Jumla

Uzuiaji wa Mimba Katika Uislamu

Kusambaza ni Kuunusuru Uislamu

Vyombo vikuu vya habari nchini Kenya na Kimataifa hivi sasa viko katika kampeni kubwa ya kupigia debe njia za uzuiaji mimba za kudumu (permanent) kupitia upasuaji zinazojulikana kama ‘ vasectomy’ kwa wanaume na ‘tubectomy’ kwa wanawake. Vasectomy na Tubectomy ni njia za kudumu, zisizorekebishika na zinahusisha oparesheni ya upasuaji. Njia hizo mbili zinadaiwa kuwa ni nzuri kwa wanaume na wanawake ambao wana uhakika kuwa hawataki tena watoto! Wanaharakati na madaktari wa huduma za uzazi wanapewa nafasi mwanana katika mahojiano na katika sehemu za uandishi ili kuwasilisha maoni yao yanayounga mkono juu ya manufaa yanayopatikana kupitia kuchagua njia hizo. Wote wanataja kuwa sababu za wao kuunga mkono ni kutokana na janga la uchache wa rasilimali na wingi wa watu!

Ni aibu kwa kwa taifa kama Kenya ambalo limejaaliwa na rasilimali tele zenye uwezo wa kutosheleza raia wake pasina kutaka msaada na mikopo ya kigeni; inakwenda mbio kupitisha na kutekeleza sheria na sera zilizochorwa na kupigiwa debe na tawala za Kimagharibi na mashirika yao kama UN. Yote ni kwa jina la kupambana na tatizo la kiuchumi linaloshuhudiwa duniani kote na linalodaiwa kusababishwa na uhaba wa rasilimali! Hakika, serikali za Kimagharibi zikiongozwa na Marekani msingi wao ni itikadi ya kisekula (kutenganisha dini na maisha/serikali) na mfumo wao ni urasilimali (kuwapa kipaumbele warasilimali kwa lengo la kukuza uchumi). Kwa hiyo sheria na sera zao zinachipuza kutoka kwa akili zao ndogo kama zilivyohifadhiwa ndani ya miongozo bandia kwa jina la katiba na kanuni ambazo zinawapa ubwana watu (akili zao). Mfumo wa kisekula wa kirasilimali unapigia debe watu wawe wabinafsi na wachoyo na unaelezea kuwa mafanikio yapo katika kumiliki mali kupindukia na kujitosheleza kiviungo! Hivyo basi, tunaendelea kushuhudia uporaji mkubwa wa rasilimali unaofanywa na masekula warasilimali wachache na kisha baadaye wanabuni suluhisho za kisanii ili kupunguza idadi ya watu mfano ni njia hizi za kudumu za kudhibiti uzazi eti kutatua tatizo la kiuchumi linalowakumba watu ambao kiasili wao ndio wanaowakandamiza na kuwatia katika lindi la umasikini!

Kwa upande mwingine, Uislamu unachipuza kutoka kwa Muumba wa mwanadamu, ulimwengu na uhai. Kwa hiyo Yeye (swt) ndiye Mteremshaji sheria na Yeye (swt) pekee ndiye anayestahili kurudiwa ili kupata muongozo wa kweli. Hivyo basi, ndani ya Uislamu tatizo la kiuchumi SIO uhaba wa rasilimali BALI ni usambazaji wa rasilimali. Kwa sababu hiyo, Uislamu ukaharamisha mzunguko wa utajiri kubakia miongoni mwa watu wachache na kufanya kuwa ni wajibu kuwepo na usambazaji wa haki katika rasilimali. Mwenyezi Mungu (swt) asema: ((كَيْ لاَ يَكُونَ دُولَةً بَيْنَ الأَغْنِيَاءِ مِنْكُمْ “ili yasiwe yakizunguka baina ya matajiri tu miongoni mwenu” [Al-Hashr: 7]

