Jumla

Upi Mwelekeo Kuhusiana na Noti za Sh1000 nchini Kenya?

Kusambaza ni Kuunusuru Uislamu

Gavana wa Benki Kuu Patrick Njoroge akizungumza wakati wa sherehe za Madaraka Day katika Uwanja wa Narok, mnamo Jumamosi, 1 Juni 2019 alitangaza kuwa noti za Sh1000 za zamani zitakuwa hazitumiki tena kufikia Jumanne, 1 Oktoba 2019. Hatua inadaiwa kuwa ni jaribio la  kupambana na mzunguko mbaya wa kifedha na vita dhidi ya ufisadi.

Matamshi hayo ambayo kihakika ni yakushangaza lakini wengi wa waliohudhuria walionekana kupiga makofi na kusherehekea! Kwa ufupi ni kwamba kupitia tangazo Rasmi la Serikali la 31/05/2019 kwamba kumetoka noti mpya ambazo ni zabuni ya kisheria. Noti za Sh50, Sh100, Sh200 na Sh500 zitaendelea kubadilishwa mpaka pale zitakapoondoka sokoni kimaumbile lakini noti za Sh1000 zinabadilishwa mwisho wake ni Jumanne, 1 Oktoba 2019! Mtu akiwa na vyeti vya kujitambulisha ataruhusiwa kubadilisha chini ya milioni Sh5 katika benki au tawi la benki lakini zaidi ya milioni Sh5 mpaka apate idhini kutoka Benki Kuu. Kufikia mwisho wa makataa ikiwa itakuwa hujabadilisha pesa zako za noti ya Sh1000 itakuwa si chochote isipokuwa ni makaratasi!

Hatua hiyo ya serikali ni hatari mno kwani imechukuliwa kwa kasi kiasi cha kwamba yeyote yule ambaye hayuko karibu na vyombo vya habari itakuwa vigumu kujifunga na amri hiyo kuhusiana na makataa ya kubadilisha noti za Sh1000. Hatari zaidi ni kuwa inawezekana ikapelekea mtu akafilisishwa na kuwa masikini! Pili wale wanaomiliki mabenki na taasisi za kifedha na ambao wameficha mali nyingi walizopora wao watafaulu kubadilisha pasina uzito wowote ama wale ambao hawamiliki mabenki na ambao wameweka akiba zao majumbani basi watakuwa na wakati mgumu mno. Inaweza kuwapelekea kuchangamkiwa na serikali kwa tuhama za ukwepaji kulipa ushuru na kuhusika katika uhalifu wa kifedha n.k!

Hakika, kuishi chini ya serikali za kisekula za kirasilimali zinazotawala kwa nidhamu yake ya kidemokrasia ni hatari kwa utulivu, maendeleo na ustawi wa mwanadamu. Kwa kuwa Serikali hizi hazina huruma wala mapenzi kwa raia wao kwa kuwa daima zinakwenda mbio kutafuta kila njia ili kuwapora na kuwaibia raia mali zao ikiwemo kuwatoza ushuru mfano VAT, PAYE, NSSF, NHIF n.k na hivi sasa inataka kuwasukumiza watu kudidimia katika umasikini zaidi kwa kisingizio cha kupambana na mzunguko mbaya wa kifedha!

Hakika, nidhamu ya kiuchumi ya kirasilimali inahalalisha na kuharamisha pesa za makaratasi na huipa kipaombele sarafu ya dola kuu duniani. Kiasi kwamba leo hii kila nchi duniani inafanya biashara kwa mujibu wa sarafu ya Marekani ambayo ni Dolari. Kwa maana nyingine nchi inaweza kuanguka au kuinuka kutegemea nguvu za Dolari ya Marekani! Na lakusikitisha zaidi ni kwamba kila nchi duniani inayo benki yake kuu ambayo jukumu lake ni kupeana zabuni ili kuchapishwe pesa za makaratasi zianze kutumika! Kwa maana nyingine pesa ni makaratasi lakini uhalali wake unategemea uhalali wa zabuni!

Kwa mujibu wa Uislamu kuchapisha pesa za makaratasi ni jambo la linaloruhusiwa (mubah) lakini kwa sharti pesa zilizochapishwa ziwe kwa kiwango cha dhahabu na fedha ambazo nchi hiyo inamiliki. Kwa maana nyingine ikiwa pesa za makaratasi ni bilioni moja basi kuweko na kiasi cha dhahabu na fedha yenye thamani ya kiwango hicho. Tokea zamani watu walikuwa wakitumia kipimo cha dhahabu na fedha katika uchapishaji wa pesa za makaratasi lakini mnamo 15 Agosti 1971 Rais wa Marekani Richard Nixon akatangaza duniani kuwa Marekani haitobadilisha tena dolari kwa dhahabu kwa kiwango maalum.

