaji wa sheria. Na akatoa wito wa kuhifadhi uhuru wa kidini kwa wote wakati wa kutunga katiba mpya ya Sudan” (Sudan Tribune, 18/11/2017)].

2- Ni kweli pia kuwa baadhi ya fununu zimesema kuwa: Sullivan alimuomba Al-Bashir kutogombea katika uchaguzi wa 2020, na kwamba Bashir hakukubali hilo, na hapo kukawa na taharuki katika mahusiano, lakini hili lina shaka kwa sababu Al-Bashir hawezi kupinga maagizo ya bwana wake, Amerika, na yeye hagombei afisi isipokuwa Amerika itake hilo. Endapo tutadhania kuwa amekataa maagizo ya Amerika na kusisitiza juu ya kuteuliwa upya katika uchaguzi wa 2020 na kusalia mamlakani, Amerika itafanya mapinduzi dhidi yake na kumng’oa kama ilivyomleta kwa mapinduzi ya 30/6/1989. Zingatia kuwa ilipotajwa katika mitandao ya kijamii kuwa afisa huyo wa Amerika alimuomba Al-Bashir kutogombea katika uchaguzi wa 2020, [Waziri wa Kigeni wa Sudan, Ibrahim Ghandoor, alikana hilo na kusema: “Amerika haikulazimisha masharti yoyote ya kutomteua Raisi wa Sudan Omar Al-Bashir kwa uchaguzi utakaofanywa mnamo 2020 kwa badali ya kuliondoa jina la Sudan kutoka katika orodha ya dola zinazofadhili ugaidi,” na akasema: “Kila kitu tulichojadili na John Sullivan, Naibu Waziri wa Kigeni wa Amerika, katika ziara yake ya hivi karibuni Khartoum kina husiana na haki za kibinadamu na uhuru wa kidini” (Al-Quds Al-Arabi, 14/11/2017)]

Ziara hiyo ni ishara ya utulivu, sio taharuki. Sullivan alikutana pamoja na sekta kadha wa kadha za dola hiyo wakati wa ziara hii na alikaribishwa kwa moyo mkunjufu. Ziara hii ilijiri baada ya kuondolewa kwa marufuku ya usafiri ya utawala wa Amerika juu ya raia wa Sudan mnamo 26/9/2017 na pia baada ya kuondolewa baadhi ya vikwazo vya kiuchumi, vilivyo dumu kwa miaka 20 juu ya Sudan mnamo 6/10/2017. Hivyo basi ziara hii haikuwa ni kujadili uteuzi huo, lakini lengo lake kuu lilikuwa ni kuliondoa jina la Sudan kutoka katika orodha ya “dola zinazofadhili ugaidi”, kwa hiyo Amerika imeweka baadhi ya masharti ili kuliondoa jina la Sudan kutoka katika orodha ya “dola zinazofadhili ugaidi” kama ilivyo tajwa juu katika tovuti ya Sudan Tribune.

Hii ni kwa upande mmoja, na kwa upande mwengine, Al-Bashir alisisitiza upya, siku kumi kabla ya ziara ya Sullivan nchini Sudan, ahadi zake zilizotangulia za kutogombea uraisi. [“Raisi wa Sudan Omar Al-Bashir mnamo Jumatatu alisisitiza upya ahadi yake ya awali ya kuachana na utawala wa nchi kufikia mwisho wa muhula wake wa pili wa uraisi mnamo 2020 … Ahadi ya Al-Bashir ilikuja katika hotuba kwa jumuiko kubwa la vijana katika sherehe ya saba ya Kongamano Kuu la Muungano wa Kitaifa wa Sudan kwa Vijana jijini Khartoum.” (Al-Khaleej Online, 6/11/2017)]. Ingawa sio vigumu kugeuza ahadi katika nchi kama hizi, taarifa na mawasiliano ya Amerika nchini Sudan zinaondoa uwezekano kuwa lengo la ziara hiyo ni kumzuia Al-Bashir kutogombea afisi, kwani mawasiliano kati ya Amerika na Sudan yaliendelea baada ya ziara hiyo na baada ya kuanza maandamano ili kuliondoa jina lake kutoka katika orodha ya dola zinazofadhili “ugaidi” tangu 1993. Kwa sababu hili liliendelea baada ya Trump kuviondoa vikwazo vya kiuchumi na kibiashara ilivyo vilazimisha juu ya Sudan tangu 1997, na Amerika imeweka sharti hilo ili kukamilisha awamu ya pili ya kuliondoa jina la Sudan ili kupanua ushirikiano wake katika “kupambana na ugaidi” na kupigia debe haki za kibinadamu na uhuru wa kidini na kisiasa … nk.

