Jumla

Umoja wa Waislamu utapatikana kwa Kuwepo na KHALIFAH na KHILAFAH na wala sio Kadhi au Mufti

Kusambaza ni Kuunusuru Uislamu

Waislamu nchini Kenya wameshuhudia mvutano kati ya viongozi wakuu serikalini uliotokamana na Sherehe za Siku Kuu ya Kuchinja (Eid ul-Adha).  Huku Kiongozi wa Walio wengi Bungeni, Aden Duale akiunga mkono msimamo wa Serikali kupitia tangazo la Waziri wa Usalama wa Ndani, Fred Matiang’i aliyetangaza rasmi kwamba siku ya Jumanne 21 Agosti 2018 ni siku kuu ya kitaifa kwa ajili ya sherehe ya Eid ul-Adha.  Kauli ya serikali ilionekana ikienda kinyume na tangazo la awali la Kadhi mkuu wa Kenya, Ahmad Muhdhar aliyetangaza kuwa Eid ni siku ya Jumatano, 22 Agosti 2018. [Daily Nation, 20 Agosti 2018] Kauli hizo za viongozi hao wawili ambao wote ni wafanyikazi wakuu katika Serikali, iliwapelekea waumini wa dini ya Kiislamu kuwa njia panda!

Viongozi wengine wakipendekeza suluhisho la kuepuka kukinzana huko akiwemo Waziri wa Utalii, Najib Balala alisema “Nitaongoza Ummah wa Kiislamu kuandaa jukwaa ambalo litajadili suala la kuwepo kwa Afisi ya Mufti. Twataka kulifanya hili ili kuwaunganisha Waislamu nchini.” Balala aliendelea kusema kuwa “Hatuhitaji kuwepo kwa sheria ili awepo, kwa sababu Mufti ni chaguo la Waislamu na sio serikali. Lakini ikiwa serikali itaonelea kuwepo na sheria kuhusiana na atakeyepewa cheo hicho cha Mufti, itakuwa jambo bora na tutalifanyiakazi liwezekane.” Naye Mwenyekiti wa Baraza la Ushauri la Waislamu Nchini (KEMNAC), Juma Ngao alisema “Twasoma Qur’an moja, twaabudu Mwenyezi Mungu mmoja, sisi ni Ummah mmoja, lakini kila mara hatuelewani kuhusiana na masuala madogo kama terehe ya Ramadhan na Eid. Sasa twahitaji mtu atakaye tuongoza.” Na alisema kwamba Rwanda, Burundi, Misri, Uganda na Tanzania wameunda afisi ya Mufti nayo Kenya inatakiwa kuiga kutoka kwa jirani zake. [The Star, 21 Agosti 2018].

Mkanganyiko huu na suluhisho linalo pendekezwa ni natija ya pigo lililoupata Ummah wa Kiislamu mnamo 28 Rajab 1342H sawia na 3 Machi 1924; pale ambapo wakoloni wamagharibi wakiongozwa na Uingereza na Ufaransa waliivunja Khilafah (Serikali ya Kiislamu) na kumfurusha Khalifah (Kiongozi wa Waislamu ulimwenguni)! Kisha kuigawa iliyokuwa Dola Moja ya Kiislamu (Khilafah) na kuifanya mataifa 54 na yakisimamiwa na watawala vibaraka ambao kibla chao ni London au Washington. Tokea wakati huo hadi sasa takribani miaka 94 Ummah wa Kiislamu ulimwenguni umebakia yatima na wenye kutapatapa huku na kule ilhali matukufu yao yakichezewa shere, damu zao kumwagwa na ardhi zao kutekwa na kupewa makafiri mfano ardhi Tukufu ya Palestina kukabidhiwa mayahudi n.k. Ummah wa Kiislamu unatungiwa sheria za kijambazi eti za kudhibiti misimamo mikali au ugaidi n.k na vijana kwa wazee wakiozea magerezani kutokana na sheria hizo za kidhalimu!

