Jumla

ZAKATUL FITRI

Kusambaza ni Kuunusuru Uislamu

Moja katika maafa ya mfumo wa kibepari yanayoshuhudiwa duniani kote ni kiwango kikubwa cha umasikini kinachoendelea kwa kasi kubwa kila uchao. Umasikini hautokamani na dhana ya uhaba wa rasilimali kama wanavyodai wanauchumi wa kibepari, bali umetokamana na sera za kiuchoyo na ubinafsi zinazofanya watu wasiweze kugawa mali kufikia umma. Kwa msingi huu, suluhisho na mikakati ya serikali za kibepari zinazodaiwa kulenga kuondosha umasikini ni urongo mtupu.

Uislamu umetangaza vita vya kikweli dhidi ya umasikini wala sio kimesemo tu kama hali tawala za kirasilimali. Ukweli wa Uislamu katika kuondosha tatizo la uchochole hudhihirika katika mafunzo mengi kuhusiana na utoaji wa  Zaka na Swadaka. Mmoja ya sheria hizi ni faradhi ya kutoa zakatul Fitri. Zaka hii pia hujulikana kama zakatul badan (zaka ya kiwiliwili) pia hutambuliwa kwa jina la Swadaqutul Fitri. Majina yote ni yenye kuashiria maana mamoja nayo ni zaka ya fitri ilioitwa kwa jina hili kwa sababu ya mahusiano yake na siku kuu ya Idul Fitri. Kwa kulingana Uislamu, Zaka aina hii ni faradhi inayompasa kila Muislamu aliye na chakula cha kumtosha akawa na cha ziada kuanzia ule usiku wa kuamkia Iddi pamoja na mchana wake. Hivyo ule mtazamo  kwamba zaka hii huwapasa pekee matajiri wanaomiliki mamalioni ya pesa ni dhana potofu.

Ushahidi wa kuwa Zakatul Fitri ni faradhi ni hadithi iliopokelewa na Maimamu wawili (Bukhari na Muslim) kutoka kwa Ibn Umar Radhi za MwenyeziMungu zimshukie alisema:

فرض رسول الله صلى الله عليه وسلم زكاة الفطر من رمضان على الناس، صاعا من تمر، أو صاعا من شعير، على كل حر أو عبد، ذكر أو أنثى، من المسلمين

“Alifaradhisha Mtume wa MwenyeziMungu Rehma na Amani za MwenyeziMungu zimshukie yeye zaka ya Fitri katika mwezi wa Ramadhani kwa watu, pishi moja ya tende, au pishi moja ya shairi kwa mtumwa, mtu huru, mwanaume, mwanamke na mtoto mdogo na mzee miongoni mwa Waislamu.”

Hadithi hii inabainisha kwamba Zakatul Firti ni wajibu kwa Muislamu nayo hutolewa mwisho mwa mwezi huu mtukufu wa Ramadhani. Licha ya kwamba Uislamu ulihimiza watu kutoa swadaka kwa wingi ndani ya kipindi chote cha Ramadhani hadithi imehusisha zaka hii maalumu kuwa sio swadaka tu bali ni swadaka kwa njia ya ulazima. Kwa maana Muislamu atakayeacha kuitoa ilhali ana uwezo basi anapata madhambi.

Kujumuishwa mtoto mdogo hapa kunajenga ufahamu wa kwamba zaka hii ya Fitri kama ile zaka ya Mali haingaliwi kigezo cha umri au utimamu wa akili. Hivyo inamaanisha mtoto mdogo japo hajakalifishwa kisheria lakini ni jukumu la wazazi wake wamtolee. Kwa maana lau mtoto anazaliwa usiku wa kuamkia idi basi ni juu ya mzazi wake amtolee. Na hapa ndio huitwa zaka hii kuwa ya kiwiliwili yaani mtu hujitolea yeye kisha kila anayemlazimu kumlisha. Watu wote hawa ambao humlazimu Muislamu kuwalisha kama vile watoto wake au wazazi wake huwapewi zaka hii bali kinacholazimu ni kuwatolea.

Ama kiwango kitolewacho cha zaka hii ni kama ilivyobainisha kwenye hadithi hii nacho ni Saa’; yaani Pishi moja. Pishi moja kwa vipimo vya leo ni sawa na kilo mbili na nusu au kilo tatu. Hatakama chakula kilichotajwa kwenye hadithi ni tende na shairi, lakini yafaa pia kutolewa chakula chochote ambacho watu huwa wanamazoea ya kukipika makhsusu kwa Idd. Kwa  haya, Mchele au Ngano hufaa kutowela kama zakatul fitr. Yafaa pia kutoa pesa baada kwa thamani ya kiwango hivyo vya kilo mbili na nusu au tatu.

Swadaka hii hutolewa kabla ya watu wa kutoka kwenda kuswali japo inafaa pia kutolewa kwa siku moja au mbili kabla ya Iddi. Ama kwa makusudi mtu akaichelewesha kwa kuitoa baada ya swala ya Idi basi haitokuwa Zakatul Fitri bali itakuwa yahisabiwa ni miongoni mwa sadaka za kawaida.

Hekima ya kufaradhishiwa zakatul fitri ni kama alivyopekea Ibn Abas katika:

فرض رسول الله صلى الله عليه وسلم زكاة الفطر طهرة للصائم من اللغو و الرفث وطعمة للمساكين

Alifaradhisha Mtume (SAAW) Zaka ya Fitri ili iwe ni kisafisho cha mwenye kufunga kutokamana na maneno machafu na mambo mabaya (yaliyompitikia ), na ni lishe kwa masikini.

Hivyo, Swadaka hii itolewapo huwa ni kuisafisha swaum. Ufahamu mwengine wa hadithi ni wale wanaostahiki kupewa zaka hii nao ni masikini miongoni mwa Waislamu ambao nao pia huhitaji kuwa na furaha siku ya Idi kwa kupika vyakula vizuri. Na kwenye hadithi hii, kunadhihirika himizo la Uislamu kwa Waislamu siku wawe na hisia ya kueneza furaha kwa ndugu zake wa Kiislamu. Sio katika mafundisho ya Uislamu kwamba Muislamu mmoja kutomuondolea dhiki nduguye Muislamu.

Twamuomba MwenyeziMungu atupe taufiq ya kuitekeleza ibada hii ya Zakatul Fitrr.

 

Shabani Mwalimu

Mwakilishi kwa Vyombo Vya Habari,

Hizb ut-Tahrir Kenya.