Katika Uislamu uzuiaji wa mimba umeruhusiwa (mubah) kwa sharti kwamba  ni njia ya muda ya kuzuia mimba. Bukhari na Muslim wameripoti kutoka kwa ‘Ataa` kwamba alimsikia Jabir (ra) akisema: “Tulikuwa tukifanya ‘Azl wakati ambapo Qur’an ilipokuwa inashuka.” ‘Azl ni pale ambapo mwanamume anafanya tendo la ndoa na mkewe na anapokaribia kumwaga; anatoa na kumwaga nje. Kwa kutumia hukmu ya ‘Azl basi inakuwa inaruhusiwa matumizi ya madawa, mipira na koili ili kuzuia mimba. Kwa upande mwingine, Uislamu umeharamisha uzuiaji wa mimba kwa njia za kudumu kama vasectomy na tubectomy na nyinginezo kwa kuwa ni aina ya kuhasiwa (kuvunjwa/castration) na yanachukua hukmu ya kuhasiwa juu yake. Bukhari na Muslim wameripoti kutoka kwa Sa’ad bin Abi Waqqas kwamba Uthman bin Maz’un alisema: Ewe Nabii wa Mwenyezi Mungu (saw), Mimi ni mwanamume ninaye pata tabu kwa kukosa mke. Niruhusu nijivunje mwenyewe.” Yeye (saw) alisema: “La! Lakini funga (saum).” Zaidi ya hayo ni kwamba udhibiti wa uzazi ni juhudi tu ya mwanadamu lakini lau Mwenyezi Mungu (swt) anataka, mtoto atazaliwa pasina babake kutaka au kutotaka. Ibn Hibban ameripoti kutoka kwa Anas kwamba Mtume (saw) alisema: “Lau maji yanamotoka mtoto yatamwagika juu ya jiwe, Yeye atatoa kutoka kwayo mtoto.”

Kusitisha kuzaa kwa kudumu kunagongana na Mteremsha sheria kwani amejaalia kizazi na ulezi ndio lengo asili la ndoa. Na ndio maana Mwenyezi Mungu (swt) akasema katika kuonyesha huruma Yake (swt) kwa watu: (وَجَعَلَ لَكُمْ مِنْ أَزْوَاجِكُمْ بَنِينَ وَحَفَدَةً) “Na Mwenyezi Mungu amekuumbieni wake katika jinsi yenu, na akakujaalieni kutoka kwa wake zenu, wana na wajukuu.” [An-Nahl: 72]. Kwa kuongezea ni kwamba Mwenyezi Mungu (swt) amefanya kuwa na watoto wengi ni kitendo kinachopendekezwa (mandoob) na kuwashajiisha watu kukichangamkia na kuwapongeza wale wanaokitekeleza. Ahmad ameripoti kutoka kwa Anas kwamba Mtume (saw) alisema: “Oeni wazuri na wanaozaa kwa hakika napenda Ummah wangu uwe mkubwa kushinda wengine Siku ya Kiyama.”

Kwa kutamatisha, ni uwazi wa kiuhakika kwamba mfumo batili wa kisekula wa kirasilimali umefeli kupambana na matajiri wachache ambao wanawakandamiza wengi, na kuwafanya kupitia mateso na majanga yasiyoingia akilini kutokana na sheria na sera ovu za kikoloni za uvamizi wa mataifa mengine na kupora rasilimali zao bila kuwa na uoga wa kuhesabiwa! Kisha baadaye kiuhadaifu wanajaribu kubuni sera ovu ambazo zinalenga kupunguza idadi ya watu kwa kisingizio cha kutatua tatizo la kiuchumi lililosababishwa na uchache wa rasilimali! Tunatoa mwito kwa kila mwenye akili timamu kuzinduka na kukumbatia ulinganizi wa kurudisha maisha ya Kiislamu kupitia kusimamisha Khilafah kwa njia ya Utume. Ni Khilafah pekee ndio itakayoipa mujtama usalama na utulivu wa kweli kwa kutekeleza kiukamilifu Shari’ah (Qur’an na Sunnah). Hivyo basi, kupelekea kupatikana kwa haki na uadilifu kwa kusambaza rasilimali/utajiri miongoni mwa watu kwa uadilifu miongoni mwa vitendo vingine na ilhali raia wataheshimiwa na kuthaminiwa pasina kuzingatia idadi ya watoto au dini au rangi.

Ali Nassoro Ali

Mwanachama wa Afisi ya Habari ya Hizb ut Tahrir Kenya

Makala Na.58: Ijumaa, 15 Dhul-Hijja 1440 | 2019/08/16