3- Ziara ya Sullivan mnamo 16/11/2017 ilikuwa sio kishajiisho cha maandamano ambayo yalianza mnamo 19/12/2018 kwa sababu msimamo wa Amerika baada ya ziara hiyo na wakati wa maandamo hayo ulikuwa upande wa serikali na sio upande wa maandamano kama mawasiliano na taarifa zinavyo ashiria hilo. Mnamo Jumapili 17/2/2019 Msaidizi Maalumu wa raisi wa Amerika na mshauri mkuu wa masuala ya Afrika katika Baraza la Usalama wa Kitaifa, Cyril Sartre, aliwasili jijini Khartoum akiandamana na Mkurugenzi wa Kitengo cha Afrika katika Baraza hilo la Usalama wa Kitaifa Darren Seraile, na kukamilisha mazungumzo yake nchini Sudan Jumatano 20/2/2019. Katika mojawapo ya taarifa zake msaidizi huyo maalumu wa Amerika baada ya mkutano katika Kasri la Kijamhuri [“nilifanya mkutano wenye natija na faida” pamoja na naibu wa raisi na kuashiria kuwa ziara hiyo ni kuendeleza mazungumzo baina ya pande hizo mbili, “Hii itapelekea kuondolewa kwa jina la Sudan kutoka katika orodha ya dola zinazofadhili ugaidi hivi karibuni,” Cyril alisisitiza kuwa: “kwa subira zaidi serikali itaweza kupata suluhisho la kisiasa na kwamba hakuna masuluhisho yatakayo lazimishwa kutoka nje juu ya Sudan, akitaja kuwa kupitia hatua shirika nchi mbili hizo zitapata ushirikiano imara” … (Habari za Ash-Shuruq 18/2/2019)]. Yote haya yaonyesha kuwa ziara hiyo haikuwa kishajiisho cha maandamano hayo, lakini inaashiria usadizi wa Amerika kwa utawala wa Al-Bashir, na wala si kulazimisha suluhisho lolote kutoka ng’ambo, na kuwekwa kwa masharti ya Amerika ili kuliondoa jina la Sudan kutoka katika orodha ya Amerika ya dola zinazofadhili ugaidi.

4- Ama kuhusu misimamo ya vibaraka wa Amerika, pia iliunga mkono utawala huo na wala sio maandamano hayo, yaani si kama ilivyotajwa katika swali hili.

Hii ni kama ifuatavyo:

A- Ama kuhusu Saudi Arabia, tangu mwanzoni mwa operesheni ya kijeshi nchini Yemen, muungano huo unaendelea kuingiza uwekezaji mpya katika sekta ya ukulima ya Sudan:

[“Saudi Arabia ndio mwekezaji mkubwa nchini Sudan mnamo 2016, ikiwa na uwekezaji unaokadiriwa kuwa $ 15 bilioni, na uwekezaji huu umemakinika katika chakula, ngano na mahindi; na unasaidia uchumi wa Khartoum.” (Al-Khaleej Online 17/7/2017)]. Balozi wa Saudia alithibitisha: [“Kuwa thamani ya uwekezaji halisi wa Saudia nchini Sudan umezidi dolari bilioni 12.” (mtandao wa Al-Bawaba 03/12/2018)] … na [“mnamo Jumatatu 7/5/2018 Sudan ilitangaza kuwa imefikia makubaliano pamoja na Saudi Arabia kwa muda wa miaka mitano.” (Sudan Tribune 7 /5/2018)].

