Jumla

Wakapanga mipango yao, na Mwenyezi Mungu akapanga yake. Na Mwenyezi Mungu ndiye mbora wa mipango

Kusambaza ni Kuunusuru Uislamu

Jumapili, 10 Februari 2019, Rais Uhuru Kenyatta aliungana na Wakuu wa Serikali na viongozi wa dunia katika kuhudhuria kongamano la 32 la Muungano wa Afrika (AU) mjini Addis Ababa, Ethiopia. Wakiongozwa na mwenyekiti mpya wa AU, Rais wa Misri Abdel Fattah El-Sisi walitangaza kutoruhusu tena ugaidi kudhoofisha nchi nyingine ndani ya Afrika. Kuongezea, Rais wa Misri Abdel Fattah El-Sisi na Mahmoud Abbas, Rais wa Shirika la Ukombozi wa Palestina (PLO) walisema kuwa ugaidi lazima uondoshwe na wadhamini wake wapatikane na waaibishwe. El-Sisi akaelezea kuwa laana ya ugaidi ni kama kansa inayoendelea kuathiri mataifa ya Afrika na kuvunja miundo msingi. Katika hotuba yake ya uchukuaji hatamu alisema, “Kuna umuhimu wa kuwajua wadhamini wa ugaidi na kutatua mzizi wake na kuweka mipango ya kupambana nao.” Kwa upande mwingine, Mahmoud Abbas alisema, “Tuko tayari kupambana na ugaidi na misimamo mikali katika miji yetu yote. Lazima tuchukie aina zote za ugaidi na misimamo mikali.” (Daily Nation, Jumatatu, 11/02/2019)

Matamshi hayo yanadhihirisha kuwa AU kama taasisi inayotumiwa kuendeleza ukoloni mambo leo imekata shauri kuendelea na utekelezaji wa mpango hatari na muovu uliochorwa na mabeberu wa kimagharibi wa kupambana na Uislamu chini ya kisingizio cha kuumaliza  ugaidi. Ni wazi kwa kua Uislamu ni mfumo kamili wa kimaisha wakoloni wamo mbioni kuunyamazisha kote duniani ikiwemo hapa Afrika. Ikumbukwe Waislamu wa bara hili tayari wanahangaishwa na kunyanyasika bali wengine hata kuuliwa kwa kile kiitwacho vita dhidi ya ugaidi.  Kinaya, ni kuwa mwenyekiti wa AU kwa sasa El-Sisi amekua akishirikiana na wamagharibi katika kufanya vitendo vya kigaidi ikiwemo kuwatia mbaroni wanaharakati wengi wa Kiislamu nchini Mwake bali hata wanahabari! Fauka ya haya amekuwa akimwaga damu tukufu za raia wake katika viwanja vya Misri na barabara zake, na bado anaendelea kuwakamata kinyume cha sheria maelfu ya watu wa Misri, huku akitafuta kuwaridhisha Mayahudi na Waamerika.

Mfumo tawala wa kisekula wa kirasilimali unaotokana na akili finyu ya mwanadamu, tangu ulipochukuwa hatamu baada ya Mapinduzi ya Ufaransa mnamo 1789 umesababisha majonzi na majanga kwa wanadamu. Hivyo basi, mnamo 1917 mfumo wa wa ujamaa unaotokana na akili finyu ya mwanadamu; ulichipuza na kuongozwa na Urusi ili kupambana na maovu ya mfumo wa kirasilimali lakini ukafeli na kuvunjwa rasmi mnamo 1992 na Amerika! Tokea wakati huo wanadamu wako katika mbio kutafuta mfumo badala kutokana na maisha yao duni wanadidimia katika umasikini wa kupindukia, sera za sumu za elimu, kusambaratika kwa miundo ya familia, sera za uchumi zenye kuzidisha pengo kati ya matajiri na masikini miongoni mwa mengine. Mfumo badala uliobakia na uliowahi kutumika na kudhihirisha kuwa unao uwezo wa kutoa utulivu, maendeleo na ustawi wa kweli chini ya kiongozi muadilifu anaye tawala kwa Shari’ah (Qur’an na Sunnah) ni mfumo safi wa Uislamu unaotoka kwa Muumba wa viumbe. Kwani umedhihirisha kivitendo uwezo wake kupita maelezo ndani ya Karne 13 zilizopita tokea kwa tukio la Kihistoria la Hijrah mnamo 622 Miladi ndani ya Madinah.

