Jumla

Ushindi wa Wanawake Waislamu katika Uchaguzi wa Marekani: Ni Ushindi wa Uislamu Poa wa Kisekula

Kusambaza ni Kuunusuru Uislamu

Mnamo Jumatano 7 Novemba 2018 vyombo vya habari vya kieneo na kimataifa vyenye umaarufu viliripoti kuwa wanawake wawili Waislamu kwa jina Ilhan Omar umri wa miaka 37 na Rashida Tlaib wa umri wa miaka 42 waliweka historia kwa mara ya pili ndani ya Amerika kwa kuchaguliwa kuhudumu ndani ya Bunge la Marekani (Congress). Historia zao za kwanza ni kuwa mnamo mwaka 2008 Rashida Tlaib alikuwa mwanamke Muislamu wa kwanza kuhudumu ndani ya bunge la jimbo la Michigan na mwaka 2016 Ilhan Omar alikuwa Msomali-Muamerika wa kwanza ndani ya taifa hilo kuhudumu ndani ya bunge la jimbo la Minnesota (Daily Nation, 07/11/2018). Uchaguzi uliopita juzi wa Marekani ulikuwa wa kihistoria kwa mitizamo miwili kiujumla; kwanza, ni kuchaguliwa kwa idadi kubwa ya wanawake kuingia Bungeni, na pili, jimbo la Colorado lilimchagua mwanamume shoga, Jared Polis kama gavana! (Evening Standard, 07/11/2018). Ilhan Omar, Rashida Tlaib na Jared Polis wote ni wanachama wa chama cha Demokrasia (Democratic Party) kilichobuniwa mwaka 1828 huko Marekani.

Historia hii mpya inayotokana na wanawake hawa wawili inakuja baada ya Rais wa Marekani Donald Trump mnamo Jumatano 27 Januari 2017 kuwapiga marufuku Waislamu kutoka Iran, Libya, Somalia, Sudan, Syria na Yemen wasiingie nchini humo kwa kisingizio eti Anailinda Marekani iwe salama kutokana na ugaidi! Kwa upande mwingine, aliyekuwa Mshauri Mkuu wa Trump katika Usalama wa Kitaifa, Michael Flynn aliwahi kusema, “Huu Uislamu ni kansa yenye sumu kali iliyoko ndani ya mwili wa watu bilioni 1.7 katika dunia na inatakiwa kutolewa.” (CNN 23/11/2016). Licha ya hayo, aliyekuwa Mshauri Mkuu na Mwanamikakati Mkuu wa White House na Rais, Steve Bannon aliwahi kuuita Uislamu “Dini yenye misimamo mikali katika dunia” (BBC, 07/02/2017). Wanawake hao wawili Ilhan Omar na Rashida Tlaib ambao machimbuko yao ni kutoka Somalia na Palestina mtawalia; nchi mbili ambazo hivi sasa zimo katika mahangaiko ambayo chanzo chake kimekitwa juu ya ulafi na sera ya umwagaji damu ya Marekani ya kuitimizia azma ya umbile la Kiyahudi ya kutambuliwa ndani ya Palestina na vita vya Somalia kuhusiana na kupambana na ugaidi. Sera hiyo bado inaendelea mpaka hivi leo na imesababisha mauaji, majanga na inachangia katika mipango ya wahamiaji waliokata tamaa kuelekea Marekani na Ulaya!

Wakati uongozi mkuu wa kisiasa wa Marekani unatamka kauli hizo za sumu na huku inaendelea na vita vya moja kwa moja dhidi ya “Misimamo Mikali/Ugaidi au Wenye Misimamo Mikali au Magaidi.” Hata hivyo, suali ni kwa nini imewaruhusu hawa Waislamu wachache kujiunga na kuwa sehemu ya nidhamu zao?! Jibu ni rahisi mno, ni kuwa yeyote anayejiita Muislamu na akaenda mbele zaidi na kutekeleza Uislamu kwa mtizamo wa kisekula uliomaarufu kama “Uislamu/Waislamu Poa” basi bila shaka amekuwa mwanachama wa mfumo batili wa kisekula wa kirasilimali. Mfumo muovu unaotenganisha dini na maisha. Licha ya hayo, unampa mwanadamu mamlaka ya kujiwekea nidhamu za kuendesha maisha na kujidhaminia uhuru aina zifuatazo: uhuru wa kuabudu, uhuru wa maoni, uhuru wa kumiliki na uhuru wa kibinafsi. Hivyo basi, Muislamu Poa anaweza kushiriki katika mipango ya kisekula na nidhamu zake ikijumuisha kushiriki katika uchaguzi wa kidemokrasia ambao unampa mwanadamu mamlaka ya kutawala kwa matamanio ya nafsi yake kinyume na yale yaliyoteremshwa na Muumba wa mwanadamu! Wakati huo huo mtu anaweza kuwa chochote mfano mwanamume anaweza kuwa shoga na mwanamke anaweza kuwa msagaji na hata kuoana! Kwa hiyo wanawake hawa wawili wanatoa mtizamo wa kirongo na hatari juu ya “mtizamo wa kufaulu” uliokitwa juu ya eti uhuru na ukombozi wa mwanamke na utambuzi wa Waislamu ndani ya Amerika!