A- Ujumbe mmoja wa mawaziri wa Saudia ulizuru Khartoum mnamo 24/1/2019 na kufanya mazungumzo na Raisi wa Sudan Al-Bashir ambapo walijadili hali nchini Sudan. Waziri wa Biashara wa Saudia, Majid Al-Qasabi, alisema katika taarifa kwa vyombo vya habari: [“Ziara hii ya ujumbe nchini Sudan ilikuja chini ya uongozi wa Mtumishi wa Misikiti Miwili Mitukufu Mfalme Salman bin Abdul Aziz ili kuimarisha mahusiano ya kiuchumi pamoja na Sudan na kuongeza ubadilishanaji wa biashara,” akiongeza: “Mfalme Salman amesisitiza kuwa usalama wa Sudan ni usalama wa Ufalme huo, na ustawi wake ni ustawi wa Ufalme huo, na kwamba Sudan inastahiki uhusiano nao zaidi kuliko nchi nyengine yoyote.” (Egyptian Al-Watan 26/1/2019)]. Yote haya yanathibitisha kuwa Saudi Arabia haikutelekeza usaidizi wake kwa Sudan.

B- Ama kuhusu nguzo nyengine, Misri, Bashir alizuru Misri mnamo 27/1/2019. Sisi alimkaribisha katika mapokezi katika uwanja wa ndege na kuonyesha ukarimu wake, na hili laashiria kuwa Amerika haikuamua kumuondoa Al-Bashir; vyenginevyo, Sisi hangefanya alivyo fanya kwani yeye ni mtiifu kwa Amerika na mfuasi wake. Ziara hiyo ilisifiwa na balozi wa Sudan nchini Misri kama: [“ziara hii ndio ziara muhimu zaidi katika upande wa wakati na yaliyomo ndani yake …” (Egyptian Al-Sabah 27/1/2019)]. Zingatia kuwa Al-Bashir alizuru Misri na kukutana na Sisi mnamo 6/11/2018 baada ya ziara ya Sisi nchini Sudan mnamo 25/10/2018 akiandamana na mawaziri 12 na kutia saini makubaliano 12. Baada ya kuzuka kwa maandamano moja kwa moja, Waziri wa Kigeni wa Misri, Samih Shukri, na kinara wa ujasusi alizuru Sudan na kukutana pamoja na Omar Al-Bashir na mawaziri wenzao. [Shukri alisema baada ya mkutano huo: “Misri ina imani kuwa Sudan itajikwamua kutoka katika dhurufu za sasa, na kwamba Misri daima iko tayari kutoa usaidizi na msaada kwa Sudan, na usalama na ustawi wa Sudan ni sehemu ya usalama na ustawi wa Misri.” (Egyptian Al-Bawaba 27/12/2018)]. Hii yaonyesha kuwa Misri ingali inaisaidia Sudan.

C- Kindani, nguvu muhimu zaidi za Amerika ni jeshi. Msimamo wa jeshi la Sudan juu ya maandamano hayo ulikuwa ni kusimama upande wa Al-Bashir na kulinda serikali yake. Jeshi hilo lilitangaza katika taarifa moja: [“Kuwa watakusanyika pambizoni mwa uongozi wake na wasiwasi wake kwa manufaa ya watu na usalama wa damu, heshima na mali za raia.” (Arabic Post 23/12/2018)]. [“Jeshi halitaikabidhi nchi kwa wamiliki wa mitazamo duni katika viongozi wa waasi walioshindwa na vibaraka wa mashirika yakutiliwa shaka nga’mbo,” alisema kiongozi wa majeshi ya Sudan, Kamal Abdul-Maarouf, katika hotuba yake kwa maafisa wa ngazi za brigedia wakuu na makanali.” (Misr Al-Arabiya 30/1/2019)]. Hii yaashiria kuwa jeshi hilo lingali linamuunga mkono Al-Bashir, na hivyo hivyo msimamo wa jeshi na sekta nyenginezo za usalama. [“Jenerali Mohammad Hamdan Daglo Himaidti, kamanda wa kikosi cha majeshi ya kutoa msaada wa haraka nchini Sudan, alitishia kuwa majeshi yake yako tayari kupambana na wale aliowasifu kama walafi.” (Al-Maseera Net 26/12/2018)]. Vile vile: [“Salah Qosh, kinara wa vyombo vya usalama na ujasusi nchini Sudan, alisema katika taarifa fupi kwa bunge kuwa kuna mipango mingi uwanjani “lakini kila mmoja anapaswa kujua kuwa mpango wowote unaokiuka utawala halali uliopo hauna nafasi,” (Al-Jazeera Net 21/2/2019)]. Amerika ililitumia jeshi hilo kutekeleza mapinduzi na imejimakini ndani yake tangu mapinduzi ya Nimeiri mnamo 1969.