Hivyo basi, walinganizi wa mfumo batili wa kisekula wa kirasilimali na nidhamu zake wakiongozwa na Amerika na washirika wake wamekata tamaa na wanajaribu kuufinika na kuuhifadhi mfumo wao kwa kuuweka ndani ya chumba cha maututi lakini kiasili umefariki kitambo! Wakati huo huo wanatishia kimaneno na kijeshi Uislamu na Waislamu wanaojifunga kikamilifu kwa kudai ni ugaidi na misimamo mikali mtawalia! Kwa kuwa kumbukumbu zao bado ziko makini na wanachelea kurudi tena kwa Uislamu kama mfumo tawala na Waislamu kuchukua tena usimamizi wa ulimwengu! Na ndio maana aliyekuwa Rais wa Amerika Obama siku ya Alhamisi, 4 Juni 2009 alitoa hotuba katika Chuo Kikuu cha Cairo ndani ya Misri na kusisitiza juhudi za pamoja dhidi ya misimamo mikali (The New York Times, 04/06/2009).  Akifuatiwa na Rais wa sasa wa Amerika Donald Trump ambaye siku ya Jumapili, 21 Mei 2017 alitoa hotuba yake katika Jumba la Kongamano la King Abdulaziz  ndani ya Saudi Arabia na kusisitiza juhudi za pamoja za kupigana na ugaidi na kuzindua Kitengo cha Kiulimwengu cha Kupambana na Mfumo wa Misimamo Mikali (GCCEI) (Arab News, 22/05/2017). Hivi majuzi Waziri wa Kigeni wa Amerika wa sasa Mike Pompeo siku ya Alhamisi, 10 Januari 2019 alitoa hotuba yake katika Chuo Kikuu cha Amerika mjini Cairo ndani ya Misri na kusisitiza juhudi za pamoja za kutathmini upya mapambano dhidi ya Uislamu wenye misimamo mikali (Cairo Informer, 10/01/2019).

Ni wazi kabisa AU na uongozi wake unaojumuisha watawala vibaraka wamesukumwa na wamagharibi katika kupambana na Uislamu na Waislamu ndani ya bara na ulimwenguni kwa ujumla. Wakati huo huo wamejitia upofu wasione kuwa ugaidi na wadhamini wake wakubwa ni mabwana zao wakoloni wamagharibi wakiongozwa na Amerika na washirika wao wakiwemo Uingereza, Ufaransa, Uchina, Urusi n.k. Kuongezea zaidi, wamekataa kuitizama historia ya enzi ya Kiislamu ya dhahabu iliyo shuhudiwa na wanadamu wote duniani na hususan Ulaya, Mashariki ya Kati na Pembe ya Afrika n.k zilizokuwa chini ya uongozi wa Khalifah mchamungu aliyekuwa sawa na mtu wa chini kicheo ndani ya Khilafah mbele ya Shari’ah. Kwa kufanya hivyo AU itaendeleza sera yake ya kuwabandikiza Waislamu waliojifunga kikamilifu kuwa ni wenye Misimamo Mikali na kuyafanya maisha yao kuwa magumu mno na wale ambao miguu yao iko kati ya urasilimali na Uislamu kuwa ni wenye Misimamo ya Kati/Wavumilivu na ambao wanawiana na mtizamo wao wa Uislamu wanao utaka.

Kwa kuhitimisha, uamuzi wa AU na uongozi wake kwa mara nyingine unaonesha kikweli maumbile yake na kwamba ni ya kusaliti watu wake hususan Waislamu na Uislamu wao kwa kushiriki katika kuwapangia njama dhidi yao ili kuwasasabishia madhara makubwa!  Na hilo ni kupata tu maslahi yao kibinafsi hasa ikijulikana wazi kwamba serikali nyingi za Kiafrika huongwa vijisenti na warasilimali ati kufadhili mikakati ya usalama duniani! Hivyo basi usaliti wao unahitaji mabadiliko msingi na ya kweli yaliyokitwa katika kuitikia mwito wa Kurudisha Tena Maisha ya Kiislamu kwa kusimamisha Khilafah kwa njia ya Utume kama inavyolinganiwa na ndugu zenu wa Hizb ut Tahrir. Ni kupitia kusimamisha Khilafah pekee ndio ukombozi wa kweli wa wanadamu ndani ya Afrika na ulimwengu jumla utafikiwa. Ukombozi utakuwa wa kutoka katika kiza cha kutawaliwa na mfumo wa kisekula wa kikoloni wa kirasilimali hadi katika nuru ya utawala wa mfumo wa Uislamu. Afrika chini ya kiongozi mwenye uwezo na kujali, Khalifah  mchamungu aliye na hamu ya Pepo ya juu atawapiga marufuku na kuwafukuza waizi wa mali nyingi za Afrika na mfumo wao wenye sumu na kisha kutekeleza kikamilifu Shari’ah ili kuboresha maisha ya binadamu (Waislamu na wasiokuwa Waislamu) chini ya usimamizi wake. Wakati wakuchukua uamuzi ni sasa kabla waandishi wa historia waondoshe kalamu zao za dhahabu kutoka katika vitabu vyao vya dhahabu. Uamuzi huo ni ule wa kusema ukweli na kudumu nao, kuwa msitari wa mbele katika njia ya ukombozi wa kweli wa Kiislamu na kutamani Pepo ya milele. Hakika ushindi upo kwa wale walioko upande wa Mwenyezi Mungu mbora wa mipango:

(وَيَمۡكُرُونَ وَيَمۡكُرُ ٱللَّهُ‌ۖ وَٱللَّهُ خَيۡرُ ٱلۡمَـٰڪِرِينَ)

“Wakapanga mipango yao, na Mwenyezi Mungu akapanga yake. Na Mwenyezi Mungu ndiye mbora wa mipango” [Al-Anfaal: 30]

Ali Nassoro Ali

Mwanachama wa Afisi ya Habari ya Hizb ut Tahrir Kenya