Yapi ya kujifunza kutoka kwa kisa cha Ibrahim (AS) na Mwanawe Ismail.

Nabii Ibrahim (AS) alitajwa katika Quran mara 73 na kwenye sura 25. Alizaliwa katika Mji Babylon nchini Iraq.  MwenyeziMungu (S.W.T) alimfanya Ibrahimi kuwa mwandani wake na  miongoni mwa wale manabii wanne wastahamilivu wakubwa (Ulul–azmi). Manabii hao ni Nuh, Ibrahim, Musa na Isa) Rehema na Amani ziwashukie wote. Walipewa sifa ya ustahmilivu kwa kujipinda kwao katika ulinganizi wa Dini ya Mwenyezi Mungu(s.w.t) huku wakijipamba na sifa kubwa ya subra katika njia hiyo.Tumuangilie Nabii Ibrahim kwenye kisa cha ndoto ya kuchinja mwanawe Ismail ambacho hadi leo umma wa Muhammad (S.a.w) hukienzi kisa kwa kutekeleza ibada ya kuchinja mnyama katika siku kuu ya Idul-Adh-ha. Tuangalie kisa hiki na kuchukua baadhi ya mafunzo makubwa kwetu.

Ibrahim alimuomba Mola wake amruzuku mtoto mwema akiwa kwenye umri wa miaka 86 na hii ni kama alivyotaja Ibn Kathir katika tafsir yake.

. { رَبِّ هَبْ لِي مِنَ الصَّالِحِينَ . فَبَشَّرْنَاهُ بِغُلامٍ حَلِيمٍ}

Ee Mola wangu! Nipe (mtoto awe) miongoni mwa watenda mema.  Ndipo tukampa habari njema ya kuwa atapata mtoto mpole.

[As-saafat: 100-101]

Hapa kuna funzo kwa wanandoa ambao bila shaka uchu wao wa kupata watoto huwa ni mkubwa sana hasa ikiwa umepita muda mrefu katika ndoa yao na hawajaruzukiwa mtoto. Shauku  hii wakati mwengine huweza kuwapelekea kuvuka mipaka kwa kumshirikisha Mwenyezi Mungu (s.w.t) baada ya kumaliza mahospitali ili angaa wapate mtoto. Katika aya hizi, Ibrahim(A.S) naye yupo kwenye umri wa uzee ambao huwa mtoto ana nafasi kubwa ya usaidizi, akamuomba Mola wake ampe sio mujarad tu ya mtoto bali mtoto mwema. Anatufundisha hapa kwamba wa kuombwa pekee ni Mwenyezi Mungu(s.w.t), pia kuwa tunatakikana kuomba watoto wema kwani huwa ni tulizo na pozo kwa mioyo na macho yetu. Bila shaka mtoto mwema ni yule ambaye atakupa utulivu bali pia katika kukusaidia katika kubeba majukumu. MwenyeziMungu(S.W.T) akajibu dua ya Ibrahim(A.S) kwa kumpa kijana wa kiume tena mwenye kupambika na sifa ya upole sifa inayovutia. Dua hii ikammakinisha zaidi Ibrahim kuwa mtoto mwenyewe ni wa kiume kisha atafika umri wa kuweza mtuma katika kazi zake.

Ismail alipofika na umri takriban wa miaka 16, Mwenyezi Mungu akamtahini Ibrahim (A.S) kwa kumuamuru amchinje mwanawe!  Amri hii inakuja kwa njia ya ndoto wakati ambapo Ibrahim ameonja mahaba ya kuwa na kijana! Hapa alijaribiwa Ibrahim baina ya mapenzi yake kwa Mola wake na ya mtoto wake yapi makubwa zaidi.

. فَلَمَّا بَلَغَ مَعَهُ السَّعْيَ قَالَ يَا بُنَيَّ إِنِّي أَرَى فِي الْمَنَامِ أَنِّي أَذْبَحُكَ فَانْظُرْ مَاذَا تَرَى قَالَ يَا أَبَتِ افْعَلْ مَا تُؤْمَرُ سَتَجِدُنِي إِنْ شَاءَ اللَّهُ مِنَ الصَّابِرِينَ .

Basi alipofika (makamu ya) kwenda na kurudi pamoja naye alimwambia: Eee  mwanangu! Hakika mimi nimeota katika ndoto ya kwamba ninakuchinja. Basi fikiri waonaje?’ Akasema: ‘ Ee baba yangu fanya unayoamrishwa utanikuta Inshallah ni miongoni mwa wanaosubiri.