5- Kuhusiana na upinzani: [“Katika siku ya nne ya maandamano hayo, Al-Sadiq Al-Mahdi, kiongozi wa Chama cha Umma, alitoa wito wa kuundwa kwa serikali mpya ya muungano kwa kushirikishwa vyama vyote,” alisema kuwa yeye “anaunga mkono maandamano hayo maarufu nchini humo … lakini akasisitiza kuwa chama chake hakitashiriki katika maandamano hayo” (Shirika la habari la BBC 22/12/2018)], lakini alipoona maandamano yanaendelea, alitangaza tabanni yake: [“Kinara wa Chama cha Kitaifa cha Umma, kinara wa chama cha Muungano wa Rufaa wa Sudan, Al Sadiq Al-Mahdi, alitangaza kuunga mkono kwake vuguvugu maarufu la kuing’oa serikali … Alitoa wito wa kusitishwa mauwaji ya waandamanaji kabla ya kumuomba Raisi Omar Al-Bashir kushuka uongozini.” (Sudan Tribune 25/1/2019)], hii ni baada ya zaidi ya mwezi mmoja wa maandamano, akijaribu kuyatumia baadaye. Al Sadiq Al Mahdi anajulikana kwa utiifu wake kwa Muingereza, na aliiongoza serikali ya Sudan kati ya 1986 na 1989, na aliondolewa kwa mapinduzi ya Al-Bashir baada ya hapo. Aliunda jumuiko la wataalamu wa Sudan na liliibuka kama shirika sambamba kwa mashirika rasmi ya wafanyikazi yanayounga mkono serikali. Jumuiko hili la wataalamu linaushawishi wa Ulaya kupitia Al-Mahdi. Ni jaribio la kuwa badali kwa mashirika rasmi ya wafanyikazi yanayodhibitiwa na serikali hiyo, na viongozi wake ng’ambo wamemakinika barani Ulaya. [“Kutokana na viongozi wake waliotajwa ng’ambo na wanaozungumza kwa niaba yake ni mwanahabari Mohammad Al-Asbat nchini Ufaransa na Dkt. Sarah Abdeljalil nchini Uingereza”. (Tovuti ya BBC 24/1/2019)]. Maandamano hayo pia yanahusisha miondoko ya kisekula na harakati nyenginezo hafifu ambazo hazina usemi katika mabadiliko. Ingawa ushawishi wa Uingereza umepenya mijumuiko hii, hususan katika chama cha Al-Sadiq Al-Mahdi, lakini ushawishi huu hauna uwezo wa mabadiliko halisi. Lakini, kuendelea kwa maandamano hayo kunayapa nguvu kutokana na ushawishi wa Uingereza katika kuyatumia maandamano hayo. Hii ndio sababu kulikuweko na ucheleweshaji wa tangazo la Chama cha Al-Mahdi la kuunga mkono kwake maandamano kwa takriban mwezi mmoja, kikidhani kuwa Al-Bashir atayazima katika siku zake za mwanzo mwanzo, lakini muda uliporefuka, alidandia wimbi lake! Kisha, baada ya zaidi ya miezi miwili, Al-Mahdi alikuwa imara zaidi, na kusisitiza juu ya kujiuzulu kwa Al-Bashir [na akadhihirisha kuwa na haja kwake kukutana na wawakilishi wa upinzani ili kukubaliana juu ya maelezo ya muda wa mpito kwa serikali mpya … (Sputnik 2/3/2019)]. Hivyo basi, kila inapochukua muda mrefu zaidi kwa serikali kuweza kukomesha maandamano hayo, nguvu za vibaraka wa Uingereza zinaongezeka; hivyo basi Amerika imelizingatia jambo hili, na katika kutarajia dharura yoyote, ilipanga pamoja na Al-Bashir kuvamia mijumuiko hii kupitia kuviondoa baadhi ya vyama vya kisiasa vinavyoshiriki ndani ya serikali, ambavyo ni miongoni mwake, na kisha kuunda upinzani kwa serikali: [Raisi wa Chama cha Umma, Mubarak al-Fadil, alitangaza kuvunjwa kwa uongozi wa chama chake na chama tawala cha Kongamano la Kitaifa  na kujiondoa kwake serikalini .. (Tovuti ya Al-Neelain, 28/12/2018)] vile vile kujiondoa kwa Ghazi Salah Al-Din: [Vuguvugu la mageuzi sasa limeamua kuwaondoa wawakilishi wake wote katika mabaraza ya bunge, hii ilikuwa ni wakati wa mkutano wa Ghazi Salah Al-Din kwa waandishi habari …” (Shirika la habari la Sawa 1/1/2019)]. Ghazi Salah Al-Din alichaguliwa kama kinara wa chama cha Vuguvugu la Kitaifa la Mabadiliko [“Vuguvugu la Kitaifa la Mabadiliko” lilimchagua Ghazi Salah Al-Din jana kama Raisi wa Baraza la Raisi la Vuguvugu hilo.” (Al-Khaleej 365 mnamo 14/2/2019)]. Kuongezea kuvamiwa huku na katika kutaraji kupamba moto kwa maandamano hayo na kutumiwa kwake na Ulaya, ilimpa Al-Bashir idhini ya kulazimisha hali ya dharura, ambayo aliilazimisha mnamo 22/2/2019. Hivi majuzi, mnamo 28/2/2019, chama cha Meghrani kilijiondoa kutoka katika serikali, ambacho kinajulikana kwa mahusiano yake na Amerika [Chama cha Muungano cha Kidemokrasia kinachoongozwa na Osman Al-Merghani kilitangaza mnamo Alhamisi kinasitisha ushirikiano wote katika utawala ilichotia saini pamoja na chama tawala cha Kongamano la Kitaifa na kujiondoa kwake kutoka katika serikali ya Sudan” (Habari za Al Ain 28/2/2019)].

