Jumla

Umuhimu wa Kuyakumbuka Mauti

Kusambaza ni Kuunusuru Uislamu

Moja katika maudhui yanayokwepwa na Jamii ya kiliberali kimakusudi kuyazungumzia ni mauti. Hii inakuja kwa kinachotokamana na itikadi yao ya Kisekula kwamba shabaha kuu ya maisha ya wanadamu hapa duniani ni kujipatia nafasi na kiwango kikubwa cha starehe. Kwa mtazamo huu ndio watu wengi leo hukataa kuyazungumzia mauti.

Uislamu umetuelekeza jinsi ya kufahamu umauti nayo humaanisha kutoka katika maisha ya duniani na kwenda kukutana na Mwenyezi Mungu (swt). Mwenyezi Mungu (swt) anasema:

Sema ‘Hakika mauti haya mnayoyakimbia, bila shaka yatakutana nanyi, kisha mtarudishwa kwa Mjuzi wa siri na dhahiri hapo atakujulisheni (yote) mliyokuwa mkiyatenda.

[Al-Jumu’ah:8]

Licha ya hayo Uislamu pia ukafafanua kuwa mtu yeyote hawezi kufa ila kwa matakwa na amri ya Mwenyezi Mungu (swt). Hivyo sababu ya umauti ni moja tu nayo ni kumalizika kwa umri wa mwanadamu. Muislamu lazima aitakidi kuwa afishaye si mwengine ila ni Mwenyezi Mungu (swt) pekee.

Kukumbuka mauti maana yake ni kuikumbuka akhera yaani kufahamu mwanadamu kuwa hana budi ila iko siku atakutana na Mola wake. Aliletwa hapa duniani pasina khiyari yake basi ataondoka pia pasina mapenzi yake. Mtume (saw) ametaka Waislamu waweze kukithirisha kukumbuka mauti kama alivyopokea Tirmidhiy, An-Nasaai na Ibn Majah kutoka kwa Abu Hurairah kwamba Mtume (saw) alisema:

‘Kithirisheni katika kukumbuka chenye kuondosha ladha, yaani mauti.’

Kuna faida nyingi mno kwa Muislamu katika kuyakumbuka mauti kila wakati lakini tutosheke na kutaja tu tano.

Kwanza; Humfanya Muislamu awe na haraka ya kufanya toba ya kikweli kwani hukumbuka madhambi yake na kumuomba msamaha Mwenyezi Mungu (swt) kabla ya kuondoka kwake duniani.

Pili; Kutosheka na kipato alichopewa na Mwenyezi Mungu (swt). Moyo kutosheka humfanya Muislamu kutokimbizana na dunia bali hushughulikia dunia huku akichunga mipaka ya Uislamu. Muislamu ana mwisho wa kuishi duniani na vilivyomo alivyoruzukiwa ataviacha na kwenda kukutana na Mola wake ambako huko ni amali njema ndiyo zinazohitajika.

Tatu; Huleta uchangamfu wa kufanya amali njema. Mwenye kukumbuka mauti utampata akijipinda kwa kufanya kila jema huku akijieupusha na kila ovu. Utamwona hachoki kuswali, kusoma Quran, kufanya da’wah na mengine mengi mema kwani anajua wakati wowote huenda akaondoka.

Nne; Muislamu anayekumbuka mauti huepukana na hasadi kwani siku zote anaonekana akiachana na mambo ya watu huku akijishughulikia zaidi yeye mwenyewe na mambo yake yatakayomfaa Akhera.

Tano; Huhuisha moyo wa mtu. Sababu kubwa inayopelekea moyo wa mtu kuwa hai kiasi cha kuwa walainika katika kusukuma mtu kufanya mema ni kukumbuka mauti. Amepokea Abu Hurairah kuwa Mtume (saw) alisema:

‘Fanyeni wingi wa kukumbuka mauti kwani hakuna mja yoyote ayakumbukaye kwa wingi ila Mwenyezi Mungu huhuisha moyo wa mja huyo na kumsahilishia uchungu wa mauti.’

Kinyume cha hayo mtu asiyekumbuka mauti siku zote utamuona akiwa mvivu katika kufanya ibada, kulevywa na maisha ya dunia pamoja na kuchelewesha toba huku akizama na starehe za dunia.

Katika kukumbuka mauti kunapaswa kumsukume Muislamu ajitayarishe na mauti kwa kufanya kila aliloamrishwa na kujieupusha na kila alilokatazwa. Mtume (saw) asema:

Mwerevu ni yule atakayedunisha nafsi yake kwa kutofuata matamanio yake kisha akafanya mema yatakayomfaa baada ya mauti, na mvivu ni yule atakayefuata matamanio ya nafsi yake huku akitamani kuwa atapewa mazuri na Mwenyezi Mungu.

Na katika Hadithi nyengine inayosimuliwa na Ibn Umar (ra), asema:

‘Nilikuwa pamoja na Mtume (saw) mara akajiliwa na mtu miongoni mwa Answar akamsalimia kisha akamuuliza Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu ni Muumini yupi aliye bora zaidi? Mtume (saw) akamjibu: ‘Ni yule mwenye tabia njema zaidi”. Kisha akamuuliza tena: na ni nani katika Waumini aliye mwerevu zaidi akasema Mtume (saw): ‘ni yule akumbukaye kwa wingi mauti na anayejitayarisha zaidi na baada ya mauti na hao ndio waerevu.’

Mambo yafuatayo tunaweza tukayatumia kama ukumbusho wa mauti:

-Kuzuru makaburi kila mara kwa kuwaombea waliotangulia mbele ya haki.

-Kumwangalia maiti akiwa amelazwa kitandani akioshwa, kukafiniwa, akiswaliwa, akiwa kwenye jeneza na hatimaye kuzikwa.

-Kufikiri watu wako wakaribu waliofariki dunia uliokuwa ukiamiliana nao kucheka, kupanga nao mipango ya maisha lakini walikufa huku mipango mingi yao bado ikiwa haikukamilika.

Hivi ndivyo inatakikana Muislamu kwa hali yoyote aonekana akikumbuka tukio hili zito ambalo ni zito sana kuliko mazito yote aliyokumbana nayo maishani mwake. Akumbuke pia kuwa tukio hilo la mauti ndilo jepesi zaidi kuliko yanayofuata baada yake. Twamoumba Mwenyezi Mungu (swt) atupe mwisho mwema, aturuzuku shahada wakati wa kufa, msamaha baada ya kufa na toba kabla ya kufa. Ameen

Shabani Mwalimu

Mwakilishi Kwa Vyombo vya Habari Hizb ut Tahrir Kenya

 

Kutoka Jarida la UQAB Toleo 12