Washindi na watakaoshindwa kwenye uchaguzi wa August wote ni mawakala wa mfumo uliofeli wa Demokrasia

Habari na Maoni

Habari:

Huku zikiwa zimesalia siku chache kabla ya kufanyika kwa uchaguzi wa Agosti 9, baadhi ya viongozi wa Kiislamu pamoja na Wanazuoni wa Serikali nchini, wamewataka Waislamu kuwafanyia tathmini na kuwahakiki wagombea wa viti tofauti ili kufanya maamuzi sahihi. Imekua ni hulka kwa wanavyuoni hawa kupindisha maana ya aya na kutumia vibaya kanuni za kifiqhi kama vile ‘uovu mdogo’ kuwataka Waislamu kushiriki kikamilifu katika uchaguzi.

Maoni:

Kutoa hukumu ya Kiislamu juu ya kushiriki kwenye chaguzi za Kidemokrasia kunatupasa kwanza kuangalia kwa kina  maana ya uchaguzi wa Kidemokrasia na hali hii itatubidi tuangalie kile kiitwacho uhalisia wa jambo (Tahqiq il Manat’) i.e yaani ni uchaguzi na nini hasa maana ya Demokrasia kama mfumo wa kiutawala. Uchaguzi ni uwakilishaji ambapo mtu huchagua mtu amwakilishe kwenye kufanya jambo kwa niaba yake. Kinachofanya uchaguzi kuwa halali au haramu sio ule uchaguzi wenyewe kwa dhati yake bali ni kile kinachofungamana nao.

Neno la Demokrasia asili ni mkusanyiko wa matamshi mawili yenye asili ya Kigriki Demos ambao humaanisha watu na cratos ikimaanisha utawala kwa maana ni utawala wa watu. Utawala huu humaanisha wanadamu wanamiliki ubwana (sovereignity) unaowawajibisha watunge kanuni ambazo ndio hutukuzwa kuliko sheria za MwenyeziMungu swt. Hivyo Bunge au baraza la seneti, la wawakilishi au Congress zote katika demokrasia ni taasisi za kutunga kanuni. Sasa Demokrasia huchukua mbinu ya uchaguzi kila baada ya miaka 5 au 4 ya watu kuwachagua watu wawe ni wawakilishi wao katika kazi ya kutunga kanuni. Kwa kifupi chaguzi za Kidemokrasia zinafungika katika kitendo cha kutunga sheria ambacho kinagongana na Uislamu.

Kwa mujibu wa Uislamu, sheria sio miliki ya yoyote yule ila ni ya MwenyeziMungu swt. Yeye MwenyeziMungu swt  ndiye mteremshaji sheria hivyo sheria yoyote ile inayotungwa na mwanadamu haifai na ya kimakosa hatakama inaafikiana na ile ya MwenyeziMungu hii ni kwa kuwa kazi ya kuweka sheria si ya yoyote yule ila ni ya MwenyeziMungu swt. Bali Uislamu umewajibisha kufuata sheria za MwenyeziMungu swt.Asema Allah swt:

فَلَا وَرَبِّكَ لَا يُؤْمِنُونَ حَتَّىٰ يُحَكِّمُوكَ فِيمَا شَجَرَ بَيْنَهُمْ ثُمَّ لَا يَجِدُواْ فِىٓ أَنفُسِهِمْ حَرَجًا مِّمَّا قَضَيْتَ وَيُسَلِّمُواْ تَسْلِيمًا

Naapa na Mola Wako Mlezi hawawi na Imani ya kikamilifu hadi wakufanye wewe ni hakimu katika yale wanayozozana kisha isipatikani ndani ya vifua vyao uzito wowote katika yale uliyowahukumia na wajasilimishe kikamilifu

[An-Nisai: 65]

Huu ndio uhalisia wa uchaguzi, hivyo kinachofanya uchaguzi uwe halali au sio halali sio uchaguzi wenyewe bali ni kazi inayofungamana nao. Kwa ujumla chaguzi za Kidemokrasia ni kinyume na sheria ya Kiislamu hivyo ni haramu kwa Waislamu kupigia debe na kuunga mkono vyama vya kisiasa vya Kidemokrasia na kushiriki kwa uchaguzi wake. Ni dhahir shahir kwamba kufanywa kwa chaguzi za kila mara za kidemokrasia ni jaribio la kuteka nyara hisia za mabadiliko kwa watu kwa mfumo uliofeli tayari. Washindi na wanaoshindwa kwenye chaguzi hizi za Kidemokrasia ni vibaraka wa mabeberu ambao kazi yao msingi ni kuziba aibu za Demokrasia zilizoitumbukiza Kenya na Afrika kwa ujumla kwenye maafa na mizozo.

Baya zaidi ni kuwaona wanavyuoni wa Serikali ambao baadhi yao wamekua ni wapambe wa wanasiasa wakipinda matumizi ya maana ya qaida madhara mepesi wakiwataka Waislamu wasijifunge na sheria za Kiislamu na kufanya kazi ya kuleta mabadiliko ya kweli, yaani kuulingania Uislamu uweze kutawala dunia chini ya Khilafah  Raashida kwa mfumo wa unabii. Kiini cha majanga yanayokabili Kenya sio nani anatawala bali ni anatawalisha kwetu mfumo gani. Maadamu nchi inaendelea kutawaliwa na kanuni na tungo za Kidemokrasia tofauti na sheria za alizoteremsha MwenyeziMungu basi hatutoona mabadiliko ya kikweli.

Imeandikwa kwa Niaba ya Ofisi kuu ya Habari ya  Hizb ut-Tahrir na

Shabani Mwalimu

Mwakilishi kwa Vyombo Vya Habari Hizb ut Tahrir Kenya

Comments are closed.