Kisha ikaja hatua mpya ya kuutuliza upinzani kupitia Al-Bashir mwenyewe kutangaza kuwa yeye yuko katikati na wala hayuko pamoja na chama chochote dhidi ya chama chengine! [Raisi wa Sudan ametoa idhini kupitia mamlaka yake kama mwenyekiti wa Chama cha Kongamano la Kitaifa (NCP) kwa makamu wake katika hatua ya kuharakisha huku machaguo yake yakipungua mbele ya mgogoro mbaya katika miongo mitatu ya utawala wake … Chama hicho kilisema katika taarifa kuwa uamuzi unaojiri “katika kutimizi hotuba ya Raisi kwa taifa, kwamba anasimama katika masafa hayo hayo kutoka katika nguvu zote za kisiasa.” (Middle East Online 1/3/2019)]. Na hivi ndivyo namna Al-Bashir anavyojidanganya mwenyewe kabla ya kuwadanganya wengine; vipi anaweza kusimama kati na kati wakati yeye ndiye kiongozi wa dola, na chama chake ndicho chama tawala? Hata kama atamteua mwengine katika wadhifa wake wa kuongoza chama, hili halina athari yoyote?!

Kwa vyovyote vile, ni miongoni mwa mbinu za kutuliza maandamano! Na yote haya ni kujaribu kushawishi upinzani na kuyadhibiti maandamano, hususan kwa kuwa serikali hiyo sasa ina nguvu zilizo penya ndani ya upinzani, na endapo nguvu hizo haziwezi kuwadhibiti, basi itajaribu kuwaongoza au kushiriki kimsemo katika uongozi wake na hivyo utawala wa Amerika kuendelea.

