Uhalisia wa chaguzi za Kidemokrasia na Hukumu ya Kiislamu juu yake.

Huku ikiwa zimesalia siku chache kabla ya uchaguzi mkuu hapo Agosti 9 chini ya kibandiko cha mageuzi, wanasiasa wanazunguka kona zote za nchi kutaka kupigiwa kura. Mazungumzo ya raia wa kawaida ambao wengi wao masikini hawajui uhalisia wa siasa ya kidemokrasia na wanasiasa wake nao wapo katika mazungumzo mikahawani, vijiweni na maskani wakishindana nani atashinda hasa kwenye kura za urais! Bila shaka pesa zinaangamizwa kwenye kampeni hizi ambazo zimejaa kila aina ya vitisho, urongo,chuki na matusi. La kutia machungu zaidi ni Waislamu kushughulika na uchaguzi huu kana kwamba ndio kadhia yao nyeti hapa duniani! Mashekh na Maustadh hutoa fatwa za kuhimiza watu kushiriki kwenye chaguzi za Kidemokrasa wakitumia Aya na Hadithi!

Kwenye Makala yangu haya sitaki kuingia katika fatawa hizi za masheikh bali napenda niweke msitari kati ya haki na batil na halali na haramu. Ili kujua hukumu ya kisheria katika suala la uchaguzi wa Kidemokrasia awali ya yote ni muhimu kubaini kile wana usuli hukiita tahqiq –manat (uhalisia na uhakika wa maana) ya chaguzi za kidemokrasia. Yaani hapa hatuna budi kueleza nini maana ya uchaguzi na nini maana Demokrasia kisha baadae ndio tututoe hukmu ya Kiislamu juu yake.

Uchaguzi ni uwakala yaani mtu kuchagua mtu mwengine amfanyie kitendo kwa niaba yake. Kwa mfano Msikitini twaeza tukatangaza nafasi za uimamu.Wakajitokeza watu watatu au wane wenye sifa za uimamu na hapa twataka imamu mmoja tu, hivyo maratibu wakachagua kati ya wanne hawa mmoja wao kwa kupitia kura.

Nabii Yunus AS : Kulipigwa ndani ya jahazi lililizidiwa na uzito ikabidi ipigwe kura na yule atakayeangukiwa na kura basi atoswe bahari. Yunus AS ikamwangukia yeye na akatoswa baharini.

فَسَاهَمَ فَكَانَ مِنَ ٱلْمُدْحَضِينَ

[Swafat: 141]

Kwa Nabii Zakaria AS: Katika kutafuta nani amlee Nana Maryam basi kura ikatumika

ذَلِكَ مِنْ أَنْبَاءِ الْغَيْبِ نُوحِيهِ إِلَيْكَ وَمَا كُنْتَ لَدَيْهِمْ إِذْ يُلْقُونَ أَقْلَامَهُمْ أَيُّهُمْ يَكْفُلُ مَرْيَمَ

Hizi ni khabari za ghaibu tunazokufunulia nawe hukuwa nao walipokuwa wakituma kalamu zao ndani ya Maji(kwa kura) wajue nani katika wao watamlea Maryam.

 [Al-Imran:44]

Mtumi Muhammad SAAW: Amepokea Imam Bukhari kutoka kwa Nana Aisha RA

” كَانَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ إِذَا أَرَادَ سَفَرًا أَقْرَعَ بَيْنَ نِسَائِهِ ، فَأَيَّتُهُنَّ خَرَجَ سَهْمُهَا خَرَجَ بِهَا مَعَهُ ،

Mtume SAW alipotaka kusafiri basi alikuwa akipiga kura baina ya wakeze na yule aliekuwa ikimwangukia basi ndiye aliekuwa akitoka naye.

Tuje katika maana ya chaguzi katika Demokrasia. Ni muhimu kufahamu kwamba Demokrasia ni mfumo wa kiutawala wala sio kupiga kura. Demokrasia asili  ni matamshi mawili yenye asili ya Kigriki Demos ambao humaanisha watu na cratos ikimaanisha utawala kwa maana ni utawala wa watu. Utawala huu humaanisha wanadamu wanamiliki ubwana (sovereignity) unaowawajibisha watunge kanuni ambazo ndio hutukuzwa kuliko sheria za Mwenyezi Mungu(swt). Hivyo Bunge au baraza la seneti, la wawakilishi au Congress zote katika demokrasia ni taasisi za kutunga kanuni. Sasa Demokrasia huchukua mbinu ya uchaguzi kila baada ya miaka 5 au 4 ya watu kuwachagua watu wawe ni wawakilishi wao katika kazi ya kutunga kanuni. Kwa kifupi chaguzi za Kidemokrasia zinafungika katika kitendo cha kutunga sheria ambacho ni kinyume na Uislamu.

Kwa mujibu wa Uislamu, sheria ni miliki ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kumaanisha kwamba Wanadamu haki yao sio kutunga sheria bali ni kufuata sheria za Mwenyezi Mungu (s.w.t). Mwanadamu hafai kabisa kutunga sheria hata kama imeambatana na sheria ya Mwenyezi Mungu(s.w.t) kwani kinachokatazwa ni kitendo cha kutunga sheria. Bali Uislamu umewajibisha kufuata sheria za Mwenyezi Mungu (s.w.t). Asema Allah swt:

فَلَا وَرَبِّكَ لَا يُؤْمِنُونَ حَتَّىٰ يُحَكِّمُوكَ فِيمَا شَجَرَ بَيْنَهُمْ ثُمَّ لَا يَجِدُواْ فِىٓ أَنفُسِهِمْ حَرَجًا مِّمَّا قَضَيْتَ وَيُسَلِّمُواْ تَسْلِيمًا

Naapa na Mola wako mlezi hawataamini mpaka wakufanye wewe ndiye muamuzi katika yale wanayo khitilafiana, kisha wasione uzito katika nyoyo zao juu ya hukumu utayo toa, na wanyenyekee kabisa

Huu ndio uhalisia wa uchaguzi hivyo kinachofanya  uchaguzi usemwe ni haramu au halali si uchaguzi kwa dhati yake bali ni kile kitendo ambacho kinafungika na ule uchaguzi wenyewe. Kwa haya chaguzi za kidemokrasia zinakiuka misingi ya Kiislamu hivyo ni batili kisheria, na haramu kwa Waislamu kuunga mkono vyama vya kidemokrasia na kushiriki ndani yake.

Shabani Mwalimu

Mwakilishi kwa Vyombo Vya Habari Hizb  ut Tahrir Kenya

 

 

Comments are closed.