Habari na Maoni

VIRUSI VYA CORONA: Wacha viendelee kuuwa watu mpaka iwe ni mradi mkubwa wa uekezaji

Kusambaza ni Kuunusuru Uislamu

بسم الله الرحمن الرحيم

Habari na Maoni

Habari:

Idadi ya vifo vilivyotokamana na mkurupuko wa maradhi yanayosababishwa na virusi vya Corona huko Uchina imefika 106 siku ya Jumane 28, Januari 2020 huku tayari watu 1,771 kuthibitishwa kuwa wameambukizwa.Hii ni kwa mujibu ya ilivyonukuliwa na wakuu wa serikali. Maambukizi ya maradhi hayo yaliyoibuka mwaka jana katika jiji la Hubei mkoa wa kati yameendelea kuenea maeneo mbalimbali. Kamati ya afya jijini Hubei kitovu cha mkurupuko huo ilisema watu 24 wameaga dunia kutokana na viini na huku 1291 wakiwa tayari wameambukizwa hali iliofanya idadi ya maambukizi kufikia 2,714. Visa vya maambukizi ya virusi hivyo hatari pia vimethibitishwa katika mataifa kadhaa ya bara la Asia- Pacific, Europa na kaskazini mwa Amerika. Kiulimwengu visa vilivyoripotiwa ni elfu 4,520 huku vingi vyake ikiwa ni Uchina na hasa jimbo la Wuhan na maeneo jirani ya mkoa wa Hubei (Duru: Aljazeera)

Maoni:

Virusi vya Corona ni vipya kugundulikwa kwake ambavyo kwa sasa kitaalamu vimepewa jina la “2019-n CoV. Virusi hivi ni sehemu ya kundi la virusi ambavyo hujumuisha vile vinavyosababisha mafua makali na virusi vyengine kama vile shida kubwa ya upumuaji inayojulikana kitaalamu kama SARS (Severe Acute Respiratory Syndrome) na vile vinavyotambulika kama MERS (Middle East Respiratory Syndrome). Wataalamu wa afya wanataja kwamba virusi vya Corona kiasili vimehamia kwa wanadamu kutoka kwa wanyama, hata hivyo maofisaa wa kiafya hawajagundua ni mnyama nani hasa aliesababisha mkurupuko. Kwa wanadamu, virusi vyake husambaa kwa mtu mmoja hadi mwengine kupitia hewa kwa njia ya kukohoa na kupiga chafya miongoni mwa njia nyengine. Virusi hivi vimeibua wasiwasi mkubwa hasa ikizingatiwa bado ni vipya na hadi sasa havijajulikana jinsi vinavyoambukiza watu. Shirika la Afya duniani (WHO) limekua likifanya kazi pamoja na wakuu wa serikali ya Uchina na wataalamu wa kidunia wamekua wakijuzwa kila siku ili waweze kufanya utafiti zaidi wa kuhusu virusi, jinsi gani huathiri watu wanaugua maradhi hayo na namna gani ya kutibiwa na hatua gani nchi zinaweza kuchukua katika kukabiliana na hali hii.