6- Ama kuhusu ziara ya Al-Bashir jijini Moscow, iliyo chukua siku nne mnamo 22/11/2017, siku sita baada ya ziara ya Sullivan nchini Sudan, lengo la ziara hiyo lilikuwa sio kwa Al-Bashir kulalamika kuhusu Amerika kwa Urusi, bali lilikuwa agizo na kwa idhini ya Amerika. ushahidi wa hilo: [Gazeti moja la Sudan lilifichua mnamo Jumatano, mkataba kati ya Khartoum na Washington, ili kupata njia ya ndege ya Raisi Omar Al-Bashir wa Sudan kutua nchini Urusi kwa badali ya kukubali kufutiliwa mbali sheria tatanishi zinazo pingwa na utawala wa Amerika, ikisadifiana na kuanza kwa ziara ya kwanza ya Al-Bashir jijini Moscow. Duru za kuaminika zililiambia gazeti la Alrakoba kuwa: “Serikali ya Sudan ilipokea uhakikisho kutoka kwa Naibu Waziri wa Kigeni wa Amerika John Sullivan, kwa ziara yake jijini Khartoum, kutoizuia ndege ya Al-bashir kwa badali ya kupitisha mapendekezo ya Amerika kwa ajili ya kuruhusu uhuru wa kidini, na kuondoa vipengee tata vya kisheria vinavyo husiana na “kuritadi, urathi, na mavazi ya uchi …” (Masrawy 22/11/2017)].

Kwa sababu ikiwa agizo hilo halikuamrishwa na Amerika, Bashir hangetumia anga ya Saudia, kwa kuwa dola hiyo ya kikoloni ambayo serikali ya Saudia ni mfuasi wake inaushawishi na udhibiti wa anga hiyo, kama ilivyotokea wakati wa utawala wa Mfalme Abdullah kibaraka wa Uingereza mnamo 2013. Uingereza haikutaka Al-Bashir kufika Iran kwa sababu haikutaka serikali ya Iran kupata umaarufu kupitia kuwasili kwa viongozi wengi kwa ajili ya sherehe ya kutawazwa Raisi, hivyo Saudi Arabia ilipiga marufuku ndege ya Al-Bashir kujibu matakwa ya Uingereza. [Uraisi wa Sudan ulitangaza kuwa Saudi Arabia ilipiga marufuku serikali ya raisi huyo mnamo Jumapili kutokana na kuvuka anga yake ili kuhudhuria sherehe ya kutawazwa Raisi wa Iran jijini Tehran, ikimlazimu kurudi alikotoka … (France 24 4/8/2013)]

7- Yote hayo ya juu yanaondoa uwezekano wa kusimama kwa Amerika nyuma ya maandamano hayo. Uingereza haina uwezo wa kuyaanzisha, hivyo yalianza vipi na kuendelea?

Jibu ni kuwa maandamano hayo yalianza kwa ghafla kwa sababu ya kupamba moto mgogoro katika maisha ya watu nchini Sudan, na kadhia yote ni kama ifuatavyo:

a- Al-Bashir na washirika wake walidhani kuwa kwa kuisalimisha Sudan Kusini kwa kutii maagizo ya Amerika, Sudan ingeishi kwa ufanisi na usalama na ingesaidiwa na Amerika baada ya kuondolewa kwa vikwazo.

Lakini kinyume chake ndicho kilichotokea; hali ya kiuchumi ilianza kuzorota na kuwa mbaya zaidi. Mgogoro huo ukaongezeka mwanzoni mwa mwaka wa 2018 baada ya kuondolewa kwa vikwazo vya Amerika kutoka Sudan! Serikali imeongeza bei ya mkate na kuongeza thamani ya ushuru wa dolari mara tatu na kushusha thamani ya sarafu ya nyumbani, iliyopelekea kupanda kwa bei ikifuatiwa na mgogoro wa mafuta. Bei za mkate zimeongezeka maradufu ikipelekea uhaba. Inamlazimu mtu kusimama kwa masaa mengi katika foleni ili kupata kipande cha mkate ambao bei yake haimudu. Kiwango cha mfumko wa bei ni karibu asilimia 70, na benki kuu imeondoa pesa kutoka katika mabenki katika jaribio la kusitisha kuporomoka kwake.

