Habari na Maoni

Vita Juu ya Ufisadi Havishindiki Chini ya Urasilimali

Kusambaza ni Kuunusuru Uislamu

Habari:

Mnamo Jumanne, 28 Agosti 2018, Naibu wa Hakimu Mkuu wa Kenya (DCJ), Philomena Mwilu, alikamatwa jijini Nairobi juu ya madai ya ufisadi. Naibu huyo wa Hakimu Mkuu baadaye alipelekwa katika Kitengo cha Uchunguzi wa Jinai ili kuhojiwa juu ya masuala ya utumizi mbaya wa afisi, hongo na ukwepaji ushuru. Na mnamo Jumatano, 29 Agosti 2018, alifikishwa katika Mahakama ya Milimani kukabiliana na mashtaka hayo. Kwa mujibu wa gazeti la ‘Daily Nation’, kabla ya kukamatwa kwake Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma, Nordin Hajj, pamoja na mpambanaji mkubwa wa uhalifu Kenya, George Kinoti, walikuwa na msururu wa mikutano na Tume ya Kuwaajiri Mahakimu (JSC). Gazeti hilo lilisema zaidi kuwa Halmashauri ya Ukusanyaji Ushuru ya Kenya iliripoti kwa afisi ya mashtaka ya umma kuwa DCJ huyo alikosa kulipa ushuru vile vile pamoja na viwango vikubwa vya pesa zenye tashwishi vikitoka na kuingia katika akaunti za benki.

Maoni:

Tangu ‘Vita juu ya ufisadi’ vilipo pambamoto Juni mwaka huu, Hakimu Mwilu ndiye mkubwa zaidi katika idara ya Mahakama ya Kenya kuwahi kukamatwa juu ya mashtaka ya ufisadi. Jaji huyo ambaye aliwahi kusifiwa na wenzake kama mwenza aliye na thamani baada ya kufaulu kuwa Naibu wa Hakimu Mkuu katika Mahakama ya Upeo. DCJ huyo alinukuliwa hivi majuzi na vyombo vya habari akisema: ‘sote tunahusika katika vita dhidi ya ufisadi na idara ya Mahakama itacheza dori yake barabara.’ Tukifuata tarakimu za kihistoria za maafisa wote wa umma waliofikishwa mbele ya mahakama juu ya kuondolewa kutokana na ufisadi hakuna yeyote aliyepatikana na hatia wala kufungwa.

Hii si mara ya kwanza kwa maafisa wa serikali kukabiliwa na kesi za ufisadi, kama vile kupokea rushwa. Mnamo 2016, jaji wa Mahakama ya Upeo, Phillip Tunoi, aliangaziwa juu ya madai kuwa alipokea kiwango kikubwa cha hongo ya dola milioni 2 ili kushawishi kesi ya rufaa ya uchaguzi dhidi ya aliyekuwa gavana wa Kaunti ya Nairobi, Evans Kidero. Idara ya Mahakama imejikuta katika sokomoko kutokana na uchunguzi mkubwa juu ya ufisadi ambao wengi wa majaji wakakamavu zaidi nchini wanatetemeka ndani ya majoho yao. Mnamo 2003, majaji wakubwa 23 walisimamishwa kazi wakituhumiwa kwa vitendo vya ufisadi, wakilazimisha kufutilia mbali keshi kadhaa zilizokuwa zinasubiri uamuzi. Maafisa hao wa mahakama wanaokabiliwa na madai ya ufisadi wanapaswa kuchukuliwa kama dalili wazi kuwa taasisi zilizoaminiwa na kupewa jukumu la kupigana na ufisadi zenyewe ni fisidifu na zimekuwa ngome za viongozi wafisadi. Taarifa za mara kwa mara za Raisi Kenyatta kuwa ‘Ufisadi ni dhambi kwa Mungu’ na ‘tishio kwa usalama wa taifa’ zinazidi kuwa maneno matupu.

Kama ilivyo serikali nyengine yoyote ya kirasilimali, Kenya imezongwa na ufisadi huku maafisa wa serikali yake wakikabiliwa na vitendo viovu vya wizi, hongo na utumizi mbaya wa afisi. Maovu haya yamekuwa janga la muda mrefu. Maafisa wote wa dola ndani ya serikali za kisekula hujilimbikizia mali kupitia uporaji wa rasilimali za umma na kusababisha maisha ya raia wa kawaida kuwa magumu kiuchumi huku yale ya viongozi wao yakiwa na ufanisi zaidi. Kwa ukweli huu, uthabiti wa kiuchumi kamwe hautapatikana katika nchi zilizolazimishiwa mfumo fisidifu.

Tatizo msingi la Ufisadi ni Urasilimali ambao tume zilizopewa kazi ya kupigana nao chini ya serikali za kirasilimali zinajaribu kuufungia macho. Suluhisho la kweli na la kihakika liko pekee katika kuachana na mfumo uliofeli, na kuubadilisha kwa mfumo adilifu ambao sio mwengine isipokuwa Uislamu ambao kipimo chake cha kipekee cha matendo ya mwanadamu ni yale ambayo Allah Ta’ala aliyoyaridhia na wala sio manufaa ya kimada.  Hivyo basi, mujtamaa unapaswa kulindwa dhidi ya vitendo vyovyote viovu kwa sababu vinamkasirisha Allah (swt). Uislamu pia unamtaka mtawala kuwahisabu na kuwaondosha mamlakani maafisa wafisadi bila ya uoga wala mapendeleo. Ni kupitia maadili haya; Uislamu ukiwakilishwa na Khilafah Rashida kwa njia ya Mtume (saw) huondoa aina zote za maovu na hueneza aina zote za kheri ulimwenguni.

Imeandikwa kwa Ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir na

Shabani Mwalimu

Mwakilishi kwa Vyombo vya Habari Kenya