[Assafat:102]

Kuna dhihirika ubusara wa Ibrahim kwa kijana wake jinsi alivyomuita kwa mapenzi makubwa ya baba kwa mwanawe … ‘ee mwanangu’ Kwa wazazi tunapata faida hapa kutumia lugha nzuri kwa watoto kwani huku hupelekea wao kuwa wachangamfu wa kutaka kutusikiliza yale tunayotaka kuwaambia. Jibu la Ismail la kumwambia Baba yake; ‘ ee baba yangu! ‘fanya unaloamrisha” ni kuoneshwa faida ya kuwa na mtoto mwema huwa hawi mpinzani wa baba yake hususan katika kufuata maamrisho  ya Mwenyezi Mungu(s.w.t). Ushauri wa Ibrahim kwa mwanawe sio kuwa alimtaka akatae amri hiyo bali ni kumtayarisha katika kujifunga na amri kutoka kwa Muumba hivyo aangalie kule ilikotoka amri hii! Hapa ndio mwana naye akafaulu kumjibu babake, yeye apaswa kutekeleza amri ya MwenyeziMungu na kuwa yeye yuko tayari kuitekeleza amri hiyo yawe yatakayo kuwa yawe.Naam, mapenzi ya MwenyeziMungu na Sheria zake hutangulizwa zaidi kuliko ya watoto,wazazi na hata biashara.Lau mahaba haya yanakuwa hai katika nyoyo zetu basi Waislamu wangejitolea ghaya ya kujitolea katika kuutangaza Uislamu hususana katika kipindi ambacho Wamaghariba wanaupaka matope na kuupiga vita.

Ibrahim na Mwananwe Ismaili (Amani za MwenyeziMunugu ziwe juu yao) wanatufundisha kwamba sheria za MwenyeziMungu hazifanyiwi mjadala bali ni watu kujifunga nazo moja kwa moja. Aidha, kujifunga na sheria hakuangaliwi upande wa maslahi bali maslahi yapo katika kufuata na kutekeleza sheria za MwenyeziMungu. Ndio, kwa kipimo cha maslahi hapa ingekuwa nabii Ibrahim kiakili ni kutotekeleza amri ya kumchinja mwanawe kwani ilikuwa ni kuhatarisha maslahi yake na ya mwanawe! Lakini wapi! Ibrahim alitambua kwamba akili sio ya kujadili sheria bali ni chombo cha kufahamu sheria ili itekelezwa pasina kuangalia kipimo cha maslahi. Funzo hili ni muhimu sana hasa kwa zama zetu leo ambapo Waislamu wengi kwa kuishi ndani ya mfumo wa kimaslahi wa kirasilimali wakikengeuka sheria za Kiislamu kwa msingi wa maslahi. Mbali na haya viongozi wengi wa kidini leo wameuza dini yao kwa ajili tu ya pochi! Kwa mfano, waislamu wengi wamekua wafuasi wa vyama vya kisiasa kwa msingi kuwa ni kutaka maslahi yetu yawe salama. Husemwa kwamba hatakama Demokrasia ni ukafiri lakini tusiposhiriki katika chaguzi zake maslahi yetu yatakua hatarini! Je haijakuwa kufuata Uislamu ndio kuna maslahi kwetu hapa duniani bali na kesho Akhera.

Wawili hawa wakawa tayari kujifunga na amri hii nzito

فَلَمَّا أَسْلَمَا وَتَلَّهُ لِلْجَبِينِ . وَنَادَيْنَاهُ أَنْ يَا إِبْرَاهِيمُ . قَدْ صَدَّقْتَ الرُّؤْيَا إِنَّا كَذَلِكَ نَجْزِي الْمُحْسِنِينَ . إِنَّ هَذَا لَهُوَ الْبَلاءُ الْمُبِينُ . وَفَدَيْنَاهُ بِذِبْحٍ عَظِيمٍ

Basi wote wawili walipojisalimisha kwa MwenyeziMungu na akamlaza kifudifudi amchinje. Palepale tulimwita: Ee Ibrahim: Umekwisha sadikisha ndoto yako (sasa usimchinje mwanao). Kwa yakini hivi ndivyo tuwalipavyo watendao wema. Bila shaka Jambo hili ni jaribio lililo dhahiri.

[ As-safat:103-104]

Hapa twaona jinsi gani familia iliojijenga katika misingi ya kumjua Mwenyezi Mungu(s.w.t) jinsi inavyoshirikiana katika kubeba majukumu mazito ya kidini kwa lengo la kumridhisha Allah. Jinsi gani kujitolea mhanga ikibidi hata nafsi zetu kwa ajili ya kujifunga na sheria za Allah. Tuko katika zama ambazo sheria za MwenyeziMungu zimedharauliwa badali yake kutukuzwa kanuni za kibinadamu. Basi bishara ilioje kwa yule atakayeenzi sifa hii ya Ibrahim na Mwanawe (AS) ya kujitolea. Leo hatuambiwi tuchinje watoto wetu bali mtihani ni kuulingania kuhuisha maisha ya Kiislamu ndani ya Khilafah juu ya mfumo wa bwana Mtume Muhammad(S.A.W).

Hakika ulikua ni mtihani mzito ambapo ndani yake tunapaswa kuzingatia kila tunapoingia kwenye Idul Adh-ha. Twapata mwisho wa kisa hiki kwamba MwenyeziMungu alimkomboa Ismail kwa kichinjwa kitukufu naye ni kondoo dhihirisho ya kuwa siku zote Allah hunusuru waja wake ambao hunusuru sheria zake na Dini yake kwa ujumla. Hivyohivyo, ili kunusurika na makucha ya mfumo wa kibepari yanayoumiza na kuangamiza viumbe na mimea basi hatuna budi kujifunga na sheria za Allah

Shabani Mwalimu,

Mwakilishi kwa Vyombo Vya habari.

Hizb ut-Tahrir Kenya.

Comments are closed.