Bei ya dolari imeongezeka hadi benki hiyo kulazimika kupunguza kiwango cha ubadilishanaji wa kifedha kwa zaidi ya asilimia 60 ikiifanya bei ya dolari kuwa pauni 47.5, na ikaanguka hadi mnamo 20/2/2019 kufikia pauni 75 dhidi ya dolari katika soko sambamba (soko huru).

b- Kasi ya umasikini miongoni mwa wakaazi wa Sudan imefikia viwango vya juu sana. Taasisi Kuu ya kunakili Takwimu ilithibitisha kuwa: [“Kasi ya umasikini ni zaidi ya thuluthi mbili ya wakaazi kwa kutegemea matokea ya utafiti uliokamilishwa mnamo 2014 kama utafiti wa kwanza tangu kutengwa kwa kusini mwa Sudan mnamo 2011”].  Yote haya yalitokea baada ya IMF kuanzisha mapendekezo yake, bali maagizo yake kama ifanyavyo kwengineko. Ilitoa wito kwa serikali kushusha thamani sarafu yake na kupunguza ruzuku juu ya mafuta, umeme na ngano, ikiahidiana pamoja na Benki ya Dunia kutoa usaidizi wa kiufundi kwa Sudan katika utabikishaji wa mpango wa mageuzi ya kiuchumi! Ahadi hiyo ilitolewa katika mkutano wa IMF / Benki ya Dunia katika ajenda ziada za mikutano nchini Bali na Indonesia, mnamo Oktoba 2018. Tambua kuwa IMF ilitoa wito kwa serikali kushusha thamani ya pauni katika ripoti yake ya kila mwaka ya Disemba 2017, na ikasisitiza kuwa hili ni muhimu ili kuunda hali muhimu za kuwavutia wawekezaji na kuimarisha maendeleo ya kiuchumi nchini humo. Ilitoa wito pia kwa serikali kuondoa ruzuku katika umeme na ngano kati ya 2019 na 2021 baada ya kushusha thamani sarafu hiyo. Utiifu wa serikali ya Sudan kwa maagizo haya ulipelekea kuzorota kwa uchumi na hali za kimaisha za watu wake.

c- Hivyo basi, hali hizi za Sudan zilikuwa tayari kulipuka. Huku kulikuwa ni kujitokeza ghafla barabarani kutokana na kuenea kwa umasikini, bei za juu, gharama ya juu ya maisha, kuongezeka kwa ukosefu wa ajira na usambazaji mbaya wa mali. Yote haya yalitokana na utabikishaji wa Al-Bashir wa nidhamu ya kirasilimali na kufuata mapendekezo ya taasisi zake za kifedha: IMF na Benki ya Dunia.

Ni serikali tiifu kwa Amerika inayotabikisha sera yake, hususan kuitenganisha kusini na kupoteza pato kubwa la dola hiyo la mafuta [na baada ya kutengwa kusini mwa Sudan mnamo 2011, Khartoum ilipoteza robo tatu za utajiri wake wa mafuta, ambayo yalikuwa yakijaza katika hazina yake takriban asilimia 80 ya utajiri wa ubadilishanaji wa fedha za kigeni. (Al Jazeera Net 26/12/2018)]. Maisha yamekuwa hayavumiliki, kisha cheche ya mapinduzi haya ya Sudan ikazuka kaskazini mwa nchi hiyo katika jimbo la Mto Nile katika mji wa Atbara mnamo 19/12/2018 na kisha kuenea katika miji yote ya Sudan, na yangali yanaendelea, na moto wake haujazimika; takwa lao ni moja pekee: kung’atuka kwa serikali hiyo.

Hivyo basi, maandamano hayo yalianza ghafla na kisha nguvu zikajiunga nayo ili kuyatumia kwa manufaa yake ili kupata maslahi yao na kuyapotoa maadamano hayo kutoka katika njia yake kama ilivyo fafanuliwa juu.