Serikali ya Kenya ni serikali iliyosimama juu ya batili kutokana na kuwa chimbuko la itikadi yake ni Usekula (kutenganisha dini na maisha) na mfumo wake ni Urasilimali (kipimo chake ni maslahi/manufaa/faida/hasara). Kutokana na msingi huo ni wazi kwamba serikali ya Kenya kattu haitokamani na Uislamu kwa kuwa haiendeshwi kwa mujibu wa Qur’an, Sunnah, Ijm’a Sahaba na Qiyas. Hivyo basi Kadhi wa Kenya ni mfanyikazi kama mfanyikazi mwengine katika serikali hii batili. Mfano mfanyikazi anayefanya katika Benki Kuu ya Taifa, kiwanda cha pombe cha Kenya Breweries au mfanyikazi mwenye kuidhinisha/kutoa vibali vya kuruhusu kufunguliwa kwa Baa/Danguro n.k. Tofauti yao ni katika majukumu ya kazi ambapo Kadhi majukumu yake yamefungwa katika masuala ya ndoa, mirathi na talaka kati ya Waislamu napia lau atatoa uamuzi wake na wahusika wasiridhishwe na uamuzi huo wanaweza kukata rufaa mahakama ya juu. Hilo linadhihirisha udhaifu wa mamlaka ya kadhi ambayo yamedhibitiwa kikatiba na pia amefungwa na mipaka ya kikoloni ya kitaifa kwani hawezi kuhukumu nje ya Kenya! Ama kuhusu pendekezo la Afisi ya Mufti pia limefungika katika mipaka ya kikoloni na lau itabuniwa Afisi hiyo nayo itakumbwa na matatizo ya udhaifu kwani Katiba (tungo za mwanadamu zinazotokamana na akili yake finyu) ndiyo muongozo wa taifa na kamwe haitarajiwi Mufti kuwa na usemi kuliko katiba, lakini atapewa kwa mujibu wa katiba usemi katika masuala fulani ili ionekane kuwa Waislamu nao wana usemi fulani katika masuala fulani. Ukweli utabakia kuwa aidha Kadhi au Mufti wote ni chimbuko la hisia za kutapatapa za Waislamu kudai uongozi ili wapate suluhisho ya matatizo yanayo wakumba kila kukicha.

Suluhisho msingi lipo katika Waislamu kujifunga kikamilifu na Uislamu.

ياأيها الذين أمنوا أدخلوا في السلم كافة ولا تتبعوا خطواتكم الشيطان انه لكم عدوكم مبين

 “Enyi mlio amini! Ingieni katika Uislamu kwa ukamilifu, wala msifuate nyayo za She’tani, hakika yeye kwenu ni adui aliye wazi.” [Al Baqarah: 208]

Kwani Uislamu pekee ndiyo mfumo ambao Allah (swt) anaoutambua.

إن الدين عند الله الإسلام

Bila ya shaka Dini (mfumo) mbele ya Mwenyezi Mungu ni Uislamu. [Aal-Imran: 19]

Uislamu kama Dini (Mfumo) ikimaanisha kuwa itikadi ya ‘Hapana Mola Apasaye Kuabudiwa kwa Haki isipokuwa Mwenyezi Mungu na Muhammad ni Mtume wake’ iwe ndiyo msingi wa matendo yote ya mwanadamu. Na kwamba Uislamu ndiyo uwe unaosimamia nyanja zote za maisha kuanzia siasa, uchumi, jamii, elimu, sera ya kigeni, jihadi n.k. Hivyo basi hakuna budi kuwa na kiongozi (Khalifah) na dola (Khilafah) itakayo waunganisha na kuwasimamia Waislamu wote mambo yao yote kwa mujibu wa Uislamu na machimbuko ya sheria yatakuwa ni Qur’an, Sunnah, Ijm’a Sahaba na Qiyas pekee.

Kwa muktadha huo Waislamu jumla wanatakiwa kujiepusha na mizozo ya kimakusudi ambayo chimbuko lake ni Ummah wa Kiislamu kugawanywa na maadui wa Uislamu. Ili kuwashughulisha Waislamu na mambo duni na badala yake wajadiliane namna gani Uislamu utakavyotekelezwa katika maisha jumla kinyume na ilivyo sasa; Uislamu unatekelezwa kibinafsi au msikitini tu. Napia kutekelezwa huko ni kwa mambo ambayo hayaendi kinyume na Kanuni/Katiba ya nchi wanazoishi ndani yake. Hivyo hakuna budi ila kujiepusha na mashirika au vyama au watu/wanasiasa waliotegemea Urasilimali Usekula kuwapa muongozo katika mambo ya Uislamu. Badala yake wajiunge na ndugu zao Waislamu wanaofanya kazi usiku na mchana wa Hizb ut Tahrir ulimwenguni kote ikiwemo hapa nchini Kenya katika kulingania Waislamu wajifunge na Uislamu wao kikamilifu, kusimamisha Serikali ya Kiislamu (Khilafah) chini ya Kiongozi (Khalifah) mmoja ndani ya nchi/mataifa ya Waislamu.

Hima Waislamu tuchangamkeni ili tufanyekazi ya kuirudisha mama wa faradhi zote nayo ni kusimamisha Khilafah kwa njia ya Utume. Kazi hii itatupelekea sisi Waislamu kuingia katika historia kama walivyongia katika historia Muhajirina na Ansar waliofanyakazi usiku na mchana kuinusuru Dini (mfumo) ya Allah (swt) na malipo yao yakawa kupata utukufu na cheo hapa duniani na akhera kudumu katika pepo kwa rehema zake Mwenyezi Mungu.

Ali Nassoro Ali

Mwanachama wa Afisi ya Habari ya Hizb ut Tahir Kenya