Wanasayansi na wataalamu wa afya wanafanya juhudi za kukabiliana na virusi hivi vipya japo hadi sasa bado shindano yake haijagunduliwa.Japo inawezekana kusemwa kwamba kwa kuwa virusi hivi vimechipukwa kwa mara ya kwanza hivyo shughuli ya kutafuta tiba huenda ikachukua miezi kadhaa, lakini la muhimu ni kuelewa uhalisia wa mfumo wa kirasilimali wenye hulka ya kugeuza kila janga kuwa mradi wa kujitengezea mapato. Mtazamo wa kina juu ya  viwanda vya  utengezaji madawa vya kirasilimali ni kuwa viwanda hivi vinasukumwa na upande wa kupata faida tu; yaani utengezaji na uuzaji wa chanjo  ni kwa kipimo cha kuzalisha tu pesa. Dawa za wagonjwa walio na maradhi sugu wanazozitumia kila siku huzalisha faida zaidi hata kuliko chanjo ya kuzuia magonjwa hayo. Viwanda vya madawa hufuata kanuni za bodi za zinazojulikana kiulimwengu kama FDA (Food and Drugs Adminstration) zinazosimamia kuchunguza na kuondosha dawa zisizotimiza viwango vya kiafya sokoni hii ni baada ya kuzifanyia tena ukakuzi wa kimaabara na kizahanati.Kwa hivyo hali hii hufanya makampuni ya dawa hayo kudai malipo ya gharama za dawa zao ambazo zimefaulu kufikia kiwango cha matumizi. Ni kweli chanjo huletea makampuni mapato sio kwa sababu kila dawa ni ghali bali ni kwa kuwa ni lazima kwanza dawa ziweze kutosheleza watu kwa kiwango cha juu. Hata hivyo jamii katika kununua kwake  chanjo huwezesha wawe na akiba zaidi ya mapeni kuliko kununua kwao madawa. Kwa mfano kununua chanjo ya kuzuia maradhi ya Polio kuna uwezo wa kupunguza hasara za ununuzi wa madawa gharama za kuingia kwenye vituo vya udhibiti wa matumizi wa madawa.

Kwa mfano mkurupuko wa ugonjwa wa Ebola katika mataifa kama vile Liberia na Congo, madaktari walipuuza kufanya utafiti wa kupatikana kwa chanjo yake kwa kuwa haina faida ya kimapato. Matokeo yake ni kufariki dunia kwa maelfu ya watu huko Afrika magharibi. Hii ni ishara wazi kwamba makampuni ya madawa hutanguliza mbele faida za mapeni hata kuliko maadili. Urasilimali haukujengwa juu ya kuchukua maamuzi au hatua kwa misingi ya maadili ispokuwa ni kwa msingi wa faida ya kiuchumi tu. Hivyo siajabu kwamba chanjo ya virusi vya Corona huenda ikavumbuliwa hivi karibuni kama itaonekana imekuwa mradi wa uzalishaji mapato.

Majanga kama haya ya mkurupuko wa virusi vya Corona hufichua dosari kubwa ya mfumo wa kibepari na uchumi wake unaoegemea sera za soko huru, hivyo kuna hitajika pakubwa mfumo mbadala unaojali utu na heshima kwa mwanadamu na kuipa afya yake kipau mbele. Kwa teknolojia za kisasa, serikali ya Khilafah itaweza kubuni mazingira mwafaka ya kuleta ufanisi mkubwa wa utafiti wa madawa. Viwanda vya utengezaji wa madawa vitatengewa pesa viweze kujikita kwenye utafiti wa kina wa kupata chanjo na madawa kutibu magonjwa. Kinyume na zifanyavyo tawala za kibepari ambazo utafiti wa madawa hufanywa kwa hesabu za kujikusanyia faida,upande wake utawala wa Khilafah utaekeza sana katika sekta ya madawa sio kwa kuwa ni fadhila kwa raia wake ama njia ya kujipatia faida bali kama jukumu la kiserikali katika kusimamia mahitaji msingi ya umma ambayo hujumuisha usalama na afya. Mtume SAAW amesema katika hadithi iliosimuliwa na Ubaidullah Bin Mihswan Al-Ansaariy:

من أصبح منكم آمنا في سربه، معافى في جسده، عنده قوت يومه، فكأنما حيزت له الدنيا بحذافيرها‏

Atakayepambaukiwa miongoni mwenu ilhali yuko na amani katika familia yake na kuwa na  afya ya kiwiliwili chake,akawa na chakula cha siku yake ni kama kwamba amemiliki dunia yote.

Ameipokea Tirmidhi

Imeandikwa kwa ajili ya Ofisi kuu ya Habari na Hizb ut-Tahrir na

Shabani Mwalimu

Mwakilishi kwa Vyombo vya Habari Hizb ut-Tahrir Kenya.