Kwa kutamatisha, kuna vitu viwili vinavyopaswa kuzingatiwa na kufikiriwa:

Ama cha kwanza, na kilicho lazimishwa na Amerika juu ya vibaraka wake ni kutia shinikizo juhudi zao kuhudumia maslahi yake. Al-Bashir ametia shinikizo juhudi yake katika hili, na hata akalisaliti kundi lake na kuitenga Kusini kutoka Sudan. Hadi leo, Amerika inaendelea kumsaidia Al-Bashir na iko katika mawasiliano naye na serikali yake inatoa ushahidi kwa hili, kama tulivyo onyesha. Lakini endapo maandamano hayo yataendelea na Al-Bashir hataweza kuyadhibiti karibuni, ataanguka kutoka machoni mwa Amerika na atashindwa kutumikia maslahi ya Amerika, hapo kuna uwezekano mkubwa kuwa Amerika itatafuta kumbadilisha, na pengine agizo la kuondolewa kwa baadhi ya watu wake kutoka serikalini ni kudandia wimbi la upinzani, hususan chama cha Merghani ambacho ni tiifu kwa Amerika. Pengine yote haya yanaendelea katika mwelekeo huu, yaani kuundwa kwa badali, kwa sababu mabadiliko yoyote kwa Al-Bashir yanahitaji kuwepo kwa badali ambayo inakubalika kwa watu. Amerika hutumia mbinu hii kwa vibaraka wake; iliitumia kwa Mubarak aliposhindwa kuyadhibiti maandamano, na ikamuamuru kung’atuka na akajiuzulu na kumteua Tantawi na baraza lake la kijeshi mahali pake. Ni mbinu inayotumiwa na Amerika, na kabla imuamuru kibaraka wake kuondoka, inahitaji badali, lakini inahofia mabadiliko hayo yatokee kabla ya kuweka badali hiyo, lau wanaume wenye ikhlasi watafikia utawala na kuwa mwiba kooni mwake bali hata kuwa kisu kifuani mwake. Kumbakisha kwake kibaraka wake Bashar mpaka sasa ni mfano wa hili.

Ama kuhusu jambo la pili, kinachohofiwa ni kuwa damu za wale waliouwawa na kujeruhiwa na zile hasara mabarabarani na katika asasi za umma zitapotea. Na maadamano hayo hatimaye yapelekee mabadiliko ya kibaraka kwa kibaraka mwengine. Na katiba iliyotungwa na binadamu isalie mahali pake nchini humo, kuuwa nafsi na kuwazonga watu. Hili ndilo tuliloonya, kwa sababu hadi leo maandamano hayo hayabebi matakwa ya Uislamu na hayalinganii kutabikishwa kwa Shari’ah, kupitia kufuata uongozi mwema wenye ikhlasi kufanya kazi ili kuregesha maisha kamili ya Kiislamu kupitia kusimamisha Khilafah Rashida. Na hivyo mgogoro huo wa kisiasa utabakia kama ulivyo, na hata huenda ukawa mbaya zaidi, na mgogoro wa kiuchumi utabakia hivyo hivyo, na huenda ukawa mbaya zaidi. Maneno ya Mwenyezi Mungu (swt) yanaweka wazi ukweli huu:

 (فَمَنِ اتَّبَعَ هُدَايَ فَلَا يَضِلُّ وَلَا يَشْقَى * وَمَنْ أَعْرَضَ عَنْ ذِكْرِي فَإِنَّ لَهُ مَعِيشَةً ضَنْكاً)

“… Basi mwenye kuufuata uongofu wangu kamwe hatapotea (duniani) wala hatateseka (Akhera)* Na yeyote atakayeupa mgongo utajo wangu basi hakika atakuwa na maisha ya dhiki” [TA-HA: 123-124]

Mwenyezi Mungu Al-A’leem Al-Hakeem  ni Mkweli

(فَاعْتَبِرُوا يَاأُولِي الْأَبْصَارِ)

“Basi zingatieni, enyi watu wenye macho” [Al-Hashr: 2]

27 Jumada II 1440 H
4/3/2019 M