Tokea wakati huo utajiri wa nchi nyingi duniani ukaanza kuporwa kupitia Sera ya Fedha inayotegemea dola kuu ulimwenguni! Kiasi kwamba leo hii Marekani ikichemua nchi zote duniani zinatetemeka kama ilivyokuwa mwaka 2008 kuanguka kwa Uchumi wa Marekani kulipelekea uchumi wa duniani kote kuanguka na kusambaratisha nchi nyingi. Napia imepelekea nchi nyingi duniani kuwa watumwa wa dola kuu kiasi kwamba itakavyosema hawana budi isipokuwa kutii amri hata kama watapiga kelele shingo upande mfano hivi majuzi Marekani iliiwekea vikwazo Iran na yeyote atakayefanya kazi na Iran atapata adhabu kali kutoka Marekani!

Kinyume chake Uislamu sarafu yake itakuwa ni dhahabu na fedha kwa sababu ndiyo ambayo Mwenyezi Mungu (swt) ameitambua kama utajiri au kipimo cha utajiri na ndio maana Mwenyezi Mungu (swt) akaharamisha ukusanyaji/urundikaji wa dhahabu na fedha pasina matumizi:

(وَٱلَّذِينَ يَكۡنِزُونَ ٱلذَّهَبَ وَٱلۡفِضَّةَ وَلَا يُنفِقُونَہَا فِى سَبِيلِ ٱللَّهِ فَبَشِّرۡهُم بِعَذَابٍ أَلِيمٍ۬)

“Na wanao kusanya dhahabu na fedha, wala hawazitumii katika Njia ya Mwenyezi Mungu, wabashirie khabari ya adhabu iliyo chungu.” [At-Taubah: 34]

Hivyo basi hivi karibuni serikali ya Kiislamu ya Khilafah itakaposimama tena duniani kwa njia ya Utume. Sarafu au pesa zake zitakuwa asilimia mia moja ni kwa kipimo cha dhahabu na fedha na lau itachapisha noti za makaratasi basi itakuwa ni kwa mujibu wa kiwango cha dhahabu na fedha zilizopo katika hazina ya Dola. Kattu haitoruhusiwa hata mara moja kuwepo na kiwango cha pesa za makaratasi ambazo hazina dhamana ya dhahabu na fedha.

Kwa kusimama Khilafah itakuwa ni kupata utulivu, maendeleo na ufanisi wa kweli kwa wanadamu jumla. Kwa kuwa mzunguko wa kiuchumi utakuwa uko katika msingi imara usioyumbayumba na kutegemea dhana kama inavyoshuhudiwa hivi leo duniani. Hivyo basi mtu anaweza kuweka akiba zake kwa kutumia dhahabu na fedha na kattu hazitegemei uchapishaji kama pesa za makaratasi hivi leo ambazo mara serikali inaweza ikaziharamisha na kuchapisha mpya usiku kuamkia asubuhi na ikawa umelala tajiri na asubuhi ukaamka ni ombaomba kwa maana umefanywa masikini na serikali yako! Kwa hiyo bei za bidhaa na huduma zitakuwa imara sio kama inavyoshuhudiwa leo bei zinapanda pasina sababu yoyote isipokuwa ni dhana tu za kiuchumi kwa mtizamo duni wa Magharibi wakoloni!

Kwa kutamatisha katika dola ya Khilafah watu watakuwa wanaweza kutumia moja kwa moja katika biashara dhahabu, fedha au pesa za makaratasi kwa sharti ziwe zimedhaminiwa kwa dhahabu na fedha katika hazina ya Khilafah. Hivyo basi hatuna budi kwenda mbio kurudisha tena maisha ya Kiislamu kupitia kusimamisha serikali ya Kiislamu ya Khilafah kwa njia ya Utume ili kunusuru uchumi na maisha yetu kwa ujumla.

Ali Nassoro Ali

Mwanachama wa Afisi ya Habari ya Hizb ut Tahrir Kenya

Makala Na.53: Ijumaa, 9 Dhul-Qa’da 1440 | 2019/07/12