Ukweli ni kwamba wanawake hawa wawili Waislamu si chochote bali wanatumika kama vikaragosi na utawala wa Marekani ili kuwahadaa Waislamu ulimwenguni kwamba Marekani inawajali Waislamu na siye adui wao! Zaidi ya hayo, uongozi wa Marekani unatumia mbinu zile zile kama za marafiki zake wa Ulaya ili kuficha nia zao ovu na mikono yao iliyojaa damu katika vita vyao dhidi ya eti “Uislamu/ Waislamu wenye Misimamo Mikali/Magaidi” ambao kiasili ni Waislamu ambao wamesema LA HATUTAKI UISLAMU WA KISEKULA. Waislamu ambao si masekula daima wanajitahidi usiku na mchana kujifunga kikamilifu na Uislamu wao safi na wanalingania kurudi tena kwa Maisha ya Kiislamu kupitia kurudi tena kwa ngao na mama yao Khilafah kwa njia ya Mtume (saw).

Wanafikra na hususan Waislamu ulimwenguni kote lazima wasiwe wahanga wa propaganda ovu za Marekani zinazolenga kupigia debe Uislamu/Waislamu Poa na kuwapiga vita kifikra na kijeshi wale Waislamu ambao hawajiungi nao na badala yake wanalingania kuondoshwa kwa mfumo batili uliofeli wa kisekula wa kirasilimali unaopgiwa debe na wakoloni wamagharibi duniani kote wakiongozwa na Marekani, marafiki zake na watawala vibaraka! Wakati huo huo tunawalingania kwa moyo mkunjufu muusome Uislamu kama mfumo badala uliokuwa na uwezo takribani Karne 14 na una uwezo leo wa kutatua matatizo na majanga mengi yaliyosababishwa na mfumo muovu wa kisekula wa kirasilimali na nidhamu zake zinazonuka. Uislamu kama mfumo utokao kwa Muumba wa dunia hautoi nafasi ya kuweko na uhuru bali unawasukuma wanadamu kuwa watumwa wa Mwenyezi Mungu (swt) ambao daima wanatafuta radhi za Muumba wao kwa kujifunga na kipimo cha Halali na Haramu katika vitendo vyao vyote kinyume na mfumo wa kisekula wa kirasilimali ambapo vitendo vyote vinapimwa kwa msingi manufaa/maslahi/hasara/faida!

Chini ya Khilafah,Waislamu na hususan wanawake watapewa nafasi ili kufikia uwezo wao hususan katika majukumu yao msingi kama wake, mama na wasimamizi wa nyumba na wakati huo huo kushiriki katika vitendo vinavyoruhusiwa mfano muamalat, biashara, kutoa maoni ya kisiasa ikiwa ni pamoja na kuwahesabu viongozi (sio kutawala na kutunga sheria kama ilivyo katika dola za kisekula) n.k. Khilafah chini ya kiongozi muadilifu anayetawala kwa Qur’an na Sunnah itahakikisha kuwa Waislamu wamejengwa kwa njia maalum ili wawe na Utambulisho wa Kiislamu ambao umeuweka Uislamu kama msingi wa kupata utukufu na hadhi na sio kupitia kumiliki kwa mada na vyeo vya kimaslahi kama inavyopigiwa debe na mfumo wa kisekula wa kirasilimali!

Kwa kumalizia, kipenzi chetu na Bwana (saw) wetu ametusimulia katika Hadith ifuatayo:

 “Watu wanaomchagua mwanamke kuwa kiongozi wao hawatofaulu”

 (Bukhari, Sahih. #4425)

Ali Nassoro Ali

Mwanachama wa Afisi ya Habari ya Hizb ut Tahrir Kenya